You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Barwany, Salum Khalfan[CUF]

Lindi Mjini Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 14 28 June 2011 Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii kwa mara nyingine tena ya kutoa mchango huu katika Hotuba ya Waziri Mkuu. Kabla ya yote, kwanza, nawashukuru Viongozi wa Chama cha Wananachi (CUF), kwa juhudi kubwa ambazo kwa pamoja wamezifanya katika kuhakikisha kwamba, wanalinusuru Taifa hili kutokana na maafa ambayo yangeweza kutokea kama siyo busara na hekima ya Viongozi hawa.

Mheshimiwa Spika, leo tunazungumzia suala zima la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambayo baadhi ya watu wanabeza kuwepo kwa Serikali hiyo.

Wananchi kwa jumla na Mataifa yote duniani, wanafahamu hali ya kisiasa Zanzibar ilivyokuwa kabla ya Umoja wa Kitaifa wa Serikali kuwepo. Tayari Chama chetu kimeonesha nyao, ndugu zetu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo huko Arusha nao wamefuata nyao hizi na ninaamini pia mwaka 2015, Jamhuri ya Muungano nayo itakuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa pia.

Mheshimiwa Spika, nije katika hoja muhimu. Miaka mitatu iliyopita, Taifa hili lilishuhudia mauaji makubwa kabisa ya kikatili, ambayo yalililetea Taifa letu fedheha ndani na nje. Mauaji ambayo yanasikitisha, binadamu wa kawaida anadiriki kumwondoa binadamu mwenzake duniani eti kwa mahitaji ya utajiri; hili limeleta fedheha kubwa katika Taifa letu. Pamoja na juhudi za Serikali katika kuhakikisha mauaji haya yanakomeshwa, lakini bado Serikali haijatoa tamko rasmi ni jinsi gani mauaji haya yanaweza kukomeshwa yasiendelee tena. Tunasikia kwamba, Serikali kupitia Mahakama zake, inajitahidi kutoa hukumu kwa wale ambao tayari walihusika na mauaji haya. Moja kubwa ambalo tayari linatakiwa liangaliwe kwa makani ni jinsi gani wale ambao walishiriki katika jambo hili, walikuwa na soko maalum kwa ajili ya viungo vya albino. Tunaamini kwamba, siyo mtu wa kawaida wa daraja la chini aliyekuwa anahusika na mauaji yale.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani; thamani ya kiungo cha albino leo tunaambiwa siyo chini ya milioni mia mbili mpaka milioni mia nne; hivi ni mtu gani mdogo wa kawaida anayeweza ku-afford gharama hizo? Tunaamini kabisa kwamba, kuna watu wa daraja la juu waliokuwa wanahusika na mauaji ya albino. Tunaomba Serikali sasa ifanye utafiti wa kina, kujua nani alikuwa soko la viungo vya albino.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mmoja; katika miaka ya sitini kulifanyika mauwaji kule katika Mikoa ya Kusini. Kuna M-Asia mmoja alimuua mkewe, alimuwekea Bima ili akifa alipwe bima hiyo yeye. Serikali kupitia Kampuni ya ile Bima ilionekana kwamba, kulipa fidia ile kupitia Bima ile, ile kampuni ingefilisika kabisa, Serikali ikatafuta vyombo vya Kimataifa kufanya utafiti juu ya mauaji yale ili kuinusuru ile kampuni isifilisike; na ni kweli baada ya muda ilibainika kwamba, Scott and Lad kutoka Uingereza, Interpol, walikuja Tanzania na kufanya utafiti juu ya mauaji yale, ikabainika kulikuwa na njama. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Awamu ya Kwanza kutoa idhini ya mauaji ya M-Asia yule. Mauaji yale yalifanyika kwa mbinu za hali ya juu. Sasa mauaji ya albino; zaidi ya albino hamsini na tatu katika Taifa hili wamepoteza maisha yao, Serikali inasubiri Mahakama, Mahakama ambayo haina uwezo wa kuendesha shughuli kwa nguvu zile.

Tunakuhitaji Waziri Mkuu, utakapotoa hitimisho katika hotuba yako, utueleze kuna mkakati gani wa Serikali wa kuondoa kabisa mauaji ya albino katika Taifa letu. Kuna taarifa zilizopo kwamba, baada ya mauaji yale sasa albino wanapotea katika mazingira yasiyoeleweka, taarifa hizo tunazo na Serikali imenyamaza kimya kabisa juu ya hilo, tunataka Serikali itueleze sasa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie katika eneo la disabilities hilo hilo; ni kwamba, hili ni kundi la mahitaji maalum katika Taifa letu; ni watu ambao wanahitaji msaada mkubwa ndani ya jamii na ndani ya Serikali yake. Kundi hili lenye mahitaji maalum limewekwa katika Wizara ya Afya, lakini kundi hili ni kundi mtambuka, kundi ambalo lina mahitaji mengi kama linavyoitwa kwamba, kundi lenye mahitaji maalum; tulitarajia kwamba, kundi hili lingekuwa katika Wizara mtambuka pia.

