You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Madabida, Zarina Shamte[CCM]

Special Seat
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 4 11 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeniwezesha kufika hapa. Lakini pia nawashukuru sana wapigakura wangu akina mama wa Mkoa wa Dar es Salaam walioniwezesha kufika hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba nami, kwa sababu ni mara ya kwanza nisimame hapa, basi nikupongeze wewe kwa kuwa Spika wa kwanza mwanamke. Namwomba Mwenyezi Mungu akuzidishie, akupe kila lililokuwa la heri katika kuendesha Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa hotuba yake nzuri na mwelekeo. Nina hakika ni baada ya kazi nzuri ya miaka mitano wakaona wamchague tena na kweli wameona jinsi alivyojipanga kuweza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama chetu pamoja na kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata mafanikio. Ninampongeza sana. Mpango wa Baraza la Mawaziri inaonekana fika kabisa kwamba Serikali imejipanga vizuri sana katika kutekeleza vipaumbele vyote 13 ambavyo ameviweka.

Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa subira, kwa sababu hapa katikati pamekuwa na vuguvugu kubwa sana, migomo na kila aina ya fujo. Lakini, Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu wamekuwa na subira na hatimaye leo tunaona kama subira inataka kuzaa matunda kwa maneno ambayo Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani aliyoyatoa kwamba yanatoa matumaini badala ya kusema kwamba nchi isitawalike, sasa tunasema itawalike na ifanye kazi ambayo wananchi wanaitarajia. Tunatarajia kuanzia leo tutakuwa wamoja na wote tutafanya kazi ambayo tumetumwa na wananchi wa Tanzania kuifanya.

Mheshimiwa Spika, naomba niangalie vipengele vitatu, vinne katika hotuba ya Mheshimiwa Rais. Naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuanzisha na kubuni mkakati wa Kilimo Kwanza. Tunafahamu sisi sote kwamba asilimia karibu 80 ya wananchi wa Tanzania wanashughulika na masuala ya kilimo ikiwa ni pamoja kulima nikimaanisha na ufugaji. Ninampongeza Rais kwa kuliona hilo na kusema kwamba sasa hivi kutakuwa na Benki ya Wakulima kwa sababu wakulima kwa kipindi kiredu sana, mimi ni mkulima mmojawapo, tumekuwa tukihangaika mahali gani pa kwenda kutafuta unapoweza kupata mkopo ili kujiendeleza kwa wote wenye mashamba makubwa na wenye mashamba madogo madogo.

Mheshimiwa Spika, nafikiri sasa hivi itakuwa ni fursa nzuri ya kuweza kuendeleza kilimo chetu. Nami naomba Serikali katika mipango yake iangalie wakulima wote. Tunaposema ukulima wa kumwagilia maji, basi uwaguse mpaka wale wakulima wadogo na tuwatumie wakulima wakubwa kuwasaidia wakulima wadogo kwa sababu huyu mkulima ambaye amezoea kulima na jembe na kuangalia rehema ya Mwenyezi Mungu ya maji, lini mvua itanyesha, ndiyo kama tunavyoiona kwamba sasa hivi kila unakopita mazao yamekauka.

Ili kuhakikisha kwamba basi matunda hayo yanapatikana kwa wote, basi tusiwasahau wakulima wadogo wadogo, tufanye kila njia ili kusudi na wenyewe washiriki.

Mheshimiwa Spika, tukitumia Kilimo Kwanza, tunaweza tukaondoa hata ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Vijana wengi sana sasa hivi hawana ajira. Nikisema vijana ninamaanisha wanawake kwa wanaume. Kilimo Kwanza inaweza ikatoa jawabu kwa sababu gani, kama Serikali inaweza ikaandaa mpango ambao wanaweza kuwatayarishia mashamba kwa sababu kumwambia kijana sasa hivi nenda kalime wakati hana mtaji, hana ardhi, hajui ataanzia wapi, inaweza kuwa ni mtihani mkubwa sana.

Lakini ikiwa Serikali itajipanga, tunaweza tukaondoa ukosefu wa ajira kwa vijana wetu kwa kuwatayarishia mashamba na kuhakikisha wamepewa sehemu za kuweza kulima na kuwapa mbegu bora. Lakini, siyo hilo tu, nilikuwa ninaangalia suala zima la ukulima kwa akinamama. Sisi wa mijini, kwa kweli hatuna mashamba na kama tunayo ni vihamba vidogo vidogo. Lakini tunao ukulima wetu ambao ni mkubwa ambao ni ufugaji wa kuku wa kisasa na wa kienyeji. Ninaomba suala hilo liangaliwe.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda, ninaomba vijana hawa ambao wanamaliza vyuo, elimu yao na vyeti vyao ndiyo iwe dhamana ya mikopo ambayo wanaweza kupewa ili waweze kufanya shughuli za kujikimu.

Mheshimiwa Spika, nataka nisimalize kabla sijagusia elimu. Napongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuangalia suala la elimu. Kwetu sisi tunasema kwamba gari liko njiani, unajiuliza umewekewa chai na mkate, uanze nini? “Uanze Sai, uanze nkate?” Unatakiwa uanze chai kwa sababu mkate utakwenda kula ndani ya gari. Ndiyo Serikali ilichofanya ni kwamba shule zimejengwa, wasingeweza kufundisha walimu ambao baadaye watakwenda wapi? Kungekuwa na maneno kwamba wametumia hela nyingi, wamefundisha walimu, hakuna mahali pa kupeleka. Lakini, sasa hivi tumekunywa chai, sasa tunatafuna mkate wakati tuko ndani ya gari, walimu wanafundishwa. Nina hakika kwamba sasa hivi kwa maneno tuliyoyasikia kwa Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake, basi walimu wanakuja.

Mheshimiwa Spika, naomba nigusie kidogo kuhusu amani kabla time yangu haijakwisha. Amani jamani na maadili ya kwetu, sasa hivi vijana wengi wamekosa maadili. Sisi humu ndani ya Bunge na wazazi wanaponisikia ninawaomba tuwarudishe watoto wetu katika maadili. Tanzania hatuna jadi ya watoto kuwatukana wakubwa, kudharau wakubwa. Kwa hiyo, mimi ninaomba hizi ni tabia ambazo sisi wazazi tunaweza tukakemea na tunaweza tukarudisha maadili ya watoto wetu wakarudi kule ambako tulikuwa. Siyo jadi ya Watanzania watoto kufanya fujo, ni kisiwa cha amani, tusichoshwe na amani. Baba wa Taifa alituambia tusichoshwe na amani, hiyo ndiyo nguzo yetu kubwa. Ninaomba ndugu zangu tuendelee. Kambi ya Upinzani leo imetoa tumaini, natumaini watawaambia vijana hii njia mliyokuwa mnatumia siyo sahihi.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.