You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Kakoso, Moshi Selemani[CCM]

Mpanda Vijijini Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 13 27 June 2011 Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Lakini napaswa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mpanda Vijijini kwa kuniwezesha kunipa kura za ushindi zilizonifikisha katika Bunge hili Tukufu. Lakini nitakuwa sio mwingi wa shukrani kama sitawashukuru kwa dhati viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi, kuanzia ngazi ya Matawi, Wilaya, Mkoa hadi Taifa, kwa kusimamia Chama cha Mapinduzi kiweze kuongoza Serikali ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuisimamia Serikali kwa uadilifu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nianze tu kwa kuunga mkono hoja ya hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu ambayo kaiwasilisha. Naamini bajeti iliyowasilishwa imegusa kila aina na karibu kwa maisha yote ya Mtanzania wa Tanzania hii. Tuna changamoto mbalimbali katika maeneo yetu, hasa Mmikoa iliyosahaulika ya Rukwa, Kigoma na Tabora. Mikoa hii ilisahaulika kwa muda mrefu sana. Nianze tu kwa kuishukuru Serikali kwa kutupa au kutuwezesha kuandaa miundombinu hasa ya barabara, reli na usafiri wa anga kwa maana ya kutujengea uwanja pale mjini Mpanda na reli, kutuhakikishia katika kipindi chote ambacho reli zilifungwa, maeneo mengine kama sisi Mpanda, tuliokuwa tunapata huduma ya reli. Hivyo, napaswa kuishukuru Serikali katika hayo waliyotufanyia wananchi wa Mpanda.

Mheshimiwa Spika, lakini bado tuna changamoto kubwa sana hasa ya miundombinu. Serikali imefanya jitihada za dhati kuanza kujenga barabara ya Tunduma mpaka Sumbawanga kwa kiwango cha lami. Lakini bado kuna barabara inajengwa kutoka Sumbawanga kuja mpanda. Barabara hii ujenzi wake unakwenda kwa kusuasua. Naiomba Serikali ielekeze nguvu sana katika kuhakikisha barabara hii inaimarishwa na kukamilika kwa wakati. Kukamilika kwa barabara hizi kutafungua milango hasa kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa na Katavi, wanaotegemea shughuli kuu za kilimo.

Mheshimiwa Spika, lakini bado tuna barabara ambazo hazijaingizwa katika mpango maalum, hasa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kasulu, mpaka Mkoa wa Kigoma. Barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Mpanda na wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Barabara hii ikifunguliwa, ikajengwa kwa kiwango cha lami, itawasaidia wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Rukwa au Mkoa wa Katavi. Wataendelea kimaendeleo kwa sababu Mikoa hii inazalisha mazao, lakini tatizo kubwa ni miundombinu michafu. Niihimize Serikali kuhakikisha barabara hii inapewa kipaumbele cha aina yake inavyopaswa.

Mheshimiwa Spika, lakini tunayo barabara nyingine ya kutoka Mpanda kupitia Sikonge, kwenda Mkoa wa Tabora, barabara hii kwa sasa inapitika, lakini tulikuwa tunaiomba Serikali nayo iwekwe katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii itakapokuwa imekamilika, itawafanya wananchi wa Mpanda wawe na mawasiliano ya karibu na Mkoa wa Tabora. Niihimize sasa Serikali katika hili liweze kutekelezwa kwa muda unaotakiwa. Lakini bado tuna changamoto ya reli. Reli hii ni ya muda mrefu, ina uchakavu na bado mabehewa wanayotumia wananchi hayaridhishi.

Nitoe tu shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi - Mheshimiwa Athumani Rashid Mfutakamba, kwa kufanya jitihada za dhati kuzitembelea reli za Mkoa wa Kigoma, Mpanda na kufika katika maeneo ya eneo la bandari inapojengwa kule Kalema na kushuhudia uwanja wa ndege wa mpanda unavyojengwa. Lakini jitihada hizi tunaomba zizidishwe ili kuhakikisha uwanja ule unakamilika kwa muda muafaka na kuhakikisha maeneo ya bandari ile ya Kalema inakamilika na kuhakikisha wananchi wanaofanya kazi katika ile bandari, hasa vibarua, wanalipwa malipo yao kwa muda na wakati sahihi.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa ili uendelee unahitaji nishati ya umeme na umeme huo tunaomba uelekezwe vijijini. Tuna maeneo ambayo ni ya muhimu sana katika shughuli za uzalishaji. Maeneo hayo yako kule katika ukanda wa Ziwa Tanganyika. Kunahitajika umeme ambao utawasaidia wananchi katika eneo hilo. Umeme ukifika eneo la Ziwa Tanganyika utawavuta wawekezaji. Kuna wawekezaji walipatikana kutoka nchi ya Norway, wanahitaji kuja kuwekeza katika Ziwa Tanganyika, kwa maana ya shughuli za uvuvi, lakini kikwazo kikubwa ni huduma ya umeme. Naiomba Serikali, ifanye jitihada za kuhakikisha inaandaa miundombinu ya umeme, uletwe katika maeneo hayo ili uweze kuwasaidia wananchi wa eneo hilo. Wananchi wa Ziwa Tanganyika ni wananchi masikini, lakini wana eneo na vyanzo vizuri vya mapato, wakitumia rasilimali ya Ziwa Tanganyika, ambalo lina samaki wengi, wakubwa, wazuri na dagaa wazuri ambao wana thamani kubwa na wanaopendwa katika nchi hii, dagaa wanaotoka Ziwa Tanganyika. Tukiwawezesha hawa wavuvi wadogo wadogo, wataweza kujikwamua katika shughuli zao za kuendeleza Taifa hili na kuongeza kipato chao.

