You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Maghembe, Prof. Jumanne Abdallah[CCM]

Mwanga Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 32 25 July 2011 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo Maji na Mifugo inayohusu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, sasa lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa mwaka wa Fedha wa 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mwanga, tunaungana na Watanzania wenzetu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampa heko Mheshimiwa Rais kwa kuongoza Chama cha Mapinduzi na kupata ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais kupata asilimia 74 wa Wabunge wote wa Bunge hili na asilimia 84.5 ya Madiwani wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushindi huo ni kielelezo cha imani na matumaini waliyonayo Watanzania kwa uwezo alionao wa kuliongoza Taifa letu. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa kuchaguliwa tena na wananchi wa Jimbo la Katavi na kwa kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais na kupitishwa na Bunge hili kuwa Waziri Mkuu. Kuteuliwa kwake kunatokana na uwezo wake mkubwa na umahiri aliouonyesha katika kutenda na kusimamia kazi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Anne Semambo Makinda, Mbunge wa Njombe Kusini kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na Spika wa Bunge letu Tukufu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai Mbunge wa Kongwa kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Nawapongeza pia wewe mwenyewe Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho, Mheshimiwa Sylvester Massele Mabumba, Mbunge wa Dole na Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe kwa kuchaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa ama kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Wabunge. Kuchaguliwa na kuteuliwa kwao kunatokana na uwezo wao wa kuongoza na kuaminika kwa wananchi waliowachagua na Rais aliyewateua. Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wananchi wamekipa tena Chama cha Mapinduzi (CCM) ridhaa ya kuliongoza Taifa hili kwa kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Wabunge wengi kutoka Chama cha Mapinduzi. Huu ni ushahidi kuwa Sera za Chama cha Mapinduzi zinakubalika na zinatekelezeka. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuzinadi Sera hizo kwa umahiri mkubwa mpaka CCM ikapata ushindi mkubwa. Kazi iliyo mbele yetu sasa ni kuzitekeleza vizuri sera hizo ili kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza Taifa hili kwa miaka mingi ijayo. Aidha, nawapongeza Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa kuteuliwa na kupewa madaraka hayo na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kwa kukipa kilimo msukumo mpya. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati alipozindua Bunge hili Tukufu tarehe 18 Novemba, 2010 aliainisha maeneo ambayo yataleta mapinduzi katika kilimo. Aidha, katika kipindi hicho kifupi tayari Mheshimiwa Rais alitembelea Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika; Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula; alizindua Kituo Mahiri cha Teknolojia (Dakawa Center of Excellence); alizindua Andiko (Blue Print) la Mpango wa Kilimo wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania- SAGCOT) Davos, Uswisi na kuwa mgeni rasmi kwenye siku ya Ushirika Duniani. Katika shughuli zote hizo alitoa miongozo na maagizo ambayo yametupa changamoto na mchango mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vilevile, katika hotuba zake za mwisho wa mwezi, Mheshimiwa Rais amekuwa akifafanua masuala mbalimbali kuhusu kilimo ambayo yametoa hamasa kubwa kwa wadau wa kilimo. Hii inaonyesha namna ambavyo Mheshimiwa Rais anavyotoa kipaumbele katika maendeleo ya kilimo nchini. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake wa karibu kwa Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo, Maji na Mifugo chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Profesa David Mwakyusa, Mbunge wa Rungwe Magharibi, kwa ushauri, maoni na ushirikiano mkubwa walioutoa wakati wa maandalizi ya bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2011/2012. Naishukuru sana Kamati kwa kuipokea na kuifanyia uchambuzi wa kina Taarifa ya Utekelezaji ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2010/2011 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2011/2012 katika kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam tarehe 1 na 2 Juni, 2011. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa yamezingatiwa katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani na pongezi za pekee kwa wananchi wa Jimbo langu la Mwanga kwa kunichagua tena kuwa Mbunge wao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2010. Nawaahidi kuwa nitaendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote na kuwashirikisha Wanamwanga wote ili kuharakisha maendeleo ya Wilaya yetu. Aidha, napenda kuishukuru familia yangu kwa kunipa ushirikiano na kuwa wavumilivu katika kipindi chote ninapokuwa katika majukumu ya Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kuwapongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo (Mb.), Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, kwa hotuba zao zilizotoa ufafanuzi kuhusu Hali ya Uchumi na Mwelekeo wa Bajeti ya Serikali na kuelezea kwa muhtasari hali ya kilimo chetu ilivyo hivi sasa na mwelekeo kwa mwaka ujao. Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliowasilishwa umeainisha kilimo kama mojawapo ya maeneo makuu ya kipaumbele. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge waliotumia mijadala ya hotuba hizo kutoa michango ya namna ya kuendeleza sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchango na Ukuaji wa Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo inatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi mpana (Broad Based Growth) kwa kutoa ajira kwa asilimia 77.5 ya Watanzania wote na kuchangia wastani wa asilimia 95 ya chakula tunachokula nchini. Katika mwaka
2010, Sekta ya Kilimo ilikua kwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 3.2 ya mwaka 2009. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta ndogo ya mazao ambayo ilikua kwa asilimia 4.4 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 3.4 mwaka 2009. Ukuaji huo ulitokana na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010; kuimarika kwa miundombinu ya umwagiliaji; jitahada za Serikali za kuongeza ruzuku ya pembejeo za kilimo; na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme-ASDP). Ukuaji wa Sekta ya Kilimo kwa kiasi kikubwa ulichangia katika ukuaji wa Pato Halisi la Taifa ambalo lilikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.0 mwaka 2009. Aidha, kilimo kilichangia asilimia 24.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 24.6 ya mwaka 2009 ikiashiria kuongezeka kwa shughuli za kilimo zinazolenga biashara zaidi kinyume na kilimo cha kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010, thamani ya mauzo ya bidhaa za mazao makuu ya biashara iliongezeka hadi Dola za Kimarekani milioni 559.0, kutoka Dola milioni 479.6 mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 16.6. Ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na kuongezeka kwa bei za mazao mbalimbali, hususan tumbaku na korosho. Mazao hayo yalichangia asilimia 41.6 na asilimia 17.3 mtawalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya chakula kwa mwaka 2010/2011 katika mwaka 2010/2011, hali ya chakula nchini ilikuwa ya kuridhisha kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula katika msimu wa
2009/2010. Tathmini ya uvunaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2009/2010 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2010/2011, iliyofanywa mwezi Desemba 2010 ilionyesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ujumla katika msimu huo ulifikia tani milioni 12.32 zikiwemo tani milioni 7.39 za nafaka na tani milioni 4.92 za mazao mengine. Uzalishaji huo ulitosheleza mahitaji ya chakula ya tani milioni 11.15 kwa mwaka 2010/2011 na kuwepo kwa ziada ya tani milioni 1.18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hali hiyo nzuri kulikuwepo na maeneo yenye upungufu. Tathmini ya kina iliyofanyika kati ya mwezi Septemba 2010 na mwezi Mei 2011, ilibaini kuwa jumla ya watu
1,484,190 walihitaji tani 36,970 za chakula cha msaada. Hadi tarehe 30, Juni 2011 jumla ya tani 30,301.9 za mahindi zilikuwa zimechukuliwa na Halmashauri husika kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kusambazwa kwa walengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza makali ya kupanda kwa bei za chakula katika soko, Serikali iliendelea na zoezi la kuuza tani 50,000 za mahindi kutoka NFRA kupitia wafanyabiashara wenye mashine za kukoboa na kusaga. Utaratibu huo ulihusisha mikoa 13 ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mwanza, Mara, Mtwara, Lindi, Shinyanga na Tabora. Hadi tarehe 30 Juni
2011, jumla ya tani 35,334.3 zilikuwa zimeuzwa chini ya utaratibu huo kwa mgawanyo ufuatao; Mkoa wa
Dar es Salaam tani 12,196.1; Mtwara tani 2,000.0; Pwani tani 1,914.0; Shinyanga tani 2,045.0; Morogoro tani
970.0; Lindi tani 1,250; Mwanza tani 962.0; Kagera tani 468.2; Arusha tani 2,625.8; Kilimanjaro tani 3,196.6; Mara tani 2,161.8; Singida tani 850.0; na Dodoma tani 5,162.9. Serikali ilipunguza bei ya mahindi yanayouzwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kutoka Shilingi 38,000 kwa gunia hadi Shilingi
30,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio ya upatikanaji wa chakula mwaka 2011/2012. Kati ya mwezi Mei na Juni 2011, Wizara kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya Tanzania Bara ilifanya tathmini ya awali ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri wa hali ya chakula kwa mwaka 2011/2012. Matokeo ya tathmini hiyo yanaonyesha kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia tani 12,810,818 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa tani 11,499,414 kwa mwaka 2011/2012. Hivyo, Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya tani 1,311,404. Tathmini hii ilibaini kuwepo na ziada ya chakula katika Mikoa saba ya Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Kigoma, Mtwara na Kagera; utoshelezi katika Mikoa nane ya Morogoro, Lindi, Tanga, Dodoma, Singida, Tabora, Kilimanjaro na Manyara; na upungufu katika Mikoa sita ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Arusha, Pwani na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa chakula nchini, hususan nafaka kwa msimu wa kilimo
2010/2011 (chakula kinachovunwa sasa) unatarajiwa kufikia tani 6,786,600 wakati mahitaji ni tani 7,200,340 na hivyo kuwa na upungufu Kitaifa wa tani 413,740 za nafaka. Aidha, uzalishaji wa mazao ya chakula yasiyo ya nafaka (viazi, muhogo, ndizi, maharagwe, n.k.) unatarajiwa kuwa tani 6,024,217 wakati mahitaji ya Taifa ni tani 4,299,073, hivyo kuwa na ziada ya tani 1,725,143. Pamoja na ziada hiyo na kwa vile wananchi wengi hutumia zaidi vyakula vya nafaka, ni dhahiri kuwa upungufu wa nafaka wa tani 413,740 unaleta tafsiri ya upungufu wa chakula nchini. Tathmini ya awali ya upatikanaji wa chakula imebainisha pia kuwepo kwa upungufu wa chakula katika Wilaya 56 zilizo katika Mikoa 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mazao ya nafaka katika masoko makuu nchini bado iko juu licha ya kuwa huu ni mwanzo wa mavuno na licha ya juhudi za Serikali kutoa akiba kutoka kwenye maghala ya Taifa ili kukabiliana na kupanda kwa bei hizo. Kwa mfano, bei ya mahindi kwa kilo kwa baadhi ya Miji ni kama ifuatavyo: Musoma ni Shilingi 630, Moshi Shilingi 550, Mwanza Shilingi 600, Singida Shilingi 485, Arusha Shilingi 465, Tabora Shilingi 420, Dar es Salaam Shilingi 430 na Shinyanga Shilingi 500. Bei ya wastani ya mahindi ya tarehe 30 Juni ilikuwa Shilingi 430 kwa kilo, bei ya mchele kwa kilo iliongezeka kutoka Shilingi
1,040 mwezi Januari hadi Shilingi 1,225 mwezi Juni 2011 wakati bei za mazao mengine hususan maharagwe nazo zimeendelea kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya chakula Duniani na nchi jirani. Taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) iliyotolewa mwezi Mei 2011, inaonyesha kuwa katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa nafaka duniani unatazamiwa kushuka kwa asilimia 1.2. Kutokana na kushuka huko takriban nchi 30 duniani zinatazamiwa kukabiliwa na upungufu wa chakula na zitahitaji chakula cha msaada.

