You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Abama, Mwanamrisho Taratibu Maalim[CHADEMA]

Special Seat
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 4 14 June 2011 Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2011/2012 – 2015/2016
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchukua fursa hii, kutoa maoni yangu kwa maandishi, ila nitachangia katika sehemu mbili; miundo mbinu, yaani nishati na huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati bado imekuwa ni tatizo katika nchi yetu ambayo inafanya kuwa kikwazo cha maendeleo ya nchi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, kwenye Kamati yetu tuliongea na Wadau mbalimbali na tukaishauri Serikali kwa kupeleka maoni kama Kamati kuhusu tatizo la umeme kwa hatua ya sasa ya muda wa kati na muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya sasa ni kutafuta mbadala wa kutegemea umeme kutokana na maji ya Mtera, kwa sababu mwisho wa siku lile bwawa litakauka, kwani miongo ya mvua inabadilika siku hadi siku. Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano haukuelezea njia mbadala ya kuiokoa nchi yetu katika suala hili ambalo ni kubwa sana, ambalo linashusha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusitumie njia mbadala ya kutumia nishati ya umeme wa mawimbi ya bahari, pamoja na gharama kubwa, lakini faida yake ni kubwa na wataalam wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za jamii, suala la kumkomboa mwanamke ambaye ni mhimili mkubwa sana kwa Taifa, Mpango haukuonesha unamsaidia vipi mwanamke na haki zake. Wanawake wa vijijini wanapata manyanyaso wanapofiwa na waume zao na kwa sababu sheria hawaifahamu, ndiyo maana wanakosa haki zao. Mpango ulipaswa uchambue kila kipengele cha sekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango pia ulitakiwa uelezee jinsi ya kumsogezea mwanamke huduma muhimu kama vile hospitali, shule, Vikundi vya SACCOS na kumpunguzia masafa marefu ya kutafuta maji. Mpango haukuonesha ni jinsi gani tatizo la maji katika vijiji litatatuliwa kwa kuchimba visima, kwani hali za wanawake zinatia huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Mpango ni mzuri kwa Maendeleo ya Taifa, ila pamoja na mambo mazuri hayataki haraka, lakini pia chelewa chelewa utakuta mtoto si wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.