Mheshimiwa Spika, sambamba na uboreshaji huu, tunahitaji barabara ya Mpanda kwenda Ziwa Tanganyika nayo iwe imekamilishwa vizuri kwa maana ya Mpanda – Ikora – Kalema. Barabara hii ikikamilika na tukapelekewa umeme katika maeneo haya, nina imani wananchi wa eneo hili watabadili maisha yao na watakuwa na uchumi mzuri sana. Lakini tuna barabara nyingine ambayo inahitajika ipewe huduma nzuri na ya kutosha ni barabara ya Mpanda – Mwese. Barabara hii ni muhimu sana, lakini nasikitika barabara hii hata kupishana magari mawili ni taabu.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iipanue barabara ya Mpanda – Mwese na isiishie pale Mwese tu, tunaomba barabara hii ishuke mpaka kule Ziwani, ikutane na barabara inayotoka Kigoma ili wananchi hawa wawe na mawasiliano mazuri yatakayoendesha shughuli zao. Kuna mazao muhimu kama kahawa na mazao ya migomba ambayo yapo pale ambayo yakipata miundombinu mizuri tutakuwa tumeimarisha na kuwasaidia Watanzania ambao uchumi wao ni mdogo sana katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto kubwa sana katika Mkoa wa Rukwa hasa vijijini. Vijiji vingi havina maji, wanaishi katika maisha ya kusuasua na kwa kudra ya Mwenyezi Mungu tu. Kuna baadhi ya vijiji toka uhuru hawajapata huduma ya maji yanayotokana na huduma ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, hasa Mawaziri wanaofanya shughuli chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wamsadie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu ni vigumu sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoa maombi, lakini wao wana nafasi sana. Pindi watakapofanya ziara katika maeneo ya eneo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, mengine mtakwenda kuyaona ninyi wenyewe, na mkiyaona mtakuwa na nafasi ya kumsaidia. Sio lazima aombe! Kuna maeneo ambayo yana matatizo makubwa sana katika Tarafa. Tarafa ya Mpimbwe, Inyonga, Mwese, Kabungu na maeneo mengine, yana matatizo ya maji. Tunaomba sana mpeleke huduma katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwaongezee mishahara walimu. Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, sambamba na majengo wanayoishi na wanayofanyia kazi. Zipo shule nyingine hazijapata hata huduma zile za MMEM, tukichukulia mfano wa shule ya Mwese, yaani ukifika maeneo yale utasikitika watoto wanasoma katika mazingira haya na mwalimu anafanya kazi hapa. Naiomba sana Serikali ichukue uzito wa aina yake kuhakikisha inawasaidia wananchi katika maeneo ambayo yalisahaulika kama ya Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali itusaidie sana kuimarisha huduma za afya katika Wilaya ya Mpanda. Wilaya ya Mpanda ina hospitali moja na ina Vituo vya Afya nane, jumla vipo tisa pamoja na cha binafsi. Lakini tuna zahanati zisizopungua 31. Zahanati hizi hazina waganga, hospitali ya Wilaya haina waganga na mbaya zaidi ni hata wale ambao Halmashauri ya Wilaya iliwaombea kuongezewa Mkataba wa muda hawajapewa nafasi ili waweze kutusaidia wananchi wa Wilaya ya Mpanda. Nawaomba sana, angalau katika hatua za mwanzo, muwape mikataba wale watumishi waliokuwa wamemaliza muda wao ili waweze kusaidia kutoa huduma katika maeneo ya Mpanda.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la kilimo. Kilimo kila siku kinahubiriwa hapa kwamba ni Kilimo Kwanza. Lakini bahati mbaya hakijapewa msukumo mzuri na Serikali. Naishukuru Serikali kwa namna moja au nyingine kwa kuelekeza nguvu hapo, lakini bado tuna changamoto. Kwanza, Serikali inapotoa ruzuku, pembejeo zile haziwafikii wakulima waliolengwa, badala yake zinaishia mikononi mwa watendaji. Karibu mbolea zote zinazotolewa na ruzuku ya Serikali asilimia 60 inakwenda nje ya nchi na karibu asilimia kubwa ya mbolea zinazotoka Mkoa wa Rukwa zinaishia katika nchi jirani ya Burundi. Wale wanaokutwa na matatizo, wakikamatwa, Serikali haiwachukulii hatua za dhati. Naomba mwadhibiti au tubadilishe mfumo.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iviangalie vyama vya ushirika, vipitie huko na ninaamini zitawafikia walengwa kuliko ilivyo sasa tunatunisha mifuko ya watendaji.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Naunga mkono hoja.