Leo Waziri wa Afya hawezi kutoa hoja kwa Waziri wa Elimu ambaye pia anahusika na walemavu; ni vyema sasa eneo hili la walemavu lihusishwe katika Wizara mtambuka; aidha liwepo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Wizara yoyote ambayo tayari inaweza kujumuisha maeneo haya yote ambayo mlemavu huyu anatakiwa ahudumiwe.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu kwenye Hotuba ya Rais alipofungua Bunge, nilizungumzia suala zima la mgawanyo wa rasilimali katika Taifa letu. Mataifa mengi Duniani yameingia katika migogoro mikubwa, yameingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kutokuwa na mgawanyo rasmi wa rasilimali katika Taifa hilo; hili nililizungumza. La kusikitisha, Serikali imekuwa kiziwi na pofu juu ya hoja hizi. Wabunge wengi hapa wanazungumza; kuna Mikoa kadhaa ambayo tayari inaonekana kwamba, iko nyuma katika maendeleo na siyo leo ni muda mrefu, kila Mbunge ambaye anatoka katika maeneo hayo anazungumzia juu ya hoja hiyo, lakini Serikali bado imeweka pamba katika masikio yake, haitaki kusikiliza kilio cha Wabunge waliotoka katika Mikoa hiyo.

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kuijenga amani ambayo inazungumzwa katika Bunge humu, isiwe hoja ya kinafiki kuzungumzia habari ya amani. Amani lazima iwe ya kweli, tutafute vyanzo vya msingi ambavyo vinaweza kuondoa amani yetu, tutafute vyanzo vya msingi ambavyo vinaweza kupelekea kutoka katika amani yetu. Haiwezekani leo Lindi ukawa ni Mkoa wa mwisho katika Bajeti ya Taifa hili. Siyo kwamba, Lindi tunahitaji maendeleo mapya, hapana; Lindi ndiyo ulikuwa Mji msifika, Mkoa msifika, wenye ustawi na maendeleo kabla ya Uhuru wetu; nani hajui hilo?

Lindi tulikuwa na mashamba ya Mkonge kumi na sita, wakati ule yaliwekwa na mabepari, leo mnawaita wawekezaji wale.

Mheshimiwa Spika, leo yako wapi Mashamba ya Mkonge Lindi? Kulikuwa na reli kutoka Nachingwea kwenda Mtwara, Waingereza waliona umuhimu wa uchumi katika Mkoa wa Kusini wakajenga Bandari ya Mtwara, wakajenga Reli ya Nachingwea, leo haipo! Ndani ya utawala wa miaka hamsini wa Chama chetu, tayari Reli hiyo imeng’olewa haipo katika Mikoa ya Kusini; nani hajui hilo?

Ndugu zangu, Lindi kulikuwa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, labda Wabunge wengine hamjui hilo; ndege ilikuwa inatoka Cairo, Misri transit Lindi, Johannesburg, Afrika Kusini kule, ilikuwa Lindi ya miaka hamsini hiyo; iko wapi Lindi yetu leo?

Mheshimiwa Spika, tumuulize nani, kuna watu wanakuja wanasema hapa eti miaka hamsini CCM haijafanya kitu; kwa nini watu wa Lindi wasiseme kwamba uchumi wao umedhoofishwa ndani ya miaka hamsini ya Uhuru wa Taifa letu?

Tulikuwa hatuna haja na Dar es Salaam, sisi tulikuwa tuna import na ku-export bidhaa mbalimbali kupitia Bandari ya Lindi. Lindi ilikuwa inang’aa Mji mzima kwa taa za usiku. Mimi katika maisha yangu zaidi ya miaka kumi katika utoto wangu, sikujua kama umeme unakatika, lakini leo kunakuja kauli kwamba, kuna mgao wa umeme; nini mgao wa umeme?

Mheshimiwa Spika, nilikuwa China juzi nikawaeleza kwetu kuna tatizo la umeme, huku mnasemaje? Wakasema sisi zaidi ya miaka ishirini, thelathini, hata nukta moja umeme kwetu haujakatwa; siyo miujiza ni kweli. Kuna haja ya kufanya mjadala wa Kitaifa sasa.

