You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Silinde, David Ernest[CHADEMA]

Mbozi Magharibi Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 4 11 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Lakini jambo la kwanza kabla sijaanza kuchangia hotuba ya Rais, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mbozi Magharibi, kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mwakilishi wao. Nawaahidi kabisa kwamba katika miaka mitano nitakuwa Kiongozi bora na wa mfano katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, napenda kumshukuru Mwenyezi Bunge kwa kuninyanyua mpaka leo hii kuwa katika nafasi niliyopo, familia yangu ndugu, jamaa na marafiki, wote nawashukuru kwa upendo mmoja.

Mheshimiwa Spika, ningependa nianze na nasaha kidogo kabla sijakwenda kutoa hoja. Nalionea huruma sana Taifa langu. Nalionea huruma Taifa kwa sababu Watanzania wanateseka kwa kiwango kikubwa na tunashindwa kusema ukweli kwa sababu ya maslahi ya itikadi za vyama. Tunakopita, tunapokwenda kila mahali tunaona ni kwa kiwango gani Watanzania wanateseka. Mfano mdogo, ni kila siku asubuhi tunapita, tunakuta katika mageti ya Bunge, watu wanaomba wakiwa na magonjwa mbalimbali. Lakini mtu anafika Bungeni anadiriki kusema hadharani kabisa kwamba nchi inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, hata kama upo ndani ya itikadi ya Chama chako tuongee ukweli katika hali halisi jamani. Taifa lilipofikia kuna mahali tumeshindwa, twende kwa mfumo fulani, kuna mahali tutakwenda vizuri tutakapoweza kukamilisha kwa pamoja, hili ndilo Taifa ambalo tunahitaji. Taifa haliwezi kuwa na amani kama Watanzania wanateseka. Taifa haliwezi kuwa na usalama kama Watanzania wanaendelea kuwa maskini na wanaendelea kulala njaa. Hatuwezi kufika kwa mfumo huu.

Napenda kusema kitu kimoja tunahitaji sana na hili ni lazima nitoe nasaha kwamba Kiongozi bora ni yule anayeliombea Jimbo lake na kuliombea Taifa lake kila anapoamka. Lakini sidhani kama hapa kuna viongozi wanaweza kutekeleza hili. Kiongozi bora ni yule anayeweza kujinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu ili yeye aweze kumnyanyua, sio unakaa unajinyanyua kwa kujisifu huwezi kufika mahali popote. Watanzania hawahitaji viongozi wa mfumo huu. Kiongozi bora ni yule anayezihisi sababu zilizomfanya afike mahali alipo, ndio kiongozi bora tunayemhitaji.

Mheshimiwa Spika, baada ya nasaha fupi, napenda niende kwenye kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Hotuba ya Mheshimiwa Rais ina vipaumbele 13 lakini ukiangalia kwa undani zaidi katika vipengele 13 utakuta vingine si vipaumbele, mengine ni mahitaji ya msingi, mengine ni utekelezaji, mengine ni mambo ya kawaida kabisa.

Suala la Utawala Bora, suala la Demokrasia, Suala la Usalama na Amani, Serikali yoyote hata wangeingia CHADEMA wangelinda usalama na amani wa nchi hii, utawala bora wangeshikilia, wangepigana kuhusu rushwa. Tunapozungumzia suala la vipaumbele tunatakiwa tuwe na mambo ya msingi matatu au manne yanajitosheleza.

Tungesema leo ilani ama hotuba ya Rais inahusisha mambo labda matatu, kwamba labda barabara, maji pamoja na kitu kingine, tunazungumzia miundombinu kwa maana ya barabara. Tunasema hivi vitu ndivyo ambavyo tunasema ndani ya miaka mitano lazima tuvisimamie na Taifa litambue ndivyo tunavyovihitaji. Lakini hatuwezi kusema amani sijui nini na nini ni vitu ambavyo kila mmoja anaweza kuvitekeleza.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa nigusie baadhi ya mambo. Katika Hotuba ya Rais, tuzungumze katika uhalisia ili tuweze kufika, tusibishane bila hoja. Kwa hiyo, ndugu zangu napenda niende katika kipengele kimoja kuhusiana na maji kwenye kukuza uchumi, maana yake ni huduma za jamii. Tunapozungumzia maji tunazungumzia uhai wa Mtanzania ndio maana ya maji. Bila maji ndio tunakosa nishati za umeme zinazoyumba, bila maji ndio akinamama unakwenda vijijini ndoa nyingine zinavunjika, akinamama wanakwenda umbali muda mrefu wanachelewa kurudi, waume zao wanawapiga, wanawafikiria vibaya, ndoa zinavunjika. Bila maji ndio haya matatizo yanatokea, watu wanazeeka kabla ya umri wao wanakaa wanateseka ni vitu viko wazi.

Mheshimiwa Spika, huwa najiuliza Serikali kwa takriban miaka 50, hatuzungumzii miaka mitano sasa, kwa sababu Chama ni Kimoja na Serikali ni ya watu wale wale. Kwa hiyo, unaangalia miaka 50 bado tumeshindwa kupeleka maji kwa asilimia angalau 50 ya Watanzania wote, kila siku tunazungumzia hayo malalamiko. Nalizungumzia hili kwa sababu nalijua na nalifahamu. Unakwenda Bonite anazalisha maji Kilimanjaro anasambaza nchi nzima mtu mmoja, Dasani anasambaza maji nchi nzima mtu mmoja, sijui uhai, Bakhresa anasambaza maji nchi nzima mtu mmoja, lakini unakuta Serikali inashindwa, unajiuliza maswali mara mbili hupati jawabu. Ni suala la kwenda na kuliangalia kwa makini.

Suala la pili ni suala la kilimo kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu ambalo Watanzania wengi kwa uwingi wao wanahitaji kupata viongozi ambao watawatoa na kuwaweka katika kilimo bora na cha kisasa. Lakini kwenye kilimo tumekuja na sera ya kilimo kwanza, kwenye kilimo kwanza tumekwenda na kauli mbiu kwamba sasa tuwawezeshe wakulima.

Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa wala siihitaji. Nakwenda kwenye mambo ya msingi.

Mheshimiwa Spika, nazungumzia suala la elimu. Jamani elimu imeshuka, unapokwenda katika Taifa la watoto wa kidato cha nne karibu nusu ya wanafunzi wamepata division zero, hatuhitaji kujadili mara mbili. Tunakubaliana na ukweli tunaujua. Lazima tukosoe ili mfanye kazi vizuri.

Lakini kitu kingine kinachosababisha elimu kushuka jamani muwe mnasikiliza vilio vya Walimu siyo tu madarasa, siyo maabara siyo maktaba, msikilize vizuri vilio vya Walimu. Mkielewana vizuri Walimu wenyewe naamini kabisa ndani ya mwaka mmoja kiwango cha elimu katika Taifa hili kitabadilika. Lakini kama hili halitaendelea kusikilizwa hata ujenge madarasa mazuri kwa kiwango gani, hata ujaze maabara vifaa vyote na maktaba ukajaza vitabu vya kila aina, elimu itaendelea kubaki vile vile kwa sababu hivi vyote vinahitaji Mwalimu ambaye atawaelekeza wale watu kutoka katika kutokujua kuelekea katika kujua ili kupata mustakabali bora wa elimu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine katika Hotuba ya Rais ukiachilia kwamba anasema sikuisikiliza lakini nimeisoma na nimeielewa. Nimetoka University juzi tu akili bado inachangamka. Kwa hiyo, nimejaribu kuipitia kwa umakini sijaona kipengele cha walemavu, watu wenye mahitaji ya msingi katika Taifa hili, watu ambao walizaliwa si kwamba walipenda, tunahitaji namna gani ya kuweza kuwakomboa watu hawa. Lakini tunaitoa na hatuwezi kuigundua.

Mheshimiwa Spika, bado muda.