| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 5 | 14 February 2011 | Kauli Kuhusu Utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini | ||
Mheshimiwa Spika, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuingia kwenye Bunge Tukufu. Pili, napenda kuwashukuru wananchi wa Korogwe Vijijini kwa kuwa na mimi na kwa kunichagua kwa kura nyingi sana. Tatu, nataka niwashukuru waganga wa tiba za jadi Tanzania nzima. Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniunga mkono. Pia nataka niwashukuru Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Tanga pamoja na Korogwe Vijijini kwa kuniona kwamba nafaa na leo hii nawakilisha wakulima wenzangu. Nitachangia katika sehemu tatu tofauti au nne hivi. Mheshimiwa Spika, sehemu ya kwanza, ni sehemu ya kilimo; kwa sababu Serikali imeamua kwamba kipaumbele ni kilimo kwanza. Katika Jimbo langu kuna Bonde la Mto Mkomazi, Bonde hili la Mto Mkomazi likitengenezwa bwawa la kuhifadhi maji, tunaweza kupata chakula cha mwaka mzima na ikalisha Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Mkoa wa Pwani. Ningeomba sana Serikali iangalie sana ili bwawa la Mto Mkomazi kwa sababu kuna wakati lilitakiwa lianzishwe, lakini kilichotokea sijui na mpaka sasa hivi ukame umekuwa mkubwa zaidi. Mheshimiwa Spika, suala la pili, katika Wilaya yangu nimezungukwa sana na mashamba ya mkonge. Haya mashamba yamewafanya wakulima wa Korogwe Vijijini kukosa kabisa sehemu za kulima. Ningeomba haya mashamba ya mkonge sasa hivi hayalimwi, yamekuwa ni msitu tu na ukizingatia kwamba eneo langu watu wengi ni wakulima, hawana sehemu za kulima. Naiomba Serikali ifute hati miliki ya mashamba haya na baadhi ya mashamba ni kama Shamba la Kwa Shemshi, Shamba la Magoma, Shamba la Hale, Shamba la Mbwazi, Shamba la Toronto, Shamba la Mswaha Darajani na mashamba mengine yamezuia eneo kubwa sana, wananchi wanapata shida sana na ukizingatia kwamba asilimia kubwa la wananchi wa Korogwe Vijijini wote ni wakulima. Mheshimiwa Spika, suala la tatu, ni suala la maji. Utashangaa sana katika Jimbo langu kuna Makao Makuu ya Tarafa mpaka leo hii hawana maji safi. Suala la maji limeathiri kwa kiwango kikubwa sana Jimbo langu ukizingatia katika Tarafa ya Bungu kuna Vijiji zaidi ya 20 havina maji hata tone. Naomba Serikali iangalie suala la Bungu, kuna matatizo ya maji, katika Kata ya Mashewa, kuna sehemu ya Bombo Majimoto, sehemu ya Kulasi, sehemu ya Lusanga, sehemu ya Makunga na sehemu ya Vingo hawa watu wanakunywa maji yanayopita mferejeni na huko mferejini watu wanaoga, watu wanafanya kila aina ya shughuli, matokeo yake kunakuwa na magonjwa kila wakati. Mheshimiwa Spika, vile vile nina suala la umeme. Katika Jimbo langu kuna Vijiji vingi havina umeme, lakini nguzo za umeme zimepita katika Vijiji hivyo, nashangaa wenzetu sehemu nyingine umeme unapatikana, lakini lah, katika Wilaya ya Korogwe Vijijini kuna Kata nyingi hazina umeme. Kata hizo ni Kata ya Kerenge, ukichukulia Kijiji cha Kerenge Kibaoni, Matalawanda, Alhamisi mpaka Makumba hakuna umeme. Katika Kata ya Dindila kuna Kata ya Dindila yenyewe, Mugwashi, Mhale, Mali, vijiji vyote havina umeme. Sasa nashangaa na nguzo zipo karibu kabisa, naomba Serikali iangalie suala hili hasa safari