You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Arfi, Said Amour[CHADEMA]

Mpanda Mjini Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 4 14 June 2011 Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2011/2012 – 2015/2016
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuipongeza Serikali kwa hatua hii. Kweli mara tu baada ya Uhuru, tulikuwa na Mpango huu, 1965 – 1970 na 1970 – 1975, baada ya hapo hatukuwa tena na Mpango bila sababu yoyote. Leo tumeona athari zake baada ya Uhuru kwa miaka 50. Tumechelewa sana, lakini tumejitambua kama Taifa tulikosea wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba, kama upo utashi wa dhamira ya kweli tutafanikiwa lakini ni lazima tuwe na utayari wa kupanga vyema na kuthubutu kuchukua maamuzi magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni maskini na nchi maskini daima zinakuwa na vipaumbele vingi ambavyo vyote ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Lazima pia tuangalie uwezo wa nchi, kwa maana ya kuwa na uwezo wa kuwekeza katika kila kipaumbele. Vinginevyo, tutaendelea kuwekeza na kutawanya rasilimali chache tulizonazo na kusiwepo na tija. Hivyo basi; ni lazima tuwe na vipaumbele vichache zaidi ambavyo tukiwekeza inakuwa ni kichocheo cha kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele vyote vilivyomo katika Mpango ni muhimu, lakini bado ninasisitiza kuwa ni lazima tuamue kwa makusudi kwamba, katika Mpango tutaendeleza maeneo yepi. Kwa uzoefu tulionao, tumekuwa hatuwekezi ipasavyo katika Mipango ambayo tunaiibua; kwa mfano, tuna Kilimo Kwanza; je ni kweli malengo yake ni lazima Wananchi wayajue? Kama tunataka kuongeza uzalishaji wa chakula au mazao ya biashara; je, masoko yapo na yameandaliwa?

Kama tunataka kuongeza pesa za kigeni basi ni lazima tuweke mkazo katika mazao ya biashara, yaainishwe, tuwekeze ili tuongeze usafirishaji wa mazao hayo; lakini kama mwaka huu wa fedha wa 2011/12, kilimo kimeongezewa asilimia 2.5 kutoka bilioni 903.8 hadi bilioni 926.2; kwa ongezeko hilo hakuna mabadiliko ya msingi yatakayoonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, elimu hapo awali ilipewa msukumo wa aina yake na mafanikio yake yameonekana pamoja na ongezeko la shule au vyuo na idadi ya wanafunzi au wanachuo, lakini pamoja na ongezeko hilo, tumetenga kiasi kidogo sana kama asilimia 12 toka bilioni 2.045.4 hadi bilioni 2.283.0.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya mawili yalikuwa ni vipaumbele vyetu namba moja katika vipindi tofauti, leo ni kipaumbele namba nne na tano katika Bajeti ya 2011/2012. Maswali ya msingi ni:-

(a) Tumefanikiwa kwa kiwango gani na je inaridhisha?

(b) Je, fedha tuliyowekeza itaendelea kuleta ufanisi tuliokusudia au Sekta hizi tunazirudisha nyuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu bado inajikita katika kuwa na Mipango Endelevu kwa kuwekeza, badala ya kila mwaka kuwa na kipaumbele kipya. Nimesema ni vyema tukafanya maamuzi sasa, kwa mfano, katika rasilimali zetu za asili; tuna Mpango gani kama Taifa. Kutafuta wawekezaji na kutegemea kodi na mrabaha hatuwezi kuendelea kama Taifa, ni vyema sasa gesi asilia iwe ni kichocheo cha kuleta mabadiliko katika Taifa letu kwa kuwekeza katika nchi na kujenga kiwanda; mfano, viwanda vya mbolea au saruji na tuvimiliki kwa asilimia 100 au kama hatujafikia hapo, viwanda hivi viwe na ubia wa asilimia 51 – 49 na tuachane kabisa na kuachia rasilimali zetu holela na kutegemea kodi na mrabaha; hatutafika ni lazima tupange na kuamua sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.