| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 17 | 1 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa | ||
Mheshimiwa Spika, ninapenda kuchangia Hotuba Waziri Mkuu kuhusu Muundo wa kupeleka madaraka yote ya Kiserikali kwa Wakurugenzi wa Wilaya, ambapo kazi zimekuwa nyingi sana kwenye Halmashauri, yaani Miradi ya Maendeleo mingine haifanyiki na kuwa viporo kwa mwaka wa fedha mwingine, jambo ambalo halileti tija thabiti ya maendeleo kwa kuzingatia muda wa utekelezaji wa Mradi husika. Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mbeya kuna baadhi ya fedha zimerudi na hazijatumika hasa kwenye Idara ya Kilimo na Miradi yake. Hali hii siyo sahihi, hatuwatendei haki Wananchi wetu kwa kuwa na visingizio vingi kwa Watendaji. Mheshimiwa Spika, ninashauri Ofisi ya Waziri Mkuu igawanywe kwa baadhi ya Watendaji, wawe kazi yao ni kufuatilia utekelezaji wa Miradi iliyopo kwenye Halmashauri nchini. Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chunya ni pana sana na inabidi igawanywe kuwa Wilaya mbili; na kwa kuwa mchakato wa kupata Wilaya mpya ulishaanza pale Mji wa Mkwajuni ambapo ndiyo Makao Makuu ya Jimbo langu la Songwe; tunaomba basi tupatiwe hadhi ya Mji Mdogo pale Mkwajuni ili kurahisisha utekelezaji kazi za Serikali na kurahisisha utoaji huduma mbalimbali kwa Wananchi. Mheshimiwa Spika, TAMISEMI, inatoa fedha kidogo sana kwa Mradi wa Barabara zinazoshughulikiwa na Halmashauri ya Chunya, ambapo mpaka sasa zilitengwa shilingi 60,000,000, kwa matengenezo ya Barabara za Kapalala – Udinde – Rukwa Km.10 na Kapalala – Gua Km. 35, pia Vijiji vya Kapalala – Ngwala Km. 46, jumla ni kilomita 91; je, fedha hizo zinatosha? Ninaiomba Serikali iongeze mgao wa fedha za matengenezo ya barabara kwenye Halmashauri ya Chunya kwenye Vijiji hivi. Mheshimiwa Spika, fedha hizo zipo mpaka sasa ila hakuna Mkandarasi anayekubali kutoa vifaa vyake toka Mjini Mbeya mpaka Vijiji hivyo vya Kapalala, Kininga, Gua, Udinde na Ngwala, kwa kutengeneza barabara Km. 91 kwa milioni sitini. Ninaomba bajeti iongezwe Wilaya ya Chunya kwenye Miradi ya Barabara. Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja. |
|||||