| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 9 | 21 June 2011 | Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2011 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2011/2012 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 | ||
Mheshimiwa Spika, ninachangia kupitia maandishi katika Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2011/2012. Bajeti hii kwa kadiri nilivyoipitia ni ya kisanii, ambayo haitoi majibu ya hali ngumu na mfumko wa bei, inayowakabili Watanzania maskini. Mheshimiwa Spika, ukiangalia bei ya petroli duniani, ambayo inatumika kama sababu ya kupanda wa gharama za maisha ni ndogo mara dufu, ukilinganisha na bei ya petroli hapa nchini. Hii inatokana na kodi kubwa ya Serikali na tozo nyingi kwenye bidhaa hiyo muhimu nchini. Ninashauri Serikali kama kweli inataka kumsaidia Mtanzania maskini wa vijijini na mjini, waondoe kabisa kodi kwenye bidhaa ya mafuta ya petroli na kufuta tozo nyingi zilizojaa kwenye bidhaa hiyo ili Watanzania waweze kufaidi uhuru wao walioupigania kwa trakriban miaka 50 sasa. Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado inaendelea kukumbatia aibu ya Wananachi wake kuishi katika nyumba za makuti katika maeneo mengi ya Tanzania, nchi iliyojaa kila aina ya rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu hakufanya makosa kuziweka Tanzania. Ninaishauri Serikali isimamie kwa uadilifu matumizi bora ya rasilimali zetu na kuzuia hongo na rushwa ndani ya mikataba na kwenye sekta zilizozunguka rasilimali zetu. Rasilimali zilizojaa ndani ya nchi yetu zikitumika vyema, hatutahitaji kukopa mikopo ya aibu, iliyojaa kila aina ya dhuluma kwa Watanzania. Mheshimiwa Spika, ninashauri Serikali iache mpango wa kukopa ovyo kwenye mabenki ya kibishara na ijielekeze katika kusimamia matumizi bora ya rasilimali zetu ili kutoa unafuu kwa maisha ya Watanzania. Bajeti hii bado imekuwa ni tegemezi, kwa kiasi kikubwa tukiwategemea wahisani kwa masuala yote ya maendeleo na kiasi kikubwa cha fedha kikipelekwa katika masuala ya utawala na uendeshaji wa nchi. Huduma za kilimo, pamoja na misamiati ya muda mrefu kwamba, kilimo ndiyo utu wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, imetengewa kiasi kidogo sana cha fedha. Mheshimiwa Spika, bado kwa bajeti hii Tanzania itaendelea kushikilia mkia kwa kuendelea kuongoza kuwa miongoni mwa nchi maskini Duniani. Utatengeneza barabara na kuweka miundombinu, lakini kama wananchi hawapati maji safi na salama, wataendelea kutumia maji yaliyochanganywa na kinyesi kwa matumizi ya nyumbani huku tukiendelea kuzika Watanzania wasio na hatia kutokana na maradhi ya kipindupindu, malaria na typhoeid. Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mchango wangu katika Bajeti hii ya Mwaka 2011/2012. Ninaomba kuwasilisha ila mambo mazuri hayataki haraka, lakini chelewa chelewa utakuta mtoto si wako. |
|||||