| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 6 | 15 February 2011 | Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete | ||
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mungu, kwa kutupa uhai na kutukutanisha tena katika Bunge hili Tukufu. Nichukue nafasi hii, kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kuteuliwa kwake tena kuwa Waziri MKuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii, kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Umeweka rekodi ya kuwa Spika wa kwanza mwanamke katika Bunge hili na kuonesha kuwa wanawake tunaweza. Tunakuombea kwa Mungu azidi kukupa afya ili uliongoze Bunge hili kwa amani na utulivu bila ubaguzi wowote, ukiamini Wabunge wote humu ni Wawakilishi wa Watanzania na Watanzania wanategemea kuona sisi tunawawakilisha vipi na tunawatetea vipi. Mheshimiwa Spika, nitakuwa siyo mwingi wa fadhila nisipoweza kuwashukuru Wananchi wa Mpanda, Jimbo la Mpanda Mjini. Nawashukuru sana kwa uamuzi wao wa busara wa kumchagua Mheshimiwa Said Amour Arfi kuwa Mbunge. Ninawaomba wazidi kumwombea ili awatumikie kwa kutatua kero za Wanampanda. Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye kuchangia Hotuba ya Rais, lakini hapa nitaongelea vipaumbele 13 alivyovieleza Mheshimiwa Rais. Naomba niongelee kipengele namba tisa, kinachoongelea kuongeza jitihada za kupanua, kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii hususan afya, maji, umeme, barabara na kadhalika. Mheshimiwa Spika, nianze na afya. Jitihada hizi za kupanua na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii, zimeleta mgawanyiko mkubwa baina ya Watanzania wa mjini na vijijini. Watanzania waishio vijijini wanaumia sana na kupoteza maisha kwa kukosa huduma muhimu za kijamii. Wananchi vijijini wanajitolea sana kuchangia Serikalini lakini hawapewi kipaumbele kwa kufikishiwa huduma muhimu za kijamii. Mfano, Wananchi hao wanajitolea sana katika ujenzi wa zahanati na majengo ya madarasa, lakini unakuta Serikali haiangalii kupeleka wafanyakazi vijijini wala dawa za kutosha. Unakuta zahanati ina muuguzi mmoja; huyo huyo ndiyo mkunga; je, Wananchi hawa wanaishi vipi? Wakati Serikali inategemea kipato kutoka kwa wanakijiji hao hao, ambao ndiyo wakulima na wafugaji. Mheshimiwa Spika, tukija upande wa barabara; Serikali inaweka kipaumbele mijini na siyo vijijini ambako ndiyo mazao ya chakula na biashara yanatoka. Hali hii haimwendelezi mkulima wa kijijini ambaye anashindwa kutoa mazao na kuyafikisha sokoni kwa sababu ya ubovu wa barabara. Je, hapa kweli tunakuza uchumi wa Mtanzania hasa mkulima wa kijijini ambaye anasomesha watoto wake katika Shule za Kata ambazo hazina walimu wa kutosha, maabara, wala vitabu vya kutosha? Je, kuna haja ya kusema Watanzania wote ni sawa na wanastahili kupata huduma sawa? Mheshimiwa Spika, kwa hali hii; Serikali inaandaa Taifa gani la baadaye? |
|||||