| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 8 | 7 | 21 June 2012 | Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2011/2012 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 | ||
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, nampongeza kwa kuchaguliwa kwake na Manaibu wake kwa bajeti nzuri ambayo imelenga Watanzania wanyonge. Mheshimiwa Spika, napenda niende moja kwa moja kwenye hoja. Jimbo la Morogoro Mjini lina wafanyabiashara ndogondogo. Katika bajeti hii nimeona wafanyabiashara ndogondogo kama bodaboda, naomba nao tuweze kuwanyanyua kwa kuwatolea kodi. Mheshimiwa Spika, kwenye ajira za vijana, vijana wengi hawana kazi na njia ya kuweza kuwasadia ni kilimo na kuwapa mikopo ya kuweza kulima kwa kuwaunganisha kwa vikundi. Ardhi tunayo kubwa sana, tutaweza kunyanyua kipato na wakapata ajira. Uchumi wa kilimo ndiyo njia fupi ya kuweza kutoa ajira nyingi katika nchi yetu. Mheshimiwa Spika, pia wanawake nao wawezeshwe kupata mikopo na hususani katika Jimbo langu la Morogoro Mjini, wanawake wengi wanategemea biashara ndogondogo. Nao vilevile tuweze kuwapatia mikopo waweze kujiajiri. Tuongeze nguvu katika mikopo. Mheshimiwa Spika, katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, tujitahidi sana kuziba mianya na hususani mapato ya Halmashauri ili tuweze kufikia malengo ambayo tunayapanga ya kuwaokoa Watanzania katika umaskini. Mheshimiwa Spika, kwenye miundombinu, namuomba Mheshimiwa Waziri anikumbuke kwenye barabara zetu na hususani barabara ya Morogoro ambayo imechongwa, ni nyembamba mno. Ukipita mkokoteni, gari haipiti na barabara iko Mjini kabisa, nadhani Waheshimiwa wengi mmepita mmeiona. Mheshimiwa Spika, kwenye elimu pia namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie madawati ili Walimu na wanafunzi waweze kusoma vizuri katika shule zetu. Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya afya, tuna hospitali yetu ambayo ni ya Rufaa. Sasa hivi ina upungufu mwingi sana, katika bajeti hii, ningeomba nayo Mheshimiwa Waziri atufikirie maana anayewahi maji, anakunywa maji mazuri. Mheshimiwa Spika, mwisho naunga mkono hoja asilimia 100 kwa 100. |
|||||