You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Amar, Hussein Nassor[CCM]

Nyanghwale Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 5 14 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Kufungua Bunge Jipya, 2010
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha leo kusimama katika Bunge lako Tukufu, huo ni uweza wake na si ujanja wangu.

Pia napenda kumshukuru Mke wangu, Bi. Ashura pamoja na familia yangu yote akiwemo mama yangu, pamoja na wananchi wote wa Jimbo la Nyang’hwale, kwa kunichagua na kuwa Mwakilishi wao. Pia napenda kuwapongeza Wabunge wote, Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kidogo Hotuba ya Mheshimiwa Rais kuhusiana na mambo machache. Kwanza, nitaanza kuchangia kidogo kuhusu suala la elimu. Kwa kweli suala la elimu Waheshimiwa wengi wamelichangia, lina matatizo mengi na mimi napenda nichangie kidogo katika Jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, Jimboni kwangu upungufu wa Walimu ni mkubwa sana. Nimejaribu kufanya ziara katika shule, nimekuta shule ina Wanafunzi 700 na Walimu wawili. Upungufu mwingine ni vitendeakazi, madawati na nyumba za Walimu. Ni matatizo sana, lakini cha kushangaza shule hizo ambazo ziko Jimboni kwangu unakuta Shule ya Sekondari ina Walimu wawili, lakini unakuta Shule ya Sekondari ya aina hiyohiyo iko mjini ina walimu 18 mpaka 30. Naiomba Serikali ijaribu kuliangalia hili suala la uwiano wa Walimu, kwa nini Vijijini Walimu wanakuwa wachache sana na shule za Mijini zinakuwa na Walimu wengi? Kwa nini? Naiomba Serikali ijaribu kuliangalia suala hilo na kuwaangalia hao Walimu ambao wako Vijijini angalau basi mishahara iongezwe labda inaweza ikawa changamoto kwa Walimu ambao wanang’ang’ania Mijini waweze kwenda Vijijini.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuchangia kidogo kwenye suala la kilimo. Katika Jimbo langu 95% ni wakulima. Wakulima hao namshukuru Mungu kwamba wanajitahidi sana katika kilimo lakini kuna mambo mengi ambayo yanakwamisha maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa soko la mazao yao. Soko la mazao si zuri na halina msimamo. Mavuno mengi yanapatikana lakini cha kushangaza unakuta gunia la mpunga linauzwa kati ya Sh.15,000 na Sh.20,000, mkulima huyu atajikomboa vipi wakati gharama za uendeshaji wa kilimo ni kubwa? Naiomba Serikali ijaribu kuliangalia suala hili la soko, tutafutiwe wafadhili, yajengwe maghala ili wanunuzi waweze kuja kununua mazao yetu kwa bei iliyo nzuri.

Mheshimiwa Spika, pia mazao mengi yanapatikana hususani ndani ya Vijiji ambavyo vina matatizo mfano barabara ni mbovu, hivyo kuyaleta mazao yale katika sehemu ambayo angalau bei nzuri inakuwa haiwezekani. Naiomba Serikali hususani Wizara ya Kilimo na Chakula, ijaribu kuwaangalia wakulima kwa kuwawezesha kwa pembejeo na kuliweka imara soko la mazao ili tuweze kumnyanyua mkulima.

Mheshimiwa Spika, pia naiomba Serikali iweze kuja kuwapimia mashamba yao ili waweze kupata hatimiliki waweze kupata mikopo Benki hatimaye waweze kupanua kilimo. Naiomba Serikali iangalie sana suala hilo la kuwawezesha wakulima kwa kupitia asset waliyonayo ikiwemo ardhi, mkulima hawezi akakopeshwa bila kuwa na hatimiliki. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kuliangalia suala hilo ili tuweze kuwanyanyua wakulima kwa kuwamilikisha ardhi yao waweze kupata hatimiliki na hatimaye waweze kupata fedha katika Benki.

