| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 4 | 14 June 2011 | Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2011/2012 – 2015/2016 | ||
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kunipa nguvu nikaweza kusimama jioni hii kuchangia mada iliyoko mbele yetu. Lakini pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili nami nijumuike na wenzangu waliotangulia kuchangia mada hii ambayo imekuja katika kipindi muafaka. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutimiza ahadi yake ambayo aliitoa wakati alipolihutubia Bunge kwamba anakusudia kuunda Tume hii ya Mipango na ametekeleza ahadi hiyo na hatimaye leo tuko hapa tunajadili mpango huo. Nampongeza pia Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha jana kwa ufasaha kabisa na hatimaye kuanzia jana na leo tumekuwa tukichangia mada hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujikita katika utekelezaji au nitoe muono wangu katika utekelezaji wa mpango huu. Wengi wamechangia, wamejaribu kuboresha, lakini nasema hivi, baada ya hayo yote, kitakachofuatia ni utekelezaji na utekelezaji ndiyo mafanikio ambayo juhudi yote hiyo iliyotokea au inayoendelea itatupa maslahi au nia halisi hasa iliyokusudiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ni wajibu wa kila Mtanzania popote alipo, kuanzia Rais mwenyewe amekwishaonyesha mfano, lakini mpaka mkulima wa kijijini tunapaswa kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake na kila mmoja kwa uwezo wake aliojaliwa na Mwenyezi Mungu ili kutimiza mpango huu kwa maslahi yetu sisi wenyewe. Itakuwa ni ndoto ikiwa katika Mpango kuna kutegeana au ni wa nani au jukumu la nani, hautaweza kufanikiwa. Wenzetu wote tunaowasikia wameendela duniani kote ni kwa ajili ya ushirikiano na commitment na kuweza kujitoa mhanga, hasa kujua kwamba naifanyia nini nchi yangu badala ya kutegemea kwanza nchi yake imfanyie nini. Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango imekwishakuja mingi kama wenzangu waliotangulia walivyoeleza na ni mizuri sana na inaishia either katika madawati au watu wengine katika nchi nyingine kutumia mipango yetu na wakafanikiwa. Tatizo hili sugu tunalo Tanzania, tunatakiwa sasa kubadilika na tubadilike kimuono kwamba wakati wa kupanga tu bila utekelezaji haupo, sasa hivi ni utekelezaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapeni falsafa moja ambayo alitoa Kiongozi wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Marehemu Shehe Abeid Amani Karume. Mheshimiwa yule alitawala kwa miaka nane, lakini alisema hivi: “Tumesoma hatukutambua, tumejifunza tumejua, twendeni”. Nataka mlichukue hilo. Through theory hatuna kitu, lakini kwa vitendo tukafanye kinachokusudiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa kipindi cha miaka nane alichotawala pale, kuna maendeleo mpaka hivi leo tuna Awamu ya Saba hajawahi kutokea hata Rais mmoja aliyefikia kipindi chake. Tumekwishapanga sana sisi kwenye makaratasi, basi sasa tufanyeni, kwa sababu kwa vitendo ndipo tu tunapoweza kufanya yale tuliyokusudia. Si kwa maneno, wanakuja kuchukua wenzetu makaratasi, tunawatengenezea, hawagharimiki kutafuta Tume ya kutengeneza au kutayarisha mipango, wanakuja kuchukua. Tena cha kushangaza zaidi na sisi tunajisifia, nchi fulani imechukua mpango fulani kutoka hapa kwetu. Leo wanaendelea, hatuna aibu sisi? Inatosha! Ndugu zetu Serikali ambao tumewapa dhamana, sisi tulioko huku, jamani chonde, ni lazima kuwe na commitment. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna kitu kimoja ambacho nimekiona, vijana wetu ambao wengi sana ndiyo wanategemea mpango huu kwa njia moja au nyingine wautekeleze utekelezaji wake, basi hawana ule muono wa kuwajibika kimtazamo hasa wa kinchi. Ni tofauti na huku nyuma tunakotokea sisi na wengi wenu ninyi Mawaziri mlioko huko mbele, ninyi mliopata matayarisho haya ya kupitia JKT baada ya kumaliza “A” Level kabla ya kuingia vyuoni. Mkapata muono na mkajua hasa uzalendo uko wapi. Leo mkajishitukia huko mlipo. Kwa nini mmesahau hivi vitu? Vijana wenu mnategemea nini? Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana ambao toka anazaliwa yeye hata kubandika sufuria ya chai inamshinda, amelelewa na house girl, amemaliza A-level, ameingia University hajui hata kufua nguo yake ya ndani, huyo unafikiri anaweza kuitumikia nchi namna gani? Ataandamana, atashawishika kwa kile ambacho anaambiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, turudishe ile na tuwatengeneze vijana wetu kimtazamo, tuwe na mabadiliko ya mindset zetu, hatuwezi kutekeleza msimamo huu kama hatukuweza kufanya hivi. Alisema Mheshimiwa Karume kwamba linalowezekana leo lisingoje kesho, tunangoja nini? Twendeni, tutajua huko huko mbele ya safari, hebu tuchukueni hatua kufanya, kama tumeshindwa tutajua tumeteleza wapi, tuchukue hatua tusiwe tunaishia kwenye makaratasi tu. Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapa tena falsafa nyingine kule kwetu Zanzibar kuna Mji mmoja unaitwa Makunduchi, sisi Wamakunduchi tunasema ‘kuchupa kwacha’ maana yake ukiwa uko juu na wewe unataka kuchupa achia nenda chini ukifika utajua nimegaragara, nimetambaa, nimekimbia, lakini unaning’inia na unataka kwenda chini huwezi kufika na huwezi kufanya kitu, twendeni tujiachie tu, tutazame mbele tutakwendaje, tukiishia kwenye makaratasi mpango huu utapita, utakuja mwingine na mwingine na mwingine, kutakuwa hakuna lolote, story tu, watakuja wenzetu wachukue, wakatumie, halafu sisi tunajigamba tu wamechukua kutoka kwetu maana yake nini? Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotuponza zaidi sisi Tanzania ni kwa sababu sisi ni matajiri sana, tuna kila kitu. Tunayo ardhi nzuri, bahari, mabonde, maziwa hatuna cha kuhangaika. Wenzetu ambao wanahangaika wana jangwa wanahakikisha wanalitumia wanaligeuza liwe na fertile na wanazalisha na kuna hawa wenzetu wa Ulaya wana miezi sita tu ya kuhangaika, miezi sita mingine hawawezi wakalima. Lakini ile rehema aliyotupa Mwenyezi Mungu kila kitu ndiyo kinatulemaza, imekuwa kama mali ya kurithi haina uchungu. Watanzania tunapenda sana starehe, hatutaki kufanya kazi. Leo ukifika barabarani kule Dar es Salaam mitaa yote, kupita Shekilango Road, kuanzia Morogoro Road mpaka ufikie barabara ya Ali Hassan Mwinyi au Bagamoyo Road utakuta pembeni meza za kunywa, watu wanakunywa full time, toka Tabata nenda Kinyerezi all the way tunalewa tu! Kazi tunafanya saa ngapi? Hatutaki kufanya kazi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nchi gani ninyi mmetembea watu wanafanya namna hii kama siyo Tanzania? Halafu hatuishi kulalamika, nchi hii maskini, Serikali hii itakwendaje? Serikali inaajiri watu kupata mshahara, haiajiri watu kufanya kazi, inawapa kazi watu just to pay salary, lakini hatuwawajibishi kufanya kazi. Tutaendeleaje? Tufanyeni kazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaibana Serikali, Mbunge wa Chama cha Mapinduzi lakini nasikia uchungu sana kuona Serikali ambayo imewekwa na Chama madhubuti, Chama imara, inayumba kwa vitu vya kijinga, jamani tuacheni hii, tuchukue ile misingi ambayo imeweza kutuvusha hapa tulipo. Tumesoma, hatukutambua, tumejifunza tumejua. Kwa kusoma si tunasoma tu hapa? Tunashindana hapa kila mmoja na uelewa wake, hebu twendeni kwenye field, si tutaona tulipokosea na tutajisawazisha na tutatekeleza majukumu yetu na mpango huu utafanikiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na Watanzania wote tuache kulalamika na tufanye kazi. Hatufanyi kazi, starehe nyingi sana, tunastarehe kiasi cha kushangaza sana halafu tume-relax. Vijana wetu ni lazima tuwabadilishe mindset zao, ile sheria ya kwamba ni lazima akimaliza Form Six kabla hajakwenda Chuo Kikuu waende JKT, wakapate msimamo, wakapate mwelekeo wa nchi inafanyaje, watakuwa na uchungu wa kuweza kufanya kazi. Ndivyo tulivyolelewa na ninyi wengi wenu hapa Mawaziri ndivyo mlivyolelewa. Sijui kwa nini mpango huu ulibadilika. Leo anakuja kusimama mtu hapa anasema kwamba, miaka hamsini yote hamna kitu kilichofanyika, nimemaliza Chuo Kikuu tu jana na nimekuwa Mbunge na nimekuwa na gari, Serikali imemsomesha mpaka hapo, bado hajaona kitu? Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni kosa lenu ninyi kwa sababu ninyi Serikali wenye mipango hii hamkumwandaa yule na wako wengi sana wako namna ile. Wengi sana wamejaa vyuo vyote, sasa hivi hakuna hata mmoja aliyepita JKT, kwa mpango tuliokuwa nao mnategemea nini? Mheshimiwa Mwenyekiti naona nisije nikaharibu mambo. Naunga mkono hoja. |
|||||