Nyingi ya nchi hizo ziko katika kundi la nchi maskini zenye kipato kidogo za Afrika, kusini mwa Jangwa la
Sahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla mavuno pungufu hasa kwa mazao ya nafaka yanayotazamiwa katika msimu wa 2010/2011, yataathiri hali ya chakula hususan miongoni mwa jamii za wafugaji katika nchi za Afrika Mashariki. Aidha, baadhi ya nchi jirani hususan Burundi, Somalia, Kenya, Uganda, Congo (DRC), Sudan ya Kusini, Madagascar na Msumbiji zinatazamiwa kuwa na maeneo yatakayokabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na sababu mbalimbali hasa ukame na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu huo, bei za nafaka katika maeneo hayo hususan, Kenya, Uganda, Somalia ya Kusini na Sudan ya Kusini zimeendelea kupanda kuanzia kipindi cha Januari hadi Mei 2011. Bei za juu zaidi zimeripotiwa katika masoko ya Kampala, Mogadishu, Juba na Nairobi ambako kwa ujumla bei za sasa za mahindi zimepanda kwa zaidi ya asilimia 120 ikilinganishwa na viwango vya mwezi Aprili 2011. Kwa mfano, katika soko la Nairobi bei ya mahindi imepanda kutoka Dola za Kimarekani 215 kwa tani au Shilingi 323 za Kitanzania kwa kilo, mwezi Januari hadi kufikia Dola za Kimarekani 465 kwa tani au Shilingi 744 za Kitanzania kwa kilo mwezi Juni 2011 sawa na ongezeko la asilimia zaidi ya 130. Kwa upande wa Kenya tatizo hilo limeongezeka kutokana na kuporomoka kwa thamani ya Shilingi ya Kenya na hivyo bei ya mahindi kupanda sana kwa walaji. Aidha, Serikali ya nchi hiyo imetangaza kushuka kwa uzalishaji wa mahindi kwa magunia milioni 14.8 au tani milioni 1.32. Hali hiyo ya ongezeko la bei ya mazao ya chakula hususan yale ya nafaka imechochea kwa kiwango kikubwa ongezeko la biashara ya mazao ya chakula kutoka nchini kwenda nchi hizo zenye uhaba wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula, hususan nafaka katika mwaka 2011/2012 na kuendelea kupanda kwa bei za vyakula, Serikali inachukua hatua zifuatazo:-

(i) Kuhamisha tani 115,000 za akiba ya nafaka iliyopo kwenye maghala yaliyopo Sumbawanga, Makambako na Songea kwenda kwenye maghala yaliyo karibu na maeneo yenye upungufu wa chakula ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga na Arusha. Hatua hiyo itaiwezesha Serikali kukabiliana na upungufu wa chakula na mahitaji mengine ya soko kwa haraka zaidi na pia itatoa nafasi ya kuhifadhi nafaka zitakazonunuliwa msimu wa ununuzi wa 2011/2012;

(ii) Kuiwezesha NFRA kununua tani 200,000 za nafaka kutoka kwa wakulima wa Mikoa ya Rukwa, Iringa, Mbeya na Ruvuma;

(iii) Kuiwezesha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kununua tani 16,000 za mazao (kwa kuanzia) kutoka kwa wakulima wa mikoa ya Rukwa, Kigoma, Iringa, Mbeya, Ruvuma na Morogoro na kuyauza katika Mikoa yenye upungufu wa chakula. Manunuzi hayo yatatumia fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 na mikopo kupitia taasisi za fedha;

(iv) Kuhimiza wananchi kutumia aina mbalimbali za vyakula ikiwa ni pamoja na muhogo, viazi vitamu, viazi mviringo, ndizi na vyakula vingine ambavyo vinapatikana kwa wingi katika maeneo yao; na

(v) Serikali imeagiza Mikoa na Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula kuongeza upatikanaji wa chakula katika maeneo yao kwa kuhamasisha wafanyabiashara wenye uwezo wa kununua chakula kutoka Mikoa yenye ziada na kuuza kwenye maeneo yenye upungufu wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na bei nzuri ya mahindi na mpunga na mazao mengine ya chakula kwa wakulima, wakulima wengi wanauzia mazao yao shambani na kuna hatari ya kuuza mavuno yote bila ya kujiwekea akiba. Hivyo, Serikali inawahimiza wananchi wote katika ngazi ya kaya hususan wakulima kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya mahitaji ya kaya zao mpaka msimu ujao. Aidha, ili kuepuka hatari ya Taifa kukumbwa na tatizo la upungufu wa chakula, Serikali imefuta vibali vyote ambavyo vilikwishatolewa kwa ajili ya kusafirisha mazao ya chakula nje ya nchi na kusitisha uuzaji wa mazao hayo nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6, kuanzia tarehe 1 Julai, 2011 hadi tarehe 31 Desemba, 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya ushirika nchini, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuimarisha Ushirika kupitia utekelezaji wa Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika nchini (Cooperative Reform and Modernization Program –CRMP). Vyama vya Ushirika viliendelea kufanya vizuri kwa kutoa huduma mbalimbali zikiwemo ununuzi wa mazao na usambazaji wa pembejeo kwa wanachama wake na jamii kwa ujumla. Hadi kufikia Machi 2011, kulikuwa na jumla ya Vyama vya Ushirika 9,397 vikiwemo Vyama vya Msingi 9,316, ambavyo vipo katika mchanganuo ufuatao: Ushirika wa Mazao (Agricultural Marketing Cooperative Societies - AMCOS) 2,811, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) 5,251, Umwagiliaji 108, Mifugo 158, Uvuvi 112, Nyumba 30, Madini 58, Viwanda 178, Walaji 102, Huduma 214 na aina nyingine za Vyama vya Ushirika 293. Aidha, kuna Vyama Vikuu 41, Benki za Ushirika mbili, Chama Kilele kimoja, Shirikisho la Vyama vya Ushirika na miradi 36 ya Pamoja ya Ushirika (Joint Enterprises). Idadi ya wanachama wa vyama vyote hivyo iliongezeka kutoka wanachama
2,100,000 mwaka 2009/2010 na kufikia 2,244,727 mwaka 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, mitaji ya Vyama vya Ushirika kwa ujumla ukiondoa SACCOS ilifikia Shilingi bilioni 7.01 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 4.32 za mwaka 2009/2010. Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo vilikuwa na mtaji wa kukopesha (hisa, akiba na amana) wa Shilingi bilioni 236.80 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 211.30 mwaka 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia
12. Aidha, mikopo iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 463.40 hadi Shilingi bilioni
539.20 katika kipindi hicho ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16. Mikopo iliyotolewa ilitumiwa katika shughuli za biashara, kilimo, viwanda vidogovidogo, ufugaji, ujenzi wa nyumba, karo za shule, ununuzi wa matrekta madogo (power tillers), matrekta makubwa na pembejeo za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya utekelezaji mwaka 2010/2011, Fungu 43, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa mwaka 2010/2011, ilikadiria kukusanya mapato ya kiasi cha Shilingi bilioni 1.438 kutokana na vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na malipo ya hati za ukaguzi wa usafi wa mazao ya kuuzwa nje ya nchi na yanayoingizwa nchini; uandikishaji wa madawa ya kilimo; na malipo ya zabuni mbalimbali. Hadi tarehe 30 Juni, 2011, kiasi cha Shilingi bilioni 2.234 sawa na asilimia 155 ya makadirio kilikuwa kimekusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kupitia Fungu 43 ilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 253.35. Aidha, Wizara ilipokea fedha za nyongeza kutoka Hazina Shilingi bilioni 57 kwa ajili ya ununuzi na usafirishaji wa nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Shilingi bilioni 4.337 kwa ajili ya deni la mbolea ya Minjingu na hivyo kufanya bajeti ya Fungu 43 kufikia jumla ya Shilingi bilioni 314.690. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 210.738 ni fedha za Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni 103.952 ni fedha za Maendeleo. Kati ya fedha za Maendeleo, Shilingi bilioni 3.416 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 100.535 ni fedha za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi tarehe 30 Juni, 2011 fedha za Matumizi ya Kawaida zilizopokelewa kutoka Hazina ni Shilingi bilioni 179.76 sawa na asilimia 85.30 ya kiasi kilichoidhinishwa. Matumizi yalifikia Shilingi bilioni 178.57 sawa na asilimia 99.35 ya kiasi cha fedha kilichotolewa. Aidha, fedha za Bajeti ya Maendeleo zilizotolewa ni Shilingi bilioni 93.88 sawa na asilimia 90.30 ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa. Jumla ya Shilingi bilioni 90.59 zilitumika sawa na asilimia 96.49 ya fedha zilizotolewa.


Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa azma ya Kilimo Kwanza. Azma ya Kilimo Kwanza katika Sekta ya Kilimo inatekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (CRMP).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo inatekelezwa katika ngazi ya Wilaya kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (District Agricultural Development Plans-DADPs) na katika ngazi ya Kitaifa kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo na Taasisi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya – DADPs. Katika mwaka
2010/2011, Wizara za Sekta ya Kilimo ziliendelea kuimarisha utekelezaji wa ASDP katika ngazi ya Wilaya kwa kuboresha Mwongozo wa kuandaa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) kwa kuongeza masuala yanayohusu mazingira, elimu ya biashara, matumizi na usimamizi wa fedha za Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji ngazi ya Wilaya (District Irrigation Development Fund – DIDF).

Aidha, mafunzo yalifanyika kwa Timu za Wawezeshaji wa Wilaya na Waratibu wa ASDP wa Mikoa kwa ajili ya kuboresha uandaaji wa DADPs. Moja ya mafanikio ya mafunzo hayo ni ongezeko la miradi ya umwagiliaji iliyoombewa fedha kutoka DIDF kutoka miradi 262 mwaka 2010/2011 hadi 358 mwaka
2011/2012. Kati ya miradi 358 iliyoombewa fedha, miradi 136 imetengewa fedha katika mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilisimamia utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji iliyoibuliwa na wakulima na kujumuishwa katika DADPs. Aidha, wataalam katika Kanda za Umwagiliaji waliendelea kutoa ushauri wa kitaalam wa utayarishaji, usanifu na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji iliyojumuishwa kwenye mipango hiyo. Kutokana na ushauri huo skimu 113 zilizosanifiwa zilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 31.107 kutoka DIDF kwa utekelezaji. Hivi sasa miradi hiyo ya DADPs iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi mingine iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa kilometa 150 za barabara za vijijini; mabwawa 18; masoko 10 ya mazao na masoko matatu ya mifugo; maghala 31 ya kuhifadhi mazao; machinjio matano na mabanda matatu ya kuanikia ngozi. Vilevile, mashine za kukoboa nafaka 26, kahawa tatu na 31 za kukamulia mafuta zilitolewa kwa wakulima kwa mfumo wa kuchangia gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya matrekta madogo ya mkono (power tiller) 430 na matrekta makubwa 42 yalinunuliwa na Halmashauri na kusambazwa kwa vikundi vya wakulima kwa utaratibu wa uchangiaji wa asilimia 20 ya gharama (cost sharing arrangement). Aidha, mafunzo mbalimbali kwa wakulima na wafugaji yalitolewa ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa Wakulima 34,685; ufugaji bora kwa wafugaji 5,590 na masuala ya masoko na usindikaji kwa wakulima na wafugaji 39,158. Vilevile, mashamba darasa 1,630 na vituo vya mafunzo tisa (9) viliendelezwa. Pia Vituo vya Taaluma vya Kata (Ward Agricultural Resource Centres – WARCs) 21 vilijengwa na Maafisa Ugani
5,814 walipatiwa mafunzo mbalimbali ili kuboresha utendaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara za Sekta ya Kilimo ziliendelea kuboresha Takwimu za Kilimo (Agricultural Routine Data System) kwa kufanya majaribio katika Wilaya za Morogoro Vijijini na Kilosa Mkoa wa Morogoro na Wilaya za Mpwapwa na Kondoa katika Mkoa wa Dodoma na kuunganishwa na mtandao wa kompyuta wa Local Government Monitoring Database System - LGMD2. Lengo ni kuwezesha upatikanaji wa takwimu na taarifa za kupima utekelezaji wa ASDP. Aidha, mafunzo yalitolewa kwa Maafisa Ugani 546 wa Vijiji na Kata, 29 wa Wilaya na wanne wa Sekretarieti za Mikoa hiyo ili waweze kutumia mfumo huo. Mfumo huo ukionyesha mafanikio utaenezwa katika Mikoa na Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project – DASIP) ambao unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya 28 za Mikoa ya Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza na Shinyanga unatumia mfumo wa DADPs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Mradi wa DASIP ulitoa mafunzo kwa wataalam
168 wa Wilaya na 10 wa Mikoa kuhusu kuandaa na kutekeleza DADPs yaliyowezesha Vijiji 780 kuibua miradi na kuandaa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Vijiji hivyo. Kutokana na mafunzo hayo, jumla ya miradi 291 ya kilimo iliibuliwa na jamii. Miradi hiyo ni pamoja na majosho 24, mabanio ya mifereji nane, maghala 23, masoko 23, Malambo 18, barabara za Vijijini 45 zenye jumla ya urefu wa kilomita 110. Miradi mingine iliyotekelezwa ni pamoja na machinjio 21, mabwawa ya kufugia samaki 17, mabirika ya kunywea maji mifugo 11, pampu ya kusukuma maji kwa njia ya upepo moja, vituo vya kukobolea kahawa 13, vituo vya afya na huduma za mifugo vitatu, Vituo vya Taaluma vya Kata vitatu, vituo vya kufundishia wanyamakazi vinne, pampu za umwagiliaji 28, zana za kupandia na kupalilia 25, vituo vya uhamilishaji vitatu na miradi ya hifadhi ya mazingira 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, jumla ya matrekta madogo (power tillers) 300 yalinunuliwa na kusambazwa kwa vikundi 300 vya wakulima katika Wilaya 17 ambavyo vilichangia asilimia 20 ya gharama. Katika kuhakikisha matrekta hayo yanaendeshwa kwa ufanisi na kwa faida, mafunzo yalitolewa kwa wataalam 35 wa zana za kilimo katika Wilaya zilizopata matrekta hayo kwa lengo la kuelimisha wanavikundi walionufaika na matrekta hayo. Mafunzo pia yalitolewa kwa ajili ya kuandaa mipango biashara kwa vikundi hivyo ili matrekta hayo yarudishe gharama za ununuzi na kuzalisha faida. Vilevile, vikundi 3,007 vilivyohitimu mafunzo ya shamba darasa msimu wa 2009/2010, vilipatiwa mafunzo ya kuandaa mipango biashara ili kuviwezesha kuzalisha kwa ufanisi na kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia DASIP, jumla ya skimu za umwagiliaji 27 zilifanyiwa usanifu wa awali mwaka 2010/2011. Kati ya skimu hizo, skimu 23 zilifanyiwa usanifu wa kina na skimu 20 kati ya hizo ujenzi utaanza mwaka 2011/2012. Skimu hizo ni Ishololo (Shinyanga Vijijini), Kahanga (Kahama), Mwasubuya (Bariadi), Mwagwila (Meatu), Nyenze (Kishapu), Masinono (Musoma), Nyamitita (Serengeti), Kisangwa (Bunda), Lutubiga (Magu), Sukuma (Sengerema), Miyogwezi (Ukerewe), Lwenge (Geita), Luhala (Kwimba), Nyisanzi (Chato), Mwiruzi (Biharamulo), Kyakakera (Misenyi), Kyamyorwa (Muleba), Kabanga (Kasulu), Mgondogondo (Kibondo) na Mkuti (Kigoma Vijijini). Skimu zote 20 zitakapokamilika zitakuwa na uwezo wa kumwagilia hekta 3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (National Irrigation Master Plan) wa mwaka 2002. Mkazo uliwekwa katika utayarishaji, usanifu, usimamiaji wa ujenzi, ukarabati wa skimu za umwagiliaji na mabwawa. Aidha, uhamasishaji wa matumizi ya maji chini ya ardhi na teknolojia za umwagiliaji zenye ufanisi katika matumizi ya maji zilipewa msukumo maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya umwagiliaji na ujenzi wa mabwawa. Katika mwaka 2010/2011, Wizara ilijenga na kukarabati skimu 47 zenye eneo la hekta 14,200 ikilinganishwa na lengo la hekta 18,000 na hivyo kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 331,490 mwaka 2009/2010 hadi hekta 345,690 mwaka 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Juni 2011, ujenzi wa mabwawa mawili ya Kahama Nhalanga (Nzega) yenye uwezo wa kumwagilia hekta 500 na Maliwanda (Musoma Vijijini) hekta 100 ulikamilika. Mabwawa mengine sita ya Lwanyo (Mbarali) hekta 1,000; Inala (Tabora Manispaa) hekta 400; Misozwe (Muheza) hekta 100; Mahiga (Kwimba) hekta 242; Mwangeza Iramba hekta 400; na Mesaga (Serengeti) hekta 250 yanaendelea kujengwa na yanatarajiwa kukamilika mwaka 2011/2012. Matarajio kutoka ujenzi wa skimu hizo na mabwawa hayo ni kuongeza eneo la umwagiliaji na uzalishaji wa mpunga, mahindi na mazao ya bustani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ililenga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa skimu za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 95,000 kwenye kanda zote saba za umwagiliaji nchini. Hadi kufikia mwezi Juni 2011, usanifu ulikamilika katika skimu 25 zenye eneo la hekta 54,010.


Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia za umwagiliaji zenye ufanisi na tija. Katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuwahamasisha wadau katika matumizi ya teknolojia za umwagiliaji kwa njia ya matone (drip irrigation systems) katika maeneo yote yenye maziwa, mito na yenye uwezekano wa kupata maji chini ya ardhi. Vilevile, uhamasishaji ulihusu matumizi ya pampu za kusukuma maji kwa miguu, upepo, mionzi ya jua na nishati ya mafuta kwa ajili ya kusukuma maji kwa matumizi ya umwagiliaji. Aidha, Wizara iliendelea kusimamia uanzishaji na upanuzi wa mashamba yanayotumia teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone kwa kutumia maji chini ya ardhi katika skimu ya Kisasida (Singida Mjini) yenye hekta 150 kwa kilimo cha mbogamboga na Chinangali (Chamwino) yenye hekta 120 kwa kilimo cha mizabibu. Umuhimu zaidi unatolewa katika kutumia kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone kutokana na maji yanayosukumwa kwa kutumia nishati ya jua. Aidha, faida ya teknolojia hizo za umwagiliaji ni kutumia maji kwa ufanisi zaidi; kuongeza tija na uzalishaji; kuongeza misimu ya kilimo kwa mwaka; na kuweza kulima mazao mengi kwa mzunguko (crop rotation). Utaratibu huo unawahakikishia wakulima usalama wa chakula na kuongeza pato la kaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilihamasisha matumizi bora na endelevu ya maji kwa umwagiliaji kupitia maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba na Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane). Lengo lilikuwa kuonesha aina mbalimbali za mifumo ya umwagiliaji yenye kutumia maji kwa ufanisi zaidi na tija katika uzalishaji wa mazao. Kadhalika fursa za kutumia nishati mbadala za upepo na jua katika kuendesha pampu za kusukuma maji kwa ajili ya umwagiliaji zilioneshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuratibu na kutoa huduma za kitaalam kwa Halmashauri za Wilaya katika kuandaa na kusimamia utekelezaji na uendeshaji wa skimu
113 za umwagiliaji zilizotengewa fedha kutoka Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji Ngazi ya Wilaya (DIDF)
na 47 zilizotengewa fedha kutoka Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji Ngazi ya Taifa (NIDF).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilishirikiana na Taasisi zinazotoa elimu ya juu ambazo ni Chuo cha Maendeleo na Usimamizi wa Maji (Water Development Management Institute - WDMI) na Chuo cha St. Joseph College of Engineering (SJCE) kuandaa mitaala ya ufundishaji wa kozi za umwagiliaji ngazi za Vyeti, Stashahada na Shahada. Kukamilika kwa mitaala hiyo kutawezesha taasisi hizo kutoa wataalam wenye uelewa wa kina wa fani ya umwagiliaji. Chuo cha Ufundi cha Arusha tayari kimeanza kufundisha wanafunzi 25 ngazi ya Shahada baada ya kukamilika kwa mitaala ya ufundishaji wa kozi za umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi wa ushirikiano wa kitaalam kati ya Tanzania na Japan (Tanzania Japan Technical Cooperation Project-TCP) itakayokuwa ya muda wa miaka mitatu imeanza kutekelezwa. Mradi huo umefuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyowezesha uandaaji wa miongozo ya kitaalam ya kutekeleza miradi ya umwagiliaji kupitia DADPs. Awamu ya pili itahusisha kufundisha namna ya kutumia miongozo hiyo kwa kutumia skimu saba za umwagiliaji za mfano zilizochaguliwa kutoka kila kanda ya umwagiliaji. Skimu hizo ni Mvumi (Kilosa); Kivulini (Mwanga); Bahi- Sokoni (Bahi); Inala (Tabora Manispaa); Mahiga (Kwimba); Mshewe (Mbeya); na Narunyu (Lindi Vijijini).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilianza kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais kupitia tamko alilolitoa tarehe 2 Februari 2011 la kuundwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itakayokuwa chombo maalum cha kuendeleza na kusimamia masuala ya umwagiliaji nchini. Katika mwaka 2010/2011, Wizara ilikusanya maoni ya wadau mbalimbali kuhusu muundo, majukumu na vipengele muhimu vitakavyotumika katika kuandaa mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa kilimo katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuimarisha huduma za utafiti ambazo ziliwezesha kubuni teknolojia bora za kumwezesha mkulima kuongeza uzalishaji wa mavuno na tija. Utafiti huo ni pamoja na mbegu bora, rutuba ya udongo na ushauri wa mifumo ya kilimo na uchumi jamii. Wizara kupitia ASDP iliimarisha Mifuko ya Utafiti na Maendeleo ya Kanda (Zonal Agricultural Research Development Fund-ZARDEFs) na usimamizi wa utafiti kwa kutumia mfumo unaowalenga wadau (Client Oriented Research and Development Management Approach-CORDEMA). Katika mwaka 2010/2011, kupitia ZARDEFs, miradi 123 ya utafiti iliendelea kutekelezwa. Kati ya hiyo, miradi
12 ilikamilika na usambazaji wa matokeo kwa walengwa unaandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara kupitia vituo vyake vya utafiti ilitoa aina mpya 21 za mbegu za mazao zenye sifa zaidi ya zile zinazotumiwa na wakulima kwa sasa. Mbegu hizo ni kahawa Robusta (4) na Arabica (1), viazi vitamu (2), dengu (4), soya (1), nyanya (2), figiri (2), mnavu (2), ngogwe (1) na mchicha (2). Mbegu hizo ziliidhinishwa kitaifa kwa ajili ya matumizi ya wakulima. Aidha, kampuni binafsi iitwayo Pioneer Hybrid Seed Ltd. ilifanya majaribio ya mbegu ya mahindi aina ya P2859 kuhusu ustawi wa mbegu hiyo katika mazingira ya Kitanzania ambapo Kamati ya Taifa ya Mbegu iliridhika na matokeo na kuidhinisha matumizi yake nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilizalisha jumla ya tani 25.92 na vipingili
450,000 za mbegu mama (Breeders‘ seed) za mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency - ASA) kuweza kuzalisha mbegu za msingi. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa mbegu bora zinawafikia wakulima. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya katika Mikoa ya Mtwara na Lindi kupitia vikundi vya wakulima, ilizalisha tani 65 za mbegu za Daraja la Kuazimiwa (Quality Declared Seeds - QDS). Kati ya hizo tani 35 ni za karanga na tani 30 za ufuta. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya za Lushoto na Babati kupitia vikundi vya wakulima ilizalisha mbegu za maharagwe aina ya Lyamungo85 tani 3 na Lyamungo90 tani 2.45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilifanikiwa kubuni mbinu za uzalishaji wa mazao ambazo zitaongeza tija. Teknolojia hizo ni pamoja na zile za kutumia mbinu endelevu za kupunguza matawi na kuelekeza mizabibu (pruning and training of grapes) na kupelekwa kwa wakulima wa Kanda ya Kati. Katika zao la korosho utafiti umependekeza kwa wakulima dawa aina ya Weedall na Kalachi zenye nguvu za kuua magugu aina zote katika mashamba ya mikorosho. Aidha, Wizara imetathmini na kupendekeza aina tatu za dawa ya Bayfidan, Timefon na Falmenol pamoja na Salfa ya maji aina ya Uganoll 580 WP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa wakulima wa zao la migomba wanakuwa na ndizi katika kipindi chote wakati wanaendelea kudhibiti ugonjwa wa mnyauko, utafiti umependekeza utaratibu wa kung’oa migomba yenye ugonjwa na kupandikiza migomba mipya kwa awamu (Sequential Uprooting and Replanting) ambao umeonyesha kuwa unarudisha uhai wa shamba la migomba bila kukosa mazao kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kudhibiti magugu, magonjwa na wadudu waharibifu wa mimea na mazao, Wizara ilitoa teknolojia za matumizi ya madawa ya asilia, madawa ya madukani na udhibiti husishi. Baadhi ya matokeo ya utafiti huo ni matumizi ya Muarobaini na Dawa ya Carbofuran 5G katika kupunguza mashambulizi ya fukuzi kwenye migomba na matumizi ya dawa aina ya ‘Amistar 330EC’ kudhibiti magonjwa ya majani kwenye ngano na shayiri. Vilevile, utafiti uliofanyika katika zao la korosho ulionyesha kuwa dawa aina ya Weedall na Kalachi zina nguvu za kuuwa magugu aina zote katika mashamba ya mikorosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, ili kupunguza matumizi ya madawa ya viwandani, gharama za matumizi ya madawa pamoja na kuhifadhi mazingira, utafiti umetathmini na kupendekeza matumizi ya manyigu (Diadegma sp.) ili kudhibiti nondo mwenye mgongo wa almasi (Diamond back moth) ambaye anashambulia zao la kabeji. Teknolojia hiyo imepokelewa na kuleta mafanikio kwa wakulima wa Arumeru na Lushoto. Aina mpya 361 za nasaba za mimea zilikusanywa ambazo ni pamoja na aina 200 za migomba, aina 24 za muhogo, aina 50 za kunde, aina 20 za mbaazi na aina 17 za soya. Pia aina 50 za nasaba za viungo zilihifadhiwa. Aidha, aina mpya ya mgomba ijulikanayo kama East African Highland Bananas ‘Sensu Lato’ ambayo ni tofauti na aina zingine za “East African Highland Banana ‘Sensu Stricto’ ilitambuliwa na hivyo kuongeza idadi ya nasaba zinazojulikana duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mifumo ya kilimo na uchumi sayansi jamii, katika mwaka
2010/2011, Wizara iliendelea kufanya utafiti wa kutathmini gharama na mapato yanayoweza kupatikana katika kilimo cha mazao mbalimbali katika maeneo tofauti. Matokeo yanaonesha kuwa faida anayopata mkulima inaongezeka kama akitumia pembejeo kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo. Kwa mfano, wakulima wa mpunga wa Kanda ya Ziwa waliopanda mbegu bora za mpunga na kufuata ushauri wa kilimo bora, walipata faida ya Shilingi 1,407,000 kwa hekta wakati wale ambao hawakutumia mbegu bora na bila kufuata kanuni bora walipata faida ya Shilingi 639,200 tu ikiwa ni pungufu kwa Shilingi 767,800 ambayo ni pungufu zaidi ya asilimia 100. Kwa upande wa kilimo cha mahindi faida inayoweza kupatikana ni Shilingi 516,100 kwa hekta kwa kutumia pembejeo zilizopendekezwa, ikilinganishwa na Shilingi 367,000 kwa wale wasiotumia pembejeo zilizopendekezwa kikamilifu. Mwelekeo huo unaonekana kwenye mazao mengine kama pamba, kahawa, mtama, korosho, ufuta na alizeti. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa matumizi ya teknolojia bora na kuzingatia kanuni za kilimo bora yana faida kubwa kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha Vituo na kuimarisha uwezo wa Watafiti katika mwaka
2010/2011, Wizara ilifanya ukarabati wa nyumba 13 za watumishi katika Vituo vya Makutopora, Ukiriguru, Uyole, Naliendele, Tumbi, Ilonga na Maruku na ujenzi wa nyumba mpya Seliani. Aidha, vituo vitano vya Utafiti vya Tumbi, Mikocheni, Uyole, Naliendele, Selian na Makutopora, vilipatiwa samani za ofisi ikiwa ni pamoja na viti, meza na kabati. Vilevile, ulifanyika ununuzi wa magari matatu kwa ajili ya Vituo vya Mlingano na Makao Makuu ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ilikamilisha ujenzi wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo kwa Wakulima Dakawa, Morogoro. Kituo hicho kilifunguliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Aprili, 2011. Kituo kitakuwa na kazi zifuatazo: kuonyesha teknolojia za Kitanzania na Kichina; kutoa mafunzo kwa wakulima ikiwa ni pamoja na ujasiriamali kwenye kilimo cha mbogamboga, mahindi na ufugaji wa kuku wa kisasa; kuzalisha miche kwa njia ya Tishu (Tissue Culture); na kufanya utafiti kwa mazao ya mahindi, mpunga na mazao ya mbogamboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliendelea kuimarisha Kituo cha KATRIN ili kukipandisha hadhi ya kuwa Kituo Mahiri cha Utafiti (Centre of Excellence) kwa zao la mpunga. Kituo hicho kimepatiwa vitendea kazi kupitia Programu ya Kilimo ya Kuendeleza Tija na Uzalishaji katika Afrika ya Mashariki (Eastern Africa Agricultural Productivity Programme). Aidha, kupitia programu hiyo, Vituo vya Dakawa, Uyole, Ukiriguru na Mikocheni vimenufaika kwa kupatiwa vitendea kazi vikiwemo magari manne, mashine

