You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 4 11 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kutoa mchango rasmi, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuingiza kwenye historia ya Taifa hili kwamba safari yangu kufika hapa ilikuwa ndefu kidogo, ilianza mwaka 2005 lakini kwa sababu ya udhaifu wa mifumo yetu ya Kikatiba na ya Kisheria ya usimamizi wa haki, safari hii imekuwa ya miaka mitano na nimefika leo hapa kwa nguvu ya umma.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii, kuwashukuru sana wazee wa Jimbo la Ubungo bila kujali tofauti za Vyama, Jimbo lenye wapigakura 450,000 ambao waliona wanitume mtoto wao nije kuwawakilisha.

Mheshimiwa Spika, vilevile nawashukuru akina mama wa Jimbo la Ubungo, wanawake ambao katika kipindi kigumu sana cha kampeni walikuwa wakiniombea kwa Mwenyezi Mungu na leo nimefika hapa salama.

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi, niwashukuru vijana wenzangu wa Tanzania nzima na Jimbo la Ubungo. Vijana wa mtaani, vijana wafanyakazi na vijana wa Vyuo Vikuu ambao walikuwa tayari kukesha kwa siku tatu kulinda ushindi mpaka tukatangazwa. Ahadi yangu kwao ni kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitano cha utumishi wangu.

Mheshimiwa Spika, leo tunavyozungumza ni wakati pekee sana kwenye historia ya Taifa letu. Tunazungumza ikiwa ni miezi michache kuelekea kuadhimisha miaka 50 toka Taifa letu lipate uhuru. Lakini tunazungumza wakati ambapo Taifa linakabiliwa na mgawo wa umeme. Miaka 50 baada ya uhuru, Taifa likikabiliwa na matokeo mabovu ya wanafunzi. Miaka 50 baada ya uhuru, Taifa linakabiliwa na kupanda kwa hali ya juu kwa gharama za maisha ambako kunasababisha tishio la migomo mbalimbali. Migomo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu tunazungumza leo wakiwa wamerudishwa nyumbani kwenye Vyuo mbalimbali, migomo ya wafanyakazi na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, mambo haya yangeweza kutupa sababu ya kukata tama lakini mimi ninayo sababu ya kuwa na matumaini. Nina matumaini kwa sababu tupo kwenye chombo hiki na natarajia kwamba hatutaendekeza itikadi na maslahi ya Vyama badala yake tutasimamia maslahi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na upungufu wake, Ibara ya 63 inasema kwamba hiki ndiyo chombo kikuu kwa niaba ya wananchi waliotutuma, chenye wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, naomba nieleweke tu hapa, tunapokosoa, tunapounga mkono, ni sehemu ya kuishauri na kuisimamia Serikali. Natarajia kwamba, Wabunge kwa umoja wetu, hatutajigeuza kuwa na jukumu la Serikali, badala yake tutaendelea kuwa na jukumu la kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba niishauri Serikali, kwa kweli ili tuweze kufika Desemba 9, tukiadhimisha uhuru tukiwa na sababu ya kuadhimisha uhuru kwa maana ya kusherehekea, lazima Serikali iamue kwa dhati, Bunge lijalo la mwezi Aprili, lilete mapendekezo ya msingi wakati tunatengeneza vipaumbele vya bajeti ya safari hii. Ni mambo gani ya haraka ambayo kama Taifa tunaweza tukafanya kwa umoja wetu, kwa makubaliano yetu ili ikifika Desemba, pamoja na yote yaliyojitokeza miaka 50 iliyopita, tuseme walau hapa tuna sababu ya kujivunia na nitasema machache.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Rais na nitaichangia kwa uchache wa maneno. Rais amezungumzia vipaumbele mbalimbali, ukurasa wa 12 na 13, amegusia suala la umoja wa kitaifa na hili ni jambo ambalo hatupishani kwa sababu hata Ngao ya Taifa letu inasema Uhuru na Umoja. Lakini kuna jambo moja napenda nitoe tahadhari, suala la udini. Hotuba ya Rais ukurasa 12 inasema kwamba Tanzania ni moja, watu hawabaguani, kwa hiyo, Tanzania hakuna mgawanyiko hata wa kidini lakini ukurasa wa 13 anasema kuna mpasuko wa kidini. Mimi naomba vyombo vya Ulinzi na Usalama, vikamshauri Rais kwamba kadri viongozi wa juu tutakavyoendelea kupiga kelele nyingi sana za udini, ndivyo kadri tunavyopandikiza mbegu ya udini kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuja kwenye kikao hiki, nimezunguka vijiweni, nimekaa vijiweni, Watanzania ni wamoja kweli kweli, viongozi tusije tukawa ndiyo tunasababisha mgawanyiko miongoni mwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nichangie eneo lingine, Rais amezungumzia kuhusu kukuza uchumi na ukurasa wa 15 amezungumzia suala la kupanda kwa bei ya mafuta kwenye Soko la Dunia na chakula kama sehemu ya matatizo ya kimaisha ambayo yalitokea mwaka 2007. Mimi naomba tu Serikali ituletee taarifa Bungeni kuhusu hali halisi. Takwimu hapa kwa mujibu wa hotuba ya Rais, inaonyesha kwamba mfumko wa bei ni asilimia 4.2. Wakati Rais anazungumza, bei ya sukari kilo moja ilikuwa Sh.1,200/=, leo tunazungumza kilo moja imepanda mpaka kufikia Sh.2,000/=. Gharama za maisha zinapanda kwa Ari, Kasi na Nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ikatuletea pendekezo la namna gani Tanzania inakabiliana na tatizo hili la kupanda kwa gharama za maisha. Tunaweza kuwalaumu wanafunzi kwa nini wanagoma kwamba wanalipwa Sh.5,000/= lakini wanalalamika, bei ya chakula inapanda! Sasa kuwalaumu wafanyakazi kwa nini wanalalamika, wanataka kuandamana, bei ya umeme imepanda, kama hatutadhibiti kupanda kwa bei, tunatengeneza mgogoro kwenye Taifa.

Mheshimiwa Spika, Rais amezungumzia kuhusu kufufua viwanda, niseme tu kwamba kazi hii ni nzito, inahitaji vilevile kama Taifa tuzungumze, hivyo viwanda vilivyokufa vilikufaje? Mimi pale Jimboni kwangu Ubungo kuna Kiwanda cha Urafiki ambacho mwanzoni Tanzania ilikuwa inakimiliki, sasa hivi ina hisa 49 peke yake. Kiwanda kinaelekea kufa na sasa hivi ninavyozungumza, wafanyakazi wamepewa likizo, tena wamepewa likizo kwa asilimia 50 tu ya malipo. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili la Urafiki nitaliletea maelezo kwa sababu ni suala la kina sana, kuuzwa kwa mitambo na kadhalika nitawaletea maelezo.

Mheshimiwa Spika, niingie kwenye eneo la msingi ambalo ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Ubungo, nayo ni maji. Mheshimiwa Rais, amezungumza kuhusu ongezeko la mgawo wa fedha za bajeti kwenye maji na amezungumza kuhusu Miradi ya Benki ya Dunia lakini mimi nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Maji na nimwahidi tu kwamba tulifanya Kongamano la Maji, tarehe 31 Ubungo, tukayajua matatizo na nitaleta taarifa kamili kwake kama ambavyo tumekubaliana na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano, tunahitaji, pamoja na mipango ya muda mrefu ya ujenzi wa mabwawa ya Kidunda, miradi ya Kimbiji, Mpera na kadhalika…

Mheshimiwa Spika, nashukuru.