You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Mlata, Martha Mosses[CCM]

Special Seat
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
5 4 11 November 2011 Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wa Mwaka 2011
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nami namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa ajili ya siku hii ya leo na baraka zake nyingi ambazo ananikirimia kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja Muswada huu uweze kupita ili ulete tija kwenye nchi yetu. Naunga mkono kwa sababu kwanza katika Mkoa wangu wa Singida kuna reli ambayo inafika pale Mjini Singida, wananchi wa Mkoa wa Singida walikuwa wanafaidika sana na reli ile, lakini sasa hivi imesitishwa, kwa hiyo, naamini Muswada huu ukipita basi Singida pia itakuwa ni ya kwanza kwenye udharura ili tuweze kukuza uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi jana wakati nasikiliza michango ya Wabunge, Wabunge wengi wameongea, kila mtu ameongea kwa kadri anavyoelewa na yote ni kwa manufaa ya Taifa hili. Lakini napata wasiwasi na mashaka mengi sana kwa kuona Mtumishi wa Mungu anayeaminiwa na watu wengi kwa kutumia maneno na lugha za matusi kwa kumnukuu mtu aliyetumia matusi kumtukana Mwafrika. Kama kweli ni mtumishi wa Mungu unaweza ukaingia ndani ya Bunge na ukatumia mfano wa lugha ya matusi, unatukana Watanzania na Waafrika wote hata wale unaowaongoza. Kwa kweli nina mashaka sana na utumishi huu. Sina uhakika hata hao anaowachunga kama kweli bado wapo au kondoo hawa walishatawanyika. Kwa sababu kazi ya mtumishi wa Mungu naamini hata Mungu amekuingiza ndani ya Bunge hili kwanza uweze kuliombea Taifa hili pale unapoona kwamba kuna upungufu, naamini hapo angeweza kutukuka katika utumishi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nasikitika lakini namwomba akatubu kwa Mungu wake ili kazi yake iweze kuwa njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza ni kuhusu suala la bidhaa ambazo zimetumika, siamini kama kweli Watanzania walio wengi wanapotusikiliza hapa wanatuelewa vizuri, nashukuru sana Wabunge wengine waliotangulia ambao wamefafanua kuhusu vifaa au bidhaa ambazo zimetumika, kwamba Serikali yetu iruhusiwe iweze kununua. Maana unapotumia neno chakavu kwa kweli si sahihi kwa sababu hata kwenye mitumba, nguo za mitumba tunazonunua kuna mitumba ambayo kwa kweli ina grade tofauti tofauti. Kuna grade ambazo wanaita malapulapu yaani unaambiwa hizi ni za mwisho mwisho, basi watu wanakwenda kama wanaokotaokota kwa bei ya kutupa kabisa. Lakini kuna mitumba ambayo ni mizuri kabisa, mtu unanunua unapeleka dry cleaner na bado unaivaa nguo ile inakusitiri kwa muda mrefu. Kwa hiyo, bado naona kwamba Muswada huu tuupitishe kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunapotaka kukimbilia kununua vitu ambavyo ni vipya, nchi yetu bado ni changa, tunahitaji mambo mengi sana, kwa ajili ya kusaidia nchi yetu.
Watanzania ni wale wale, uzalishaji bado si wa kutosha sana kuweza kupata pato ambalo linaweza likanunua bidhaa zilizo mpya au kwa mfano, ndege mpya, hiyo hela Mtanzania utamkamua mpaka wapi ili aweze kutoa hela ya kununua ndege mpya? Kwa hiyo, bado naunga mkono hoja kwa ajili ya vifaa ambavyo vimeshatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua shetani mara nyingi sana anapokuona wewe unataka kufanikiwa, basi shetani atatanguliza vikwazo vingi sana mbele yako na anaweza hata akakukatisha tamaa kama una safari ya kwenda labda mahali ambapo pana mafanikio, shetani anaweza akakukatisha tamaa. Nawaomba Watanzania tushirikiane kwa pamoja, hebu tumkatae huyu shetani anayetaka kuirudisha nyuma nchi yetu. Kwa sababu tusipokwenda kwa pamoja hakika hatutaweza kufika, maana tukianza kukwaruzana njiani, mara Watendaji hawafai, mara sijui huyu kaiba, mara sijui hiki kimekaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nina shaka hata Watendaji wetu Serikalini wamekuwa hawawezi kutoa maamuzi ipasavyo kutokana na woga wa maneno mengi. Yaani siasa zimekuwa nyingi kiasi kwamba watendaji wetu wanashindwa kufanya kazi ipasavyo. Mtu anaogopa kutoa maamuzi kwa sababu anajua ndani ya Bunge mle kutachemka au sijui itakuwaje kutachemka. Kwa hiyo, tunarudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu. Hebu tuwape basi uhuru Watendaji wetu waweze kufanya kazi, kwani sheria tunatunga wenyewe, kama mtu atakiuka basi sheria hiyo ichukue mkondo wake, mtu aliyekiuka achukuliwe adhabu au jinsi atakavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ninachotaka kusema ni kwamba, Mheshimiwa Lucy Mayenga na Mheshimiwa Mpina walitangulia kusema kwamba, Tanzania bado hatuna ule mfumo wa kuwapa tuzo watu ambao wamefanya