You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Malima, Adam Kighoma Ali[CCM]

Mkuranga Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
6 6 7 February 2012 Taarifa ya Serikali Kuhusu Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge Yaliyotolewa na Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini kuhusu Uendeshaji wa Sekta Ndogo ya Gesi Nchini
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kusema machache ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusiana na Maazimio haya ambayo Bunge lako Tukufu lilileta kwa ajili ya kuboresha sekta nzima ya gesi na mwelekeo wake wa jumla wa namna tunavyokwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa William Ngeleja, Katibu Mkuu Bwana Eliakim Maswi na watendaji wote wa Wizara yetu na Taasisi zake na hasa TPDC kwa kazi kubwa iliyofanywa ya kufanyia kazi Maazimo haya lakini pia naomba kwa namna ya kipekee niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wakiongozwa na Mheshimiwa January Makamba na Makamu wake Mheshimiwa Diana Chilolo.

Mheshimiwa Spika, mimi niliongoza ujumbe wa Wizara kwenye kikao cha mwisho cha kupitia ripoti hii Jumamosi kwa sababu Waziri alikuwa amehitajika mkoani kule kwa shughuli za chama na naomba nikiri kwamba pamoja na kazi kubwa ambayo sisi tulikuwa tumeamini kwamba tumeifanya ndani ya Wizara kujibu zile hoja, lakini bado palijitokeza maeneo mengi ya ushauri mzuri tu ambayo Kamati ilikuja nayo kwa siku ile ya Jumamosi na kwa kipindi chote ambacho tulikuwa tukilifanyia kazi suala hili.

Mimi kwa upande wangu pamoja na kwamba nimelifanyia kazi jambo hili kwa muda mrefu, lakini nilifarijika sana na kiwango cha kazi kilichofanywa na Kamati kwenye masuala very specific, kwa mfano suala la human resource capacity building na umuhimu wake na suala la kuboresha watendaji mle ndani ambalo limekuwa tunalifanyia kazi, lakini kwa sasa kwa kuwa limepata msukumo wa Kamati naamini litapata utekelezaji mzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ni hili la financial management na masuala yote yanayohusiana na mapato na matumizi ya gesi. Lazima niseme naamini kwamba tumeyafanyia kazi kwa kina sana na baada ya hapa tulipofikia huko mbele tunakokwenda hakuna sababu ya kurejea nyuma na kulalamika kusema kweli tumeshajiwekea misingi mizuri sana ya kufanyia kazi jambo hili na kuweza kupata utekelezaji mzuri zaidi. Niseme tu juzi kulikuwa na mkutano baina ya watendaji wakuu wa Benki ya Dunia na wale watendaji wakuu wa EITI na nchi mbalimbali za Kiafrika, Afrika ya Kusini mimi niliwakilisha ujumbe wa Tanzania na katika hayo sisi ni miongoni mwa nchi ambazo tuko kwenye mpango unaitwa Gas for Development (G for D) ambao ni mpango mpya ambao umeletwa na Benki ya Dunia kujaribu kuangalia namna ambavyo gesi inaweza kupata matumizi zaidi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea, lakini hata kwa nchi ambazo zinazalisha gesi na kiini chake ni kwamba imeonekana hata zile nchi ambazo zinazalisha sana mafuta, gesi walikuwa wanaichoma tu moto. Sasa ikiangaliwa kama resource, gesi ni more cost
effective lakini ni more friendly to the environment. Kwa hiyo, hata hizo nchi nyingi ambazo zina mafuta ya kutupa kwa sasa hivi zinaangalia namna ya kuelekea kwenye gesi na sisi kama a future country of a future export of our gas tumeshakaa vizuri na tunaamini kwamba kuna forum kama Gas Exporters Country Forum ambazo tumeshapata mwaliko wa kuwa observe country, naamini kwamba ushiriki wetu katika maeneo kama haya yanatupa uwezo wa kufahamu mengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika hili nilitaka nizungumzie tu hili suala ambalo Mheshimiwa Festus Limbu na Mheshimiwa Mariam Kisanji wamezungumzia suala la matumizi ya gesi majumbani. Ni kweli ni suluhisho kubwa sana hasa kama mkakati huu ambao upo unalenga miji mikubwa kwa Tanzania itakuwa ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza ambayo generally speaking katika miji hii tu watu ambao wanatumia mkaa kila siku hawapungui watu milioni 15 between Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na kadhalika. Sasa ukipata strategy ya kuwa na mitungi ambayo kwanza utaanza na Dar es Salaam na ni culture/ni kitu ambacho lazima iwe ni tamaduni ambayo tunaifanyia kazi.

