You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Kamani, Dr. Titus Mlengeya Dismas[CCM]

Busega Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 3 10 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi kuchangia katika hotuba hii ya Rais.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijaalia afya njema na kwa kunipa nafasi nikateuliwa kama Mbunge wa Jimbo la Busega. Vile vile niwashukuru wapigakura wa Jimbo la Busega ambao walionesha imani kubwa kwangu na Chama cha Mapinduzi kikaniteua kugombea na nikashinda kwa kishindo. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile nawapongeza Wabunge wenzangu ambao tumepita kwenye kinyang’anyiro kigumu cha uchaguzi na sasa leo tupo kwenye Bunge hili, naomba niwapongeze, lakini tufanye kazi kwa imani na kwa uadilifu ili tusiwaangushe wapigakura wetu.

Mheshimiwa Spika, napenda na mimi niipongeze sana hotuba ya Rais, wakati anazindua Bunge hili, kimsingi hotuba hiyo imeleta matumaini makubwa kwa Watanzania. Ilikuwa ni hotuba nzuri na mimi kwa ufupi tu naweza nikasema imeonesha upeo mkubwa alionao Rais wa kimaono kuhusu Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza tu kwa kuonesha shukrani za kwanza za jinsi mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne ni kwa kuifanya Busega kuwa Wilaya kitu ambacho kilikuwa kilio cha muda mrefu. Hii inaendana kweli na dhamira ya Serikali ya kusogeza maamuzi na huduma muhimu kwa wananchi. Kwa hiyo, wananchi wa Busega wanapongeza sana Serikali, lakini wamenituma niseme kwamba wangeomba sana mchakato wa kukamilisha taratibu za Wilaya kuanza kufanya kazi, zifanyike na zikamilike kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, ningependa nizungumzie kwenye kipaumbele cha pili katika hotuba ya Rais, katika kuimarisha, kukuza uchumi wa wananchi na kwa kutumia kilimo kama njia muhimu sana ya kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Spika, kilimo ndiyo kinaajiri takribani asilimia themanini ya Watanzania, na kwa kushughulikia suala la kilimo ina maana ndiyo njia ya uhakika na ya haraka ya kupunguza umaskini wa watu wetu. Lakini tunapozungumza kuleta mapinduzi ya kilimo ambayo kweli yamekwenda sambamba na mpango wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi wa Kilimo Kwanza, kuleta mabadiliko ya haraka, hatuwezi tukakwepa suala la Agro Mechanisation, yaani matumizi ya zana kuondokana na jembe la mkono kwenda kwenye zana kubwa na za kisasa. Lakini kwa hali ilivyo hadi sasa bado matumizi ya matreka uko chini sana.Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Magu ambako tangu mwaka jana 2010 watu 17 waliomba kupatiwa mkopo wa matrekta kupitia mfuko wa pembejeo, hadi leo hii mwaka mzima baadaye hawajapata. Kwanza matrekta 17 ni machache sana kwa Wilaya, lakini vile vile mlolongo mrefu wa namna ya kuyapata unafanya dhamira yetu ya kufikia haya mageuzi uende polepole sana.

Mheshimiwa Spika, napenda kuishauri Serikali iweke mpango wa makusudi kuwezesha upatikanaji wa matrekta kwa haraka zaidi, lakini kwa wingi zaidi ili wananchi wengi wahame sasa kwenye kilimo cha mkono kwenda kwenye kilimo kikubwa.

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji. Tanzania ina bahati nzuri kwamba ina maji mengi, tunayo maziwa makuu, ziwa Victoria, ziwa Tanganyika, ziwa Nyasa, lakini inasikitisha kwamba kunapotokea kiangazi hata cha muda mfupi tu, watu wenye mashamba wanaoishi hata mita mia tano tu kutoka ziwani mazao yanakauka kwa sababu tu hawawezi wakayatumia yale maji. Kwa kweli hali hii ni muhimu sana, tufanye juhudi za makusudi.

