| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 31 | 22 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa | ||
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani aliyoionyesha kwangu kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara hii. Pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Ghalib Bilal kwa ushindi wao na ushindi wa CCM katika uchaguzi Mkuu wa 2010. Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshukuru kipekee Mheshimiwa Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa msaada wake mkubwa na wa dhati kwangu kwa kuniongoza vema na kunielekeza ili kufanya kazi zangu kwa ufanisi. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa uongozi wake mahiri ndani ya Bunge hili. Aidha, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Spika na Naibu Spika, kwa kuchaguliwa kwao katika nafasi hizo na kwa namna wanavyoliongoza Bunge hili. Pia napenda kuwapongeza Mheshimiwa Jenista J. Mhagama, wewe mwenyewe Mheshimiwa George B. Simbachawene na Mheshimiwa Sylvester Massele Mabumba kwa kuchaguliwa kuwa Wenyeviti na kwa namna mnavyoonyesha uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge katika kipindi hiki kifupi. Pia nawashukuru sana Wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa. Nawaombea kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao hapa Bungeni na kwenye Majimbo yao. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa namna ya pekee, kuwashukuru wananchi wenzangu na wapigakura wangu wa Jimbo la Muyuni. Nawashukuru kwa imani kubwa waliyoionyesha kwangu kwa kunichagua kuwa Mbunge wao. Nitaendelea kuwa nao karibu na kushirikiana nao kuliletea Jimbo letu maendeleo. Kwa pamoja tutapiga hatua kubwa ya maendeleo katika Jimbo letu la Muyuni. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kuishukuru sana familia yangu kwa uvumilivu wao kwangu na kwa namna inavyonisaidia na kuniunga mkono katika majukumu yangu. Aidha, shukrani za dhati ziende kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Mabalozi, Viongozi na wafanyakazi wakiwemo wasaidizi wangu katika Wizara ya Mambo ya Nje, kwa ushirikiano, ushauri na msaada wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, sasa nianze kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, wote waliochangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Ni dhahiri kwamba michango yao itatusaidia sana katika kufanikisha shughuli za Wizara na kuimarisha ufanisi. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ufinyu wa bajeti. Kuna michango mingi iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ya aidha kugusia moja kwa moja suala la ufinyu wa bajeti katika Wizara hii au kutoa michango mingine ambayo jibu lake ni tatizo la ufinyu wa bajeti katika Wizara. Naomba nikubali, kwa mfano hoja ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Dkt. Augustino Mrema na Mheshimiwa Sanya ambazo moja kwa moja waligusia tatizo la ufinyu wa bajeti. Ni kweli Wizara yetu kutokana na majukumu yake fedha inazozipata hazitoshi kutekeleza majukumu hayo. Kuna matatizo mengine ambayo yameelezwa na Waheshimiwa Wabunge, yanathibitisha tatizo hilo la fedha katika utekelezaji wa majukumu yetu. Hata hivyo, napenda kuwashukuru Wizara ya Fedha kwa sababu kuna mambo ambayo licha ya tatizo hilo la ufinyu wa bajeti lakini mara zote matatizo ya Balozi zetu yamekuwa yakishughulikiwa hata mara nyingine kunakuwa na uchelewaji kidogo kwa mfano suala la mishahara tofauti na ilivyoelezwa hapa na baadhi ya wachangiaji, pango la nyumba, ofisi katika zile sehemu ambazo Wizara haina nyumba zake za ofisi na pia huduma muhimu za maji au umeme. Fedha hizi zimekuwa zikitolewa kila baada ya miezi mitatu na mara moja inaweza kuchelewa lakini hazikosekani. