| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 4 | 14 June 2011 | Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2011/2012 – 2015/2016 | ||
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kupewa nafasi hii ili niweze kuchangia Mpango wa Miaka Mitano. Kabla sijaingia kwenye mada, ninapenda nitoe shukrani nyingi kwa wote walioshiriki kuandaa Mpango huu, tunauita Mpango wa Kitaifa. Sentence ya kusema kwamba ni Mpango wa Kitaifa, mimi binafsi imenifurahisha sana kwa sababu kila mmoja atatakiwa awajibike kwa kufuata Mpango huu wa Kitaifa. Ninapenda nisisitize kuwa, ninaiomba Serikali kwamba, kwa kuwa huu ni Mpango unaolenga madhumuni makubwa na umeweka vipaumbele kwa undani na kila mmoja inabidi ausome na auelewe ili tuweze kutimiza hii miaka yetu mitano, tunaondokane na hali ngumu ya umaskini. Sasa nilikuwa ninaomba tupate copy nyingi sana za Kiswahili, kwa sababu Mpango huu utakwenda katika Wilaya zetu na Kata zetu, wataweza kusoma kila mmoja aelewe tunakwenda wapi. Mheshimiwa Spika, ninaomba nijikite kwenye vipengele ambavyo vimeoneshwa katika Mpango huu. Tukiangalia kipengele kinachohusiana na masuala ya kilimo; katika Mpango huu masuala ya kilimo yameelezwa kwa undani sana. Sehemu kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo. Ninashukuru sana katika Mpango huu tumeweza kuelezea kwa undani kuhusiana na kilimo, lakini kuna jambo moja ambalo ninapenda niliongelee, nalo ni kwamba katika Mpango huu kuna mambo yanatakiwa yaoneshwe ili kukiimarisha kilimo. Kwa mfano, ndani ya miaka mitano, Mpango bado haujafafanua ni kiasi gani katika nchi yetu ya Tanzania tutakuwa na viwanda vya mbolea ili kuondokana na tatizo kubwa la upandaji wa bei ya mbolea. Wananchi wengi sana katika vijiji vyetu hivi sasa tunakabiliana na tatizo kubwa la upandaji wa bei kwa upande wa mbolea. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango wangu, kuhusu kipengele cha Kilimo kwanza, ili tuweze kufikia mahali lengo letu litimie, jana ulisema kuna matrekta yameshaletwa kwa ajili ya kukopesha wakulima na bahari nzuri sana, Wananchi wangu wameanza kunipigia simu wanataka wapate mwongozo unaojieleza vizuri kuhusu ukopeshwaji wa matrekta ili tuondokane na kilimo cha mkono. Kwa hiyo, ninashukuru sana. Pili, nilikuwa ninaomba niongelee masuala ya barabara. Katika Mpango wetu wa Miaka Mitano, imeshaoneshwa kabisa kwamba, barabara katika Wilaya kadhaa zitakuwa za kiwango cha lami. Hilo ni suala la msingi kabisa katika maendeleo yetu; ili tuendelee nchi yetu inahitaji kuwa na viwanda vinavyojitosheleza, viwanda vinavyozalisha. Sasa nilikuwa ninajaribu kupitia katika Mpango huu, nimeangalia katika Mkoa wa Iringa, nikajikita moja kwa moja kwenye Wilaya yangu ya Mufindi; Mufindi kuna viwanda vingi sana ambavyo vimejitosheleza katika uzalishaji mali wa kitaifa. Kwa mfano, ukienda kule, tuna Kiwanda cha Chai ambacho ni kikubwa katika Afrika; tuna Kiwanda cha Karatasi kikubwa sana katika Afrika; tuna Viwanda vya Mbao na Misitu ya kutosha kabisa. Tatizo linalotufanya tusiweze kuzalisha vizuri ni la lami. Tuna barabara moja inayotoka katika Kijiji cha Nyololo, imepita kwenye mashamba ya chai, ninadhani katika Kijiji cha Igowole, ikaenda Kijiji cha Kibao, imekatiza imekwenda mpaka katika Kiwanda cha Mgololo. Hii barabara katika Mpango wa Mkoa, tumeweza kukaa kwenye vikao vyetu vya RCC tumejadili na kila anayetoka Mkoa wa Iringa ukimwuliza lazima ataongelea Barabara ya Mufindi kuweka kiwango cha lami. Sasa katika Mpango huu, nimejaribu kuusoma nikaona barabara hiyo haijawekwa na bahati nzuri sana kama sisi Wabunge tumekaa tunaujadili na mimi nikiwa Mbunge ninayetoka kule, lazima niweke kipaumbele katika Barabara ya Mufindi kwani ni muhimu sana kwa uzalishaji wa Kitaifa. Suala la pili, ninaomba niongelee masuala ya Viwanja vya Ndege. Viwanja vya Ndege, Mpango huu umeeleza vizuri kabisa, lakini bado kuna Viwanja vya Ndege ambavyo ni muhimu sana. Kuna Mjumbe mmoja jana alieleza vizuri sana, alisema katika Mpango lazima tuangalie Kitaifa, lakini tunashuka katika Mkoa, tunashuka katika Wilaya. Katika Mkoa wa Iringa sisi tuna viwanda vya ndege viwili. Sasa nimesoma katika Mpango huu kuna Kiwanja cha Ndege cha Nduli, Kiwanja cha Ndege cha Njombe, hakijaguswa kabisa na tusipokiweka kwenye Mpango, maana yake ndani ya miaka mitano hivi viwanja