Mimi nadhani ushauri wa Kamati ni mzuri na kwa kuwa limeshazungumzwa sana humu Bungeni nadhani tunaelekea kwenye kulipatia ufumbuzi wa utekelezaji na nimefarijika sana hili la Mheshimiwa Kabwe Zitto na Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed aliyezungumza suala la domestic mobilisation and financing. Lazima tufike hatua ambayo tuache utegemezi wa bajeti za Serikali, lakini kama jambo lina misingi ya kibiashara na lina generate income na commercial viability halina sababu kwa nini saa zote tulielekeze kwenye bajeti za Serikali. Kwa hiyo, hilo naomba niseme kwamba na sisi tumekuwa tunaliangalia, tumekuwa tunalizungumza miongoni mwetu nataraji kwamba tutalifanyia kazi kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kupeleka gesi Kenya, Mombasa ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Festus Limbu, naomba nilisemee, hili pia limejadiliwa kwenye East African Community Sectoral Council. Wakenya walikuwa wameomba kwamba bomba liende mpaka Mombasa which is fine na hapo walipoomba Wakenya na Waziri wa Rwanda akasimama akasema na sisi tunataka gesi na Mganda akasema na sisi tunataka gesi. Kama ambavyo na sisi tutakavyosema wakati Uganda wanaanza kuzalisha mafuta na sisi tutawaambia na sisi tunataka mafuta yenu kwa concession tutakapofika kwenye Community. Lakini tulisema wazi na hili naomba niliseme kwa sababu naona linasemwa hata kwenye magazeti linapotoshwa. Hatujasema kwamba tutaanza kupeleka gesi Mombasa na wapi kabla sisi wenyewe hatutajitosheleza na sisi wenyewe we have our own priorities na la kwanza kabisa ni umeme, la pili ni mbolea, la tatu ni LPG kwa maana ya kupata compress natural gas ya kutosha na kupeleka majumbani. Sasa tukifika hatua ambayo tume-address maeneo ambayo ya kwetu wenyewe yanatutosheleza then tuna excess, hatuna sababu ya tusizungumzie masuala ya kuwa gas exporter. Lakini kwanza tukifanikiwa kuweka gesi kwenye hayo maeneo matatu niliyoyasema umeme, mbolea na hili la matumizi ya gesi majumbani hata gharama za maisha ya watu itapungua kwa kiasi kikubwa sana na hilo lazima tuliseme ndio lengo ambalo tunataka tulipeleke.

Mheshimiwa Spika, hili nimeona pia nilisemee pamoja na lile la royalty za gesi na haki za wananchi wa Kilwa ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Murtaza Mangungu. Hili mwaka jana tulipokuwa Kilwa na mwaka juzi pia tulipokwenda Kilwa, limesemwa na wananchi wa Kilwa na wanalizungumzia lina mkakati kidogo wa kisheria ili liweze kufanyiwa kazi. Lakini mimi naomba niseme tu nalo limekuwa linafanyiwa kazi na naamini kwamba limefika wakati ambao sasa lipatiwe ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, naomba nilisemee hili la makampuni haya makubwa ya duniani ya gesi ya Kitaifa ambayo yametajwa Petro gas, Petro Brass na kuna Kampuni hasa hii ya Trinidad and Tobago ambayo nadhani kwetu sisi zaidi ndio Kampuni ya mfano. Kwa sababu Trinidad and Tobago wameanza muda mrefu wanavuna gesi kama miaka 70 na hawakuwa na teknolojia ya kuvuna gesi kama ambavyo sisi tulianza. Sisi tulikuwa hatuna hiyo taaluma, lakini wameleta uwekezaji kutoka nje, sasa wamekwenda, wame-review hili jambo na kwa bahati nzuri Mwanasheria wao Mkuu anasema ni jambo ambalo tumekaa tumezungumza nae anasema ni jambo ambalo linataka maamuzi ya msingi na tulifika hatua ya kusema labda tungekaa nao wenzetu hawa ambao sio tu kwamba wana resource za gesi lakini wamepitia process ile ya kufanya mabadiliko ya mikataba na ya kisheria na kadhalika ili kwenda na wakati na mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nimeshukuru kwamba hili limesemwa, kwanza ndani ya Kamati limesemwa sana na hapa Bungeni leo limesemwa na naomba niseme tu kwamba ni jambo ambalo tumelipokea na tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni hili la structural adjustment ambalo Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed amelisema lakini hata kwenye Kamati limezungumzwa sana. Suala la taaluma kuwa na mfumo wa specialized capacity building. Hili sisi tuna tatizo moja na ni jambo ambalo tunalifanyia kazi na lazima lifanyiwe kazi kwa haraka. Huwezi ukamchukua Mwanasheria au Mhasibu ametoka Chuo Kikuu uende ukampambanishe kwenye masuala ya nishati na gesi. Kwenye ma-contractual, accounting and auditing, wenzetu hawa have specialized accountants na auditors wa masuala ya gesi na nini na nini. Sasa hili ambalo limezungumzwa hapa ni so relevant, ni jambo muhimu sana. Kwa maana hiyo hata CAG mwenyewe tukimwambia twende ukaangalie masuala ya TPDC lazima mwisho wa siku aende akawaone wataalam wenyewe wa TPDC ndiyo wamsaidie kwa kiwango hicho kidogo walichonacho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nadhani hili ambalo Bunge lako Tukufu limelisemea leo la kwamba ni lazima tuwe na specialized accounting, auditing na legal framework, specialized to the field of gas ambalo hata watu wa extractive industry EATI wameji-commit pamoja na Benki ya Dunia kutusaidia naamini kwamba kuanzia wiki ijayo hili jambo litaanza kupata ufumbuzi na ikifika mwezi wa nne tutakuwa na nafasi zaidi ya kusema tutafika nalo wapi.

