| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 2 | 1 | 8 February 2011 | UFAFANUZI KUHUSU KAMBI RASMI YA UPINZANI | ||
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed na Mheshimiwa David Zacharia Kafulila, waliwasilisha kwako maombi kwa maandishi kuhusiana na kupata nafasi ya kurekebisha fasili ya 11 ya Kanuni ya 113 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007. Baada ya Spika kupokea maombi hayo ya marekebisho ya Kanuni hiyo ambayo katika maombi hayo walitaka neno’RASMI’ lililopo kwenye Kanuni hiyo ambayo inaiweka nafasi ya Kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma kuwa chini ya Chama kimoja cha Upinzani cha CHADEMA, kitu ambacho kwa maoni yao kinavinyima vyama vingine vya Upinzani vinavyowakilishwa Bungeni fursa ya kuongoza Kamati hizo. Aidha, Wabunge hao waliomba neno hilo Rasmi lifutwe katika Kanuni hiyo ili kutoa haki na fursa kwa Mbunge yeyote anayetoka katika Chama chochote cha Upinzani kinachowakilishwa Bungeni kugombea na kuchaguliwa kuongoza Kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma. Wabunge hao walihitimisha ombi lao kwa kuomba marekebisho waliyoyapendekeza yafanyike kabla ya kuundwa kwa Kamati za Kudumu za Bunge. Ombi la Waheshimiwa hao lilikuwa na masuala mawili ndani yake ambayo yalipaswa kushughulikiwa kwa pamoja, masuala hayo ni:- (a) Kufanya mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge ambalo ni suala la Kikanuni. (b) Uundwaji wa Kamati za Kudumu za Bunge ambalo nalo ni suala la Kikanuni. Kwa kuwa suala lenyewe ni la kikanuni na kwa kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 3(3)(a) na (b) cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la 2007, suala lolote la kikanuni linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya Kanuni ni dhahiri kwamba suala hili lisingeweza kushughulikiwa iwapo Kamati ya Kanuni za Bunge isingeundwa kwanza. Kwa kuzingatia hali hiyo busara za Mheshimiwa Spika zilitumika katika kulifanyia kazi suala hili kwa kufanya uamuzi ufuatao:- (a) Kwamba, kwa kuwa suala husika ni la kikanuni na linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya Kanuni za Bunge ni lazima Kamati hiyo iundwe kwanza kabla ya Kamati nyingine za Kudumu za Bunge kuundwa ili ilifanyie kazi suala lenyewe; (b) Kwamba, baada ya kuundwa Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Kifungu cha 3(3)(a) na (b) cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, lilifanyie kazi pendekezo hilo na suala la uundaji wa Kamati za Kudumu za Bunge na kutoa mapendekezo yake Bungeni kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 152(1) ya Kanuni za Bunge; (c) Kwamba, ili kuondoa utata wa tafsiri Kamati ya Kanuni za Bunge ijadili na kupendekeza tafsiri iliyowazi ya maneno “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.” (d) Kwamba ili kuwezesha mchakato wa uundwaji wa Kamati za Kudumu za Bunge kukamilika, Kamati ya Kanuni za Bunge ishughulikie pia mapendekezo ya mabadiliko ya majina ya Kamati hizo ili yaendane na muundo wa sasa wa Wizara za Serikali; na (e) Kwamba, kwa ajili ya uendeshaji bora wa Shughuli za Bunge, Azimio la Kufanya mabadiliko ya Kanuni husika na pia pendekezo la kutengua Kanuni ya 153(1) yawasilishwe Bungeni na Mheshimiwa Naibu Spika katika Mkutano huu wa Pili wa Bunge ili kuwezesha mchakato wa kuunda Kamati za Kudumu za Bunge kukamilika haraka iwezekanavyo. Katika kutekeleza uamuzi wa Spika kama ulivyoelezwa kwenye aya niliyokwishaitaja hapo juu, Mheshimiwa Spika aliunda na kuteua Wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 113 (4), pamoja na Kifungu cha 3(1) cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge ili kulifanyia kazi suala hili. Kamati hiyo iliundwa na jana jioni ilifanya kikao. Wajumbe wa Kamati hiyo ni pamoja na Mheshimiwa Spika Anne Semamba Makinda, Mwenyekiti; Mheshimiwa Job Ndugai, Makamu