| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 3 | 10 February 2011 | Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais | ||
Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni mara yangu ya kwanza katika Bunge lako Tukufu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Spika, kabla ya yote niwashukuru kwanza wapiga kura wa Jimbo langu la Lindi Mjini, wamenipa heshima kubwa, heshima ya kihistoria, pamoja na heshima yangu lakini pia na heshima ya Jimbo la Lindi Mjini. Ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Mlemavu ambaye ametokana na kura za wapiga kura wenyewe, hili limeleta heshima katika Taifa letu. Mheshimiwa Spika, pia nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa familia yangu na wale wote ambao waliniunga mkono katika harakati zangu zote za kisiasa. Pia niwashukuru viongozi wangu wa chama ambao wamenipa malezi mazuri mpaka kufika hapa nilipofikia leo. Mheshimiwa Spika, moja kwa moja nianze hoja yangu juu ya suala zima la hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwanza katika hili nimpongeze, ni hotuba nzuri, hotuba ambayo imejaa matumaini makubwa. Lakini katika yote nianze katika neno moja muhimu sana, tangu tumefika katika Bunge hili hapa la Kumi bado inaonekana kwamba hoja ya amani ni hoja ya kundi dogo la watu. Inaaminika kabisa kwamba tunazungumzia suala la amani, inaonekana kwamba suala la amani ni vitisho kwa Watanzania, kwamba Watanzania wakae katika tahadhari juu ya amani, lakini suala zima la amani halipo katika watu wachache tu, suala la amani ni la Watanzania wote. Mheshimiwa Spika, suala la amani lichukuliwe kama ni ajenda katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maendeleo yao. Taifa hili lina miaka 50 ya uhuru (makumi matano), nusu karne, amani hii imetumikaje katika kuwaletea maendeleo Watanzania? Kwa miaka 50 ya uhuru ambayo tayari tunayo, haikuwa sahihi kwenda kuomba kura kwa Mtanzania eti kwa ahadi ya maji! Miaka 50 ya uhuru bado tunakaa tunazungumzia habari ya amani, amani, Watanzania wana matatizo chungu nzima, wanatarajia Bunge hili likae, litatue matatizo ya msingi ambayo Watanzania wanakabiliana nayo. Miaka 50 ya uhuru tunashuhudia jinsi gani mgawanyo wa rasilimali unavyojenga matabaka katika Taifa letu. Tunaona jinsi gani mauaji katika nchi hii yanavyoendeshwa ni kwa sababu bado Serikali haijajipanga katika kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi yetu zinawafikia watu katika maeneo husika. Mheshimiwa Spika, suala zima la Upinzani, tayari imejengeka kwamba Upinzani ni uadui katika Taifa, hii ndio dhana ambayo imejengeka katika Taifa letu. Upinzani si uadui, ni utaratibu wa kistaarabu wa kugawana madaraka katika Taifa. Leo nchi ambazo zinatufadhili, nchi ambazo zinatusaidia duniani kote, chukua mfano Amerika, wapo ndani ya demokrasia ya Vyama Vingi zaidi ya miaka 200 na ndio Taifa kubwa na tajiri duniani. Ni utaratibu wa kistaarabu kabisa kugawana madaraka katika Taifa na utaratibu ambao tayari unajenga amani katika dunia kwa sababu watu wanasubiri tu baada ya miaka mitano sera zako zimetekelezwa kwa kiasi gani. Ni utaratibu wa kistaarabu, ni utaratibu wa kiungwana kabisa. Isifikiriwe kwamba kukubalika kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa katika Taifa letu basi tayari ni uadui mkubwa. Tujaribu kujenga taratibu maalum, tuwaelekeze Watanzania kwamba suala zima la kuwepo kwa Mfumo wa Vyama Vingi katika Taifa letu, ni utaratibu wa kiungwana. Tunabadilishana madaraka, wananchi wanapewa mamlaka ya kufanya lile ambalo wao wanaona kwamba kwa kufanya hivi ndiko kutawaletea maendeleo katika Taifa letu. Mheshimiwa Spika, nizungumzie mgawanyo wa rasilimali katika nchi. Imeonekana katika nchi yetu … Mheshimiwa Spika, utaniongeza muda wangu kidogo. Mheshimiwa Spika, nafasi ya mgawanyo wa rasilimali katika nchi yetu tayari imeonekana kwamba maeneo mengi katika nchi hii ni wachangiaji wakubwa katika pato la Taifa letu lakini ni kwa namna gani katika maeneo hayo wananufaika na rasilimali hizo? Ni mpango gani ambao Serikali umeuandaa kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi yetu zinatoa maslahi katika maeneo husika? Mheshimiwa Spika, leo katika maeneo ya Mikoa ya Kusini, tayari kuna rasilimali za kutosha, tuna gesi ya Songosongo, kuna gesi ya Mnazibay, ni rasilimali ya kutosha kwa maendeleo ya watu wa Kusini. Tuna gypsum