| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 38 | 2 August 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka 2011/2012 | ||
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutufikisha katika Bunge lako Tukufu tukiwa hali ya uzima wa afya. Pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwa kazi kubwa anayoifanya katika kujenga nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia hotuba hii nikijikita kwenye ujenzi wa barabara katika kuunganisha Mikoa yetu ya Tanzania. Mheshimiwa Spika, Wakandarasi ambao wanapewa tenda za barabara zetu, wanahitaji kuangaliwa vizuri kwani Wakandarasi hao ndio wanaosababisha ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara, kiasi kwamba baadhi ya Mikoa wamekata tamaa kuwa barabara zao zitajengwa. Wakandarasi hao wanapochukua tenda ili kujenga barabara hizo baada ya kufanikiwa, baadhi yao huenda hadi site ambayo wamepangwa na kuanza kusafisha barabara hiyo, kiasi kwamba wakazi wa eneo hilo kuhisi kuwa barabara imo kwenye matengenezo. Baada ya kitendo hicho, Wakandarasi hao ambao sio waaminifu wanaishia hivy hivyo bila kumalizia barabara hiyo. Mheshimiwa Spika, ukifanya upembuzi wa hali hiyo unaweza kukuta Wakandarasi hao hawajalipwa fedha zao, sijui ni Hazina ndio wanaochelewesha fedha hizo. Naomba Waziri achukue hatua kali dhidi ya wafanyakazi wazembe kwani hawa ndio wanaozorotesha maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania. Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri awe makini sana katika malipo ya wanaobomolewa nyumba zao kwa ajili ya kupitisha barabara. Kumekuwa na malalamiko juu ya malipo hali inayopelekea kuwa raia wanakosa imani na Serikali yao hali ya kuwa bila ya raia wema hakuna Serikali. Namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuwa makini katika eneo hili; ni kero kubwa kwa wananchi wa kila eneo ambalo linapita barabara. Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. |
|||||