You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Khamis, Kheir Ali[CCM]

Kwamtipura Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 4 11 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwa kuanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na uzima na kuweza kusimama hapa leo katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nakishukuru Chama changu, Chama cha Wananchi CUF, kwa kuniteua na hatima yake wananchi wa Jimbo la Mkoani wakanipa kura. Tatu, napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mkoani kunipa kura zilizotosheleza na leo naendelea kuwa Mbunge kwa mara ya pili.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Rais katika ufunguzi wa Bunge hili la Kumi alikuwa na vipaumbele kumi na tatu, kati ya hivyo, cha kwanza ni umoja na amani. Kama inavyoeleweka kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, kwa hivyo, kunapoonekana ishara ya kutokuwa na amani Zanzibar basi hali kadhalika inaathiri Tanzania Bara au Tanzania kwa ujumla. Uwepo wa Serikali ya Kitaifa Zanzibar, umeondoa wasiwasi wa kutokuwa na amani katika Zanzibar na umeleta umoja.

Mheshimiwa Spika, sasa yote haya anayebugudhi habari hizi za kweli hatumfahamu, kwa kweli tuseme nia yake ni kwamba, Wazanzibar waendelee kupigana na kufanyiana mambo ambayo si ya kistaarabu. Niseme kuwa viongozi wawili waliochukua hatua hizi za kuleta maridhiano inawezekana walichukua historia za chaguzi nne ambazo zimefanyika Zanzibar katika mfumo wa Vyama Vingi, chaguzi ambazo zilianza mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa yako uchaguzi wa mwaka 1995 kwa matokeo ambayo yametajwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, CCM ilishinda kwa asilimia 50.2 na CUF ilipata asilimia 49.8. Huu ni uchaguzi wa mwanzo wa Vyama vingi Zanzibar, karibu asilimia 50 kwa 50. Lakini vile vile uchaguzi huu wa 2010 ukiachana na zile chaguzi mbili za 2000/2005 lakini huu wa 2010 kwa sababu ya muda haupo, CCM kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi ilishinda kwa asilimia 50.1, CUF ikawa mshindi wa pili kwa asilimia 49.1.

Mheshimiwa Spika, sasa matokeo kama haya busara gani zitumike katika kuwaokoa wananchi wa visiwa hivi. Kwa hiyo, nadhani kilichofanyika ni sahihi, kwa hiyo, ipo haja ya Watanzania wote kwa ujumla wetu kukiunga mkono kwa kweli kilichotokea Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi namshukuru sana Rais Mstaafu Mheshimiwa Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, na pia namshukuru Rais Dokta Ali Mohamed Shein kwa kusimamia na kutekeleza maamuzi ya Wazanzibar kwa kupitia kura za maoni ambayo walisema wanataka Serikali ya Kitaifa kwa asilimia 66.4. Nampongeza Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na nampongeza Balozi Mheshimiwa Seif Ali Idd kwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais.

Mheshimiwa Spika, kumezuka maneno hapa, ya Wabunge na Majimbo yao. Nahesabu unapowahusisha Wabunge na ukubwa wa Jimbo na udogo wa Jimbo, nahesabu huo ni ubaguzi, kubaguliwa anayebaguliwa sawa lakini tatizo moja la ubaguzi haliishii hapo, utawabagua wale ambao unawaona watu ambao hampo pamoja, ukimaliza hapo utakuja kuwabagua wale ambao mpo pamoja, tahadhari ni hiyo tu. Kwa hivyo, nashauri hii si habari nzuri na kwa kweli ipo haja iachwe.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha saba ambacho Mheshimiwa Rais alikieleza ni suala zima la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Mitaa na kuweka nidhamu ya matumizi. Ni sahihi kusema hivyo na vizuri kutekeleza lakini naomba niiambie Serikali kuwa njia moja ambayo nahisi inavujisha mapato ni misamaha ya kodi.

Mheshimiwa Spika, tukumbuke Tanzania ni nchi maskini, ina matatizo mengi, bajeti bado tegemezi, kwa hivyo, nakubali vilevile kuna taasisi na mashirika yanahitaji kusamehewa kodi, lakini kwa kweli kusamehe kodi kwa kupitiliza kwa kweli ni kuwabebesha mzigo wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa taarifa ambayo ameitoa iliyoishia Juni, 2006, Serikali ilisamehe shilingi bilioni 15,970,713,769/= kwa mwaka 2006. Kuna utatanishi mkubwa, Hazina wanasema yao na TRA wanasema yao, siendi huko wakati hauniruhusu. Lakini ripoti hii ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya 2009 inayoishia Juni, fedha ambazo Serikali imesamehe, ni 752,398,800,000/=.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia pesa hizi leo nchi imetikisika kutokana na DOWANS, 94,000,000,000/=, lakini ukichukua hesabu ya bilioni 752 hizi ni DOWANS nane, Serikali imeweza kusamehe pesa hizo, kwa sababu DOWANS imetangazwa kwa hiyo hata Serikali inasema itafute mbinu ya kuweza kuona uwezekano wa kutolipwa lakini hizi ni DOWANS nane. Sasa hali hii kwa kweli ni ngumu. Kwa hiyo, nahisi katika njia moja katika kuboresha mapato ni suala zima la misamaha ya kodi, ipunguzwe sana.

Mheshimiwa Spika, kuna masuala ambayo mashirika ambayo tulitegemea sisi yachangie uchumi wa Serikali kinyume, Wizara ya Afya ambayo yahitaji ipewe ruzuku na Serikali hata Shirika la Reli nalo hivyo hivyo wakati Shirika la Reli ni Shirika la kiuchumi litoe mchango kwa Serikali, Shirika la Ndege ATCL sijui hilo liko wapi, umeme ndiyo hali kadhalika…

Mheshimiwa Spika, ahsante.