You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Mntangi, Herbert James[CCM]

Muheza Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 3 10 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia na kutafakari yale ambayo Mheshimiwa Rais aliyazungumza. Naomba niseme kwamba tumempongeza sana Mheshimiwa Rais, tumekupongeza wewe kwa kuwa Spika na tunawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuteuliwa, lakini naomba pia niwakumbuke wananchi Wilaya ya Muheza ambao wameweza pia kunirejesha upya katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nitachangia katika maeneo makubwa mawili. Moja, nitatizama hali ya amani na namna ya kudumisha amani kama alivyozungumza Mheshimiwa Rais. Lakini vilevile nitatizama katika sekta ya maji na mazingira. Nianze kwa kusema haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, tusipolijengea heshima Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dhahiri kwamba ile hadhi yake kama mmiliki mmojawapo itashuka. Bunge ni chombo na mhimili wa kitaifa na lazima hilo tulijue na tuhakikishe tunalijengea heshima Bunge hili. Tusipofanya hivyo, heshima ya Bunge itashuka. Tutizame sana kauli zetu, tutizame sana vitendo vyetu tuweze kuhakikisha tunalo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge lisilokuwa na itikadi za chama, Bunge lenye heshima, Bunge linalotarajiwa kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, niseme tena jambo lifuatalo, “giza haliwezi kuondoa giza.” Methali hii nimeipata kwa Padri mmoja wa Kanisa Katholiki kule Bukoba. Kwanini giza haliwezi kuondoa giza? Tujikumbushe huko tulikotoka, tuna miaka 50 ya uhuru na katika miaka hiyo 50 miaka 34 tumekuwa na mfumo wa chama kimoja na katika mfumo huo wa chama kimoja na Katiba tuliyokuwanayo ilikuwa inatuelekeza na kutuongoza na imetuongoza na tumeweza kupata heshima duniani na amani na utulivu katika taifa hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya miaka hiyo ya 1995 tukabadilisha mfumo, tukaingia katika Mfumo wa Vyama Vingi. Ni dhahiri kwamba lazima Katiba ibadilike. Lakini utaratibu wa kubadilisha Katiba ulikwishafanyika na ndiyo maana ile Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1991 na vilevile Tume ya Jaji Kisanga mwaka 1998 zilifanya kazi kwa kupita na kuwashirikisha wananchi kutoa maoni yao. Ni kweli hali ya maisha inaendelea kubadilika, na kwa msingi huo ni lazima tukubali na sasa wote tunakubali kwamba ipo haja ya kuipitia upya Katiba. Tuweze kwenda na hali ya maisha yetu ya leo. Hilo Mheshimiwa Rais amekwishalikubali na sisi wananchi tumeridhia.

Mheshimiwa Spika, giza haliondoi giza. Giza lilikuwepo na lipo kwenye Katiba na ndiyo maana lazima tufanye marekebisho. Tutaondoaje giza hilo? Si kwa giza, tutaliondoa giza kwa kuweka mwanga. Mwanga kwetu sisi maana yake nini? Mwanga kwetu sisi ni elimu. Elimu ya nini? Kwanza wengi hata hiyo Katiba iliyokuwepo sasa hivi tunayoitumia ambayo imetuwezesha hata sisi kufika hapa Bungeni leo kwa nafasi mbalimbali wengi hawaifahamu. Giza hilo. Lakini ni kweli tunasema yapo matatizo yanayohitaji marekebisho katika Katiba. Matatizo hayo ni yapi? Giza hilo. Mwanga ni elimu.

Kwa hiyo, lazima tutoe elimu ya Katiba kwanza iliyopo na pili kuchambua na kutathmini mapungufu yaliyopo katika hiyo Katiba na la tatu ni kupendekeza na kuridhia marekebisho ya mapungufu ya Katiba iliyopo kwa kuwashirikisha wananchi wote. Tumpe nafasi Mheshimiwa Rais, aunde Tume ya kuanza mchakato mzima wa marekebisho ya Katiba. Tuunge mkono na tufanye kazi kwa dhati. Tutakuwa tumepata elimu, tutafanikiwa kuliondoa giza. Giza haliondoi giza.

Mheshimiwa Spika, wanaotaka kutekelezwa kwa Katiba mpya ambayo wala haijaanza kuandaliwa wala haijafanyiwa tathimini ndiyo wanaotuletea matatizo na migogoro katika nchi. Wanawashawishi watu ambao hata hao wananchi, hata yale mahitaji muhimu ya hiyo Katiba mpya bado hawayafahamu. Migogoro isiyokuwa na sababu, kauli zetu viongozi tuzitathimini tunapozizungumza. Zipo kauli, hamnijui mimi! Hamumjui Fulani! Tanzania haitatawalika? Hizo kauli gani? Tuziondoe, hazitusaidii, zinawaweka watoto wetu mahali pabaya, familia zetu na Watanzania kwa ujumla. Likitokea tatizo, sisi wenye uwezo ndio wa kwanza kukimbia tunawaacha wale wasiokuwa na uwezo, wao ndiyo wanapambana na hayo ambao tumeambiwa hapa si mabomu yale. Tunayaita mabomu. Giza haliondoi giza.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye maji na mazingira. Muda unakimbia sana. Ahadi za Mheshimiwa Rais ni nyingi, lakini nina uhakika Baraza alilounda litasaidia kuziondoa. Maji Muheza na hali ya mazingira ni mambo ambayo ni muhimu sana. Hizo ndiyo ahadi zilizoko mbele yetu katika Wilaya yetu ya Muheza na kwa uhakika viongozi mliopo mumsaidie Mheshimiwa Rais kuhakikisha yanatekelezwa. Maji Muheza Mjini, Mheshimiwa Waziri wa Maji yupo, najua jitihada anazofanya, tunakuombea Mwenyezi Mungu akubariki na asaidie Taifa hili tatizo la maji Muheza Mjini litakwisha.

Lakini vilevile barabara, ahadi za Mheshimiwa Rais, barabara ya Muheza kwenda Amani, mashamba makubwa ya chai, chai inachelewa kufika katika masoko ya kimataifa, minada inayofanyika Mombasa, lakini tunategemea sana mapato ya fedha za kigeni kutokana na mashamba makubwa ya chai yaliyoko Amani Muheza. Tusaidie barabara ile kwa hakika itengenezwe.

Mheshimiwa Spika, ahadi kubwa nyingine ya Mheshimiwa Rais inahusu mashamba. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, yupo pale, ni mtaalam mzuri sana. Asilimia 60 ya ardhi ya Wilaya ya Muheza imechukuliwa na mashamba ya katani, mashamba ambayo hayaendelezwi mpaka sasa. Tumeomba hati zifutwe, mashamba yarejeshwe kwa wananchi wapate ardhi, Kilimo Kwanza iwe kweli Kilimo Kwanza kwa dhati na kwa vitendo. Nitaendelea kukumbusha, Wizara zinazohusika nilizozitaja kuhusu maeneo hayo.


Lakini mwisho niwakumbushe pia Watanzania wote hali ya hewa sio nzuri sana, hali ya mazingira tumeharibu sana mazingira, ukame unakuja kwa kasi kubwa. Matatizo ya maji yatazidi kuongezeka kwa sababu tumeharibu sana kwa kiasi kikubwa vyanzo vya maji. Wizara inayohusika na mazingira isaidie Halmashauri zetu. Wapime maeneo ya vyanzo vya maji na kwa hakika tutunze vyanzo vya maji. Muheza tunategemea Mto Zigi na umeanza kukauka.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.