vizuri. Kuna mashirika mengine unakuta Mtanzania amekabidhiwa shirika, amefanya vizuri, shirika lile limekwenda vizuri, ni sawa kuna matatizo madogo madogo ambayo yanakuwa yakijitokeza, lakini unakuta mtu anakwenda kumshupalia mtu, anamlaumu kuanzia mwanzo mpaka mwisho as if hajafanya kitu chochote, tunawavunja moyo. Naamini kabisa Serikali yetu kama itawezekana tuweke utaratibu wa kuweza kuwapa tuzo watu waliofanya vizuri ili waweze ku-perfom vizuri hata wengine watakaokabidhiwa madaraka kwenye maeneo watakayokuwa wamepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala lingine kwenye manunuzi ya vitu ambavyo vimetumika, kwa watendaji ambao si waaminifu, kwanza tumesema vifaa ambavyo vimeshatumika ni kwa udharura, si kwa sababu kila kitu tu kinunuliwe, ni pale inapotokea dharura. Juzi hapa tumepata udharura wa kutindikiwa na mitambo ya kufua umeme tukaanza kutazamana, tena nilikuwa ni mmoja wa wale niliouliza hivi kweli ile mitambo hatuwezi kuinunua? Nikajibiwa kwamba hapana, sheria haituruhusu, wakati nikifika nyumbani kwangu ninakuta giza, ukienda huku giza, eti mitambo iko pale, lakini kwa sababu ya sheria huwezi kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie udharura unakuwa wapi, watu wengi wengine wamepoteza maisha, kwa sababu ya sheria hii tu, tumekwenda pale Muhimbili umeme hamna, unakatika, lakini mitambo iko pale inatuangalia, eti kisa sheria hii iliyokuwepo ya manunuzi hairuhusu sisi kuweza kununua ile mitambo. Sasa tukipitisha yale masuala ya dharura basi tununue. Kama wazungumzaji waliotangulia kusema kuwe na Kamati au Tume maalum ambayo itasimamia ununuzi wa vifaa vile, kutakuwa hakuna kuchakachuliwa, kwa sababu si kila siku na si mara kwa mara, si ajabu inaweza ikatokea kwa mwaka mara moja au baada ya miaka mitano au huwezi kujua Mungu anaweza akanusuru Taifa letu lisiingie kwenye udharura na sheria yetu ikabakia pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu ninachowaomba jamani chonde chonde, kweli tumekuja hapa kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania, tusiwapotoshe Watanzania kuwaonesha kwamba eti tunataka kuwaletea vitu vibovu! Si kweli. Ni kwamba hivi vitu ni kwa faida ya Mtanzania mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda pale Dar es Salaam nikakuta saluni, watu wametandika tu kanga zao chini wamelala, unawauliza nini, wanasema umeme, mtambo upo pale umekaa umetulia hauzalishi, leo tunataka tupitishe sheria, mnawadanganya Watanzania
mnawaambia ooh, mnaletewa vitu chakavu. Mtanzania anataka asaidiwe ili aweze kujikwamua katika maisha yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukasema labda kwa mfano MV Victoria ilizama halafu hakuna usafiri mwingine na tunataka usafiri pale, hivi tunafanyaje? Si lazima tufanye manunuzi ya udharura ambapo tunaweza tukapata kitu ambacho hata kimeshatumika lakini kwa ubora. Sasa tusiwarudishe na tusiwapotoshe Watanzania, Watanzania wajue kwamba tumeleta sheria hii kwa sababu tunataka kusaidia Taifa letu ili liweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanalalamikia ndege, Baba wa watu amejieleza vizuri sana pale, ni mtaalam aliyesoma, amepoteza muda wake mwingi darasani, anaelewa ndiyo watalaam tunaowategemea Tanzania lakini bado tunawabeza watalaam wetu wenyewe. Wapo wataalam wengi wamejaa kule wanafahamu lakini sasa hivi wanakunja mikono kwa sababu ya maneno yetu sisi wenyewe. Hebu tuwape nafasi waweze kufanya kazi vizuri. Hata sheria tunazopitisha hapa tutajuaje sasa kama sheria hii ime-perfom namna gani? Tuwapeni nafasi ili na sisi tuweze kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sitakuwa na mengi ya kusema, ninachosema naomba wote tuunge mkono sheria hii, iweze kupita, watendaji wetu ni wazuri, wamesoma ndio wameajiriwa. Ni kweli sisi kwetu tunasema unapochemsha kunde huwa kuna kunde ile ambayo huwa haiivi, wapo wengine wana matatizo sisi tunaita “nsensela”. Kama wapo kama hao basi, wachambuliwe, watolewe, tuweke utaratibu ni namna gani tuwatoe, lakini tusije tukajinyima haki zetu wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde nimtake Mchungaji akatubu, aliombee Bunge hili, aliombee na Taifa hili, aombee na sheria hii iweze kupita na Watanzania waweze kunufaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nasema Mungu aibariki sana Tanzania, abariki umoja wetu katika miaka hii hamsini ambayo tunakwenda kuiadhimisha, ni mambo mengi tumeyafanya, ni mambo mengi yametekelezeka na ndiyo maana mpaka sasa hivi kuna Wabunge wa Upinzani ndani ya Bunge, yote haya tunasema ni mafanikio ndani ya miaka hamsini. Basi tuanzie hapa tushikane kwa pamoja, tuache tofauti zetu ili tuweze kujenga Taifa letu. Asante sana.