| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 21 | 8 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) | ||
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mpanda Vijijini ambao walinipa dhamana ya kuwa hapa Bungeni kwa heshima kubwa ya kuwa mwakilishi wao, naomba niwashukuru kwa dhati sana. Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia suala la Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ambao ulizaa Taifa moja la Tanzania. Muungano huu ni muhimu sana kwa wananchi wa pande mbili za Muungano wa nchi hizi mbili zilizoungana kwa hiari na makubaliano yaliyofanywa na waasisi wawili, Hayati Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambao waliunganisha nchi hizi mbili. Mheshimiwa Naibu Spika, waasisi hawa walitumia busara kubwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Mimi naunga mkono muundo wa Muungano uendelee kuwepo wa Serikali mbili na ziangaliwe kasoro zilizopo kwenye Muungano, zirekebishwe kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili. Maeneo ambayo yanatakiwa kuangaliwa ni mgawanyo wa fedha kwa Serikali zote mbili, ushirikishwaji wa masuala ya kimataifa na mfumo wa kodi uangaliwe upya. Haya yakiangaliwa, naamini Muungano huu utadumu kwa muda mrefu. Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazingira ni muhimu sana katika maisha ya Watanzania. Tusipoangalia kwa undani zaidi, Taifa hili litaingia katika wakati mgumu sana. Serikali lazima iandae mpango mkakati wa kulinda mazingira, vinginevyo Taifa hili litakuwa Jangwa. Eneo la kwanza la kuangalia ni suala la mifugo. Mifugo inaharibu sana mazingira ya nchi hii. Serikali isipodhibiti ufugaji wa bila mpangilio maalum, basi vyanzo vyote vya mito, mabwawa, ziwa na misitu itatoweka, kwani idadi ya mifugo ni mingi sana iliyopo katika nchi hii inayoendelea kuharibu maeneo mbalimbali na kuhamia katika eneo lingine la nchi hii. Hivyo naiomba Serikali idhibiti ufugaji wa kuhamahama. Tukiacha ufugaji holela, basi vyanzo vyote vya maji na misitu itakuwa katika hali ya kutoweka. Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba Serikali iandae mpango mkakati wa kueneza nishati ya umeme vijijini ili nishati hii ikienezwa itoe misitu inayotakiwa kwa wingi kwa ajili ya nishati ya kuni. Taifa hili pamoja na kuwa na misitu mingi, ipo hatari ya kutoweka kwa sababu wananchi karibu wote wa nchi hii wanatumia nishati inayotegemea misitu. Mheshimiwa Naibu Spika, endapo hayo yatafanyiwa kazi, naamini tutafaulu kuliona Taifa hili. Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba kuunga mkono hoja. |
|||||