| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 14 | 28 June 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa | ||
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii walau na mimi nizungumze kuhusu suala zima la Hotuba ya Waziri Mkuu katika jioni hii ya leo. Nilikuwa nimetoka kwa ajili ya matatizo ya kidunia, nimerudi na nimemaliza kazi niliyokwenda kuifanya. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nipende kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa hatua iliyofikia, sasa hivi tuko mbele na nafasi yetu ni nzuri tu kimaendeleo. Mimi nilishangaa wakati Mheshimiwa Wasira alipozungumza kwamba nchi hii tulipewa uhuru na umeme wa diesel, nilichoka! Nikasema ama kweli, kumbe tumetoka mbali hivyo! Pamoja na umri wangu huu kumbe tumetoka mbali hivyo? Hongera Serikali ya Tanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia suala zima la Mwanza. Katika Hotuba ya Waziri Mkuu wametaja Manispaa ambazo zimepitishwa ikatajwa ya Lindi. Kipindi kilichopita tu katika Bunge hili walitamka Mwanza pia imo katika kupewa Manispaa. Kwa kweli nilishikwa na butwaa, nikatetemeka, nikasema tutawaambia nini wana Mwanza, kwamba tumeanza hatua zote, tangu wadau tukafuata Baraza, tukafuata RCC na mpaka tukafikisha kila hoja hapa Taifani na mpaka Taifa likatamka, kuna nini? Kama kuna kitu, sisi tupo tayari kukifuatilia na nimeshaanza kusikia watu wanataka kuhodhi madaraka kuitwa wanajiji fulani na nani wa jiji, tutayaleta humu na sisi tutasema. Mwanza inataka maendeleo katika maeneo madogo, hatutaki kuwa na maeneo makubwa yanayotushinda, tunataka maeneo ambayo yatakuwa muafaka ili tuweze kuendelea. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata usafi wa Mwanza tulikuwa tunapambana na Moshi tukiwa bado ni Manispaa, sisi usafi umeanza tukiwa Manispaa, mimi nikawaambia wana-Mwanza sisi ni lazima sasa tuweze kuwa wa kwanza, tukipambana na Manispaa ikiwemo Manispaa ya Moshi. Wakati huo mimi nikiwa Naibu Meya, nilimwambia Naibu Meya mwenzangu sasa Mwanza inachukua ushindi, leo tumekuwa washindi wa usafi kwa mara ya sita mfululizo, kwa sababu tumedhamiria. Leo tumedhamiria kuwa na Manispaa tufanye mambo yetu inatokea nini? Nahitimisha katika hilo kwamba tunataka Manispaa. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu maji katika Mji wa Mwanza. Bomba kuu lile linalotoa maji Lake Victoria linapeleka Shinyanga mpaka Kahama kwa binadamu kama sisi sina tatizo kabisa cha kushangaza kilio cha wana Mwanza wanaozunguka Ziwa Victoria hawana hata tone la maji ya bomba. Ukianzia Ihelele pale na wananisikia, Kwimba yote haina maji hayo ya bomba, hivi kweli tuwe tunaangalia kwa macho tu maji yanakwenda? Sisi mnadhani hatupendi kuona maji ya bomba yakoje, yanapitiliza tu! Mheshimiwa Mwenyekiti, mwamba ngoma huvutia kwake, hebu na sisi mtufikirie katika hili, hawa watu wa Kwimba hawana kabisa maji, wanaliona hilo bomba linapita. Lingekuwa ni la plastiki tungeshawishi vinginevyo, lakini kweli inatia uchungu sana. Tunaomba na sisi linamopita bomba basi watuwekee mabomba ili hao akina mama wa maeneo yale wapate maji. Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa kuna majibu yanayotoka kwamba ninyi mna Ziwa karibu, hivi mnaifahamu Kwimba ilivyo? Kuna sehemu inaitwa Kinduru ni kilomita sijui ngapi tena inawezekana hata Ziwa hawalijui lakini linapita kwake, tunaomba Serikali iliangalie suala hili kwa mara ya pili. Mimi naelewa kabisa Waziri wa Maji Mwandosya ni mwamba kweli, ana sifa zake za kipekee kabisa katika Wizara hii ya Maji, siwezi nikambeza hata kidogo, anatosha kabisa lakini atufikirie, wale watu wapate maji. Natoa ombi rasmi wapate maji, maji yanapita kwao wanabaki wanaduwaa Wasukuma hawa. Tunaomba maji ya bomba hilohilo kubwa tupate na sisi maji yanayokwenda kwa wenzetu. Tunapongeza Serikali imefanya vizuri sana lakini hebu irudi nyuma sasa ifanye hilo. Mheshimiwa Mwenyekiti jambo la pili ni maji ya visima, visima hivi vimechimbwa vingi sana hongera sana, lakini visima hivi ni vya muda mfupi siyo vya mwaka mzima. Nadhani lengo la kisima