| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 3 | 1 | 5 April 2011 | Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa UNESCO wa Kulindwa kwa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika wa 2003 | ||
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hili Azimio. Kwa kuwa leo ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu basi na mimi ninaomba nimshukuru sana Mungu aliyeniwezesha kufika mahali hapa. Pili, napenda kuchukua nafasi hii pia kuwashukuru wananchi wa Geita walioniamini na kunituma mahali hapa, zaidi nawashukuru akinamama wa UWT Mkoa wa Geita kwa kunichagua kwa kura nyingi sana wakiamini kwamba nitakuja kuwawakilisha sawa sawa. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa namna ya pekee tena kwa kuwa nimepata nafasi hii. Kwanza kabisa niwaombe Wabunge wenzangu tuunge mkono hoja hii asilimia mia moja, ninasema hivyo kwa sababu nilichokiona hapa kinalenga kutusaidia Watanzania kwa hali ya juu sana. Kwa kuchangia zaidi ningependa nijielekeze moja kwa moja kwenye kipengele kimoja kinachohusu muziki, hapa ninamaanisha muziki wa kisasa na muziki wa asili. Mheshimiwa Spika, sanaa inaleta maendeleo makubwa sana katika nchi yetu hasa tukianzia sisi wenyewe majumbani kwetu, lakini kwa kuwa bado tuna hali ngumu wanamuziki na hasa burudani ya muziki kwa kifupi na hawa watu wa ngoma za kiasili na kwa kuwa tuna nafasi nzuri hii ya kujiunga na hawa UNESCO, tukijiunga na UNESCO ninaamini kabisa tutaweza kubadilisha baadhi ya vitu ambavyo vinatukwamisha. Mheshimiwa Spika, mataifa mengine yaliyoendelea wana nafasi nzuri sana hasa katika muziki na shughuli zingine mbalimbali. Wanamuziki wenzetu walioendelea huko duniani wanafanikiwa sana hata akitoa wimbo mmoja, wanafanikiwa kwa kufanya nini? Wanafanikiwa kwa sababu akitoa wimbo mmoja unapigwa ule muziki na ukipigwa anaweza kuwa analipwa percent fulani kutokana na hiyo kazi hata kama hajafanya album nzima. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mimi naongea kwa mara ya kwanza na kwa sababu mtoto anapoanza kuongea huwa anaanza na neno “ba” baadae anakuja kuunganisha inakuwa “baba” inakamilika kuwa sentensi nitaomba nieleweke kwa kuwa ndiyo kwanza ninaanza kuongea kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu. Mheshimiwa Spika, naomba katika maandalizi haya ya kuingia katika huu mkataba niombe basi wazingatie kitu kimoja ambacho kitatusaidia sisi wasanii wa muziki pamoja na ngoma hizi za asili kwamba kila wakati inapotokea muziki umepigwa mahali popote au vikundi vya ngoma vimetumbuiza mahali popote au umepigwa katika redio ama katika television, basi wakiongezee hiki kipengelee kwamba wawe wanapata percent fulani wale walioandaa hiyo kazi, ili iweze kuwa-motivate zaidi kuendelea kufanya kazi. Mheshimiwa Spika, kwa haya machache naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja, asante. |
|||||