| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 17 | 1 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa | ||
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii nami niweze kuchangia angalau kwa maandishi kuhusu Bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2011/2012. Mheshimiwa Spika, napenda kujielekeza zaidi kuhusiana na hali ya njaa kwa mwaka huu ambapo maeneo mengi ya nchi yetu hususan ukanda wa Ziwa Victoria kwenye Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza ambapo hapajapatikana chakula cha kutosha. Nafahamu kuwa Shinyanga kuna maghala ya chakula, lakini maghala hayo yanategemea kuletewa nafaka kutoka maghala yaliyoko Kusini mwa nchi yetu pamoja na Dar es Salaam. Napenda kushauri kuwa Serikali ihakikishe chakula cha kutosha kinapelekwa kwenye maghala hayo ya Shinyanga mapema ili kiweze kuwafikia kwa urahisi wananchi pale kitakapotakiwa kugawiwa. Hata hivyo, kuna dalili ya wafanyabiashara wasio waaminifu wameanza kuvusha chakula kidogo kilichopatikana katika maeneo haya kukisafirisha kwenda nje kwenye nchi jirani ya Kenya kwa njia za panya. Tunaomba Serikali ifanye kila iwezalo kuidhibiti hali hiyo hadi hapo tutakapokuwa tumevuka kutoka kwenye janga hili. Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa linaloikumba nchi yetu katika Sekta ya Uchukuzi ni ukosefu wa reli ya uhakika kutoka Dar es Salaam kwenda bara. Sina hakika kama kuna njama ya makusudi ya kuiua reli inafanywa na wafanyabiashara wa barabara ili isifanikiwe, lakini reli ndiyo njia muhimu ambayo inaweza kupunguza gharama katika kusafirisha bidhaa kwa Mikoa ya bara, lakini kwa jinsi inavyosuasua, kwa hakika inafanya watumiaji wa vifaa vya viwandani na kutoka nje waliyoko kanda ya Ziwa wawe na maisha ya ghali sana. Mheshimiwa Spika, pia abiria wanaotegemea reli ni wale wanaoishi kwenye maeneo ambapo barabara hazifiki. Sasa wafanyeje? Hata hivyo, reli ya kati pia inahitajika sana kwa biashara na uchumi wa nchi za ukanda wa Maziwa Makuu. Nasikitika kusema kuwa Tanzania tumeshindwa kabisa kuitumia vyema fursa hii tuliyopewa na Mungu. Mheshimiwa Spika, sasa wananchi wamechoka kusikia mipango tu ya kwenye karatasi ambayo haitekelezwi kwa vitendo ya kuifufua na kuimarisha reli ya kati. Nahitaji maelezo ya kutosha kwanini reli ya kati haiamki? Mheshimiwa Spika, Madiwani ndio wasaidizi wa karibu sana wa Wabunge. Hata hivyo posho wanazolipwa Madiwani wa Tanzania ni ndogo sana kiasi cha kufanya wasifanye kazi zao kwa ufanisi. Naomba Madiwani warekebishiwe sheria ili nao walipwe mishahara kama ilivyo kwa Wabunge. Madiwani kwa mazingira ya kazi zao, wanahitaji sasa vyombo vya usafiri ili kuwafikia wananchi ambao ufahamu wao na uelewa juu ya haki zao umeongezeka sana. Wananchi wanahitaji Madiwani wachacharikaji na wanaofuatilia shughuli za maendeleo na huduma za jamii kwa karibu. Bila usafiri na kuwaboreshea mishahara na posho, itakuwa vigumu kufanya kazi yao vema. Vinginevyo hata wale Madiwani wazuri watakuwa wanaachwa wakati wa uchaguzi kwa kushindwa kuwafikia wapiga kura wakati siyo kosa lao. Naomba sana suala hili la maslahi ya Madiwani liangaliwe upya ili Madiwani wetu waweze kuendana na mahitaji halisi ya jamii kwa sasa. Mheshimiwa Spika, ili uchumi wa Tanzania uweze kukua na watu wengi waweze kuboresha maisha, ni muhimu sana Serikali ikajielekeza kwenye kuimarisha uchumi wa akina mama na vijana. Pesa inayotengwa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Maendeleo na Vijana na kupitia Serikali za Mitaa, bado ndogo mno kuweza kuleta matokeo chanya katika jamii ya Watanzania milioni 40 sasa. Mheshimiwa Spika, hata tatizo la ajira linalopigiwa kelele na Wabunge wengi lingeweza kupungua iwapo Serikali ingeendelea kuanzisha na kuimarisha makundi ya kujitegemea ya vijana na wanawake na kuyapa maarifa zaidi ya ujasiriamali na ubunifu. Ina maana makundi haya yangeweza kushiriki kiushindani ndani na nje ya nchi na hivyo kuongeza kasi ya uchumi. Taasisi kama vile SIDO na VETA ni za muhimu sana katika dhana hii ya kuwawezesha akina mama na vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wote. Hivi kwanini Serikali isiiangalie njia hii ya mkato ya kupunguza umasikini katika jamii? Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba nisisitize juu ya dhamira ya Serikali ya kuupatia mji wa Bariadi maji ya kutosha kutoka Ziwa Victoria. Mpango huu uko katika ahadi za Rais. Lakini umuhimu wa mpango huu ni kuwa utatoa huduma ya uhakika kwa wananchi wa Mkoa mpya wa Simiyu pamoja na vijiji vingi ambapo mradi huu utapitiwa. Pia tunaomba Halmashauri za Wilaya zisisitizwe kutenga fedha ya kutosha ili kujenga mabwawa kwa ajili ya binadamu na mifugo ili kupunguza kero kubwa iliyopo hususan katika Wilaya za Busega, Bariadi, Meatu na Maswa. Lakini pia fedha inayotengwa kwa kazi hiyo ya maji ni muhimu ikasimamiwa vema ili kuwe na kazi inayoendana na thamani ya fedha. Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja. |
|||||