| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 17 | 1 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa | ||
Mheshimiwa Spika, tatizo la upungufu mkubwa wa madawati katika nchi yetu linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuandaa mpango maalum wa kimkakati wa angalau mwaka mmoja wa kuondoa kabisa tatizo hilo kwa nchi nzima kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali nchi nzima. Wananchi, wazazi, taasisi na Serikali wote kwa pamoja tushirikiane kuchangia kutatua tatizo hili. Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa Wilaya zenye ukame mkubwa wa mvua na hivyo kusababisha kila mwaka Wilaya hii imekuwa ikipatiwa msaada wa chakula na Serikali. Lakini Wilaya hii ina fursa kadhaa za mito na maji yanayotiririka wakati wa masika ambayo kimsingi yangeweza kuhifadhiwa kwa njia ya mabwawa kwa shughuli za umwagiliaji. Hivyo naishauri Serikali iangalie kwa namna ya pekee fursa hizi zilizopo hasa mito na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya hii kwa kufanya utafiti wa kina juu ya uwezekano wa kuanzisha mradi kabambe wa kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya hii hasa kwa kuziangalia upya skimu kumi za umwagiliaji zilizoko katika Wilaya hii ambazo ama hazijakamilika au zimechakaa sana. Naamini kama Serikali itaamua kusaidia sekta hii ya umwagiliaji katika Wilaya hii basi itakuwa fursa muhimu ya kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa chakula katika Wilaya na kuzalisha ziada. Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bahi ni Wilaya mpya, inahitaji sana Serikali kuelekeza jicho lake katika kuwezesha mambo yafutayo:- (a) Kuwezesha watumishi kuhamia Makao Makuu ya Wilaya toka Dodoma Mjini kwa kutoa fedha za ujenzi wa nyumba za watumishi, manunuzi za furniture za ofisi na mahitaji kadhaa ya watumishi. (b) Kusaida juhudi za Halmashauri za kutatua tatizo kubwa la maji kwa kutoa fedha za kuleta maji umbali wa kilomita 40 toka Wilaya ya Manyoni ili kumaliza tatizo la uhaba wa maji katika mji wa Bahi ambao ndio Makao Makuu ya Wilaya. (c) Kupewa fedha za kutosha ili kuanza kujenga miundombinu za ndani ya mji wa Bahi hasa barabara, maji safi na maji taka. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. |
|||||