| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 4 | 14 June 2011 | Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2011/2012 – 2015/2016 | ||
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta Mpango huu katika muda muafaka. Mpango huu ni mzuri kama utakuwa na utekelezaji mzuri. Watanzania ni mabingwa wa kuandaa mipango isiyo na utekelezaji. Hivyo, tunaomba ipewe kipaumbele ili iweze kutekelezwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia katika sekta ya kilimo. Kilimo bado hakijapewa msukumo mkubwa. Ili tuendelee, tunahitaji kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ambao ndio wengi katika nchi hii, unapowawezesha wananchi walio wengi, umepandisha uchumi wa nchi. Wawezeshwe vipi? Wakopeshwe matrekta na Serikali, watafutiwe masoko ya uhakika na kuwa na mpango endelevu wa kujenga viwanda vya kusindika mazao. Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi haijafanyiwa kazi kwani tuna rasilimali kubwa ya maziwa ya Nyasa, Tanganyika, Rukwa, Victoria na Bahari ya Hindi lakini sehemu zote hizi hazijafanyiwa kazi. Endapo wavuvi wadogowadogo wakiwezeshwa na Serikali wakaanza kuvua uvuvi wa kisasa, wananchi wangekuza uchumi wao na kukuza uchumi wa Taifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukuza uchumi kama nishati ya umeme haijapatikana, maendeleo yoyote yale yanahitaji nishati ya umeme. Tunapozungumzia nishati hii ilenge na vijijini kwani nishati hii ikiishia mijini bado hatutakuwa tumewasaidia, walio wengi wanaishi vijijini hivyo nishati ikifika vijijini wakulima watasindika mazao yao na kuyaongezea thamani. Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwenda mbele bila miundombinu kwa kuboresha barabara zinazounganisha Mkoa hadi Mkoa, Wilaya hadi Wilaya, zijengwe kwa kiwango cha lami. Reli iboreshwe, huwezi kuwa na maendeleo bila reli, ni mhimili mkubwa wa uchumi katika nchi. Hivyo, tunaomba Mpango huu ujielekeze zaidi katika reli sambamba na ujenzi wa bandari katika maziwa na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Mpango huu uangalie uwiano wa mgawanyo wa rasilimali, tusipoangalia Mpango unaweza kuwanufaisha zaidi wale ambao wamepiga hatua. Ni vizuri ikaangaliwa Mikoa ambayo iko nyuma kimaendeleo ikapewa kipaumbele ili iweze kunyanyuka. Vinginevyo tunaweza tukaandaa Mpango usiwasaidie sana wale ambao Mikoa yao iko chini kimaendeleo. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini yote mazuri hayawezi kufaulu kama Watanzania hawatafanya kazi. Lazima tuandae utaratibu utakaombana Mtanzania yeyote mwenye uwezo wa kufanya kazi kufanya kazi. Nchi haiwezi kwenda mbele bila kufanya kazi, tuna wananchi walio wengi wanaoishi vijijini na mijini hawafanyi kazi. Naunga mkono hoja. |
|||||