| E-mail this to a friend | Printable version |
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To |
|---|---|---|---|
| 2 | 6 | 15 February 2011 | Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete |
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia kuwa Mbunge ili niwawakilishe wananchi wa Tanzania wa Jimbo la Mtoni, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Nawaahidi wananchi wa Jimbo hilo, sitawaendea kinyume katika kufikisha kilio chao na kuzima kiu yao ya kupata maendeleo. Aidha, nitatekeleza ahadi zangu pasipo kuvunja Kiapo cha Utii cha Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani nyingine maalum kwa mke wangu Nachum pamoja na wanangu, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na timu yangu ya Kampeni, kwa jinsi walivyovumilia taabu na shida, dhiki ya maisha na tashtiti za kisiasa hadi ushindi wa Jimbo la Mtoni katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali yetu ukaja kwangu mwaka 2010. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani nyingine za dhati kwa Chama changu cha The Civic United Front (CUF), Chama cha Wananchi tangu ngazi ya tawi la Kidatu “A”, Jimbo la Mtoni, Wilaya ya Magharibi hadi Baraza Kuu la Taifa, kwa kunipatia kura za maoni za kutosha na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea. Kwa namna ya pekee, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Mtoni kwa uamuzi wao thabiti wa kunichagua kwa kura nyingi sana bila ya kujali tofauti zao za kiitikadi na kisiasa. Nawaahidi kuwanao bega kwa bega ili kuondoa kero zilizopo katika Jimbo hususan maji, huduma ya afya na kadhalika. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana Mama Anne Makinda, kwa kuruhusu michango ya maandishi kwa wanaokosa nafasi za kuchangia kwa kusema hapa Bungeni. Ninakupongeza sana kwa kuipata bahati ukiwa mwanamke, ya kuliongoza Bunge letu katika nafasi uliyonayo. Ni jambo la historia ya heshima kwa Taifa letu, Mungu akujalie umri mrefu na maisha ya fanaka pamoja na hekima, busara na umakini katika kazi yetu hiyo. Mheshimiwa Spika, aidha, nampongeza sana Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuchaguliwa na Watanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia namshukuru mno, kwa hotuba yake fupi, yenye hoja za msingi katika kuiendesha nchi yetu kwa ufanisi, maendeleo na utangamano, wakati wa kikao cha Bunge letu, cha tarehe 18 Novemba, 2010 alichokiitisha yeye mwenyewe. Mheshimiwa Spika, napenda nichangie vipaumbele viwili tu katika hotuba ile. Kipaumbele cha kwanza na cha nane kati ya vipaumbele kumi na tatu alivyovieleza. Mheshimiwa Spika, kipaumbele namba moja, umoja, amani na usalama wa Muungano wetu. Tangu 26/4/1964, tunao Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar unaoitwa Tanzania. Mwalimu Julius K. Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, wakiwa Wakuu wa Nchi hizo mbili, walikubaliana kuunganisha baadhi ya vipengele vya kuendesha nchi na kutangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila ya kujali ukubwa au udogo wa Tanganyika au Zanzibar na bila kupiga kura ya maoni ya wananchi wa pande hizo mbili. Watanzania tuliwakubali na kuwaunga mkono viongozi wetu wawili hao, kwa nia ya kutaka umoja, amani na usalama wa Muungano kama Taifa moja. Leo kumezuka Wanasiasa na wasemaji wanaobeza Zanzibar na hata kudiriki kusema kuwa Majimbo 23 ya Zanzibar ni sawa na Jimbo moja tu la Tanzania Bara! Huu ni uchochezi na dharau ya hali ya juu inayoashiria ubaguzi, utengano, shari na mparaganyiko wa Taifa. Mheshimiwa Spika, nilidhani Bungeni tutaheshimu historia ya nchi yetu na kuchangia kuisaidia Serikali namna ya kukabili changamoto zinazokwaza juhudi za Serikali za kuleta maendeleo. Kumbe sivyo! Baadhi yetu tunapitikiwa! Hali ni hivyo kwamba wapo watu bado wanatoa kauli za kukatisha tamaa dhidi ya Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar hata ndani ya Bunge lako Tukufu. Kwa taarifa yao, hivi sasa Zanzibar ni tulivu na ina amani ya kutosha na hali hiyo ndio ishara bora kwa umoja, amani, usalama wa Muungano wetu. Naiomba Serikali kupitia Bunge hili, kudhibiti maadili ya Muungano wa Tanzania na kuwadhibiti wale wote wanaotaka kuyamomonyoa kwa nguvu yote ya Kikanuni, Sheria na Katiba yetu. Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 21-29, Mheshimiwa Rais ametoa ufafanuzi kwa ufupi juu ya azma aliyokuwanayo kuhusu elimu kabla ya kutangaza Baraza la Mawaziri. Kama utekelezaji wa sera zilizopo na maelezo yale vitakwenda sambamba na hali halisi ya utendaji kazi wa watendaji wa Serikali, tutajenga Tanzania mpya mapema sana. Naziunga mkono jitihada za Serikali katika fani ya elimu ila napenda kutoa maoni yangu yafuatayo:- (1) Mshahara wa Walimu uendelee kukua ili watu wapende kuwa Walimu; (2) Vifaa vya kufanyia kazi mfano vitabu, vifaa vya maabara na maabara zenyewe ziendelezwe; (3) Mitihani ya Kidato cha Pili irejeshwe kama kule Zanzibar; na (4) HESLB ipate marekebisho yanayostahiki baada ya mapendekezo ya hiyo Tume ya watu 11 bila ya kujali undugu na urafiki. Mheshimiwa Spika, nimetembelea UDOM na kuona tatizo kubwa sana la ukosefu wa maji. Wanafunzi wanasema maji hupatikana kikawaida siku za ziara za Wakuu wa Nchi au Mawaziri. Aidha, kuna tatizo la makaro na mabomba ya maji machafu. Ni hatari kwa afya ya jamii ya Chuoni UDOM. Mzabuni wa chakula hapo chuoni anapika chakula kisichoridhisha. Wanafunzi wanadai, mzabuni wa mwanzo alikuwa akipika vyakula vizuri lakini amekoseshwa nafasi hiyo na kupewa huyo wa sasa. Wanafunzi wanatilia mashaka kama rushwa haikutumika katika kumpata mzabuni wa pili. Juhudi za Serikali zifanyike ili wanafunzi wa Vyuoni waweze kupata mazingira yanayowashawishi kusoma na kujifunza. Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. |
|||