| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 9 | 21 June 2011 | Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2011 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2011/2012 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 | ||
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Manaibu wake, pamoja na Watendaji wa Wizara, kwa kazi nzuri ya kutengeneza Bajeti nzuri ya mahitaji ya Watanzania. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Mwaka 2011/2012, imetupa matumaini makubwa kutokana hatua zilizochukuliwa za kuleta unafuu wa maisha kwa Wananchi. Hatua ambayo hata wapiga kura wangu wameipongeza ni ile ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwa mafuta ya petroli. Hatua hii italeta afueni katika huduma zote ambazo zilitegemea mafuta ya petroli hususan usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali. Hatua nyingine inayostahili pongezi ni ile ya kuboresha kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati ya umeme. Ninaomba sambamba na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, pia uwepo mkakati wa kuongeza usambazaji umeme vijijini ili kuweka mazingira mazuri ya kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao kama matunda na nafaka. Mheshimiwa Spika, ninapenda kuipongeza Wizara kwa kuahidi kuharakisha maboresho yanayoendelea katika Sekta ya Fedha na utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji, ambazo zitasaidia upatikanaji wa mikopo kwa Wananchi ili waweze kupata mitaji, pamoja na kujiajiri. Hatua hii itasaidia kupunguza matatizo ya ajira kwa vijana. Ninaomba hatua hii iharakishwe kweli kweli. Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kusaidia uboreshaji wa upatikanaji wa pembejeo hususan matrekta ili tuweze kufanikisha Kilimo Kwanza hususan katika maeneo yenye rutuba kama yalivyoainishwa kwenye Hotuba yake. Mheshimiwa Spika, ninaomba nimpongeze sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwa kazi nzuri anayoifanya. Ninaomba waongeze kasi ya kukagua Hesabu za Serikali za Mitaa na ikiwezekana waangalie hali ilivyo kwenye Miradi ya Vijijini. Huko vijijini matumizi ya hela za Serikali pamoja na michango ya Wananchi ni mbaya sana. Hali hii inakatisha tamaa Wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo. Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba, mikakati yote ya kuboresha maisha ya Watanzania inayoahidiwa katika Bajeti ya 2011/2011, itakelelezwa kwa wakati kufuatana na upatikanaji wa fedha. Mheshimiwa Spika, ninaitakia Wizara kila la kheri katika kutekeleza Bajeti hii kwa mafanikio. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. |
|||||