You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Kakoso, Moshi Selemani[CCM]

Mpanda Vijijini Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
3 5 12 April 2011 Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Maeneo ya Maendeleo ya Kiuchumi wa Mwaka 2011 (The Economic Zones Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2011)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kupewa nafasi hii niweze nami kuchangia Muswada wa Sheria. Awali ya yote namshukuru Waziri mwenye dhamana ambaye ametoa Muswada huu na kuuwasilisha ndani ya Bunge lako Tukufu. Pili, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa maoni yake aliyotoa. Pia namshukuru Mwakilishi wa Kambi ya Upinzani ambaye ametoa mchango wake.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kwa ujumla katika maeneo ya Muswada huu ili kuweza kutoa tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda tuangalie maeneo ya wananchi wanaotoka katika maeneo husika yatakayokuwa yamewekezwa. Daima wawekezaji wamekuwa wakilinda maslahi yao binafsi kuliko wale wananchi wanaokutwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri sheria ikaweka malengo ya kuandaa mazingira ambayo yatajenga nia halisi ya kumsaidia mwananchi husika.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ni vyema tukaliangalia kwa kina, tunapoandaa mazingira ya uwekezaji, lazima tujenge mikakati ya kuwalipa fidia wananchi ambao wataguswa katika maeneo husika. Wananchi wengi wanapofika wawekezaji, Serikali imekuwa ikiwatoa na kuwafukuza katika maeneo husika na wala hawatafutiwi maeneo ambayo wataendeleza shughuli zao za kiuchumi. Jambo ambalo ni hatari kubwa sana kwa wananchi wetu. Ni vizuri eneo hili likaangaliwa kwa kina. Kuna maeneo mengi sana yamejitokeza na bahati nzuri Mwasilishaji na Mwenyekiti wa Kamati hii ameeleza katika maeneo ya Mkoa wa Ruvuma maeneo ambayo yamejitokeza kwa wananchi kiasi kwamba kunatokea kutokuwa na imani na Serikali.

Sambamba na hayo yaliyojitokeza katika maeneo ya Mkoa wa Rukwa sasa hivi kuna vurugu kubwa sana kati ya wawekezaji na wananchi. Ni vyema maeneo haya tukayaangalia kwa kina ili tuepuke migogoro isiyokuwa na ulazima.

Mheshimiwa Spika, tunapounga mkono Muswada huu, ni lazima napo tuangalie vyombo vya Serikali ili viweze kushughulikia haraka urasimu usiokuwa wa lazima kama vile TRA. TRA wamekuwa wasumbufu sana hasa kwa Sheria wanazozitumia kuwabana hawa wawekezaji. Kupewa tu kibali inachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, ule urasimu nao ni lazima tuangalie kuutoa ili kuwajengea mazingira mazuri ya uwekezaji waweze kuwa na fursa hasa hawa wanaokuja kuwekeza katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa zaidi ni kuwapa fursa wananchi ambao nao wana haki ya kuwekeza. Serikali inaweza kuelekeza mawazo kwa watu wa nje ili waweze kuwekeza. Lakini bahati mbaya hawa wananchi ambao wanahitaji kukuza uchumi wake wakapewa mgongo. Mimi nilikuwa naomba Serikali ijenge mazingira mazuri kwa wananchi ambao nao wanaweza wakawekeza. Leo hii uwekezaji mkubwa tunauonesha kwenye ardhi na ardhi ndiyo ambayo wanaitumia wananchi na kuitegemea wananchi wote.

Ni vyema Serikali ikajenga mazingira ya kuwapa nguvu hawa wananchi wa kawaida nao wakawa sehemu ya uwekezaji. Wapewe upendeleo maalum ili wawe na maeneo ambayo yatawasaidia wananchi wa Kawaida kukuza uchumi wao.

Mheshimiwa Spika, naomba niwasilishe na naunga mkono hoja.