Mheshimiwa Spika, hili la contractual review na masuala ya kuvunja Mikataba, mimi nilikuwa nashauriana na Waziri hata pale anasema ni jambo zuri kwa sababu kwanza sisi sio wa kwanza ambao tutalifanya. Kwa bahati mbaya huwa tunapokaa na wawekezaji au nini huwa inatoka impression kwamba sisi Watanzania tunataka kulifanya kwa mara ya kwanza, si kweli. Wenzetu wengi wamelifanya; lakini nao litataka kuangalia legal precedents na mimi sio Mwanasheria lakini naamini kwamba Wanasheria wakilikalia chini hili jambo tunaweza kulifanya na likawa na manufaa kwa Taifa letu, si kuvunja mikataba lakini even to review the contractual obligations za nchi katika misingi hii na naishukuru sana Kamati kwa sababu kwenye taarifa yao na kwenye mjadala wa face to face hili jambo limesemwa sana.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge waliozungumza kuhusu utaratibu wa kisheria wa humu ndani Bungeni wa kuchukua hatua kali za kisheria pale ambapo pana upotoshaji wa makusudi, false declaration ya revenue na expenditure. Hili linatokana na masuala ya udhaifu kwenye reconciliation ambalo tumeanza kulisemea na tumegundua kwamba nchi nyingi ambazo hawa mabwana wakifika sehemu ambayo na ninyi wenyewe mnakiza kidogo na wao wanaendelea. Lakini sasa hivi kuna a deliberate process kwenye nchi nyingi duniani kama sisi ambao tunaangalia mikakati ya kuboresha taaluma ya reconciliation ili usifike hatua mtu anakwambia “ahha!! risiti zangu za miaka saba iliyopita sizioni.”

Kwa hiyo, naomba niseme hili limezungumzwa kwenye Kamati Jumamosi na tumeafikiana na tumekubaliana nao kwamba hivi tunavyokwenda kwenye Mabunge yanayofuata tulete taarifa kwenye Bunge lako kwamba tumefikia hatua gani za kuboresha capacity building hasa kwenye masuala haya ya kuwawezesha watu wetu kuwa makini zaidi kwenye monitoring of income and expenditure za makampuni haya makubwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kasi ya utendaji kazi kwenye Sheria, kwenye miongozo na kwenye utendaji wa GNT na ni kweli kwamba tukikaa tunasema labda GNT itafanya kazi lakini kwenye masuala ya time frame nadhani pia Mheshimiwa Waziri atalisemea tumeridhia kwamba ni vyema tukajiwekea time frame. Haya mambo yanapokwend endlessly hayatusaidii wote.

Mheshimiwa Spika, mwisho, Tanzania ina estimated reserves za 10 TCF trillion cubic feet za mafuta ndiyo tunazotaraji kuwa nazo huko mbele. Tunaweza tukazipata zingine ziko offshore, nyingi ziko baharini lakini zinataka uwekezaji mkubwa sana ili mwaka 2018 tuwe nchi ambayo ni gas exporter mkubwa dunia nzima, tutashindana huko na kina Qatar na nani. Lakini lazima tukubaliane kwamba pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu ametupa hizi resources, ni lazima tuingie kwenye deliberately expenditure and some of it lazima iwe domestically mobilized lazima itokane na sisi wenyewe humu humu ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kuweza kufikia huu uzalishaji wa gasi mkubwa wa gesi namna hii ni lazima tutaingia humu Bungeni na tujue kwamba itabidi tujifunge kwenye kuacha mengine ili tufanye
mengine kwa maana ya kwamba kama wanavyosema wataalam wa choice theory tunachukua hili ili baadae tuweze kuingia kwenye nini. Hili jambo ni muhimu sana kwa sababu tutakapokuja Bungeni na masuala ya kuongeza uwezeshaji kwa ajili ya sekta ya gesi sio haya tu, ya TPDC yenyewe iwe na participation kwenye uchimbaji huo. Sasa mtu anapokuja pale kuna risk element na wewe unataka uweke pesa yako ili tutakapofika sehemu na sisi tunasema tuna asilimia 40 ya mapato yote yanayotokana humo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakapofika hapo ni lazima tukubaliane kwamba tutakuja Bungeni na mapendekezo ambayo yatakuwa yamefanyiwa kazi na tutawaomba Wabunge wenzetu waturidhie. Hili tutabana matumizi fulani ili ndani ya miaka minne, mitano Tanzania iweze kufikia kwenye uzalishaji wa 10 TCF.

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii naomba nilishukuru Bunge lako Tukufu na naunga mkono hoja.