You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Nchimbi, Dr. Emmanuel John[CCM]

Songea Mjini Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
3 1 5 April 2011 Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa UNESCO wa Kulindwa kwa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika wa 2003
WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO:

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu, likubali mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa Kulindwa kwa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika wa 2003 (Convention for the Safeguarding of the Intagible Cultural Heritage, 2003).

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie fursa hii, kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Spika, Naibu Spika Job Ndugai na Wenyeviti wa Kamati. Kipekee, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kuchaguliwa kwao katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba 2010, ambao ulikuwa mgumu, huru na wa haki.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge wa Peramiho, kwa maelekezo na michango yao waliyoitoa wakati wa kujadili Azimio hili wakati wa vikao vilivyofanyika baina ya Kamati na Wizara yangu, kati ya tarehe 22 na 28 Machi 2011. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kwamba, michango yao tunaithamini na pia tutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa kutoa maelezo kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba uliokusudiwa, ambao ninaliomba Bunge lako liweze kuridhia.

Mheshimiwa Spika, usuli wa Mkataba wa UNESCO wa Mwaka 2003 wa Kulindwa kwa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika (Convention for the Safeguarding of the Intangible Cultural Heritage, 2003) ni Mkataba wa UNESCO wa Mwaka 1972 wa Kuhifadhi Urithi wa Kiutamaduni wa Asili wa Ulimwengu (Convention for the Protection of the World Cultural and Natural Heritage).

Mkataba huo ambao Tanzania imeshauridhia na hivyo kuwa mshirika wake, unahusika na urithi wa kiutamaduni unaoonekana kwa macho na kushikika kama vile majengo na makazi ya zamani na pia urithi wa asili kama vile mabonde, milima na mbuga za uoto na wanyama. Tanzania inayo maeneo saba yanayotambuliwa Kimataifa na kulindwa chini ya Mkataba huu, yaani:-

1. Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
2. Mji Mkongwe wa Zanzibar.
3. Michoro ya Mapango ya Kondoa (Kondoa Rock Art Sites).
4. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
5. Hifadhi ya Serengeti.
6. Hifadhi ya Kilimanjaro; na
7. Hifadhi ya Selous.

Mheshimiwa Spika, japo Mkataba huu wa Mwaka 1972 ulihusisha maeneo muhimu sana ya urithi wa kiutamaduni, ilibainika kuwa, haukugusa kabisa urithi wa kiutamaduni usioshikika, ambao Tanzania inao kwa wingi. Urithi usioshikika ni ule unaorithishwa kwa mapokeo ya kusimuliana kwa mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hujumuisha utambaji wa hadithi; vitendawili; sanaa za maonesho kama vile michezo ya kuigiza, ngonjera, uimbaji wa mashairi na tenzi, majigambo na kadhalika; lugha; matambiko; ujuzi; na ufundi wa jadi kama vile uganga wa jadi.

Mkataba huu wa Mwaka 2003 umedhamiriwa kuutambua urithi wa kiutamaduni usioshikika na kuweka taratibu za kuulinda kwa kuwa ni sehemu muhimu ya utamaduni wa ulimwengu. Mkataba huu una jumla ya ibara (Articles) 40. Napenda kuchukua fursa hii, kuelezea vipengele vichache muhimu zaidi vya Mkataba huu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ibara ya kwanza ya Mkataba huu inaelezea madhumuni yake ambayo ni pamoja na:-

(i) Kulinda urithi wa kiutamaduni usioshikika.
(ii) Kuhakikisha urithi huo unaheshimiwa.
(iii) Kuinua utambuzi wa urithi huo miongoni mwa jamii husika, kitaifa na kimataifa.
(iv) Kutoa fursa ya kushirikiana na kusaidiana kimataifa katika kulinda urithi wa kiutamaduni usioshikika.

Kila nchi mshirika wa Mkataba huu, haina budi kuweka taratibu na kanuni za kulinda na kuendeleza urithi wa kiutamaduni usioshikika, ikiwa ni pamoja na kutengeneza orodha ya urithi wa kiutamaduni usioshikika uliomo ndani ya mipaka yake.

Mheshimiwa Spika, ibara ya pili inahusu fasili au ufafanuzi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika. Urithi wa Utamaduni Usioshikika ni mapokeo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Urithi huo siku zote huundwa na jamii, makundi na wakati mwingine, mtu mmoja mmoja kwa mujibu wa mazingira na historia inayotoa hamasa ya kuwa na utambulisho na kuwa endelevu. Jamii hazina budi kuhamasishwa juu ya umuhimu wa urithi wa kiutamaduni usioshikika kitaifa na kimataifa.

Mheshimiwa Spika, ibara za nne na tano za Mkataba huu zinahusu vyombo vya maamuzi. Mkataba huu una vyombo viwili vikuu vya maamuzi, yaani:-

(i) Mkutano Mkuu wa Wanachama wote, ambacho ndicho chombo cha juu zaidi.
(ii) Kamati ya Utendaji yenye Wajumbe 18 ambao watachaguliwa kutoka miongoni mwa Wawakilishi wa Nchi Wanachama. Wajumbe wa Kamati wataongezeka kufikia 24 pindi nchi Wanachama wa Mkataba zitakapofikia 50.

