You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Kibona, Aliko Nikusuma[CCM]

Ileje Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 3 10 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adimu ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa wakati akifungua Bunge lako Tukufu tarehe 18 Novemba, 2010.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyeniwezesha kuwepo miongoni mwa Wabunge wenzangu walio katika Bunge lako Tukufu. Nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi na wapiga kura wote wa Jimbo la Ileje kwa imani yao kubwa kwangu, kwa kunipa kura nyingi na baadaye nimeweza kuingia na kuungana nanyi katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe pia kwa kupata nafasi hiyo ambayo umeweka historia katika nchi yetu, nakupongeza sana. Niwapongeze pia Wabunge wenzangu wote wa Chama cha Mapinduzi na kwa kweli pia watani zangu wa upande wa pili, Wabunge wa Upinzani, hongereni kwa kupata nafasi ya kufika katika jengo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda, naomba sasa nichangie hotuba ya Rais, nitazungumzia mambo machache, mengi yameongelewa na wenzangu lakini walau nizungumze machache hasa kwenye eneo la elimu, afya, mazingira, amani na utawala bora.

Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari sana, wenzangu wengi wamezungumzia juu ya elimu, sasa hivi nchi yetu tunajiandaa kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa kweli tumeshaingia, tumeamua, tunatakiwa sasa kujua, je, tumejipanga sawasawa kushindana na wenzetu kwenye eneo la elimu? Hatutaweza kufanya chochote, tutakuwa watu wa kushangaashangaa, wenzetu wataendelea kuchota ajira, sisi hatutafanikiwa tusipokuwa na mkakati mkubwa na maalum kwa ajili ya kuboresha elimu yetu.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri na maamuzi mazuri ya Chama cha Mapinduzi, kuamua kila Kata katika nchi yetu iwe na Shule ya Sekondari, hilo ni jambo jema. Wale tunaokumbuka enzi za miaka ya sabini, miaka ya themanini na kwa kweli miaka ya tisini, vijiji vingine vilikosa kabisa vijana wa kwenda sekondari, vijiji vingine vilitoa mtoto mmoja, lakini sasa vijana wetu wengi wanakwenda sekondari.

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto ambazo ni lazima tukabiliane nazo, Walimu wengi wanafundisha katika mazingira magumu mno. Ninao mfano wa Jimbo langu la Ileje, jiografia yake ni ya milima, barabara ni vigumu kupitika, Mbunge yeyote aliyepo hapa afikirie kwamba anaishi Dar es Salaam au Dodoma na mtoto wake anapangiwa katika Jimbo ambalo miundombinu haipo, kwa maana ya barabara, mitandao, hospitali za uhakika, halafu anafika Makao Makuu ya Wilaya anaambiwa aende, haendi. Ninavyo vijiji mbalimbali katika Jimbo langu ambavyo kwa kweli mtoto yeyote anayetoka mbali hasa wale wanaotoka mjini, wakimaliza Vyuo vya Ualimu wakipangiwa katika Kata zile, wengi wanakimbia kwa sababu wakifika kwanza wanaanza kutembea kwa miguu, barabara hazipitiki, anatembea kilometa hamsini au kilomita arobaini kutoka Makao Makuu ya Wilaya, akifika kule anakuta nyumba hamna, akifika kule anakuta maji hamna, katika hali hiyo wengi wanakimbia.

Mheshimwia Spika, naomba nitoe ushauri katika eneo hilo, pengine kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu inayokuja, nishauri na ninaamini kila Mbunge aliyepo hapa angependa kusikia hivyo kwamba Walimu waliopo katika maeneo magumu kwa utendaji wa kazi, wapewe malipo ya ziada ya mazingira magumu ya kazi. Halmashauri zetu, Wakurugenzi, Maafisa Elimu na Utawala wa Wilaya kwa ujumla, unaweza kulifanya hilo kwa kuainisha Kata fulani na Walimu wanaoishi maeno haya wapewe pesa ya ziada, posho ya hali ngumu ya mazingira mpaka hapo hali itakapotengemaa.

Mheshimiwa Spika, kwenye afya, siwezi kuzungumzia mifano nje ya Wilaya yangu na Jimbo langu la Ileje, tunayo Hospitali moja ambayo imeendelea kutumikia Watanzania walioko katika Wilaya ya Ileje, wapigakura ambao wamechangia kuunda Serikali hii tuliyopo, kura zao zipo, lakini hospitali hiyo ilikuwa ya misheni baadaye Serikali imeingia ubia nayo na kuwa DDH. Nasikitika kwamba toka mwaka 1976 mpaka leo hospitali hiyo haijawahi kupewa gari na Serikali ili lisaidie wagonjwa badala yake tumeendelea kutumia gari za mmiliki wa hospitali ambaye ni misheni ambapo sasa hivi kwa kiwango kikubwa, kwa asilimia zaidi ya themanini amepunguza misaada yake. Naomba Serikali katika bajeti ijayo pamoja na maeneo mengine iainishe, iangalie uwezekano wa kuwapatia vitendea kazi watumishi wanaoishi katika hospitali hii.

Mheshimiwa Spika, lakini pia watumishi wanaofanya kazi katika mazingira yale, Madaktari wakifika kuripoti wanaondoka, Clinical Officer wanaondoka, Assistant Medical Officers wanaondoka, Manesi wanaondoka, je, Serikali inachukua hatua gani? Mawazo na ushauri wangu ni tuone namna ya kumaliza shida hii, wahudumu hawa wa afya wapewe motisha kwa kuishi maeneo haya.

Mheshimiwa Spika…

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.