Mheshimiwa Spika, Busega, Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Mara, Mkoa wa Kagera watu wana hamasa ya kutumia kilimo cha umwagiliaji lakini maarifa, teknolojia ya kuyavuta yale maji na kwa bahati nzuri sana yale mabonde hata hayana mwinuko mkubwa kwamba utapata shida sana kusukuma maji, lakini yake maarifa ya kutumia bado hawana. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali ielekeze nguvu, aidha, kwa scheme ndogo ndogo, lakini nyingi hata scheme kubwa ili tuhakikishe kwamba tunanufaika na maji ya maziwa yetu haya.

Mheshimiwa Spika, nipongeze tu wakati fulani aliyekuwa Waziri Mkuu alishiriki kwenye mchakato wa kupinga ule mkataba gandamizi ambao ulikuwa unafanya Watanzania tusiwe na ruhusa ya kuyatumia maji ya Bonde la mto Nile na Ziwa Victoria. Kwa kweli haifai wala haipendezi Sudan, Misri wananufaika na kilimo cha umwagiliaji cha maji ambayo yanakusanywa huku kwetu na sisi tunakufa njaa na kulia njaa hata sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nafikiri Serikali iweke juhudi ya makusudi, watu wanufaike na maji ya maziwa haya. Mipango hii ikifanyika vizuri, kwenye Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ziwa Tanganyika, Bonde la Ziwa Nyasa hii hali ya kulalamika njaa ya kila mwaka isingekuwepo na ninahakika ingekwisha kabisa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ningependa kulizungumzia ni suala la masomo ya kilimo na mazao ya mifugo. Tukiwa na masoko mazuri ya mazao na hata tukaingia kwenye processing, naamini kwamba wafugaji wetu, wakulima wetu watahamasika na kuanza kufuga na kulima zaidi kwa sababu watakuwa na hakika ya masoko. Kwa mfano, mifugo, tunazungukwa na nchi nane ambazo wakati wote zina upungufu wa mifugo. Hatuwezi tukanufaika na masoko hayo kwa sababu minada yetu iko duni na hivyo Serikali inakosa mapato, lakini na wafugaji wetu hawapati mapato.

Mheshimiwa Spika, upunguzaji wa umaskini ungekwenda sambamba sana na kuimarisha Vyama vya Ushirika, SACCOS, VICOBA. Ushirika ni mwokozi na mkombozi wa watu maskini. Nafikiri ni muhimu sana Vyama vya Vshirika Wilayani vikaimarishwa, havina vitendea kazi, havina wafanyakazi. Ni muhimu sana eneo hili likaimarishwa ili waweze kufanya kazi kuwafikia wananchi wengi zaidi waweze kushiriki.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ningependa kuipongeza Serikali kwa kuimarisha mamlaka za EPZ na SEZ (Export Processing Zone na Special Economic Zone). Mamlaka hizi kimsingi zilikuwa zinafanya kazi zinazoshabihiana, lakini kwa sababu sasa tunataka tuimarishe utengenezaji wa bidhaa za kusafirisha nje, lakini nafikiri hili lingekwenda sambamba na kuyatumia maeneo yetu ya mipaka vizuri. Maeneo yetu ya mipaka ukienda Sirari, ukienda Horiri, Kajumulo, maeneo ya upande wa Tanzania hayakupimwa na hayakupangwa vizuri. Hayavutii uwekezaji. Hii ni rasilimali ambayo tunaiachia, maeneo hayo sasa ni vizuri yakapimwa tukavutia uwekezaji na watu wakafanya biashara kubwa ili wenzetu waweze kuja kuchukua bidhaa kwetu tupate kodi na wananchi wapate mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, nimekwenda pale Holili upande wa Kenya ambako kimsingi ni pakame kama jangwa na upande wa Tanzania ndiyo wenye neema, wenye ardhi yenye rutuba, wenzetu wametengeneza soko zuri sana ili wavutie bidhaa za Tanzania ziende kwao, lakini Serikali yao inakusanya kodi, sisi kwetu hatukusanyi chochote. Kwa hiyo, nafikiri sasa kuna daraja la mto Ruvuma limejengwa la umoja, nafikiri tuanze mapema kuweka maeneo hayo vizuri kwa uwekezaji na mipaka mingine ya Rwanda, Burundi na Uganda kama kawaida.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa nafasi.