You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Mgalu, Subira Khamis[CCM]

Special Seat
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 6 15 February 2011 Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa maandishi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na wapigakura ambao ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT kwa kuniwezesha kuwa Mbunge wa Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Kikwete na Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hivyo kupata ridhaa ya kuendelea kushika dola.

Mheshimiwa Spika, pia nakupongeza sana kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili la Kumi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajielekeza katika kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri aliyoitoa iliyojikita kwenye vipaumbele 13 vilivyotokana na Mkataba wa Chama cha Mapinduzi na wananchi, yaani Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Mchango wangu utajielekeza zaidi kwenye kipaumbele Na. 7 juu ya: “kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele Na. 7 ni muhimu sana kikatiliwa mkazo. Katika kupitia ukusanyaji mkubwa wa mapato, Serikali itaweza kutekeleza vipaumbele vingine vyote mfano, kupitia mapato, Serikali itatoka huduma bora ya elimu, afya maji na uwezeshaji wa wananchi na kadhalika.

Ni kweli ulio wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imeongeza sana jitihada katika kukusanya mapato. Hata hivyo, bado ipo mianya ya uvujaji na ubadhirifu katika mapato yanayokusanywa, vitendo vinavyofanywa na watumishi wasiokuwa waaminifu hasa katika Serikali za Mitaa. Naipongeza sana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa jitihada zao katika ukusanyaji mapato na kuweza kuvuka lengo kila mara.
Mheshimiwa Spika naiomba Serikali ya Awamu ya Nne kuendelea kudhibiti vitendo vya hujuma dhidi ya mapato yanayokusanywa na Halmashauri zetu. Pamoja na nia nzuri ya uboreshaji na ukusanyaji mapato kupitia mawakala hasa katika adhima ya kupinguza gharama za kukusanya mapato kupitia watendaji, bado utaratibu huu umechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mapato kutokana na Mawakala kukosa uaminifu. Mikataba ya ukusanyaji mapato humnufaisha zaidi Wakala kuliko Halmashauri husika kama ilivyojitokeza kwenye mkataba wa ukusanyaji mapato wa kituo kikuu cha mabasi ya kwenda Mikoani, Ubungo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, naiomba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kuangaliwa upya utaratibu wa ukusanyaji mapato kupitia Mawakala hasa juu ya faida na hasara zake kwa kulinganisha utaratibu wa zamani na ikiwekezakana Serikali izishauri Halmashauri mbalimbali kuacha utaratibu wa kutumia Mawakala katika ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali za Mitaa ziimarishe vitengo vya mapato kwa kuajiri wataalam waaminifu na kufanya tafiti za vyanzo/uwezo wa Halmashauri husika katika ukusanyaji wa mapato kabla hawajaingia mkataba na wakala na ukusanyaji mapato.

Mheshimiwa Spika, katika suala la kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, naunga mkono msimamo huu wa Mheshimiwa Rai wetu kwani ni miaka mingi sasa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mapungufu ya nidhamu katika matumizi ya pesa za Serikali hasa katika Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana hatua ya Serikali kuanzisha Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa ndani ambapo Wakaguzi Wakuu wa hesabu wa Ndani wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa watawajibika kwake moja kwa moja.

Wakaguzi Wakuu wa Hesabu wa Ndani ni wadau muhimu sana katika usimamizi wa matumizi ya pesa za umma hasa katika Serikali za Mitaa. Pia nawashauri Waheshimiwa Madiwani katika eneo la usimamizi wa raslimali fedha.

Mheshimiwa Spika, nashauri:-
(i) Serikali iwezeshe zaidi Ofisi mpya ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani kwa kupitia raslimali fedha na rasilimali watu ili iweze kutekeleza majukumu yake;

(ii) Serikali Kuu ihakikishe vitengo vya ukaguzi wa ndani katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa inaimarishwa kirasilimali fedha na watu ili kitengo cha ukaguzi wa ndani kijitegemee;

(iii) Serikali iendelee kuimarisha na kiwezesha Ofisi ya CAG kwa kuipa uwezo wa kuajiri na rasilimali fedha ili iweze kutekeleza majukumu yake kiufanisi ya usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali; na

(iv) Serikali ichukue hatua madhubuti mara kwa mara katika kutekeleza mapendekezo ya Ripoti ya CAG na za Wakaguzi wa ndani ili kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa watendaji inapodhibitiwa kuwa kuna ubadhirifu wa pesa za umma.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.