za kurudufia 13 na kompyuta 29. Serikali itawekeza zaidi katika vifaa vya maabara, mafunzo kwa wataalam na nyenzo za utafiti katika kukitayarisha Kituo cha KATRIN ili kifikie matarajio ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iligharamia mafunzo kwa watafiti kwa lengo la kuwajengea uwezo. Jumla ya watafiti 20 walipatiwa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu. Kati ya hao watafiti 11 ni wa Shahada ya Uzamili (MSc) na watafiti tisa (9) ni wa Shahada ya Uzamivu (PhD). Vilevile, Watafiti 45 walipata ufadhili wa mafunzo kupitia fedha zilizotengwa kuimarisha uwezo wa Watafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Kati ya hao Watafiti 33 ni wa Shahada ya Uzamili na 12 ni wa Shahada ya Uzamivu. Watafiti wengine 20 walipata mafunzo ya muda mfupi ya mbinu za utafiti (research methodologies) na wengine 40 walipata mafunzo katika fani ya Uandishi wa Tungo (Winning Proposal Writing). Pia, Watafiti Wachumi 35 walipata mafunzo ya wiki moja ya jinsi ya kufanya uchambuzi wa mnyororo wa thamani ya mazao (value chain analysis) na jinsi ya kufanya uchambuzi wa upokeaji wa teknolojia na matokeo yake (Adoption and impact analysis) kwa kutumia programu ya kompyuta ijulikanayo kama Data Analysis and Statistical Software (STATA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ikishirikiana na TAMISEMI iliendelea kuimarisha Huduma za Ugani kwa wakulima kwa kutumia mbinu shirikishi jamii katika kilimo, hususan Shamba Darasa. Wizara ilitoa mafunzo rejea ya Wakufunzi Wawezeshaji (Training of Trainers-TOT) wa Shamba Darasa kwa Maafisa Ugani 73 kutoka Halmashauri 40 za Mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Kagera, Tabora na Shinyanga. Aidha, kupitia Programu ya Kilimo ya Kuendeleza Tija na Uzalishaji (Eastern Africa Agricultural Productivity Programme- EAAPP), Tanzania ikiwa ni kinara katika kilimo cha mpunga, Wizara ilitoa mafunzo ya Wakufunzi Wawezashaji katika kilimo cha mpunga kwa Maafisa Ugani 100 kutoka Halmashauri 20 za Igunga, Nzega, Bahi, Bagamoyo, Rufiji, Kilombero, Mvomero, Kilosa, Kahama, Shinyanga, Sengerema, Misungwi, Kwimba, Bukombe, Maswa, Kibondo, Magu, Mbarali, Kyela na Iringa ambayo yalifanyika Kilimanjaro Agricultural Trainning Center (KATC). Pia ziara za mafunzo zilifanyika kwa wakulima 40 na Maafisa Ugani wanne kutoka Halmashauri za Mvomero, Mwanga na Moshi. Wakulima kutoka Kilombero na Mwanga walitembelea wakulima wenzao katika skimu za umwagiliaji za Mkindo na Lower Moshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliboresha Mwongozo wa kuanzisha na kuendesha Vituo vya Taaluma vya Kata (Ward Agricultural Resource Center - WARC) na kutoa toleo la pili ambalo lilifafanua zaidi matumizi ya WARCs na namna ya uendeshaji wa vituo hivyo kwa kushirikisha Sekta binafsi. Aidha, Wizara iliwezesha wakulima 593,400 kupata mafunzo ya kilimo bora na taarifa mbalimbali zikiwemo bei za mazao katika vituo hivyo kwa kuandaa mashamba ya majaribio na kutoa machapisho kupitia Ofisi za Kiungo za Kanda za Utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuimarisha mfumo wa mkulima kufundisha mkulima (Farmer-to-Farmer Extension) kwa kutoa mafunzo kwa wakulima 26,400 ambao wanaendelea kuwafundisha wakulima wenzao mbinu bora za kilimo. Aidha, elimu ilitolewa kwa wakulima kupitia vipindi vya redio, vijitabu, machapisho, vipeperushi, mabango na kuonyesha sinema Vijijini kwa kuzingatia kanda za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI iliajiri vijana ambao ni Wagani tarajali 742 na hivyo kufanya idadi ya Maafisa Ugani kufikia 5,181. Kati ya hao, wataalam 64 wana Shahada ya Uzamili (MSc.), 475 wana Shahada ya Kwanza (BSc.), 4,100 wana Astashahada (Diploma) na 542 wana Cheti (Certificate). Mahitaji ya wataalam katika ngazi ya Kata na Vijiji ni 15,082. Pia, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ilianzisha mchakato wa kuweka vigezo vya kupima utendaji kazi wa Maafisa Ugani wa ngazi ya Kata na Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliratibu na kushiriki maadhimisho ya Nane Nane ambayo yalifanyika kitaifa Mkoani Dodoma kwenye Uwanja wa Nzuguni. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa “Kilimo Kwanza, Mapinduzi ya Kijani, Uhakika wa Chakula na Kipato”. Katika maadhimisho hayo, Wizara ilitoa zawadi mbalimbali kwa washindi ambapo mkulima bora kitaifa alitoka Halmashauri ya Kongwa ambaye alizawadiwa trekta lenye jembe la thamani ya Shilingi 27,000,000, madawa yenye thamani ya Shilingi 12,000, fedha taslim Shilingi 350,000 na Cheti. Mshindi wa pili alitoka Halmashauri ya Manyoni ambaye alizawadiwa trekta dogo la mkono (power tiller) lenye thamani ya Shilingi 7,000,000, madawa ya Shilingi 12,000, fedha taslim Shilingi 300,000 na Cheti. Mshindi wa tatu alitoka

Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na kuzawadiwa jembe la kukokotwa na ng’ombe, mbolea na mbegu vyenye thamani ya Shilingi 1,921,400 na Cheti. Washindi kutoka makundi ya Vyama vya Ushirika akiwemo mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu walipewa zawadi mbalimbali zenye thamani ya Shilingi 5,675,000. Vilevile, washindi watatu kutoka Bodi za Mazao ya Kahawa na Chai walipewa zawadi zenye thamani ya Shilingi 3,750,000 na mshindi kutoka sekta binafsi alipewa zawadi ya Shilingi 10,000,000. Katika kuhamasisha matumizi bora na endelevu ya maji, washindi bora watatu wa kilimo cha umwagiliaji walipewa vifaa vya umwagiliaji vyenye thamani ya Shilingi 7,500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwatambua wadau 15 wa kilimo waliochangia katika kutoa zawadi hizo kama ifuatavyo: Kihelya Auto Tractor-Mwanza, Suba Agro, NMB, INCAR Dar es Salaam, AGRICOM, Tanzania Farmers Service Center (TFSC) Arusha, YARA (CHAPA MELI), Tanzania Fertilizer Company Ltd. (TFC), Export Trading, Minjingu Company Ltd., Pannar Seed Company Ltd., PASS, Bodi ya Chai, Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai–Tanzania Smallholder Tea Development Agency - TSHTDA na Bodi ya Kahawa. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wadau hawa na wengine kuendelea kuchangia katika kutoa zawadi kwa washindi watakaopatikana katika maadhimisho ya mwaka huu yatakayofanyika Nzuguni, Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo kwa wakulima, katika mwaka 2010/2011, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI na Shirika la Maendeleo la Japan - JICA kupitia DADPs ilitoa mafunzo ya msingi (standard training) ya kilimo bora cha uzalishaji wa zao la mpunga kwa njia ya umwagiliaji. Mafunzo yalitolewa kwa wakulima 3,072 katika skimu 12 za Tungamalenga (Iringa Vijijini), Kasyabone/Kisegese (Rungwe), Mshewe (Mbeya Vijijini), Mfumbi (Makete), Madaba (Tunduru), Mvumi (Kilosa), Lupilo (Ulanga), Mbarangwe (Morogoro), Ngongowele (Liwale), Sawenge (Magu), Chereche (Rorya) na Ngage (Simanjiro). Aidha, mafunzo ya uzalishaji wa mpunga aina ya NERICA inayolimwa kwenye maeneo ya juu (Upland) yalifanyika kwa wakulima katika wilaya za Muheza, Kyela, Makete, Morogoro Vijijini, Ulanga, Bagamoyo, Bukombe, Lindi Vijijini na Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya kilimo kwa wataalam, katika mwaka 2010/2011, Wizara iligharamia mafunzo ya wanafunzi 5,557 ngazi ya Stashahada (Diploma) na Astashahada (Cheti). Aidha, wanafunzi 1,942 walihitimu masomo mwezi Novemba 2010 na wengine 2,588 wamehitimu mafunzo yao mwezi Juni 2011. Wizara pia ilidahili wanafunzi 1,072 katika Vyuo vya Kilimo ambao watahitimu mwezi Juni
2012. Wakufunzi wa kilimo 57 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu sahihi za ufundishaji pamoja na usimamizi na uendeshaji wa Vyuo. Mafunzo ya Astashahada ya Kilimo yameanza kutolewa kwa wanafunzi 45 katika Chuo cha Mtakatifu Maria Goreti (Ilula- Iringa) kupitia mfumo wa Public-Private Partnership (PPP) kuanzia Aprili 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilitoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi ili kuimarisha utendaji kazi. Jumla ya wataalam watatu waliendelea kupata mafunzo ya Shahada za Uzamivu (PhD.), 25 katika Shahada ya Uzamili (MSc.) na 23 Shahada ya Kwanza (BSc.). Mafunzo hayo yalihusu Uhandisi wa Kilimo, Uchumi Kilimo, Umwagiliaji, Kanuni Bora za Kilimo na Usimamizi wa Fedha. Wizara pia ilitoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi katika fani mbalimbali. Jumla ya watumishi 149 walipatiwa mafunzo kuhusu uchambuzi wa sera; uandaaji wa bajeti; usimamizi wa fedha; matumizi ya zana za kilimo; usindikaji wa mazao; uchumi; matumizi bora ya maji; uendeshaji, utunzaji, usanifu, usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji; na matumizi ya teknolojia ya kuvuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, makadirio ya mahitaji ya mbolea yalikuwa tani
385,000 zikiwemo tani 200,000 za mbolea ya ruzuku na tani 185,000 za mbolea isiyo ya ruzuku. Jumla ya tani 275,684.8 za mbolea sawa na asilimia 72 zilipatikana. Kati ya hizo, tani 201,050 zilikuwa ni mbolea ya ruzuku ikiwemo mbolea ya kupandia tani 100,525 na mbolea ya kukuzia tani 100,525 ikilinganishwa na tani
150,000 ambazo zilitolewa mwaka 2009/2010. Mbolea ya ruzuku ilinufaisha wakulima 2,011,000 ikilinganishwa na wakulima 1,500,000 walionufaika mwaka 2009/2010. Wakulima walioongezwa walitoka katika Wilaya za Sikonge, Urambo na Igunga (Tabora); Tarime, Serengeti, Rorya na Bunda (Mara); Kahama na Bukombe (Shinyanga); Chato na Karagwe (Kagera); Geita na Sengerema (Mwanza); Mtwara, Newala na Masasi (Mtwara); Lindi (V), Nachingwea na Ruangwa (Lindi); Korogwe, Lushoto, Kilindi, Handeni na Muheza (Tanga); Mpwapwa, Kongwa na Bahi (Dodoma); Bagamoyo na Rufiji (Pwani); Singida (V), Manyoni na Iramba (Singida).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, upatikanaji wa mbegu bora ulifikia tani 26,545 ikilinganishwa na tani 16,148.20 mwaka 2009/2010. Mbegu hizo zinajumuisha mbegu za mazao ya mahindi tani 22,725; mpunga tani 896; mbegu za mafuta tani 676; mikunde tani 486; ngano tani 138; na mtama tani 1,624. Mbegu hizo zilitokana na sekta binafsi na sekta ya umma ambapo sekta ya umma ilizalisha tani
5,678.6, kati ya hizo tani 1,881 ni kutoka ASA; tani 1,489.1 kutoka Magereza na JKT na wakulima wadogo walizalisha tani 2,308 za mbegu za Daraja la Kuazimiwa (Quality Declared Seed – QDS). Aidha, sekta binafsi ilichangia jumla ya tani 20,866.4. Kati ya hizo tani 8,149.4 zilizalishwa nchini na tani 12,717 ziliagizwa kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilitoa ruzuku ya tani 20,357.86 za mbegu bora za mahindi na mpunga ikilinganishwa na tani 15,150 zilizotolewa mwaka 2009/2010. Aidha, Wizara ilitoa tani 15,375 za mbegu ya pamba kwa utaratibu wa vocha. Mbegu za mahindi na mpunga zilisambazwa katika Mikoa
20 inayozalisha mazao hayo kwa wingi na mbegu za pamba zilisambazwa katika Mikoa tisa inayozalisha zao hilo. Vilevile, Wizara ilitoa ruzuku ya mbegu bora za mtama tani 356.25 na alizeti tani 50 nje ya utaratibu wa vocha ikilinganishwa na tani 289.8 za mtama na tani 85.4 za alizeti mwaka 2009/2010 ambazo zilisambazwa kwenye Mikoa ya Singida, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Dodoma na Morogoro. Jumla ya wakulima 110,600 wa zao la mtama na wakulima 10,392 wa zao la alizeti walinufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Taasisi ya Zao la Kahawa (Tanzania Coffee Reserach Institute-TaCRI) ilizalisha miche bora ya kahawa 14,430,000 sawa na asilimia 96.2 ya lengo la kuzalisha miche 15,000,000. Aidha, kupitia Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai, wakulima 2,227 katika vikundi 178 walizalisha miche bora ya chai 10,141,000 na Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (Tea Research Institute of Tanzania- TRIT) ilizalisha miche 3,200,000 na hivyo kufanya uzalishaji wa miche kufikia
14,341,000. Uzalishaji huo ni sawa na asilimia 96 ya lengo la kuzalisha miche 15,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilitoa ruzuku ya madawa ya pamba na korosho ambapo jumla ya acrepack 4,653,159 za madawa ya pamba zilizotosheleza ekari 1,537,500 zilitolewa. Madawa hayo yalinufaisha wakulima 576,710 wa Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Kigoma, Morogoro, Manyara na Pwani. Aidha, jumla ya tani 148 na lita 153,395 za madawa ya korosho zilisambazwa kwa wakulima wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Ruvuma na Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na taasisi ya Citizen Network for Foreign Affairs (CNFA) ilitoa mafunzo kwa Mawakala 3,855 wa Pembejeo za Kilimo (Rural agro-dealers). Mafunzo hayo yalihusu uendeshaji wa biashara, matumizi na hifadhi salama ya pembejeo. Mawakala hao walitoka katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Manyara, Kigoma, Tabora, Mara, Tanga, Shinyanga, Kagera, Mwanza, Lindi, Singida, Dodoma, Pwani na Mtwara. Aidha, kati ya hao, Mawakala 511 walidhaminiwa kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 6.7 kutoka NMB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa utoaji wa pembejeo kwa kutumia vocha, Wizara ilifanya tathmini kuanzia mwezi Oktoba 2010 hadi Aprili 2011 katika Mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Singida, Dodoma, Pwani, Lindi na Mtwara. Tathmini hiyo ilibaini kuwa wakulima walionufaika na pembejeo kuanzia mwaka 2010/2011 wanatarajia kuongeza mavuno kwa ekari kutoka wastani wa tani 0.7 hadi wastani wa tani 2 kwa ekari kwa zao la mahindi na kutoka wastani wa tani 0.4 hadi wastani wa tani 2.5 kwa ekari kwa zao la mpunga. Aidha, Wakulima walionufaika na utaratibu huo kuanzia miaka ya nyuma tangu mpango uanze, wanatarajia kuongeza uzalishaji kuanzia wastani tani 2 hadi tani 2.7 kwa ekari kwa zao la mahindi na mpunga kwa wastani wa tani 2.5 mpaka tani 3.5 kwa ekari. Aidha, uelewa wa wakulima kuhusiana na matumizi ya pembejeo, hususan mbegu bora na mbolea umeongezeka. Hii inadhihirishwa na wakulima kununua pembejeo hizo nje ya mfumo wa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, tathmini hiyo ilibaini mapungufu yafuatayo:-

(i) Kushindwa kukidhi mahitaji ya ruzuku ya pembejeo ambayo ni makubwa kuliko uwezo wa Serikali; (ii) Usimamizi hafifu wa ruzuku ya pembejeo katika baadhi ya Wilaya, Kata na Vijiji;
(iii) Uteuzi wa Mawakala wa Pembejeo wasiokuwa na sifa katika baadhi ya Kamati za Pembejeo za
Wilaya;
(iv) Baadhi ya wakulima kutoelewa umuhimu wa kutumia pembejeo za kilimo; na

(v) Baadhi ya wakulima kutouelewa vizuri utaratibu wa ruzuku na hivyo kurubuniwa na Mawakala wa
Pembejeo ambao hushirikiana na Watendaji wa Vijiji kuwaibia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu huo, Serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na:-

(i) Kuagiza Wakuu wa Mikoa walete taarifa inayoainisha yafuatayo: orodha ya pembejeo zilizopelekwa katika kila Wilaya, Kata na katika kila Kijiji majina ya wakulima waliopewa pembejeo kwa utaratibu wa vocha;

(ii) Kwa kushirikiana na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali inaandaa Ukaguzi Maalum (Special Audit) kuhusu utekelezaji wa mfumo wa pembejeo kwa utaratibu wa vocha kwa lengo la kubaini waliokiuka utaratibu na kuwachukulia hatua za kisheria;

(iii) Kuhimiza usimamizi wa karibu wa utoaji wa ruzuku kwa kushirikiana na Kamati za Vocha za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji katika kutekeleza Waraka wa Serikali uliotolewa kuhusiana na usimamizi wa utaratibu huo; na

(iv) Kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa pembejeo katika kilimo na Mfumo wa Vocha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya zana bora za kilimo yameanza kuongezeka kutokana na jitahada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya zana hizo. Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya trekta yameongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 12 mwaka 2010. Aidha, matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyamakazi yameongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2005 hadi asilimia 24 mwaka 2010. Kutokana na ongezeko la matumizi ya zana hizo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua kutoka asilimia 70 mwaka 2005 hadi asilimia 64 mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, sekta binafsi iliingiza nchini matrekta makubwa
986, matrekta madogo ya mkono 991 na majembe ya kukokotwa na wanyamakazi 103,343. Aidha, Wizara ilitoa matrekta madogo ya mkono 35 kwa vikundi vya wakulima 35 vyenye wakulima 880 kwa utaratibu wa vikundi kuchangia asilimia 20 kufuatana na mwongozo wa DADPs. Matrekta hayo yalitolewa kwenye vikundi vilivyoko kwenye skimu za umwagiliaji za Ruvu (Bagamoyo), Mkula na Njagi (Kilombero), Minepa (Ulanga), Bahi na Matajira (Bahi), Lumuma (Mpwapwa), Mwangeza (Iramba), Kisasida (Singida Mjini) Chikuyu (Manyoni), Nyanzwa na Irindi (Kilolo), Mlenge (Iringa Vijijini), Mpitimbi (Songea), Lekindo (Tunduru), Kasyabone (Rungwe), Mshewe (Mbeya Vijijini), Ngana (Kyela), Mbebe (Ileje), Naming’ongo (Mbozi) Sakalilo (Sumbawanga), Uruira (Mpanda), Ochuna na Chereche (Rorya), Buswahili (Musoma Vijijini), Nyatwali (Bunda), Rungwe Mpya (Kasulu), Rumashi na Ruhwiti (Kibondo), Kitivo (Lushoto), Mombo (Korogwe), Ngage na Lemkuna (Simanjiro), Lekitatu (Meru) na Kitere (Mtwara Vijijini).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, matrekta mengine madogo ya mkono matano yalitolewa kwa utaratibu huo ili kuendeleza Kilimo Hifadhi kwenye Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa vikundi vya: Kilimapunda na Merikinoi (Meru), Mwangaza B (Karatu), Lukundo na Jitegemee (Moshi Vijijini). Aidha, Wizara ilianzisha mashamba darasa yenye ukubwa wa ekari moja katika skimu hizo ambapo wakulima walipatiwa mafunzo kuhusu kilimo bora cha mpunga na matumizi bora ya matrekta madogo ya mkono. Vilevile, mafunzo kuhusu matumizi na huduma ya matengenezo ya matrekta madogo ya mkono yalitolewa kwa maopereta 72 kutoka skimu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilitayarisha mwongozo kwa ajili ya watumiaji wa matrekta makubwa na matrekta madogo ya mkono (powertiller) ili kuwawezesha watumiaji hao kuyatumia matrekta hayo kwa usahihi kwa lengo la kuongeza tija. Vilevile, Wizara ilitoa viwango vya ufundi (technical specifications) kwa ajili ya matrekta madogo ya mkono, mitambo ya kukobolea mpunga na mashine za kukamulia mafuta. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na ya Kusini ilifanya ukaguzi wa matrekta ya mkono kabla ya kupokelewa (pre-delivery inspection) kwa lengo la kudhibiti ubora wa matrekta yanayotolewa na makampuni yaliyoshinda zabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilitoa mafunzo kwa wakulima na maopereta 215 juu ya matumizi na matunzo ya zana mbalimbali ikiwa ni pamoja na matrekta makubwa na madogo, mashine za kupandikiza mpunga (rice transplanters), mashine za kunyunyizia dawa (boom sprayers), mashine ya