ambayo tayari inatengeneza saruji lakini maeneo yale yako nyuma katika sekta zote kwa sababu uchumi wake uko chini katika sekta zote, nenda katika sekta ya afya, elimu ni maeneo ambayo yako nyuma. Mheshimiwa Spika, jana hapa kumezungumzwa katika Bunge lako Tukufu kwamba kuna Hospitali za Rufaa katika nchi yetu na yameelezwa maeneo ambako hospitali hizo zipo lakini haikuonyeshwa kwamba Kusini Hospitali ya Rufaa iko wapi? Katika sekta ya elimu imezungumzwa hapa kuna Vyuo Vikuu Dar es Salaam, Iringa, Morogoro, Dodoma na katika maeneo mbalimbali lakini baada ya miaka 50 ya uhuru wetu bado hatujaona maendeleo ya elimu katika maeneo ya Kusini. Hii ni kuonyesha kwamba pamoja na rasilimali zilizokithiri katika maeneo yale lakini bado wananchi wa Mikoa ya Kusini hawajanufaika na rasilimali zao. Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ambayo tayari Mheshimiwa Rais ameeleza, kusimamia na kugawanya rasilimali katika nchi, Bunge hili la Kumi, safari hii lihakikishe kwamba linapeleka maendeleo katika Mikoa ya Kusini. Hii itasaidia kujenga Umoja wa Kitaifa na itasaidia kuleta amani katika nchi yetu. Yale maeneo ambako sasa hivi kuna migogoro katika nchi nyingi ni kutokana na kukosekana kwa mgawanyo rasmi wa rasilimali katika nchi zao. Chukulia leo Sudan ya Kusini na sehemu zingine, ukiangalia ni sababu za kiuchumi hasa ambazo zinapelekea kutokuwa na amani katika nchi zao. Hivyo Bunge letu hili lihakikishe kwamba linajenga utulivu ndani ya Bunge hili kwanza kama Wabunge, ningetarajia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wamsaidie Rais na sisi Wabunge ambao sio wa Chama hicho, tutakuwa tayari kumsaidia Rais katika kuhakikisha kwamba mipango ambayo ameisimamia, tumeisimamia sote kwa pamoja. Kwa sasa inaonekana dhahiri tayari kuna mgawanyiko ndani ya Mawaziri, ndani ya Bunge, sasa sisi Wabunge ambao hatupo ndani ya Chama, tunapata maelekezo kutoka wapi? Mheshimiwa Spika, Watanzania wanatutazama huko, mamilioni ya Watanzania wenye matatizo ya msingi wanajiuliza, je, Bunge letu linafanyaje, Bunge letu linazungumza nini juu ya hali ya maisha yetu. Watanzania ni maskini, umaskini wa Watanzania umekithiri. Tunazungumzia hapa habari ya njaa, miaka 50 ya uhuru Watanzania leo hawana hakika ya kula kwa siku ya leo. Hivyo wana matarajio makubwa Watanzania na sisi kuhakikisha kwamba tunaisimamia Serikali, tunaielekeza Serikali na ndio wajibu wetu sisi kama Wabunge, hatukuja hapa na Vyama vyetu, kazi ya Chama imemalizika kule juu, Watanzania wametuleta hapa kama Wabunge kwa ajili ya utetezi wa maisha yao. Hivyo, suala zima la kusema kwamba mimi CUF, CHADEMA, CCM halitopata nafasi katika Bunge hili. Hivyo, ni vyema sasa tukawahakikishia kwamba tupo hapa kwa ajili yao. Mheshimiwa Spika, mimi nimepigiwa kura Lindi sio na Wanachama wangu tu, naamini nyote pia, Wanachama wa Vyama vya Siasa wako wangapi, ni wachache. Watanzania sasa wameondokana na dhana ya Vyama vya Siasa, Watanzania wanaangalia nani anaweza kuwaletea maendeleo na ndio msimamo uliopo sasa hivi huko nje, hivyo tunawashangaza, tunawastaajabisha kwamba tuko nje ya dhamira ya Watanzania. Tuongoze katika Bunge lako, tumia Kanuni, Taratibu ili kukidhi matakwa ya Watanzania leo. Hali si nzuri, matokeo ya mtihani wa shule za msingi na sekondari ni mabaya, ni Taifa la kesho lile. Tunawaandaje na Serikali tunaisukumaje kusimamia maendeleo ya elimu katika nchi yetu? Tunasimamia vipi vijana ambao leo wapo vijiweni, vijana wanavuta bhangi huko, wamekosa mwelekeo wamekata tamaa ndani ya Taifa lao, tuzingatie hilo. Mheshimiwa Spika, nina hoja nzito kabisa, tuweke picha hapa mbele yetu sasa itakayoonyesha taswira ya Mtanzania ambaye tunamsemea kuonyesha yukoje kule nje ambao tumekuja hapa kwa ajili yao. Watanzania wanateseka huko nje, mauaji ya Albino ambayo tayari yametuletea aibu katika Taifa letu, yalipoteza maisha ya watu wengi sio kwamba Albino wameathirika katika mauaji yale, Albino amezaliwa na wazazi na wazazi ndio wameathirika, wengine walikuwa ni tegemeo kwa watu wale. Haya yote Bunge linatakiwa likae katika Bunge la Kumi, litengeneze mazingira bora, miaka 50 ya uhuru sio kipindi kidogo kama kweli tuna dhamira ya kuleta maendeleo. Nchi zingine ambazo leo wanatufadhili hapa ni miaka 10 tu baada ya uhuru wao wameendelea, walichagua mambo, wakayapa kipaumbele. Mheshimiwa Spika, nashukuru sana |
|||||