hii ukizingatia nimekuja mimi mkulima. Muwaangalie na muwape kipaumbele sana wakulima. Mheshimiwa Spika, suala la mawasiliano, napenda kukuhakishia katika Wilaya ambayo haina mawasiliano ya simu kabisa ni Wilaya ya Korogwe Vijijini, Makao Makuu ya tarafa mpaka leo hii watu mawasiliano hawayapati na ukichunguza ndiyo kwamba ndiyo sehemu kubwa ambapo kunatoka vyakula mbalimbali ambavyo vinapelekwa katika Mikoa mbalimbali, hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga na Kilimanjaro. Unashangaa kuona kwamba katika Tarafa ya Bungu, Makao Makuu ya Tarafa hakuna mawasiliano ya simu ya aina yoyote, lakini ukienda sehemu nyingine nyingi unakuta mawasiliano. Mheshimiwa Spika, ukienda katika Kata ya Mkalamo unakuta kule hakuna mawasiliano, wakati mifugo mingi inatoka kule na wafugaji wanaleta mifugo kwa ajili ya minada na watu leo hii Dar es Salaam wanakula nyama kutoka katika Kata hizo. Ukienda Kata ya Kizara ambako kunatoka wakulima wengi wa mpunga, mahindi pamoja na mazao mbalimbali na embe, lakini hawawi na mawasiliano ya simu na Mbunge aliyepita alishazungumza hili, lakini nashangaa halijafanyiwa utafiti wa aina yoyote na kupata ufumbuzi wake. Mheshimiwa Spika, ningeomba sana masuala kama haya wayashughulikie kwa sababu nawajali sana wakulima na safari hii nimekuja mkulima. Kwa hiyo, naomba Serikali inione vizuri sana. Mheshimiwa Spika, ukichukulia masuala ya miundombinu, katika Jimbo langu hakuna barabara ambayo inapitika wakati wote, sasa naiomba Serikali kwa sababu kule ndiyo kuna wataalamu wa kulima chai, iliki, kahawa, mahindi, mpunga na maharage. Hizi barabara zitengenezwe kwa mfano, barabara ya kutoka kwa Shemshi kwenda kwa ndugu yangu Januari haipitiki kabisa na ndiko yanakotoka maharage na majani ya chai kwa wingi. Naomba Serikali hizi sehemu iziangalie sana. Mheshimiwa Spika, nimefarijika sana na Bunge lako hili Tukufu, lakini nitashukuru sana kama watanisaidia kwenye masuala ya hospitali na zahanati na vituo vya afya, lakini vituo hivi vya afya havina huduma za kutosha, havina Madaktari na kama wapo ni wachache na watu wanapata shida mno na vituo hivi ni Kituo cha Mombo, Kituo cha Bungu na Kituo cha Magoma. Wako wagonjwa wengi wanaotoka katika hizi Tarafa, lakini kupata huduma inakuwa ni muda mdogo sana kufuatana na uchache wa Madaktari. Sasa naiomba Serikali, hivi vituo vya afya waviangalie kwa makini sana ili na mimi nisiwe Mbunge wa mwaka mmoja, watakaponipelekea huduma hizi itakuwa ni vizuri zaidi na mimi nitafanikiwa sana. Mheshimiwa Spika, nataka nimalizie kwa kuwashauri Wabunge wenzangu wanapochangia hoja zao wasituchanganye na sisi Waganga wa Jadi katika kila wanachoongea wasitufananishe na waganga, kwa sababu kila mtu na fani yake na kila mtu na imani yake. Kama imani yako haikuruhusu mambo ya uganga, lakini msituingize kila mahali mnatudonoadonoa, tunakerwa sana na hili. Kwa sababu kila mtu ana fani yake hapa ndani, sasa na mimi fani yangu ni miti shamba. Mnapokuwa mnatufananisha tunadharaulika kiasi fulani, naomba Waheshimiwa Wabunge na hili nanyi mlione. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache, ahsante sana. Napenda kuunga mkono hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Rais. |
|||||