kupukuchua mahindi na mashine ya kupura mpunga. Wakulima hao walitoka katika Wilaya za Korogwe, Muheza, Tunduru, Njombe, Kongwa, Babati, Morogoro, Mbozi, Ileje, Mbeya Vijijini, Kyela, Sumbawanga, Nkasi, Mpanda na Simanjiro. Aidha, mafunzo kuhusu kuendesha, kufanya matengenezo madogo na kutunza mashine za kuchakata muhogo na kusindika mbegu za mafuta kwa wakulima 53 yalitolewa katika Wilaya za Kisarawe, Mkuranga na Rufiji. Vilevile, Wizara iliandaa na kutoa mafunzo kwa wakulima
85 katika fani za matumizi bora ya maji, uendeshaji, utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji na matumizi ya teknolojia ya kuvuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashamba Darasa 94 yenye wakulima 8,612 yaliendelezwa katika Wilaya za Meru, Arusha, Karatu, Babati, Hanang na Moshi Vijijini ambapo wakulima waliendelea kujifunza kwa vitendo juu ya matumizi ya zana bora za kilimo hifadhi kama vile ripa na mashine za kupanda bila kukatua (direct seeders). Aidha, wakulima wengine 527 walipata mafunzo katika Mashamba Darasa hayo na kuwezeshwa kuanzisha mashamba ya mfano ya nusu eka kila moja katika mashamba yao binafsi. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Mtandao wa Kilimo Hifadhi Afrika (African Conservation Tillage Network - ACT) na Halmashauri za Wilaya za Kiteto, Kongwa, Kilosa na Mvomero ilianzisha Mashamba Darasa 20 ya matumizi ya zana bora za kilimo hifadhi zinazokokotwa na matrekta. Mashamba Darasa hayo yana ukubwa wa eka tano kila moja na yanasimamiwa na wakulima wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkopo wa masharti nafuu kutoka India, katika mwaka 2010/2011, Serikali ilipata mkopo wenye masharti nafuu (line of credit) kutoka India wa Dola za Kimarekani milioni 40 uliowezesha kuingiza nchini matrekta makubwa 1,860 na zana zake, matrekta madogo ya mkono 400 na pampu za kusukuma maji 1,100 ambayo yanauzwa na SUMA JKT. Wakulima wanashauriwa kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (Tanzania Investment Bank-TIB), Mfuko wa Taifa wa Pembejeo na taasisi zingine za fedha zitakazowawezesha kununua matrekta hayo na pembejeo nyingine za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, katika mwaka 2010/2011, Mfuko wa Pembejeo ulitengewa jumla ya Shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kutoa mikopo ya kununulia na kusambaza pembejeo na zana za kilimo. Aidha, Mfuko ulikusanya marejesho ya madeni ya nyuma ya kiasi cha Shilingi bilioni 3.94. Hadi mwezi Juni, 2011 Mfuko ulipata jumla ya Shilingi 6,484,738,294 kwa ajili ya kutoa mikopo na matumizi ya ofisi. Kati ya kiasi hicho Shilingi 2,540,002,000 zilitoka Serikalini na Shilingi
3,944,736,294 ni marejesho ya mikopo. Mfuko ulitoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 4,516,770,056 ikiwa Shilingi 3,498,768,556 kwa ajili ya ununuzi wa matrekta makubwa 96, Shilingi 217,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa matrekta madogo 19, ununuzi wa pembejeo za kilimo na mifugo yenye thamani ya Shilingi
717,001,500, kukarabati matrekta makubwa manne Shilingi 34,000,000 na kununua zana za umwagiliaji zenye thamani ya Shilingi 50,000,000. Mikopo hiyo ilitolewa kwa wakulima binafsi, wasambazaji wa pembejeo za kilimo na mifugo na zana za kilimo kupitia Benki ya Biashara na Uchumi ya Mkoa wa Kilimanjaro, Benki ya Wananchi Mbinga, Benki ya Ushirika Kagera na Benki ya Wananchi Tandahimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi bora ya ardhi, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilipima maeneo ya ardhi ya Wizara katika Kituo cha Utafiti cha KATRIN (Kilombero) na shamba la mbegu la Bugaga (Kasulu). Aidha, upimaji unaendelea katika shamba la mbegu la Dabaga (Kilolo) na eneo la utafiti wa kilimo ARI-Seliani (Arusha). Lengo ni kupata hatimiliki ya ardhi ya Serikali na kupunguza migogoro inayotokana na uvamizi unaojitokeza mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilitoa mafunzo kwa wataalam 31 waliopo kwenye Vituo vya Kanda na Halmashauri 23. Mafunzo hayo yalihusu teknolojia mbalimbali za hifadhi ya udongo na maji mashambani; utambuzi wa aina za udongo na virutubisho vyake; tathmini ya ubora wa udongo kwa kilimo; uchukuaji wa sampuli za udongo kwa ajili ya tathmini kwenye maabara za udongo; uandaaji wa kina wa mipango ya matumizi bora ya ardhi; kilimo mseto; na ukusanyaji na utunzaji wa takwimu za rasilimali ardhi. Lengo lilikuwa kupata taarifa sahihi za kutumia wakati wa utoaji wa huduma za matumizi bora ya ardhi kwa wakulima. Halmashauri zilizohusika ni Mufindi, Mbeya, Sumbawanga Vijijini, Sumbawanga Mjini, Iringa, Mbarali, Ileje, Mpanda, Tarime, Kishapu, Magu, Bunda, Musoma, Maswa, Bukoba, Kondoa, Iramba, Singida Vijijini, Hanang, Mbulu, Chamwino, Dodoma Mjini na Dodoma Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ilianza kutekeleza Mpango wa Usimamizi na Matumizi Bora ya Ardhi ya Kilimo (Agricultural Land Use Management Plan) katika kijiji cha Zegero kilichoteuliwa kama kijiji cha mfano kwa kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya kutathmini ubora wake. Wakulima 50 wa kijiji hicho walifundishwa kuandaa mipango ya kina ya usimamizi na matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambao wamekuwa chachu kwa wakulima wenzao katika kuhimiza matumizi endelevu ya ardhi ya kilimo. Kazi nyingine zilizofanyika ni kupima eneo la kila mkulima na kukusanya takwimu zinazohusu uwepo wa rasilimali za asili, uzalishaji wa mazao ya kilimo na vyanzo vya upatikanaji wa kipato kwa wakulima. Wizara itatumia matokeo ya kazi hiyo katika kuimarisha na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo mengine nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya mazingira, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kutathmini athari za shughuli za kilimo kwenye mazingira katika Halmashauri 10 za Wilaya za Hanang, Babati, Mbulu, Kilolo, Iringa Vijijini, Kisarawe, Kibaha, Lindi Vijijini, Ruangwa na Kondoa. Tathmini hiyo ilibaini uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji na ardhi, ukataji na uchomaji ovyo wa misitu, mifugo mingi kuliko uwezo wa malisho pamoja na uchafuzi wa maji kutokana na matumizi mabaya ya mbolea na madawa ya kuua wadudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilitoa mafunzo ya Tathmini ya Mazingira Kimkakati kwa wataalam wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika waliopo katika ngazi ya Kanda. Mafunzo hayo yalitolewa kwa wataalam 57 kutoka Kanda za Umwagiliaji, Idara ya Matumizi Bora ya Ardhi, Vituo vya Utafiti, Vyuo vya Mafunzo na Vituo vya Afya ya Mimea. Aidha, Wizara iliandaa Mpango Kazi wa Mazingira wa Miaka Mitano (5) utakaotumika kutekeleza shughuli za mazingira katika sekta ya kilimo kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kilimo na uelewa mdogo wa wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa visumbufu vya mimea na mazao ya kilimo, katika mwaka
2010/2011, Wizara ilidhibiti kikamilifu Nzige Wekundu makundi yapatayo 400 yenye ukubwa wa kuanzia nusu eka mpaka eka 50 kwa kila kundi katika Mbuga za Katavi, Ikuu, Bonde la Ziwa Rukwa na Wembere. Nzige hao walidhibitiwa katika eneo la hekta 19,778. Kutokana na udhibiti huo katika maeneo ya mazalia zaidi ya eka 800,000 za mazao ya nafaka katika Mikoa ya Rukwa, Tabora na Kigoma zilisalimika kutokana na mashambulizi ya nzige hao. Hivyo, wananchi katika maeneo hayo waliweza kuvuna mpunga, mahindi, mtama na ndizi pasipo kuathirika. Aidha, kutokana na kazi nzuri inayofanyika ya udhibiti wa nzige wananchi wengi hawajui kuwa Tanzania kuna nzige wengi kuliko nchi nyingine yoyote ile Kusini na Kati mwa Afrika na mlipuko mkubwa uliotokea kwa mara ya mwisho mwaka 1944 haujatokea tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani ilidhibiti ndege aina ya Kwelea Kwelea milioni 110.4 na hivyo kuokoa tani 1,104 kwa siku za mazao ya nafaka ikiwa ni pamoja na mpunga, mtama, uwele, ulezi na ngano. Ndege hao walidhibitiwa katika Halmashauri za Wilaya za Same, Chamwino, Bahi, Kongwa, Mpwapwa, Dodoma Vijijini, Kondoa, Igunga, Misungwi, Bunda, Musoma Vijijini, Singida Vijijini, Mvomero, Kilosa, Mbarali na Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa 2010/2011, Wizara ilitoa mafunzo ya utabiri shirikishi na udhibiti wa Viwavijeshi kwa wakulima 160 katika Wilaya za Bahi, Kongwa, Mvomero na Kilosa. Vilevile, wakulima 391 wa pamba kutoka Mikoa ya Mara, Shinyanga na Mwanza walipatiwa mafunzo kuhusu udhibiti husishi. Aidha, uzalishaji na usambazaji wa viumbe vya kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao kibiolojia uliendelea katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Morogoro, Arusha, Dar es Salaam, Ruvuma, Dodoma, Kigoma, Mwanza, Kagera na Mara. Vilevile, ili kupunguza athari katika mazingira na kwa afya ya binadamu zinazosababishwa na matumizi mabaya ya viuatilifu, mafunzo ya matumizi sahihi ya viuatilifu yalitolewa kwa wadau 35 katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, jumla ya Hekta 4,836.9 za mazao ya nafaka zilizovamiwa na Viwavijeshi katika Wilaya za Newala, Masasi, Morogoro Vijijini, Mvomero, Lindi Mjini, Lindi Vijijini, Moshi Vijijini, Korogwe, Handeni na Arusha Mjini ziliokolewa. Aidha, kutokana na jitihada za kushirikisha jamii, utabiri na udhibiti hufanyika mapema na hivyo, milipuko mikubwa ilipungua kutoka Wilaya 19 mwaka 2009/2010 hadi kufikia Wilaya 10 zilizovamiwa katika mwaka 2010/2011. Milipuko ya panya ilidhibitiwa katika vijiji 636 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Mtwara, Pwani, Lindi, Mbeya, Arusha, Ruvuma na Shinyanga kwa kutumia chambo chenye sumu ambapo kilo 160,252 za sumu hiyo zilitumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa nzi wa matunda anayeitwa Bactrocera Invadens ulifanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tabora na Tanga. Katika udhibiti huo wakulima walifundishwa na kuhimizwa kutumia mbinu za Udhibiti Husishi (Integrated Pest Management - IPM) ikiwa ni pamoja na usafi wa mashamba na kutumia kivutia wadudu (pheromone) aina ya Methyl Euginol na kutumia nyigu aitwaye fopius arisanus anayekula nzi hao. Serikali imewaleta mabuu (pupa) wa nyigu huyo 30,000 kutoka International Center for Insect Physiology and Ecology – ICIPE ili wazalishwe kwa wingi na kusambazwa kote nchini kwa ajili ya kuwadhibiti nzi hao. Aidha, wakulima 300 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani walipatiwa mafunzo husika kwa njia ya vikundi shirikishi. Kutokana na udhibiti wa Nzi wa Matunda, wakulima waliweza kuongeza mavuno hususan wilaya ya Muheza (Tanga) ambapo inakisiwa walipata Shilingi bilioni 2.16 kwa kuvuna tani 72,000 za machungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilifanya ukaguzi wa mazao yanayoingia nchini na yanayosafirishwa nchi za nje katika vituo vya mipakani ili kudhibiti ueneaji wa visumbufu vya mimea na kurahisisha biashara ya mazao ndani na nje ya nchi. Jumla ya tani 447,738.82 za mazao mbalimbali zilikaguliwa na kusafirishwa nchi za nje ambapo vyeti 8,952 vya usafi vilitolewa. Aidha, jumla tani
750,251.32 za mazao ziliingizwa nchini na vibali 511 vya kuingiza mazao vilitolewa. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (Food and Agriculture Organization-FAO) ilitoa mafunzo kwa wakaguzi 22 wa mazao na Afisa Maabara sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendelezaji wa mazao ya kilimo, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara ya kahawa, chai, korosho, miwa, pamba, mkonge, pareto na tumbaku ulikua kwa viwango tofauti. Kwa ujumla kulikuwa na ongezeko la uzalishaji kwa mazao ya tumbaku, pareto, mkonge, kahawa na korosho na kupungua kwa uzalishaji wa pamba, chai na sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa chai ulipungua kutoka tani 33,160 mwaka 2009/2010 hadi tani 32,000 ikilinganishwa na lengo la kuzalisha tani 35,000. Upungufu huo ulitokana na ukame na kufungwa kwa Kiwanda cha Chai Lupembe ambacho kilisababisha chai katika shamba la Mlangali lenye ukubwa wa hekta 200 kutovunwa. Aidha, Serikali inaendelea kusuluhisha mgogoro kati ya Chama cha Wakulima Wadogo wa Chai Rungwe (RSTGA) na waliokuwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Chai Rungwe (RUTECO) ambacho kilifutiwa usajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa sukari ulipungua kutoka tani
279,850 mwaka 2009/2010 hadi tani 263,460.69 mwaka 2010/2011. Lengo la uzalishaji wa sukari kwa mwaka huo lilikuwa tani 317,000. Upungufu huo ulitokana na ukame ulioyakumba maeneo yanayozalisha miwa. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni yale ya viwanda vya Tanganyika Planting Company Ltd. (TPC) na Kagera hali iliyosababisha kufungwa kwa viwanda mapema kutokana na kukosekana kwa malighafi ya miwa ya kutosha. Aidha, kuharibika kwa mtambo wa kusindika sukari katika Kiwanda cha TPC kumechangia kushuka kwa uzalishaji wa sukari katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa tumbaku uliongezeka hadi tani
130,000 ikilinganishwa na tani 60,900 mwaka 2009/2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 113. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa bei ya tumbaku katika soko la dunia kulikotokana na kupungua kwa uzalishaji wa tumbaku nchini Brazil uliosababishwa na mafuriko yaliyotokea msimu wa 2009/2010. Hali hiyo ilisababisha bei ya tumbaku nchini kupanda kutoka wastani wa Shilingi 1,100 hadi Shilingi 3,100 kwa kilo ya tumbaku ya mvuke na Shilingi 682 hadi 2,000 kwa kilo ya tumbaku ya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mafuriko nchini Brazil, uzalishaji wa tumbaku nchini humo katika msimu wa 2010/2011 uliongezeka kuliko hali ya kawaida. Ongezeko hilo pamoja na ongezeko la uzalishaji hapa nchini lilisababisha uhaba wa soko la tumbaku yetu. Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inafanya jitihada ya kutafuta masoko mengine kwa ajili ya kuuza ziada ya tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa pamba mbegu ulipungua kutoka tani 267,004 mwaka 2009/2010 hadi tani 163,644, ikiwa ni chini ya lengo la kuzalisha tani 260,000. Sababu kuu iliyochangia kushuka kwa uzalishaji wa pamba ni bei ndogo iliyotolewa katika msimu uliotangulia ambayo ilisababisha wakulima kulima mazao mengine. Sababu nyingine ni ukame ulioyakumba maeneo

