You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Omar, Rashid Ali[CUF]

Kojani Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
3 1 5 April 2011 Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa UNESCO wa Kulindwa kwa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika wa 2003
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kuweza kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja hii juu ya Mkataba kuhusu masuala ya Utamaduni wetu.

Kwa kweli hii ni fursa adhimu kabisa niliyoipata ikiwa hii ni mara yangu ya kwanza katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo kuweza kusimama hapa mbele yenu na mimi kutoa mchango wangu. Hii si kwa sababu ya uzembe au kwa sababu ya kutoelewa lakini ni kuwa mara nyingi tunavyotakiwa sisi wanadamu tujifunze kutokana na wenzetu waliotutangulia.

Pili, natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri aliyewasilisha hoja hii. Kwa kweli hii ni hoja adhimu kabisa kwa sababu Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na ng’ombe aliyeachiwa na kuweza kuharibu kila kilichobakia katika maeneo.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kulielewesha Bunge lako Tukufu kwa kuiunga mkono hoja hii kabla kwa asilimia mia moja kwa sababu moja kubwa ya msingi ni kuwa sisi Watanzania yaani Watanzania wa huku Tanganyika pamoja na Zanzibar nahisi utamaduni wetu kwa kiasi kikubwa umepotea. Kwa fursa hiyo tuliyoipata adhimu ya kupitishwa hoja hii leo katika Bunge hili Tukufu nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu hoja hii tushikamane na tuifikirie vizuri sana kwa sababu kukosekana kwa utamaduni ni sawa sawa. Narudia tena ni sawa na ng’ombe aliyeachiliwa na kuharibu kila kitu kilichopo katika maeneo.

Tatu, kwa mfano naona kwa kiasi kikubwa siku hadi siku zinavyozidi kuendelea Watanzania tunapoteza hadhi yetu kutokana kuhadaliwa na watu binafsi wanaotumia fedha zao kwa kupotosha utamaduni wetu. Maadili ya watoto wetu wa Tanzania kila leo mpaka kesho, kila tukienda mbele yanazidi kuporomoka. Nachukua nafasi hii kutoa mfano mdogo kama huu ufuatao;

Kwanza, kuna hiki kitu kinachotangazwa kinaitwa Miss Tanzania, jamani hili si kosa kuitumia nafasi hii kwa kujipatia maendeleo sisi Watanzania lakini watu wenye fedha zao wanachukua nafasi hii kuturudisha nyuma kabisa katika tamaduni ambazo zilikuwa ni asili zilizokuwa zinachunga malezi ya watoto wetu na sisi wenyewe kwa ujumla. Kwa kweli ni kitendo cha aibu na fedheha kuwachukua watu kwa kutumia fedha zao wakawa wanawatembeza utupu na aliyetakiwa atembee utupu nadhani katika maumbile yetu kwa Mwenyezi Mungu ni wanyama tu hata wao wamepewa sehemu zao za kuwahifadhi ili wasionekane tupu zao.

Mheshimiwa Spika, leo Watanzania tumefikia pahala kwa sababu ya umaskini wetu tunawakaribisha matajiri au watu wenye fedha zao na kuweza kutukashifu kiasi ambacho watu wanatembea hovyo katika maeneo yasiyo halali.

Jamani Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nakuombeni suala hili tuliangalieni vizuri, tukichukua nafasi ya sisi tunatafuta maendeleo kwa kupatiwa fedha na watu wenye fedha zao, tutafikia mahali hata watoto wetu watatukataa na hii imeshatokea. Watoto wanathubutu hata kutusonya ndani ya daladala, hiki kitendo kama hiki utoto wetu sisi wenye umri wa miaka 50 sasa hivi tunaona ni kitu cha ajabu sana, halafu lingine tukiangalia hata hivi vyombo vyetu vya habari tumeviachia nafasi kubwa sana ya kupotosha utamaduni wetu, utawakuta watu wanacheza utupu jambo ambalo watoto wetu wadogo nao wanarithi kwa kuviangalia vyombo vile.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nisizungumze sana, naona nichangie hapa padogo tu kwa sababu uzoefu wangu bado ni mdogo kabisa na ni mara yangu ya kwanza, lakini nawaomba hoja hii tuiunge mkono mia juu ya mia kwa sababu tunaelekea pahali pabaya sana sisi Watanzania kwa watu wanaotumia fedha zao kwa kuanza kutuchuuza hovyo hovyo.

Mheshimiwa Spika, kule Zanzibar sasa hivi tumefikia pahala watoto jambo ambalo kwa utamaduni wetu wa Wazanzibari ilikuwa ni kitendo haramu kabisa kumuona mtu anatembea utupu, leo watu wanakuja kwa sababu tu tunahitaji tupate fedha kupitia watalii. Sasa mimi naishauri Serikali, hao watalii au hata watu wengine wanaokuja hapa ni njia moja ambayo tunazalisha au tunapata maendeleo kutokana na watu wanaokuja, lakini Serikali iangalie kuhusiana na suala zima la utamaduni wetu.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nikae na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi leo angalau nikaanza kujifunza katika Bunge lako hili Tukufu, asante sana.