Mheshimiwa Spika, napenda kidogo kuchangia kwenye suala la maji. Jimboni kwangu kwa kweli kuna tatizo kubwa sana la maji. Kuna sehemu akina mama wanaondoka saa tisa za usiku kufuata maji umbali wa kilomita tano, ni shida. Cha kushangaza sisi katika Jimbo letu, Ziwa Victoria ni kilomita moja unayapata maji lakini Jimbo langu halina maji, kwa nini? Miaka ya nyuma, mwaka 1972 palifungwa pampu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na kusambazwa baadhi ya Kata. Lakini cha kushangaza mwaka 1975 pampu hiyo ikawa imesimamishwa kusukuma maji na hivi ninavyoongea mashine hiyo leo miaka 36 karibu ipo, pampu yake ipo na baadhi ya matenki yapo, lakini maji hatupati. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kutuangalia kwa jicho la huruma, yaletwe maji hayo ili waweze kupunguza adha ya kufuata maji umbali mrefu. Kwa kweli tatizo la maji ni kubwa hata mifugo yenyewe wananyweshwa yale maji kwa kufuata kilomita tano kwenye baiskeli. Mtu anachukua baiskeli kufuata maji umbali wa kilomita tano kuja kuwanywesha ng’ombe na ng’ombe hao hawana afya nzuri, afya yao ni mbovu kwa sababu hawapati maji.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuzungumzia kidogo upande wa afya. Katika Jimbo langu, Zahanati zipo, Vituo vya Afya viko viwili, Kituo kimoja kimeelemewa. Kituo kimoja kipo Kharumwa ambapo sasa hivi ndio Makao Makuu ya Wilaya. Kituo kingine cha pili kiko Nyang’wale, ni kituo kizuri, kina majengo mengi lakini kimetelekezwa, hivi ninavyoongea popo ndio nyumba yao ya kuishi. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kukihuisha hicho Kituo ili kiweze kutoa huduma kwa sababu Kituo kimoja cha Kharumwa kimezidiwa. Tuko wananchi zaidi ya 350,000, kituo ni kimoja. Zahanati pia zipo lakini na zenyewe zina upungufu, Wauguzi, madawa pamoja na vitendea kazi. Lakini pamoja na hivyo Zahanati hizo hazitoi huduma inavyopaswa kwa sababu huduma zenyewe zinatolewa kwa upendeleo. Nikizungumza kwa upendeleo kila mmoja anaelewa upendeleo huo ni upi. Kwa kweli naiomba Serikali ijaribu kulifuatilia suala hili, kwa nini upungufu wa madawa upo na ukienda kwenye maduka ya madawa binafsi unakuta dawa zile za MSD zimo kwenye maduka yao, wao wanazipata wapi? Lakini ukienda Zahanati na kwenye Vituo vya Afya unakuta dawa hizo hazipo. Ukweli ni kwamba naiomba Serikali ijaribu sana kufuatilia hususan Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Spika, napenda nichangie kidogo upande wa miundombinu. Miundombinu ya Jimbo la Nyang’wale, tunashukuru kwamba kuna barabara moja tu ambayo ndio inapitika kipindi chote lakini baadhi ya barabara za ndani ni mbovu na pia kuna mito ambayo haipitiki hususan wakati wa masika na Mito hiyo inasababisha mpaka wanafunzi wanashindwa kusoma kwa sababu ya kujaa. Mto huo ukijaa, unakata mawasiliano kati ya Kijiji hiki na Kijiji kingine na kusababisha wanafunzi wasiende kusoma hata huduma zingine zisifanyike. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kuliangalia sana suala hili ili tuweze kujengewa angalau daraja ili mawasiliano yawepo kipindi chote. Kuna Mito kama mitano ni matatizo makubwa, naiomba Serikali kilio hiki ijaribu kukisikia.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kwenye upande wa usalama wa raia hususan upande wa Polisi. Jimboni kwangu Polisi kwa kweli wanaishi kwa taabu, nyumba zao ni mbovu kuliko, Vituo vya Polisi karibu vinaanguka, nyumba hamna, Mahabusu zile ni mbovu kabisa. Kwa hiyo, naomba angalau basi Serikali iweze kujenga nyumba nzuri za ofisi za Polisi pamoja na kuwajengea nyumba za kuishi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia wananchi wanalalamika sana kwa huduma ambayo inatolewa na Polisi wa Jimboni kwangu. Kuna unyanyasaji wa hali ya juu na pia rushwa imekithiri. Nazungumza hivyo kwa sababu kuna matukio mbalimbali ambayo yamejitokeza yanawahusu Polisi. Mfano mwezi uliopita, kuna watoto takribani watano wameliwa na fisi, lakini taarifa zikitolewa kwa Polisi hebu njooni muangalie tatizo hili, wakifika pale wanawanyanyapaa waliofiwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais.