| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 6 | 15 February 2011 | Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete | ||
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Spika wa kwanza mwanamke kwa kura nyingi sana. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Rais kwa kuchaguliwa kwake na kupeperusha bendera ya CCM vyema. Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wote wa Jimbo la Kalambo na Wilaya mpya ya Kalambo kwa kura zao nyingi sana kwa Chama cha Mapinduzi na mimi binafsi kuniwezesha kuingia Bungeni kuwatumikia, nawaahidi kuwatumikia kwa uwezo wangu wote ili kauli mbiu yetu ya nuru mpya ya Kalambo: “Kwa Pamoja Tunaweza” iweze kutimia. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huu, naomba nichangie hotuba ya Rais. Naomba nijielekeze katika vipengele vifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kuja na mkakati maalum wa Kilimo Kwanza. Sera hii imekuwa na tija pamoja na kwamba imekuwa na changamoto za hapa na pale, naomba kutoa ushauri kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, bei ya pembejeo zimekuwa kubwa kiasi kwamba imekuwa vigumu sana kwa wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu bei kubwa na bei hizi kubwa zikiwa zimetokana na waagizaji binafsi kupandisha bei kiholela na hasa baada ya Shirika la Serikali kushindwa kuagiza pembejeo baada ya kupata hasara iliyotokana na kushuka na kuanguka kwa bei kutokana na mdororo wa uchumi wa dunia. Nashauri shirika hili lifidiwe mapema ili kusiwe na upandaji bei kiholela. Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iangalie upya uwezekano wa kuwapatia bure pembejeo kwa wananchi wasio na uwezo kabisa kama inavyofanya kwa kila kaya. Pia nashauri vituo vya kununulia mahindi viongezwe na wakala NFRA kuliko vichache vilivyopo ambavyo vinakuwa na usumbufu mkubwa kwa wananchi wa Kalambo. Mheshimiwa Spika kuhusu naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayoifanya ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zinazoendelea Mkoani Rukwa na Katavi, zile za kutoka Sumbawanga - Tunduma, Sumbawanga - Mpanda, Sumbawanga - Kasanga. Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ifikirie kwa umakini sana ujenzi wa barabara iliyokuwa ikitumika zamani maarufu kama barabara ya Mjerumani itokayo Isanga Tunduma kupitia Ilonge Jimbo la Kalambo kupitia Legezamwendo, Kalepula, Mwimbi, Kamawi, Tatanda, Nondo, Kamkolwa daraja la Kalambo na kuunganisha barabra ya kwenda bandari ya Kasanga. Mheshimiwa Spika, barabra hii ni muhimu sana kiuchumi lakini pia inapunguza mzunguko kwa zaidi ya kilomita 70 kwa mtu ambaye hana haja ya kwenda mpaka Sumbawanga akiwa na nia ya kwenda bandari ya Kasanga. Mheshimiwa Spika, kuhusu Uvuvi, naishukuru na kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwajali sana wananchi wajiongezee kipato. Naomba niikumbushe Serikali kwamba ijielekeze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Kalembo waishio mwambao wa ziwa Tanganyika ambao shughuli yao ni uvuvi ambao kwa bahati mbaya wanavua kwa kutumia zana ambazo ni duni sana. Mhehsimiwa Spika, naiomba Serikali ijielekeze kuwasaidia wananchi ili wawe na uvuvi wenye kuleta tija. Kutokana na zana duni uvuvi, wetu umekuwa wa kuhabahatisha na unafanyika muda wa usiku tu na kipindi cha giza na kuishia kuvua samaki wadogo tu na kushindwa kuvuna samaki kama aina moja ijulikanayo kama English fish. Aina hii ya samaki wakubwa na wazuri hatuwezi kuwavua kwa zana zetu duni. Naiomba Serikali ielekeze nguvu kwa kuwakopesha na kuweka ruzuku kwenye zana za uvuvi. Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika suala zima la ardhi ambalo Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa nia yake thabiti ya kuhakikisha kwamba ardhi inapimwa na kumilikishwa kwa vijiji kwenye mabenki na vyombo vya fedha. Mheshimiwa Spika, ardhi imekuwa na migogoro mingi juu ya umiliki kwa mfano katika Jimbo langu la Kalambo, ardhi walioiachia Serikali yao wakati wa uanzishaji wa ranchi ya Kalambo ya Serikali wamejikuta hawana ardhi ya kilimo baada ya shamba hilo la Kalambo kumilikishwa kwa watu binafsi bila hata kuihusisha Halmashauri na vijiji husika, vijiji vilivyoathirika ni pamoja na vijiji vya Katapulo, Mbuluma, Mao na Mkowa. Mheshimiwa Spika, kuhusu maliasili na mazingira, ninashauri Serikali iongeze nguvu katika kuvitangaza vivutio vyetu vya maporomoko ya mto Kalambo ili yawe na manufaa kama wenzetu wa upande wa pili wa Zambia wanavyofaidi japo maporomoko yanaonekana vizuri zaidi ukiwa upande wa kwetu. Mheshimiwa Spika, mazingira yanaharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukataji miti kwa ajili ya mkaa. Naishauri Serikali ijikite katika utafiti ili wananchi watumie makaa ya mawe katika shughuli za majumbani kwani wananchi wamekuwa wakilalamikia hewa ya mkaa na kutoboka kwa masufuria. Naomba utafiti ufanyike ili tuweze kutumia makaa ya mawe yanayopatikana kutoka machimbo ya Namwele na Mpanda. |
|||||