You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Abdallah, Rashid Ali[CUF]

Tumbe Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 3 10 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini la pili sina budi kuwashukuru Wananchi wa Jimbo langu na ninawatakia kila la kheri.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake. Ni hotuba nzuri na inafahamika, hotuba hii siyo ya Wabunge tu, ni hotuba ya Watanzania wote, kila mmoja ana haki ya kuijadili na kutoa mapendekezo yake.

Mheshimiwa Spika, mimi ni vyema niende katika kipaumbele cha kwanza kinachozungumzia amani, utulivu na Muungano wetu. Mheshimiwa Habib Mnyaa ameeleza zaidi kuhusiana na dhana nzima ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nasema kwamba, katika Bunge la Tisa, Mheshimiwa Rais aliona hali hii tete ya kisiasa Zanzibar na akaahidi kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana na viongozi wa siasa kule Zanzibar na bahati alifanikiwa sasa Zanzibar iko tulivu, wananchi wanaelewana, wanafanya kazi pamoja bila bughudha yoyote, wanachangia Taifa lao na maendeleo yao.

Mheshimiwa Spika, nimeshangazwa sana kwa baadhi ya Waheshimiwa kuubeza umoja wetu. Nashangaa kwa sababu ni sawasawa na mtu anakwenda Dar es Salaam, akaambiwa aingie kwenye gari, yeye akasema atakwenda kwa mguu, kwa hiyo nitamshangaa sana. Niseme kwamba, Serikali ya Zanzibar chini ya Ibara ya 102 ina mamlaka yake. Zanzibar wenyewe ni Wazanzibari wana haki ya kuamua ni aina gani ya Serikali wanayoitaka.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibar wenyewe, wana haki ya kuamua kubadili vifungu vya Katiba au kuiandika upya. Wazanzibari wameamua kwa 64.2% kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Hakuna hata mmoja awe wa ndani au wa nje ambaye anaweza kubadili maamuzi ya Wazanzibar. Tutaendelea kuheshimu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa gharama yoyote ile.

Mheshimiwa Spika, kwa hali hii sina budi kwa heshima kubwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, kwa juhudi kubwa alizozifanya ili kufika hapa alipofikia sasa. Pia sina budi kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Aman Abeid Aman Karume, lakini pia sina budi kumpongeza kwa dhati kabisa Katibu wangu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamadi. Wote nawatakia umri mrefu na maisha bora.

Mheshimiwa Spika, baada ya haya, sasa niende katika ukurasa wa ishirini na nne kuhusu ukuzaji wa ajira Tanzania. Naelewa kwamba ziko Wizara zinatoa ajira, yako makampuni binafsi yanatoa ajira, viko viwanda vinatoa ajira na ziko sekta binafsi zinatoa ajira, lakini ni ukwerli usiopingika kwamba ajira ni chache Tanzania. Ajira ndiyo inayoleta heshima ya mwanadamu na kama huna ajira basi huna heshima, utakuwa ni omba omba tu. Hata kule nyumbani kutakuwa hakuna amani.

Mheshimiwa Spika, bado ajira ni chache, yako makundi ya vijana ambao wanamaliza sekondari kila mwaka, yako makundi ya vyuo vikuu hawa ni watalaam, hawa wanamaliza vyuo kila mwaka na wako wale ambao wanashindwa kuendelea na masomo yao, nao wanamaliza kila mwaka. Kwa hiyo, wengine wanaamua kuihama nchi yao kwa sababu ya ajira. Tunawasomesha kwa gharama kubwa ya Serikali lakini hatimaye wanakwenda kutumikia Mataifa mengine, ni kwa sababu hakuna ajira. Wengine wanaamua kufanya biashara ya madawa ya kulevya ambayo ni hatari kabisa, lakini wengine wanaamua kujiunga na uhalifu. Hii ni kwa sababu ya ukosefu wa ajira.

Mheshimiwa Spika, lakini kama si hivyo wengine wanaamua kufanya biashara ya ukahaba. Ukienda Dar es Salaam kuna watoto wanaomba omba njiani, ni watu wamekwenda kufanya biashara zao na wana Wazee wao wale wanawatuma kwenda kuomba. Hili Taifa tunalipeleka wapi? Litakuwa ni Taifa hatari kabisa, tutaliangamiza hivyo, ni lazima Wizara inayohusika ihakikishe kwamba suala hili tunalivalia njuga na kuongeza ajira ziwe nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, nashangaa kwamba wanafunzi wetu wa vyuo vikuu kila siku wanaandamana. Wanafunzi ambao tunategemea waje kuwa Wabunge, kuendeleza Taifa hili, lakini kila siku kuna maandamano. Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya kuchunguza migomo. Naomba litakapopatikana jibu sahihi basi huu mgomo uweze kukomeshwa kabisa. Kwani watu hawalipwi? Wanalipwa shilingi 5,000/=, hii ni pesa kidogo sana. Hebu tumlipe Mbunge hapa shilingi 5,000/= ataishije hapa? Hawa wanasoma, wananunua vitabu, wanafanya shughuli mbalimbali, leo unawalipa shilingi 5,000/=? Kwa hiyo, tunaomba Wizara husika iliangalie kwa makini suala hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, naunga mkono hoja.