yanayolimwa pamba hususan katika Kanda ya Magharibi kati ya mwezi Desemba 2009 na Machi 2010; mvua kubwa kupita kiasi iliyonyesha katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Magharibi kati ya mwezi Aprili na Juni 2010; na kutoeleweka vyema kwa utaratibu wa ruzuku ya pembejeo ambako kulisababisha watoa huduma wa pembejeo hususan madawa kutoratibiwa ipasavyo na hivyo kutoa madawa yasiyokidhi viwango. Suala hilo sasa limepatiwa ufumbuzi ambapo ruzuku ya pembejeo kwa zao la pamba kuanzia msimu ujao itatolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Zao la Pamba ambapo uratibu wa watoa huduma utaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, uzalishaji wa pareto uliongezeka kutoka tani
3,320 mwaka 2009/2010 hadi tani 5,000. Ongezeko hilo lilichangiwa na kupanda kwa bei ya pareto kutoka wastani wa Shilingi 1,200 kwa kilo mwaka 2009/2010 hadi wastani wa Shilingi 1,700 kwa kilo mwaka
2010/2011. Kutokana na hali hiyo, uuzaji nje sumu ghafi (crude extracts), pyrethrum grist na unga (powder) wa pareto uliliingizia Taifa wastani wa Dola za Kimarekani milioni tano (5) ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 4.8 mwaka 2009/2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mkonge uliongezeka kutoka tani 26,363 mwaka 2009/2010 hadi tani 35,000 mwaka 2010/2011. Ongezeko hilo lilitokana na kupanda kwa bei ya mkonge kutoka wastani wa Dola za Kimarekani 820 kwa tani mwaka 2009/2010 hadi Dola za Kimarekani 1,200 kwa tani mwezi Machi, 2011 kwa mkonge wa daraja la UG. Aidha, ongezeko la bei lilisababishwa na kuongezeka kwa mahitaji ya mkonge na bidhaa zake katika soko la dunia, hususan kwenye nchi za China, Saudi Arabia, India, Hispania, Uingereza, Ujerumani, Kenya, Uganda na Nigeria. Pamoja na ongezeko kubwa la bei, bado kasi ya kufufua mashamba ya mkonge ni ndogo. Serikali inaendelea kujadiliana na wadau na kuhimiza Bodi ya Mkonge kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa kahawa uliongezeka kutoka tani 40,000 mwaka 2009/2010 hadi tani 60,575 mwaka 2010/2011. Ongezeko hilo lilichangiwa na hali nzuri ya hewa na tabia ya zao la kahawa kuongeza tija msimu unaofuatia msimu wa uzalishaji mdogo (biannual bearing). Aidha, bei ya kahawa katika msimu wa 2010/2011 iliendelea kuwa nzuri na kufikia Shilingi 7,000 kwa kilo ya kahawa safi ya Arabica kutoka wastani wa Shilingi 5,000 mwaka 2009/2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa korosho uliongezeka kutoka tani 74,169 mwaka 2009/2010 hadi tani 121,070 mwaka 2010/2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 63.2. Ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa lilitokana na bei nzuri waliyopata wakulima kutokana na kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Maghala. Kupitia Mfumo huo, wakulima walipata malipo ya ziada (majaliwa) na kuweza kupandisha bei ya kilo ya korosho kati ya Shilingi 1,420 na 1,660.70 ikilinganishwa na bei waliyokuwa wakipata kabla ya Mfumo, ya kati ya Shilingi 200 na 350 kwa kilo. Aidha, mfumo huo umeepusha ununuzi holela usiomnufaisha mkulima. Sababu nyingine zilikuwa ni hali nzuri ya hewa na utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, hususan madawa ya kuua wadudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilishirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na makampuni binafsi katika kuendeleza uzalishaji na usindikaji wa mazao ya alizeti, ufuta, karanga, michikichi, mbegu za pamba na soya. Uzalishaji huo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, uzalishaji wa alizeti uliongezeka kutoka tani 348,877 mwaka 2009/2010 hadi tani 786,902 mwaka
2010/2011. Ongezeko la uzalishaji wa mbegu za mafuta lilitokana na kupanuka kwa soko la ndani kufuatia kuenea kwa teknolojia ya usindikaji wa mbegu za mafuta na kilimo cha mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mazao ya bustani, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilitunza bustani za Mpiji (Bagamoyo), Jaegetal (Lushoto), Songa na Kizugu (Muheza), Igurusi (Mbarali) na Bugaga (Kasulu) kwa ajili ya kupata vikonyo vya mazao ya bustani ili kuzalisha miche bora. Miche 365,000 ya matunda ilizalishwa katika bustani hizo na kusambazwa kwa wakulima. Aidha, Wizara kwa kushirikana na Baraza la Kuendeleza Mazao ya Bustani (Horticulture Development Council of Tanzania - HODECT) na wadau wengine iliandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Mazao ya Bustani (National Horticulture Development Strategy).

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kimkakati yatakayozingatiwa katika utekelezaji wa programu ya kuendeleza sekta ya mazao ya bustani ni pamoja na: kuongeza uwekezaji na ugharamiaji wa muda mrefu katika sekta ya mazao ya bustani; kuainisha na kushughulikia changamoto na vikwazo vya

miundombinu katika sekta ndogo ya mazao ya bustani; kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya bustani; kuongeza uzalishaji wenye tija na ubora; na kujenga uwezo wa rasilimali watu ili kutekeleza kwa mafanikio mkakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika kilimo, mwezi Julai, 2010, Serikali ilisaini makubaliano ya kutekeleza Programu Kabambe ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP). Makubaliano hayo yataiwezesha Tanzania kunufaika na fursa zilizopo katika Umoja wa Afrika za kuendeleza kilimo hususan kuimarisha usalama wa chakula. Makubaliano hayo yatatekelezwa kupitia mfumo wa utekelezaji wa ASDP utakaoboreshwa kuhusisha wadau wengi zaidi. Tayari Wizara za Sekta ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zinakamilisha uandaaji wa Mpango wa Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilishiriki katika kuandaa Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT) ambao utatekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Aidha, Mpango utatekelezwa pia Zanzibar. Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 (Public-Private Partnership Policy 2010). Kwa upande wa Serikali, Mpango huo utasimamiwa na Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rufiji Basin Development Authority- RUBADA). Mamlaka hiyo itafanyiwa maboresho ili iweze kumudu majukumu hayo mapya. Wizara pia kwa kushirikiana na wadau imekamilisha maandalizi ya miradi ya Bread Basket na Feed the Future ambayo nayo inalenga kuongeza usalama wa chakula na kuzalisha ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi RUBADA imeendelea kutekeleza makubaliano ya ubia na kampuni ya Agrica ya Uingereza katika kuendeleza kilimo cha mpunga katika shamba la Mngeta kwa kushirikiana na Kampuni ya ubia ya Kilombero Plantations Ltd. Ubia huo umewezesha uwekezaji wa Dola za Kimarekani milioni 25 na kuendeleza eneo la hekta 4,150 za kilimo cha mpunga. Hadi tarehe 30 Juni, 2011 jumla ya tani 12,000 za mpunga zilikuwa zimevunwa katika eneo la hekta 3,000. Matarajio ya mavuno kwa hekta zote 4,150 ni kati ya tani 15,000 hadi tani 16,000 za mpunga. Aidha, ili kuongeza tija, kampuni imeanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji na eneo lote la hekta 5,000 litalimwa msimu ujao. Vilevile, kampuni imetoa ajira mpya 172 ya wafanyakazi wa kudumu na vibarua 650. Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa namna hiyo katika maeneo mengine nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha iliendelea kupitia kodi mbalimbali zinazohusu Sekta ya Kilimo katika kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo. Kutokana na mapitio hayo, Serikali imefanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye zana za kilimo kama ifuatavyo:-

(i) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mashine za kupura (threshers), mashine za kukaushia na kukoboa mpunga (rice dryers and mills), mashine za kupandia mbegu (planters) na matrekta ya kukokota kwa mkono (power tiller); na

(ii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya mashine za kunyunyizia na kutifua udongo (Sprayers and Harrows) na mashine za kupandishia nafaka (Grain Conveyors).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010, Wizara pia ilishiriki katika utekelezaji wa Roadmap ya maboresho ya mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara kupitia viashiria vilivyoainishwa katika ripoti ya Benki ya Dunia (World Bank Doing Business Report 2010), kwa kuandaa kanuni za Bodi za Mazao na kupendekeza marekebisho katika Sheria ya Hifadhi ya Mimea (The Plant Protection Act, 1997) kwa lengo la kuondoa kero zinazokwaza wawekezaji na wafanyabiashara katika mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilifanya mafunzo kwa watoa taarifa na takwimu za mvua na hali ya mazao mashambani wapatao 284. Watoa taarifa hao walitoka katika Halmashauri za Wilaya 73 za Mikoa ya Kanda ya Mashariki (Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es Salaam); Kanda ya Kati (Dodoma na Singida); Kanda ya Ziwa (Shinyanga, Mwanza, Mara na Kagera); na Kanda ya Kusini (Mtwara na Lindi). Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuboresha ukusanyaji wa taarifa na takwimu hizo kwa kutumia mfumo wa moja kwa moja wa kutumia simu za viganjani na