havitashughulikiwa. Tumetaja Viwanja vya Ndege ambavyo vilikuwa vinapewa pesa, lakini viwanja vyetu hivi vya Iringa na Njombe bado havijawekwa kwenye Mpango. Ninaiomba Serikali ivishughulikie viwanja hivi, ione kwamba ni viwanja muhimu na ukizingatia Mkoa wa Iringa ni Mkoa ambao una neema kubwa; tuna Ruaha National Park, tuna kilimo cha maua na sasa hivi tuna Bonde la Mgololo ambapo kilimo cha umwagiliaji kinaendelea. Sasa bila kuwa na Viwanja vya Ndege ambavyo vinajitosheleza, tutaweza kushindwa kusafirisha hata mazao yetu kupeleka nje. Suala la pili, ninaomba nijikite kwenye elimu. Ninashukuru sana kwenye Mpango huu, kipengele cha elimu kimeelezwa vizuri sana. Jana nimesikia kwamba, kila Wilaya tutajaribu kujenga Vyuo vya Ufundi. Vyuo vya Ufundi ni sahihi, vinasaidia sana vijana wetu wale ambao wanashindwa kufaulu kwenda Vyuo Vikuu, lakini tunapata changamoto kubwa sana ambayo nimeiona katika mwaka huu. Ukiangalia idadi ya wanafunzi wanaomaliza Form Four, wamefeli mtihani; sasa tukisema kwamba kila Wilaya itajenga angalau chuo kimoja bado hakitoshi. Mimi nilikuwa ninapendekeza kuwa, kila Tarafa iwe na Chuo cha Ufundi ili vijana wetu wanaoshindwa kuendelea na masomo ya juu waweze kupata elimu ya ufundi. Sisi Wabunge hili ni tatizo kubwa, kwa sababu tukipita katika Kata zetu, tunapata changamoto kubwa sana, vijana wetu hawana kazi, mpaka sasa hivi wako mitaani. Kwa hiyo hivi vyuo vinasaidia sana kuepusha wimbi kubwa la vijana ambao wanakaa mitaani bila kazi. Suala lingine ni la ajira kwa vijana. Taifa letu sasa linaingia changamoto kubwa sana kwa ajili ya vijana na katika Mpango huu bahati nzuri wameeleza kwamba, ajira ya vijana itazingatiwa. Bahati mbaya hawajaelezea tuna vijana wangapi wanamaliza katika Vikuo Vikuu na wangapi tunategemea ifikapo mwaka 2015 watakuwa wameshapata ajira. Hivi sasa changamoto hii inatukabili na ukiangalia vijana wengi wamemaliza vyuo vikuu hawana kazi. Hii ndiyo baadaye itatuletea shida; hawa vijana watashindwa maisha na ili kuwapa maisha ni lazima kila mmoja afanye kazi. Tukitaka ku-create employment kwa vijana wetu, ni lazima tuimarishe viwanda vyetu vifanye kazi na bahati nzuri Serikali imeanza kuchukua jukumu la kuingiza Wahisani waweze kuanzisha viwanda ili kusaidia vijana wetu wapate ajira. Hii bado haitoshi, inabidi viwanda vinavyokufa vifufuliwe. Serikali ijikite sana kwenye viwanda ili vijiana wetu waweze kuajiriwa. Mwisho, ninapenda nijikite katika masuala ya maji. Masuala ya maji yanaongelewa sana. Ninashukuru sana, Wizara ya Maji katika Mpango wa World Bank, kwenye Jimbo langu la Mufundi Kusini, nimeshachimbiwa visima kumi na huo ni Mpango mzuri ambao Chama cha Mapinduzi kimeanza kuutekeleza. Kwa hiyo, ninashukuru sana, isipokuwa ninapenda niongezee kwamba, vile visima vimeshachimbwa lakini bado havijawekwa mabomba na hatujui yatawekwa lini. Mpango ni mzuri., nadhani ndanii ya miezi mitatu Wananchi wataanza kupata maji safi na salama. Kwa kuwa kengele imeshagonga, ninaomba nimalizie kwa kusema kwamba, katika Mpango huu wa Miaka Mitano ili tuweze kufikia mahali pazuri, Viongozi wote; Wabunge na Mawaziri, tuwajibike kwa pamoja. Tuungane pamoja, tushirikiane katika kuutekeleza Mpango wetu tuliojiwekea wenyewe ili ikifika miaka mitano tukianza kupima Mpango wetu tumetekeleza vipi, kila mmoja anakuwa na majibu yake. Tukianza kuoneshana vidole itakuwa siyo sahihi. Mpango huu unamgusa kila mtu na bahati nzuri umeeleza kwamba, huu Mpango utakwenda mpaka vijijini na utamgusa mtu wa chini kabisa. Tukitaka kupata maisha bora ni lazima wote tufanye kazi, kuanzia Wabunge, Madiwani, matangazo ya vijiji na watu wotem lazima tusimame tufanye kazi. Tukinyoosheana vidole, itafika mwaka 2015 kila mmoja atamwuliza mwenzake, lakini hakuna mtu atakayetoa jibu. Kwa hiyo, ninaomba nisisitize kwamba ni Mpango wa kila mtu. Lengo kubwa ni kuondokana na umaskini na kunyanyua uchumi. Kitu kingine ambacho huwa sikipendelei sana, sisi Waafrika tuna tabia ya kuwasifia wenzetu wa nje, wale wenzetu wa nje wanafanya kazi kubwa sana; kwa nini na sisi tusijitume tufanye kazi kama wale? Ninaona muda umeshafika, tujitume tufanye kazi kama wao, kila mmoja anajua utandawazi umezagaa kila kona, kwa hiyo, lazima tufanye kazi kama inavyotakiwa. Mheshimiwa Spika, mchango wangu ni huu. Ninaomba niunge mkono hoja. |
|||||