| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 9 | 21 June 2011 | Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2011 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2011/2012 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 | ||
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuchangia kwenye Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2011/12 kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, ninaomba niainishe mambo machache, ambayo ningependa kujikita nayo kwenye kuchangia Bajeti iliyopo mbele yetu. Mheshimiwa Spika, kwanza, ninapenda kuchangia kwenye kipaumbele namba mbili, yaani maji. Kiasi cha shilingi bilioni 621.6 zilizotengwa kwa ajili ya maji ni kidogo sana, ukilinganisha na mahitaji ya maji katika Nchi yetu Tanzania. Tunavyosema “Maji ni Uhai” tunamaanisha kwa vitendo. Ninachelea kuona inawezekana kabisa hata hizo asilimia zinazotakiwa zipate maji kwa mwaka huu, zisipate hata kile kidogo. Mheshimiwa Spika, wanawake wanapata tabu sana kufuata maji mbali na maeneo wanayoishi; hivyo, kuwafanya muda mwingi kupotea katika kutafuta maji, ambapo maji yangekuwa karibu na maeneo, wangeweza pia kufanya shughuli zingine za kilimo na kadhalika. Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Serikali kwa kuwaona Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga, kwa kuweka Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria. Naishukuru na kuipongeza Serikali kwa asilimia 200. Mheshimiwa Spika, kasoro zilizoko kwenye Mradi huu ni kwamba, Mradi umelenga kuwasaidia Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, lakini ninaona ni Mradi wa kuwanyonya Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga. Ninasema hivyo kwa sababu kuna mamlaka mbili za maji ambazo zote ni mali ya Serikali, yaani KASHUWASA na SHUWASA, maana KASHUWASA ni Mradi ambao unatoa maji Ziwa Victoria na kuleta Shinyanga huku msambazaji ni SHUWASA. Kwa nini Serikali isiipe mamlaka moja tu kufanya kazi zote ili kupunguza gharama? Mheshimiwa Spika, suala la maji liangaliwe kwa mapana yake na hasa tukiangalia mwanamke ndiye mhanga wa suala hili pande zote za nchi yetu. Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Nina wasiwasi na mfumo mzima wa ulipaji wa VAT hasa kwa Mwananchi mmoja mmoja. Wengi wa Wananchi hawajui umuhimu wa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani. Ninasema hivyo kwa sababu wafanyabiashara wengi wamekuwa wakisaidia wanunuzi wasilipe Kodi ya Ongozeko la Thamani (VAT). Utakuta mfanyabiashara anamwambia mnunuzi kuwa, bei hii ukitaka risiti na bei hii kama hutahitaji risiti. Hii maana yake ni nini? Ni watu wangapi nchini wanacheza huu mchezo na kukosesha nchi mapato? Ningependekeza wafanyabiashara waelezwe umuhimu wa kodi kwa Taifa na wasiangalie faida zao tu. Mheshimiwa Spika, mwisho, ninapenda kuongelea kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168. Sheria hii ikipita, traffic wote watapiga makofi kwa kucha. Sheria hii itaongeza kwa kiwango kikubwa sana; hakuna mwananchi au dereva atakayeweza kulipa shilingi 50,000 kama traffic notification fee, wakati walikuwa wanashindwa shilingi 20,000 na kuwafanya wawe wanatoa shilingi 5000 – 10000 kwa traffic ili waachiwe. Mheshimiwa Spika, shilingi 50,000 ni kubwa mno, hapa traffic atapata Sh 10,000 – 15,000 kwa kosa moja; hili hakuna asiyejua. Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali ibatilishe Sheria hii ili kunusuru mianya ya rushwa ambayo inaweza kulichafua Jeshi letu la Polisi. Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, ninaomba kuwasilisha. |
|||||