Mwenyekiti; Mheshimiwa William Lukuvi, Mjumbe; Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe, Mjumbe; Mheshimiwa Jaji Frederick Werema, Mjumbe; Mheshimiwa Anna Magreth Abdallah, Mjumbe; Mheshimiwa Mustapha Akunaay, Mjumbe; Mheshimiwa Tundu Lissu, Mjumbe; Mheshimiwa Andrew Chenge, Mjumbe; Mheshimiwa Makani Ramo Matala, Mjumbe; Mheshimiwa Angela Jasmine Kairuki, Mjumbe; Mheshimiwa Felix Mkosamali, Mjumbe; Mheshimiwa Mohammed Habib Mnyaa, Mjumbe; Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, Mjumbe; Mheshimiwa George Simbachawene, Mjumbe; Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mjumbe na Mheshimiwa Nimrod Mkono, Mjumbe. Kifungu cha 3(3) cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, pamoja na mambo mengine kinaeleza kwamba, moja ya majukumu ya Kamati za Kanuni za Bunge ni kwamba:- (a) Kujadili na kutoa mapendekezo juu ya kufanya mabadiliko katika Kanuni za Bunge; na (b) Kuchunguza na kutoa taarifa juu ya pendekezo lolote linalohusu Kanuni za Kudumu za Bunge ambalo limepelekwa kwa Kamati hiyo na ama Spika, au Mbunge yeyote. Kwa Mamlaka iliyopewa Kamati hiyo kwa mujibu wa vifungu hivyo, Kamati ya Kanuni za Bunge ilikutana jana kama nilivyokwishasema tarehe 7 Februari, 2011 mara baada ya kikao cha briefing, kujadili mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Katika kushughulikia mapendekezo hayo, Kamati hiyo ilijadili na kupitia kwa makini Kanuni za Bunge zinazohusika ili kubaini kama ni kweli au la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaundwa na Chama chenye haki ya kuchagua kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kama inavyodaiwa na Wabunge waliowasilisha maombi ya marekebisho ya Kanuni. Katika mjadala huo kuhusiana na tafsiri ya maneno Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Kanuni ya 14 hadi ya 16 zinafafanua kuhusu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na jinsi anavyochaguliwa, Kanuni ya 14,15 na 16. Kanuni hizo pia zinafafanua kwamba, Chama chenye haki ya kuchagua kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kile chenye idadi ya Wabunge wengi wasiopungua asilimia 12 na nusu ya Wabunge wote. Aidha, Kanuni ya 15(2) inafafanua pia kuwa, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni atateua Wabunge wa Chama chake au Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao watakuwa wasemaji wakuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara zilizopo Serikalini. Kutokana na masharti ya Kanuni hiyo, Kamati ya Kanuni za Bunge iliridhika pamoja pasipokuwa na mashaka yoyote kwamba tafsiri sahihi ya maneno Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni Kambi inayoundwa na Vyama vya Upinzani vinavyowakilishwa Bungeni kwa mujibu wa masharti ya fasili ya pili ya Kanuni za kudumu za Bunge. Kwa tafsiri hiyo si kweli kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaundwa na Chama cha Upinzani chenye Wabunge wengi na chenye haki ya kuchagua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hitimisho, kwa kuzingatia ukweli huo Kamati ya Kanuni za Bunge yenye wajumbe niliokwishawataja ilipendekeza maneno Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yawekewe tafsiri, kwa maneno mengine hakuna badiliko lolote ambalo litafanyika ndani ya kitabu cha Kanuni mahali popote pale zaidi ya ufafanuzi kwenye eneo la tafsiri, ambao utasomeka kama ifuatavyo:- “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni maana yake ni Kambi ya Upinzani inayoundwa na Vyama vya Upinzani vinavyowakilishwa Bungeni kwa mujibu wa masharti ya fasili ya (2) ya Kanuni ya 14 ya Kanuni hizi.” Kamati hiyo iliyokutana jana ilijiridhisha pia kwamba tafsiri hiyo itaondoa utata uliopo na kulifanya ombi la Wabunge wahusika la kuifanyia marekebisho ya Kanuni ya 113(11) kutokuwa na ulazima wowote. Kutokana na uamuzi huo Kamati ya Kanuni za Bunge imetoa mapendekezo ili yaridhiwe na Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 152(2). Mapendekezo yenyewe ni:- (a) Tafsiri iliyo wazi ya maneno Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; (b) Kufanya marekebisho kwenye nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 ili majina ya Kamati za Kudumu za Bunge yaendane na Muundo wa sasa wa Wizara za Serikali; na (c) Kutengua Kanuni ya 153(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 ili kuwezesha mabadiliko hayo kuanza kutumika baada ya kupitishwa na Bunge. Kwa mujibu wa Kanuni ya 152(1) mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni yanapaswa kupitishwa na Bunge kwa Azimio la Bunge. Ili kuliwezesha Bunge kupitisha Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Kamati ya Kanuni za Bunge ya Mabadiliko katika Kanuni zetu, sasa naomba kusoma Azimio husika. Kwa kuwa, Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed Mbunge wa CUF na Mheshimiwa David Zacharia Kafulila Mbunge wa Chama cha NCCR Mageuzi waliwasilisha kwa Mheshimiwa Spika maombi kwa maandishi ya kurekebisha fasili ya 11 ya Kanuni ya 113 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007; Na kwa kuwa, baada ya kupokea Spika kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Kanuni ya 53(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, aliyapeleka maombi hayo kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge; Na kwa kuwa, kifungu cha 3(a) cha nyongeza ya Nane ya Kanuni hizo, kinaelekeza kwamba majukumu ya Kamati ya Kanuni za Bunge ni pamoja na kujadili na kutoa mapendekezo kuhusu kufanya mabadiliko katika Kanuni za Bunge na kuchunguza na kutoa taarifa kuhusu pendekezo lolote linalohusu Kanuni za Kudumu za Bunge ambalo limepelekwa kwa Kamati hiyo na Spika au Mbunge yeyote; Na kwa kuwa, Kamati ya Kanuni za Bunge kwa madaraka iliyonayo kwa mujibu wa kifungu hicho cha nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge imejadili na kutoa taarifa yake kuhusu pendekezo la kufanya mabadiliko katika Kanuni ya 113(11) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007; Na kwa kuwa, Kamati ya Kanuni za Bunge imejadili na kupendekeza kwamba tafsiri ya 11 ya Kanuni ya 113 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 haina ulazima wa kufanyiwa marekebisho kama ilivyoombwa na Wabunge husika niliokwishawataja; Na kwa kuwa, kwa ajili ya kuondoa utata wa tafsiri, Kamati ya Kanuni za Bunge imependekeza pia kuwepo kwa tafsiri ifuatayo:- “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni maana yake ni Kambi ya Upinzani iliyoundwa na Vyama vya Upinzani vinavyowakilishwa Bungeni kwa Mujibu wa Masharti ya Fasili ya Pili ya Kanuni ya 14 ya Kanuni hizi” ; Na kwa kuwa, Kamati ya Kanuni za Bunge imejadili na kupendekeza kwamba nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 inahitaji kufanyiwa marekebisho kwa kubadilisha majina ya Kamati za Kudumu za Bunge ili yaendane na muundo wa sasa wa Wizara za Serikali ambayo natumaini Waheshimiwa Wabunge natumaini kila mmoja ana kiambatanisho chenye kuonesha jina la Kamati na Wizara ambazo Kamati hiyo itasimamia; Na kwa kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 152(1) Bunge lina mamlaka ya kupitisha Azimio la kufanya mabadiliko katika Kanuni yoyote kutokana na mapendekezo ya Kamati ya Kanuni za Bunge, ili kuwezesha marekebisho yaliyopendekezwa kuanza kutumika mara baada ya kupitishwa na Bunge, Kamati ya Kanuni za Bunge inapendekeza Kanuni ya 153(1) itenguliwe; Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 zinafanyiwa mabadiliko kwa kuweka tafsiri ya maneno Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa kupitisha muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge, kama ulivyopendekezwa na Kamati ya Kanuni za Bunge kwenye kiambatanisho cha Azimio hili na pia kwa kutengua Kanuni ya 153(1). Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. |
|||||