You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Mlata, Martha Mosses[CCM]

Special Seat
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 2 9 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kabla ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake makubwa kwa kunijalia na kuwapa moyo wananchi na wanawake wa Mkoa wa Singida, kwa kuweza kunichagua tena ili niweze kurejea katika Bunge hili na kuwawakilisha, nashukuru sana kwa hilo, Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niungane na wale wote ambao wameipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati analifungua Bunge. Kwa kweli, mambo yote aliyoyasema Mheshimiwa Rais na yale ambayo amekusudia Serikali yake iyafanye, ninaamini kabisa mambo mengi yatatekelezwa kwa sababu Baraza lake la Mawaziri alilolipanga, ni chapakazi, hivyo kila kitu kitakwenda barabara, nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisingekuwa mbali na Mheshimiwa Rais katika kuzungumzia suala la amani. Kuna watu wengi, kila mtu kwa tofauti yake, amekuwa akitafsiri kivyake kuhusu amani lakini mimi binafsi naomba niseme kwamba amani tunayoizungumza na amani ambayo Mheshimiwa Rais alikuwa anaizungumzia na amani ambayo tumekuwa nayo Watanzania mpaka sasa hivi, ni amani iliyo na utulivu na uhuru na mtu anaweza akafanya jambo lolote kwa wakati wowote ilimradi aweze kujipatia kipato katika maisha yake, si amani ile tunayosema kwamba kwa sababu mtu ana kipato kidogo basi amani hakuna, hapana, amani tunayoitaka sisi Watanzania ni utulivu, kuheshimiana na kuwa na staha lakini na kuwa na uzalendo wa nchi yetu. Usimchokoze mtu aliyetulia kwa kuitafuta amani. Muendee mtu kwa staha kwa kuitafuta na kuilinda amani. Kwa hiyo, nataka kuwaomba Watanzania wote, shetani ambaye ameanza kuinyemelea Tanzania yetu, anaonekana ameshaanza kuning’iniza kucha zake kutaka kunyakua amani tuliyonayo, naomba kila mtu kwa dini yake amkemee shetani huyu ili ashindwe katika jina la Mungu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nachotaka kuzungumzIa ni kuhusu Afya ya mama ambayo Mheshimiwa Rais aliizungumzia hasa ya uzazi. Kwanza, naomba kila mtu atafakari na aangalie tulikotoka na hapa tulipo. Serikali yetu, kwa miaka mitano ambayo nimeingia ndani ya Bunge, imefanya kazi kubwa sana hasa vijijini. Wakati naomba Ubunge mwaka 2005, kuna maeneo ambayo sikuweza kwenda hata kwa baiskeli ilibidi nitembee lakini sasa hivi unapita kwa gari na pikipiki. Sasa mafanikio hayo tusiyabeze na sasa tunazungumzia mchakato mzima, ni namna gani tutakavyoweza kupunguza vifo vya akina mama. Kina mama zetu walikuwa wanabebwa kwenye machela, wengine kwenye matenga, wengine kwenye vitanda lakini Serikali yetu imeona kwamba kwa sababu barabara zetu zinapitika na huwezi ukapeleka Ambulance kila Kata, basi hata hizo pikipiki ambazo na Mataifa mengine yanatumia zitumike. Sasa kwa nini tusishukuru hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Watanzania wote tulipokee hilo kwa sababu kila Kata, kila Zahanati au Kituo cha Afya kikiwa na pikipiki ambayo inaweza ikamfikisha mama mjamzito aliyeshindwa kujifungua na anahitaji msaada wa haraka, pikipiki ile itamfikisha kuliko kubebwa kwenye machela. Tukubali kwamba huwezi ukaanza kila kitu ukawa na mambo makubwa, utaanza kwa kidogo lakini baadaye utapanda, tuwe na shukrani mbele za Mungu. Hivyo, naiomba Wizara ipige mbiu, ifanye haraka ilete hizo pikipiki sisi wengine tunazihitaji ili kuokoa maisha ya akina mama, wasiozitaka waache lakini wananchi na akina mama wanazihitaji kuokoa maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Kilimo Kwanza, sitaki kuzungumza mengi, naomba masharti ya kukopesha pembejeo, zile power tillers, trekta, hebu yapunguzwe ili watu wengine, wakulima wetu wengi waweze kukopa kwa sababu masharti yale ni makubwa mno. Huwezi ukasema mimi niwe na ekari 50, akina mama wakiungana hata kama mtu ana ekari tano, tatu au ngapi hazifikii masharti husika. Kwa hiyo, naomba masharti yapunguzwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuuliza ni kwa nini Bodi ya Mikopo inataka kutuchonganisha na wanafunzi? Naomba Bodi ya Mikopo ichunguzwe na ikiwezekana ivunjwe. Utaratibu wa kufikisha pesa kwa wananafunzi wetu ni mbovu, Serikali yetu inakuwa imetoa pesa lakini hazifiki kwa wakati. Naomba ichunguzwe na ikiwezekana ivunjwe na utaratibu ubadilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi alizozifanya kuhusu kukuza Sanaa ya Muziki. Nataka kusema, ile Mastering Machine aliyoitoa, Wizara inawaeleza nini Wasanii wa Tanzania? Kwa sababu ilikokwenda imekwenda mahali ambapo Msanii hawezi kufaidika nayo au Wizara mnapanga nini kuendeleza yale ambayo Rais wetu ametoa? Kwa sababu ile mashine imekwenda mahali ambapo ukimtoa Msanii Singida kule Isanzu hawezi kufaidika nayo. Sasa Wizara naomba nijue Watanzania Wasanii wanafaidikaje na ile Mastering Machine aliyoitoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la wanafunzi waliofanya mitihani ya Kidato cha Nne. Tusifu mafanikio yale kwa sababu wale waliofaulu na hata wale waliofeli, huwezi ukamlinganisha na aliyemaliza Darsa la Saba, lazima tuwe na pa kuanzia. Kwenye shule moja ya Kata unakuta wamefaulu watoto 20, ni sawa tunasikitika kwamba 70 wamefeli lakini wale 20 waliofaulu kama tungekuwa hatuna zile shule za Kata wangekuwa wapi? Kwa hiyo, ni mafanikio makubwa naomba sana kwa sababu pale ndipo tunapoanzia na kujua changamoto zetu kwamba Walimu ni wachache ili tujue tufanye nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu awabariki Watanzania kwa kuiombea amani nchi yetu, amina.