| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 6 | 15 February 2011 | Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete | ||
Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa hotuba ambayo imetoa dira na matumaini kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais amekuwa ni hodari sana hasa katika kushughulikia kero za wananchi ambazo zilionekana kushindikana. Tunampongeza sana. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia katika eneo la maji. Kwanza, naomba fedha zaidi zitengwe kwenye bajeti ijayo katika sekta ya maji. Hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo mengi, si nzuri ila katika Jimbo langu la Lulindi hali ni mbaya sana na kufanya wananchi kuhangaika na kukata tamaa. Ndoo moja ya lita 20 huuzwa kwa shilingi 1,000/= hali inayofanya wananchi wengi kutomudu kupata maji. Naishauri na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuwanusuru wananchi hawa. Mheshimiwa Spika, elimu, afya na huduma za jamii. Katika maeneo haya, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa kuonesha dira. Naishauri Serikali kuimarisha Serikali za Mitaa na kuziondolea vikwazo na kero zinazowakabili. Pia kuongeza posho za Waheshimiwa Madiwani ili wazisimamie Halmashauri zao vyema. Pia Halmashauri kuzijali Ofisi za Serikali za Vijiji na Mitaa. Pia kwa kupeleka fedha kwenye Kata kwa ajili ya kuzihudumia Ofisi hizi na Wenyeviti wake. Mheshimiwa Spika, pili, naiomba Serikali kuacha kunyofoa shughuli zinazofanywa na Halmashauri na kuzirudisha Serikali Kuu. Kwa mfano:- (i) Serikali kuamua magari yote yanunuliwe na Wizara ya Miundombinu. Jambo hili limesumbua na kurudisha nyuma juhudi za Halmashauri kujiletea maendeleo yao. Naishukuru Serikali kurekebisha utaratibu huu; na (ii) Serikali Kuu kuamua ajira zote zifanywe na Wizara inayoshughulikia na Utumishi. Jambo hili litadhoofisha juhudi zilizoainishwa kwenye hotuba yake. Naishauri Serikali kurudisha Mamlaka hayo kwa Halmashauri ili ziendelee kuajiri. Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kuanzisha mkakati wa Kilimo Kwanza. Naiomba Serikali izingatie kuhakikisha kwamba wakulima wanapatiwa pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Wataalamu wetu wawe karibu na wakulima na pia Serikali isimamie ipasavyo kuhusu masoko ya mazao kwa kuwasimamia wapate bei nzuri. Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kutafuta soko la korosho kwa kuanzisha utaratibu wa Stakabadhi Ghalani, umeleta manufaa sana. Ombi la wananchi ni kulipwa fedha yote ya bei inayotangazwa na Serikali na wakulima wasubiri bonasi baada ya mauzo ya korosho. Jambo hili litawasaidia wakulima wadogo ambao huzipata fedha hizi huku wakikabiliwa na mikopo ya pembejeo. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais. |
|||||