Watanzania wana fikra, wana mawazo, tushirikiane sasa katika kuiona Tanzania yetu inakwendaje katika kujiletea maendeleo. Kuna hoja hapa ambayo tayari inazagaa juu ya stakabadhi ghalani; stakabadhi ghalani Waheshimiwa ni taarifa ambayo Serikali inapata upande mmoja; bado Serikali haijahusisha wadau katika hoja nzima ya stakabadhi ghalani mpaka sasa miaka hamsini ya Uhuru, mkulima mpaka anafika katika meza ya mnunuzi wa bidhaa yake, hajajua bei ya bidhaa yake leo ni bei gani. Miaka hamsini ya Uhuru leo, mkulima anakopesha kilo tano za ufuta analipwa baada ya miezi mitatu kwa bei ya majaliwa; tunampeleka wapi mkulima huyu?

Mheshimiwa Spika, kuna soko, Wananchi wanaliona lakini wanaambiwa chini ya mtutu wa bunduki kwamba, huruhusiwi kwenda kuuza pale, soko lako ni lile. Kuna haja ya kukaa na wadau, kuna Wabunge wawakilishi wa Wananchi, kuna Wizara ya Kilimo, tukae tujadili mstakabali wa wakulima, siyo kauli ya Kilimo Kwanza ambayo tayari Wananchi bado hawaoni manufaa yake. Huu ni wakati mwafaka sasa Watanzania kukaa kutengeneza mjadala wa Kitaifa juu ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la ahadi za Rais. Ahadi za Rais siyo kitu cha kukifanyia mchezo; Rais ni mtu mwenye heshima kubwa, Rais anatarajiwa na Wananchi wake, Rais ni Kiongozi ambaye kauli yake ina thamani mbele ya Wananchi tena zaidi ya sheria, kauli ya Rais siyo kitu kidogo. Rais na Marais waliopita, wametoa ahadi kadhaa kwa Wananchi kupitia kampeni za uchaguzi na kupitia ziara mbalimbali, lakini tukiangalia ahadi nyingi bado hazijatekelezwa.

Rais ameahidi Soko Kuu la Mkoa, ameahidi mandhari ya Lindi, ameahidi maji katika mtandao wa Lindi na mambo chungu mzima; bado miaka mitatu anamaliza mkataba wake wa Urais, hakuna hata moja ambalo limetekelezwa na Serikali. Kwa nini tuseme Serikali yake inamdharau Rais wao? Kwa nini tusijenge hoja hiyo? Kama ninyi mnamdharau Rais wenu; watu wengine wa kawaida wanafanyaje katika hilo? Rais ameahidi Wananchi wakampa kura nyingi, kulikuwa na wagombea wengi wa Urais lakini walitoa kura zao kwa mujibu wa ahadi ambayo Wananchi walikuwa na matumaini nazo, ahadi za Rais ziko wapi leo? Tumeambiwa hapa kwamba, tutaishughulikia Bandari ya Lindi, nimeangalia katika Bajeti sioni Bandari ya Lindi iko wapi.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nizungumzie suala la ajira. Majeshi yetu; Polisi na Magereza ni Majeshi ya Kitaifa, yana sura ya Kitaifa, lakini imefikia mahala sasa nafasi hizi zinatolewa kwa wateule wachache; ni watu wachache tu ambao tayari wamekumbatia dhamana hiyo kwa kutoa ajira kwa watu ambao wako karibu nao. Mashaka yangu, tutakuwa na Jeshi la Polisi, tutakuwa na ulinzi, tutakuwa na Majeshi ya Polisi, ambayo tayari yatakuwa na tabaka katika Taifa letu, yatakuwa majeshi ambayo yanatoka katika eneo moja tu la nchi yetu. Nini hatima yake; ni majeshi ambayo yanatoka kwa mujibu wa Kanda. Leo ukiwa RPC Lindi, ukiwa OCD Mtwara, tayari unaita watu wa kwenu huko kuna nafasi zimetoka njoni nikupeni ajira huku. Hilo lipo, watu wananung’unika, manung’uniko ya Wananchi tusiyalazie damu, Wananchi wananung’uka sasa hivi kila kona wanainung’unikia Serikali yao, wakulima wanainung’unikia Serikali yao, wanafunzi wananung’unika juu ya Serikali yao. Kila kona, tukae tutengeneze mjadala wa kitaifa, tunalinusuru vipi taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nisipoteze muda, yangu yalikuwa hayo. Ahsate kwa kunisikiliza.