kinapochimbwa sehemu kihudumie mwaka mzima, lakini kisima kinakaa miezi mitatu kinakauka maana yake ni nini? Ukienda vijijini huko ni uyoga wa visima ambavyo havina maji kabisa, maana yake nini? Napendekeza, kama tulifanya makosa mwanzo, vile ambavyo havitoi maji mwaka mzima Halmashauri ya eneo lile ifanye sensa ya hivyo visima ivizibue tena viweze kufanya kazi kama inawezekana kwa gharama ya Halmashauri kwa sababu miradi hii inapitia huko. Maana kila kitu ukizungumza unaambiwa sijui kuna NGOs gani inazungumzwa kila kitu kinapelekwa Halmashauri, sasa kama hata hivyo visima vinapitia Halmashauri na Halmashauri siyo makini basi walijue hilo. Waripoti kwenye WDC zao kwamba visima kadhaa vilikabidhiwa Halmashauri, tuzungumze upya juu ya mauyoga ya visima ambavyo havitoi maji. Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanateseka, akina mama wa Tanzania sasa hivi nao ni wastaarabu tu kwa sababu wanatengeneza vinywele vyao halafu bado mnawabebesha ndoo vichwani kwa misingi ipi? Anataka na yeye ashinde kutwa tangu asubuhi mpaka jioni akiwa msafi, leo mnataka tena akahemee maji sijui kutoka wapi. Mheshimiwa Mwenyekiti, anapita huko visima vimekauka, anaenda kutafuta maji mbali, tulifanye zoezi hili na shauri hilo kabisa kila Halmashauri ijue inawajibika vipi na visima na je vinafanya kazi au havifanyi kazi na kama havifanyi kazi ni vingapi, je tuna mikakati gani ya kuvifufua visima hivi? Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linalofuata ni kuhusu njaa... Mheshimiwa Mwenyekiti, najibiwa huku na wanaopita, wachelewaji, wanasema eti tuwe tunalima. Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mwanza huwezi ukatufundisha jembe, hata hayo matrekta lete tu tena wanawake wa Kisukuma wanasukuma power tillers wala hawatishiki katika hilo, lakini ni Mwenyezi Mungu hakuleta mvua. Watu wa Kusini wanatamba hapa wana mahindi ambayo hayana kazi, wamekula wameshiba hayana kazi, yapandishwe yaende Kaskazini huko. Tunangoja nini mpaka tunazungumza wenyewe humu na wananchi wanatusikia na njaa zao kule. Watu wa Kusini wanatutangazia hapa Serikali inasema nini juu ya suala hili? Sisi tutaendelea kusema kwamba Serikali imekaa lakini chakula kipo Kusini. Hatutaki kusema hivyo, Serikali ya Tanzania ni sikivu, naomba mlisikie jambo hili mpeleke chakula hiki kiweze kutumika kwenye maeneo ya watu wenye njaa. Tanzania hii imegawanyika katika mkondo huo, wengine wanapata na wengine wanakosa, wanaopata basi wawape wanaokosa. Serikali ilifanyie kazi suala hili na kama ndiyo hali halisi hiyo, sasa nadhani tutakwenda vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ufupi sana nizungumzie suala la umeme. Mheshimiwa Simbachawene hapa nilisikia sehemu akisema kwamba hatuhitaji kuzungumza zaidi, sisi tunataka umeme, Mwanza imejaa viwanda, viwanda bila umeme ni magofu, tunataka umeme hatuhitaji tena historia. Fikiria mpaka Wabunge wanafikia hatua ya kusema hatutaki semina, ujue uchungu walionao kuhusu suala zima la umeme, kwa hiyo, leteni umeme. Umeme una gharama gani, yatajitokeza mbele ya safari, weka umeme basi, sisi tunataka umeme. Jamani katika maeneo yanayoathirika na umeme ni pamoja na Mwanza, tunataka umeme. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Watanzania tunaomba tutunze amani. Msemo wangu siku zote ninasema kwamba amani ina gharama ikitupotoka na hasa sisi akina mama ndiyo wenye mateso makubwa. Mwanamke ni jasiri lakini mwanaume ni mwoga. Katika njaa mwanaume atakimbia, katika vita mwanaume atakimbia, sasa anayebaki anasota ni mwanamke na familia. Huwa wanatuambia ingia humu jifungie na watoto wako! Kwenye matatizo watoto wanakuwa wa mwanamke kwenye starehe hawa ni watoto wangu tena anaweka besi kama ya kwangu. (Kicheko/Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuitunze amani ili familia zidumu na familia ikidumu yote haya tunayoyaongelea hapa katika kuchangia Serikali yetu itafanya kazi katika amani, upendo na katika utulivu. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, naunga mkono hoja, Serikali yangu endeleeni kuchapa kazi. |
|||||