| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 3 | 2 | 6 April 2011 | Hoja za Kamati | ||
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutoa pongezi kwa Kamati kwa kazi kubwa ya uchambuzi ambayo imefanywa. Naunga mkono taarifa iliyoletwa na Mwenyekiti na maainisho yote ambayo Mwenyekiti ameainisha. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwenye Halmashauri zetu nchini kwa dhamira ya kuboresha maendeleo kwa wananchi wetu, kama ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyosema. Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ambazo Serikali imekuwa inatoa zitawekewa mikakati thabiti na usimamizi wa kina toka kwetu Wabunge na Madiwani katika Halmashauri zetu. Ni dhahiri kuwa dhamira ya Serikali katika kutoa huduma stahili kwa wananchi wetu, itakamilika na wananchi wataona matunda ya Uhuru. Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wa Halmashauri na viongozi wa kuchaguliwa katika Halmashauri zetu nchini wamekuwa ndio chanzo cha Serikali kushindwa kutekeleza majukumu yake. Wote wameweka mbele mahitaji au maslahi binafsi badala ya umma wa Watanzania. Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuonyesha wametumia shilingi 15,000,000/= kwa ununuzi wa injector pump ya gari Toyota LandCruiser na Kamati kugundua kwamba gharama halisi ya Injector pump hiyo ni shilingi 3,000,000/= ni kielelezo tosha Halmashauri nyingi nchini kuna ubadhirifu mkubwa katika fedha za Serikali na ubinafsi kwa watendaji badala ya kutumikia watu. Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni wizi wa makusudi na ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuchukua hatua za makusudi kwa Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji hawa wabadhirifu katika Halmashauri zetu na Serikali kuu kwa ujumla. Kwa kuwapeleka Mahakamani kwa kosa la wizi wa kuongeza gharama halisi za kusudio. Watendaji hata kama wamehamishwa katika Halmashauri husika warudishwe kule kule walikoharibu na kushitakiwa. Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ningeomba kwa Serikali nadhani wakati umefika kuajiri Watendaji Wakuu wa Halmashauri, Wakurugenzi (DED) wakaajiriwa kwa mikataba ya miaka miwili, miwili ili tuweze kupima uwezo wao na kuona kama kuna haja ya kuendelea nao. Wakimaliza mikataba yao na wakishindwa wasipewe mikataba mipya, itasaidia kufanikisha malengo ya Serikali. Nashukuru. |
|||||