| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 6 | 15 February 2011 | Kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete | ||
Mheshimiwa Spika, napenda kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Masasi kwa kuniamini kuwa ninatosha kuwa Mbunge wao, hivyo kunichagua kwa kishindo sana. Ninasema asante sana. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, ametoa vipaumbele 13 ambavyo ndiyo itakuwa dira ya utendaji kazi wetu na Serikali kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuzungumzia suala la amani katika nchi yetu na kudumisha Muungano wetu. Mheshimiwa Spika, tuna haki ya kuwapongeza viongozi wetu wakuu wa pande zote za Muungano kwa maridhiano yaliyotokea ya kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa hali ambayo imeleta heshima kubwa kwa Taifa letu na kuleta umoja katika utendaji kazi ili kuleta maendeleo na amani huko Zanzibar. Mheshimiwa Spika, katika kudumisha amani na kuwa na Taifa tulivu, ni lazima majibu ya Tume iliyoundwa ya kuchunguza migomo katika Vyuo Vikuu yatolewe. Mheshimiwa Spika, binafsi napata utata, wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanapodai kupata Sh. 10,000/= kwa siku kwa maana kwamba wapate Sh.300,000/= kwa mwezi wakati mfanyakazi aliyeajiriwa wa kima cha chini hajafikia kupata mshahara wa kiwango hicho. Hivyo, nashauri wanafunzi hawa pamoja na wazazi waelimishwe kutambua wajibu wa kuchangia katika elimu ya juu na Serikali isaidie kwa wale ambao uwezo wao ni mdogo. Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni juu ya ukusanyaji mapato ya Serikali za Mitaa. Katika eneo hili la ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zetu ni tatizo kubwa sana kwani watendaji wetu wamekuwa wabadhirifu wakubwa. Mapato mengi yanakusanywa, lakini hayafiki katika Halmashauri zetu, yanaishia mifukoni mwa watendaji wachache, hivyo kuzorotesha miradi na shughuli nzima za maendeleo ya wananchi wetu. Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Masasi ni Wilaya ambayo hali ya uchumi ni nzuri, lakini fedha inayopangiwa kuendeleza miradi ya maendeleo ni ndogo sana hivyo kusababisha kuwa na miundombinu mibovu. Kwa mfano, upungufu wa madarasa katika shule za msingi, shule za sekondari, nyumba za watumishi, barabara za Vijijini na Mjini na kadhalika. Mheshimiwa Spika, naomba Serikali pale wanaporipotiwa watendaji wanaohujumu mapato ya Halmashauri wachukuliwe hatua kali ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vinachelewesha maendeleo ya wananchi. Mheshimiwa Spika, katika kuondoa umaskini kwa wananchi wetu, Serikali yetu ilipanga utaratibu wa kutoa fedha mkopo maarufu kama fedha za JK. Lengo hili ni zuri sana, lakini hadi hivi sasa wananchi wetu hawajanufaika sana hasa wananchi wa Vijijini ambao ndio hawa wanaoathirika na umaskini uliokithiri. Lakini wanashindwa kunufaika na fedha hizi kutokana na masharti yaliyopo kukidhi kukopesheka. Ushauri wangu kwa Serikali ni kutafuta njia mbadala ya kuwafikia wananchi Vijijini na kutoa mikopo hii kwani kwa kupitia Benki, wamekuwa wakinufaika wachache wenye uwezo waliopo Mijini tu, wale waliopo vijijini wakiendelea kuwa maskini. Mheshimiwa Spika, ninaomba awamu hii tuzingatie hili ili mikopo hii ifike Vijijini kwani maisha ya wananchi wetu yanadidimia siku hadi siku. Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kulitakia heri Bunge hili liwe la amani. Mwenyezi Mungu atuzidishie busara ili tuweze kusimamia maendeleo ya wananchi wetu na kukidhi matarajio ya wananchi waliotupa dhamana kubwa ya kusimamia maendeleo yao. Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsanteni. |
|||||