Taratibu za uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji pamoja na majukumu ya Kamati hiyo zimefafanuliwa katika ibara ya (6) na (7).

Mheshimiwa Spika, ibara za 19 – 24 zinahusu ushirikiano wa Kimataifa. Mkataba huu unahimiza Nchi Wanachama kushirikiana, kusaidiana na kujalizana uzoefu katika harakati zote za kulinda na kuhifadhi urithi wa kiutamaduni usioshikika. Mashirikiano yanaweza yakahusu: Ubadilishanaji wa mbinu za kutunza urithi huo; upatikanaji wa wataalam; utoaji wa mafunzo kwa watumishi; ujengaji wa miundombinu; utoaji wa vitendea kazi na ujuzi wa kuvitumia; na utoaji wa aina nyingine ya misaada ya kifedha na kiufundi.

Mheshimiwa Spika, ibara za 25 - 28 zinahusu Mfuko Maalum. Mkataba huu unaunda Mfuko wa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika (Intangible Cultural Heritage Fund), kwa ajili ya kusaidia umuhimu wa majukumu yaliyoainishwa katika Mkataba wenyewe. Nchi washiriki wa Mkataba huu, zinaweza kuomba msaada kutoka katika Mfuko utakaoundwa. Taratibu zimewekwa bayana katika Mkataba wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Mkataba huu pia umezungumzia masuala mengine ya msingi yatakayoweza kufanikisha utekelezaji wake. Masuala hayo yanahusu Haki za Binadamu, uhusiano na Mikataba mingine, umuhimu wa kujiunga na Mkataba, Matokeo ya kujiunga na Mkataba, utaratibu wa kujiunga na Mkataba, gharama za kujiunga na Mkataba, Mawasiliano na Wadau na Maoni yao kuhusu Mkataba na namna ya utekelezaji wa Mkataba wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Haki za Binadamu, Mkataba huu unasisitiza haki ya kila jamii kufurahia utamaduni wake pasipo kubaguliwa au kuzuiliwa. Mradi kwa kufanya hivyo, jamii haikiuki Haki za Binadamu. Kwa mfano, mila zinazonyanyasa watu wa jinsia fulani au kutesa watu wa umri fulani, haziwezi kutetewa eti kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa jamii maana mila hizo zinakiuka Haki za Binadamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uhusiano na Mikataba mingine, Mkataba huu hauathiri uhalali wala umuhimu wa Mkataba wa Kuhifadhi Urithi wa Kiutamaduni na wa Asili wa Ulimwengu wa Mwaka 1972. Tanzania tayari ni mshirika wa Mkataba huo na haina budi kuendelea kuutekeleza kwa kuwa malengo yake yanajitegemea.

Mheshimiwa Spika, maelezo juu ya umuhimu wa kujiunga pia yametolewa. Kwa mujibu wa Ibara ya 32 ya Mkataba huu, kila Nchi Mwanachama wa UNESCO anahitajika kuridhia Mkataba huu. Tanzania ni Mwanachama wa UNESCO na ilishiriki katika mikutano kadhaa iliyoandaa na kupitisha Mkataba huu; kwa hiyo, haina budi kuridhia kama ilivyokuwa wajibu wa wanachama wote. Mkataba huu ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa unalenga kuzisaidia Nchi Wanachama kulinda tamaduni zake na kunufaika na tamaduni hizo pasipo kukiuka Haki za Binadamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matokeo ya kujiunga na Mkataba huu ni kwamba, kutaiwezesha Tanzania kutumia fursa zifuatazo:-

- Kushirikiana na nchi nyingine duniani kulinda utamaduni wake na wa nchi nyingine kwa uwazi pasipo shinikizo la kisiasa au kiuchumi. Kwa mfano, Tanzania inaweza kutumia vipengele vya Mkataba huu kuamua ni asilimia ngapi za matangazo yote ya redio na televisheni yawe ni ya Kitanzania (muziki, filamu, lugha na kadhalika) ili kulinda utambulisho wake. Hatua za namna hii ni muhimu katika kuendeleza utamaduni wa taifa pasipo kufunga kabisa milango kwa tamaduni za nchi nyingine.

- Kupata fursa ya kuchagua na kuchaguliwa kuongoza vyombo vya kimataifa vinavyoundwa na Mkataba huu, hususan Kamati ya Utendaji na Mfuko wa Fedha uliopo.

- Sheria za nchi kama vile Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki zitapata msukumo wa Kimataifa kupitia mkataba huu wa mwaka 2003.

- Kunufaika na utaalamu na fedha zinazopatikana chini ya Mkataba huu, hasa Mfuko wa Urithi wa Kiutamaduni Usioshikika (Intangible Cultural Heritage Fund).

Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kujiunga na Mkataba, Ibara ya 32 ya Mkataba huu, inazitaka nchi zinazotaka kujiunga zifanye hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Katiba yenyewe. Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndilo lenye madaraka ya kujadili na kuridhia Mikataba ya Kimataifa kama huu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na gharama za kujiunga na Mkataba huu; ziko za aina tatu. Kwanza, ni ile michango ya kila mwaka ambayo ni kiasi kisichozidi asilimia moja ya mchango wa kila mwaka kwa UNESCO. Kiasi hiki ni sawa na Dola za Marekani mia moja na themanini na tatu. Pili, ni gharama za utekelezaji wa Mkataba ambazo zitakuwa ni sehemu ya bajeti za Idara na Mashirika ya Serikali yatakayokuwa yameainishwa kutekeleza Mkataba huu. Aina ya tatu ya gharama ni michango ya hiari ambayo inaweza kulipwa na Tanzania kwa Mfuko ulioanzishwa na Mkataba endapo uwezo utaruhusu. Utekelezaji unaweza kuanza kwa kutumia Bajeti ya sasa ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mawasiliano na Wadau na maoni yao juu ya Mkataba huu, Wizara yangu ikiwa katika mchakato wa kuandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu pendekezo la kuridhia Mkataba huu, iliwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni na ushauri wao. Wadau hao ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Sheria na Katiba, Wizara ya Maliasili na Utalii (Idara za Mambo ya Kale na Makumbusho ya Taifa), Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ofisi ya Kanda ya UNESCO – Dar es Salaam.

Wadau wengine ni Tume ya Taifa ya UNESCO, Vyuo vikuu, Asasi za Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Mfuko wa Utamaduni Tanzania, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), pamoja na wasanii binafsi.

Mheshimiwa Spika, kulingana na maoni ya wadau hawa, Mkataba huu ni muhimu sana kwa Tanzania, kutokana na utajiri mwingi wa urithi usioshikika ilionao na ambao unahitaji kutambuliwa rasmi Kitaifa na Kimataifa na pia kulindwa ipasavyo.

Ninaomba nielezee kipengele cha mwisho kinachohusu utekelezaji wa Mkataba wenyewe. Mkataba huu ulianza kutumika tarehe 20 Aprili, 2006 na kufikia tarehe 15 Machi, 2011 jumla ya nchi 134 zilikwishajiunga, zikiwemo 35 za Bara la Afrika. Miongoni mwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi sasa (2011) ni Rwanda na Tanzania tu ndizo hazijaridhia Mkataba huu. Tanzania itakuwa mshirika wa Mkataba huu miezi mitatu baada ya kuwasilisha Hati za Kuridhiwa kwa Mkataba kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO. Hata hivyo, utekelezaji Kitaifa utaanza mara tu baada ya Mkataba kuridhiwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, marekebisho ya Mikataba ya Kimataifa ya aina hii yanapaswa kuridhiwa na Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kusoma Azimio lenyewe kama ifuatavyo:-

KWA KUWA Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi Mwanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Uamaduni (UNESCO);

NA KWA KUWA Mwaka 2003 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini Mkataba unaohusu Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika. Utamaduni usioshikika hujumuisha simulizi na mapokeo yake, sanaa za maonesho, lugha, matambiko na sherehe, ujuzi na ufundi wa jadi, ambavyo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine;

NA KWA KUWA lengo na madhumuni ya Mkataba huu ni kuutambua urithi huu kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuweka taratibu za kuulinda kwa kuwa ni sehemu muhimu ya utamaduni ulimwenguni;

NA KWA KUWA Mkataba huu unazingatia kila Nchi Mwanachama kuweka utaratibu na kanuni za kulinda na kuendeleza urithi wa utamaduni usioshikika, ikiwa ni pamoja na kutayarisha orodha ya urithi wa utamaduni husika uliomo ndani ya mipaka yake;

NA KWA KUWA Mkataba huu unaunda Mfuko wa Fedha kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa na Mkataba wenyewe. Kwa kuridhia Mkataba huu, Tanzania itafaidika kama ifuatavyo:-

(a) Kuomba msaada kutoka katika Mfuko ulioanzishwa na Mkataba huu;


(b) Kushirikiana na nchi nyingine duniani kulinda utamaduni wake na wa nchi nyingine kwa uwazi pasipo shinikizo la kisiasa wala uchumi;
(c) Kupata fursa ya kuchagua na kuchaguliwa kuongoza vyombo vya Kimataifa vinavyoundwa na Mkataba huu;

(d) Sheria za Nchi kama vile Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki zitapata msukumo wa Kimataifa; na

(e) Kunufaika na utamaduni, utaalamu na fedha zinazopatikana chini ya Mkataba huu hasa Mfuko wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika (Intangible Cultural Heritage Fund).

HIVYO BASI kwa kuzingatia umuhimu wa Mkataba huu na kwa kuzingatia manufaa ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itapata kutokana na kuwepo kwa Mkataba huu, Bunge hili katika mkutano wake wa tatu na kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, sasa linaazimia Kuridhia Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuhusu Kuhifadhi Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa Mwaka, 2003, yaani The Convention for Safeguarding of the Intagible Cultural Heritage.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa heshima kubwa, sasa naomba kutoa hoja.