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa zile shughuli nyingine muhimu nazo wakati mwingine ni kweli kumekuwa kuna tatizo kubwa la fedha na hili linaonekana hata katika kiwango ambacho tumekipata licha ya kwamba bajeti yetu ilikuwa kwa mwaka uliopita ni bilioni 112 ambazo hazitoshi lakini katika upatikanaji pia tulipata bilioni 94 ambazo ni sawa na asilimia 83. Hiyo bila shaka inaathiri utendaji wetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihusishe suala hili la ufinyu wa bajeti pia na michango mingi iliyotolewa kwa mfano, ya kufungua Balozi ndogo katika sehemu mbalimbali au ya kufungua Balozi katika nchi mbalimbali. Wizara inapenda na bado inashughulikia kuhakikisha kwamba tunakuwa na Balozi au Balozi ndogo katika sehemu ambazo ni muhimu katika kuimarisha mahusiano na nchi hizo na pia kwa maslahi yetu ya kiuchumi. Lakini tumekuwa tukikwama katika kutekeleza azma hiyo kutokana na saa nyingine tatizo la kuwa na bajeti ndogo. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo limechangiwa na wajumbe wengi kidogo na ambalo napenda kuligusia ni suala la mahusiano yetu na Israel pamoja na Palestina. Ni kweli Tanzania tulivunja uhusiano wa Kibalozi na Israel mwaka 1967 kufuatia vita vya siku sita baina ya Israel na Misri na Rais wa Misri wa wakati huo Anwar El-Sadat kuziomba nchi za Kiafrika kumuunga mkono kwa kuvunja mahusiano na Israel. Kwa hiyo, nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania tulivunja mahusiano. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jitihada za Misri na Israel wenyewe kuleta amani ambazo zilizaa makubaliano ya Camp David au Camp David Accords baina ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel Begin pamoja na Anwar El–Sadat na kwa hiyo, wenyewe Israel na Misri kurejesha uhusiano na sisi pia zikiwemo nchi nyingi pia za Kiafrika tulirejesha tena na Israel na kwa hiyo, tuna uhusiano wa Kibalozi baina ya Tanzania na Israel. Ubalozi wetu ambao uko Misri ndio ambao unatuwakilisha nchini Israel na Ubalozi wa Israel ulioko Nairobi ndio unawakilisha Israel nchini Tanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale ambao walikuwa wakisema tufungue ubalozi nchini Israel, ni kwamba, tayari Ubalozi upo hata kama haupo ndani ya Israel lakini upo Misri na unafanya kazi hizo. Lakini uhusiano wetu na Palestine tangu miaka ya 1960 umeendelea kuwa imara na unaendelea vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nigusie suala la Diaspora ambalo limeguswa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamesisitiza umuhimu wa Watanzania ambao wanaishi nje katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kadhalika. Wapo ambao pia wamegusia kwamba hatua za kuhakikisha kuwa Watanzania hawa wanachangia vizuri katika maendeleo ya nchi yetu imekuwa ni taratibu mno hasa likiwemo suala la uraia wa nchi mbili. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoelezwa katika Bajeti ya Mheshimiwa Waziri, tayari hatua zimechukuliwa na kuna kitengo cha Diaspora ambacho kinaratibu masuala ya Watanzania hawa ambao wanaishi nje ya Tanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uraia wa nchi mbili tusilione kama limechelewa kwa kiasi kikubwa hatua zilizochukuliwa na Wizara zimeweza kuamsha mwamko kwa suala hili kwa Watanzania walio wengi. Miaka michache iliyopita tusingepata Wabunge wengi ambao wangeliunga mkono na kulishabikia kama ambavyo wamefanya safari hii. Kwa hiyo, hatua hizo zimewezesha sasa kuweza kujipanga vizuri na suala hili kuweza kukubalika kwa Watanzania walio wengi na kwa Waheshimiwa Wabunge kama mlivyoonyesha. Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nigusie suala ambalo limegusiwa katika suala la diasporas ambalo linahusu Watanzania wanaume wanapooa wao wana uwezo wa kutoa uraia kwa wake zao pamoja na watoto. Lakini wanawake wa Kitanzania wanapoolewa na wageni wao hawana fursa hiyo. Hii ni kweli kwamba sheria hii inaonyesha kupitwa kidogo na wakati na kwa wale wanafuatilia masuala ya haki za binadamu na hasa haki za jinsia watatambua kesi ambayo ni maarufu ya Unit DAU dhidi ya Attorney General ya Botswana ambayo tangu miaka 1990 Mahakama ilitoa uamuzi kwamba Sheria kama hiyo haiwezi kusimama na kwamba ni lazima ili kuleta usawa wa kijinsia haki hiyo ipatikane kwa wote. Kwa hiyo, tunaamini katika kushughulikia suala la Diaspora pia tutaweza kulishughulikia suala hilo kwa pamoja ili kweli tuweze kuwa na usawa wa jinsia kama ilivyo katika Katiba yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. |
|||||