kompyuta (Automation). Pia, ukaguzi na ukarabati wa vituo vya kutoa taarifa za mvua na hali ya mazao mashambani ulifanyika katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Mwanza na Kagera ili viweze kutoa taarifa na takwimu kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya chakula na usindikaji, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliainisha wasindikaji wa mazao mbalimbali ya nafaka, mbegu za mafuta, matunda na mbogamboga katika Halmashauri za Wilaya za Kilosa, Tunduru na Korogwe ambapo jumla ya wasindikaji 30 waliainishwa. Lengo lilikuwa ni kuwatambua, kubaini shughuli zao na kubuni utaratibu wa kuanzisha ubia wa usindikaji kati ya Serikali na wakulima/wajasiriamali (Public Private Partnership –PPP). Katika kuhakikisha kuwa wakulima wanapata bei nzuri kwa zao la mpunga, Wizara ilitoa mafunzo kwa wakulima
150 wa zao hilo kuhusu usindikaji na upangaji wa madaraja. Mafunzo hayo yalitolewa katika skimu za umwagiliaji za Mbarali, Lower Moshi na Mkindo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi na ununuzi wa chakula kupitia NFRA, katika mwaka 2010/2011, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (National Food Reserve Agency - NFRA) ilipanga kununua jumla ya tani 200,000 za mahindi. Hadi tarehe 30 Juni 2011, NFRA ilikuwa imenunua tani 181,019 za mahindi sawa na asilimia 90.5 ya lengo. Hata hivyo, lengo la ununuzi halikufikiwa kutokana na kupungua kwa mahindi katika maeneo ya ununuzi na kupanda kwa bei ya mahindi katika kipindi hicho. Ununuzi huo ukijumuishwa na akiba iliyokuwepo mwanzoni mwa msimu ya tani 47,685.6 za mahindi na tani 9.2 za mtama, ulifanya akiba ya chakula kufikia tani 228,713.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kurekebisha na kuhuisha Sera na Sheria, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilisambaza nakala za vitabu vya Sera ya Taifa ya Umwagiliaji ya mwaka 2010 kwa wadau. Wizara pia iliandaa mapendekezo ya kuhuisha Sheria ya Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (The Agricultural Inputs Trust Fund Act, 1999) na Sheria ya Hifadhi za Mimea (Plant Protection Act, 1997). Vilevile, Wizara iliandaa mapendekezo ya Miswada ya Sheria za Kusimamia Rasilimali za Kilimo (The Agricultural Resource Management Legislation); Sheria ya Nasaba kwa ajili ya Kilimo na Chakula (The Plant Genetic Resource for Food and Agriculture Legislation); na Sheria ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika (The Cooperative Development Commission Legislation). Pia Kanuni za Sheria ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; Sheria ya Mbolea (The Fertilizer Regulations); na kanuni za Sheria za Mazao ya Pareto, Chai, Sukari, Korosho, Tumbaku, Pamba, Kahawa na Mkonge ziliandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya watumishi, katika mwaka 2010/2011, watumishi 234 walipandishwa na kubadilishwa cheo katika madaraja mbalimbali kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma. Aidha, Watafiti Wastaafu 36 walipewa mikataba mipya ya kazi. Wizara ilikamilisha mapitio ya Mkataba wa Huduma kwa Mteja kwa ajili ya kuboresha huduma zake. Katika utekelezaji wa malengo ya utawala bora, Wizara ilisimamia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji kazi (Open Performance Review Appraisal System - OPRAS) ambapo asilimia 73 ya watumishi wote walifanyiwa tathmini katika mfumo huo. Watumishi wengine waliendelea kufanyiwa mafunzo ya OPRAS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kupunguza makali ya UKIMWI, Wizara iliendelea kuwapatia vyakula vyenye virutubisho pamoja na matibabu watumishi 17 wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuhamasisha upimaji wa afya wa hiari miongoni mwa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliendelea kujenga uwezo wa Kamati ya Jinsia ya Wizara kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe sita wa Kamati hiyo katika Chuo cha Eastern and Southern Africa Management Institute (ESAMI). Aidha, rasimu ya Mwongozo wa Jinsi ya Kuingiza Masuala ya Jinsia kwenye Sekta ya Kilimo iliwasilishwa kwa wadau ili kupata maoni yao kabla ya kukamilishwa. Wizara inaendelea kukamilisha mwongozo huo baada ya kupata maoni ya wadau na utakuwa tayari kwa matumizi katika mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu 24, katika mwaka 2010/2011, Wizara kupitia Fungu 24 ilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 6.708. Kati ya hizo, Shilingi bilioni 6.608 ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi milioni 100.0 ni Fedha za Maendeleo. Hadi tarehe 30 Juni, 2011, Fedha za Matumizi ya Kawaida zilizopokelewa kutoka Hazina zilikuwa Shilingi bilioni 5.576 sawa na asilimia 83.13 ya kiasi kilichoidhinishwa. Matumizi yalifikia Shilingi bilioni 5.497 sawa na asilimia 98 ya kiasi cha fedha kilichotolewa. Aidha, hadi

tarehe 30 Juni, 2011, Fedha za Bajeti ya Maendeleo zilizopokelewa ni Shilingi milioni 30.0 sawa na asilimia
30 ya fedha zilizoidhinishwa ambazo zote zilitumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliimarisha Ushirika kupitia utekelezaji wa Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika nchini. Maeneo yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kuimarisha uongozi wa Vyama vya Ushirika; kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Ushirika; kuimarisha masuala ya mazao ya wakulima kwa kueneza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Maghala; kufufua na kuimarisha Vyama vya Ushirika; kuimarisha uendeshaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo - (Savings and Credit Cooperative Society - SACCOS) na Benki za Ushirika; kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika; kuimarisha taasisi za ushirika; na kuendelea na mchakato wa kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarisha uongozi wa Vyama vya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ilisimamia chaguzi za theluthi moja ya wajumbe wa Bodi katika maeneo ya Vyama Vikuu ambao muda wao uliisha. Vyama hivyo ni Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (Savings and Credit Cooperative Union League of Tanzania Ltd. – SCCULT), Biharamulo Cooperative Union Ltd. (BCU) (1986) Ltd., Mradi wa Ushirika wa pamoja Kanyovu (Kanyovu Cooperative Joint Enterprise), Chama Kilele cha Tumbaku (Tanzania Tobacco Cooperative Apex - TTCA) na Central Tobbacco Cooperative Union Ltd. (CETCU).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilisimamia na kufuatilia kwa karibu hatua za ujenzi wa mitaji ya Benki za Kilimanjaro Cooperative Bank Limited (KCBL) na Kagera Farmers Cooperative Bank Limited (KFCB) kwa ajili ya kuimarisha Benki hizo. Wizara pia iliendelea na usuluhishi wa migogoro mbalimbali ya Vyama vya Ushirika vikiwemo Rusaba, Matiazo na Mkabogo Cooperative Society (RUMAKO), Coast Region Cooperative Union (1984) Ltd. (CORECU), Chama cha Mazao RUARUKE, Mosemo Cooperative Marketing (MCM) SACCOS, Buguruni Traders SACCOS, Luiche SACCOS na Dar es Salaam Airport Tax Drivers Cooperative Society.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Wizara iliendelea na uhamasishaji na uimarishaji wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Mara (WAMACU) na ilishughulikia ufilisi wa Vyama vya Ushirika vya Vumilia Producers Cooperative Societies (VUPO), TUKE Consumers Cooperative Society, Mbinga Cooperative Union Ltd. (MBICU) na ufufuaji wa Mbinga Farmers Cooperative Union Ltd. (MBIFACU).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha utendaji wa viongozi wa Vyama vya Ushirika, mafunzo ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika yalitolewa kwa viongozi 40 kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo Cooperative Union Ltd. (ICU), Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (Tanzania Federation of Cooperatves Ltd. - TFC), SCCULT, Kilimanjaro Native Cooperative Union Ltd. (KNCU), KCBL, Vuasu Cooperatve Union Ltd. (VCU) na Arusha Cooperative Union Ltd. (ACU) kwa lengo la kuviwezesha vyama hivyo kuzingatia misingi ya utawala bora. Aidha, mafunzo ya cheti yalitolewa kwa watendaji wa SACCOS kutoka Mikoa ya Arusha, Tabora na Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilihamasisha wananchi ama kuanzisha au kujiunga na Vyama vya Ushirika kupitia maadhimisho ya Nane Nane na Siku ya Ushirika Duniani. Siku ya Ushirika Duniani ilijikita katika kuhamasisha wanawake kushiriki katika ushirika, kaulimbiu ikiwa “Ushirika Hujasirisha Wanawake”. Siku ya SACCOS duniani ililenga katika kuhamasisha wanachama na kuzitaka jamii kujiunga kwa wingi kupitia kaulimbiu ya “SACCOS zetu ni Tegemeo kwa Maendeleo ya Jamii”. Katika maadhimisho hayo vyama vilivyoshiriki ni pamoja na TFC, KNCU, Karagwe District Cooperative Union Ltd. (KDCU), BCU, KFCB, KCBL, Kagera Cooperative Union Ltd. (KCU), Tanga Diary Cooperative Union Ltd. (TDCU), Western Zone Tobacco Growers Cooperative Union Ltd. (WETCU), Masasi Mtwara Cooperative Union Ltd. (MAMCU), Tunduru Agricultural Marketing Cooperative Union Ltd. (TAMCU), Dar es Salam Region Cooperative Union Ltd. (DARECU), Tandahimba Newala Cooperative Union Ltd. (TANECU), ICU, ACU, Riftvalley Cooperative Union Ltd. (RIVACU), Songea Namtumbo Agriculture Marketing Cooperative Union Ltd. (SONAMCU), Kigoma Tobacco Growers Cooperative Union Ltd. (KTCU), Central Zone Tobacco Growers Cooperative Union Ltd. (CETCU), SCCULT na Chunya Tobacco Growers Cooperative Union Ltd. (CHUTCU). Vilevile, Vyama vya Msingi vya mazao
20, Ufugaji/Maziwa vitano, SACCOS 35 pamoja na vikundi 20 navyo vilishiriki kwenye maadhimisho hayo.

Kutokana na uhamasishaji huo vyama vyenye mitaji na uwezo mdogo wa kujiendesha vilihamasishwa kuungana. Kutokana na jitihada hizo idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika imeongezeka.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Maghala, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilieneza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Maghala katika Mikoa inayozalisha korosho, kahawa, pamba na alizeti. Kupitia Mfumo huo, Vyama vya Ushirika vya Korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma (Tunduru) viliwalipa wakulima malipo ya ziada (majaliwa) na kuwezesha kupata bei nzuri ya korosho. Aidha, mfumo huo umewezesha Vyama vya Ushirika kukopesheka, kuongeza ubora na thamani ya zao, matumizi ya vipimo sahihi, upatikanaji wa ushuru wa Halmashauri za Wilaya na uchangiaji wa huduma za kijamii kama shule na zahanati. Kwa mfano wakulima wanaohudumiwa na Chama cha TANECU wameweza kuchangia ushuru wa Halmashauri Shilingi bilioni mbili (bilioni 2), Vyama vya Ushirika vya Msingi Shilingi bilioni 2.5, mchango wa madawati shuleni Shilingi milioni 360 na ujenzi wa maghala Shilingi milioni 900. Pia mfumo huo umewasaidia kuepuka ununuzi holela usiomnufaisha mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ilifanya tathmini ambayo ilibaini kuwa baadhi ya gharama za masoko na uendeshaji wa Mfumo huo zilikuwa kubwa na hivyo kushauri kupunguza gharama hizo kwenye usafirishaji, ushuru wa Vyama na Halmashauri za Wilaya ili kumwezesha mkulima kupata malipo mazuri zaidi. Aidha, Wizara ilihamasisha matumizi ya Mfumo huo kwenye mazao ya kahawa katika Wilaya za Mbinga na Tarime; pamba katika Wilaya za Igunga, Nzega, Musoma na Bunda; ufuta kwenye Wilaya zote za Mikoa ya Lindi na Mtwara; na alizeti katika Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufufua na kuimarisha Vyama vya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kulipa madeni ya Vyama vya Ushirika ambapo jumla ya Shilingi 745,925,000 zilitumika kwa ajili ya kulipa mafao ya watumishi na madeni ya Vyama vya Nyanza Cooperative Union Ltd. (NCU), ACU, Mbeya Ileje Cooperative Union Ltd. (MICU) na Kyela Cooperative Union Ltd. (KYECU). Aidha, baadhi ya Vyama vya Ushirika vilivyofutiwa madeni vya KCU, KNCU, ICU na TDCU vimeonesha mafanikio makubwa. Kwa mfano, Chama Kikuu cha KCU (1991) Ltd. kimeweza kuongeza uzalishaji wa Kahawa Hai (Organic Coffee) aina ya Robusta kwa kuuza na kuwalipa wakulima Shilingi 3,600 kwa kilo ikilinganishwa na kahawa ya kawaida Shilingi 1,800 kwa kilo ya kahawa safi. Vilevile, KNCU (1984) Ltd. iliwalipa wakulima Shilingi 3,200 kwa kilo ya kahawa aina ya Arabica ikilinganishwa na malipo ya awali ya Shilingi 3,000 kwa kilo. Vyama hivyo viliajiri Maafisa Ugani 77 (45 KCU na 32 KNCU) wanaohudumia wakulima katika vyama wanachama. Aidha, TDCU iliwezesha idadi ya wafugaji katika Vyama vya Msingi kuongeza upatikanaji wa maziwa kutoka lita 6,200,000 hadi lita 7,750,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25. Vilevile, wafugaji walipata bei nzuri ya maziwa kutoka wastani wa Shilingi 350 kwa lita mwaka 2009/2010 hadi Shilingi 550 kwa lita mwaka 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuviongezea nguvu Vyama vya Ushirika, baadhi ya Vyama viliungana kwa kuunda miradi ya pamoja na hivyo kuweza kuuza mazao nje ya nchi. Kwa mfano, mradi wa pamoja wa ushirika wa KANYOVU (Kigoma) uliuza kahawa aina ya Arabica kwenye soko maalum la fair trade ambapo wakulima walilipwa hadi Shilingi 5,600 kwa kilo ikilinganishwa na malipo ya Shilingi
3,400 kwa kilo mwaka 2009/2010. Chama hicho kilipewa tuzo ya kahawa bora Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuimarisha Vyama vya Ushirika vinavyolima tumbaku vya WETCU, Kahama Cooperative Union Ltd. (KACU), CETCU SONAMCU, Lake Tobacco Growers Cooperative Union Ltd. (LATCU), CHUTCU, KTCU na Vyama vya Msingi vya wakulima wa tumbaku wa Iringa vya Mfyome, Magubike, Mhanga na Kiwemu ili viweze kukopesheka. Vyama hivyo vilipata mikopo ya jumla ya Shilingi bilioni 123.6 (sawa na Dola za Kimarekani 85,802,212 wakati mkopo ulipochukuliwa) kutoka benki za CRDB plc. na NMB kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima. Pembejeo zilizonunuliwa ni pamoja na mbolea aina ya NPK 10:18:24 mifuko
925,683, CAN 27% mifuko 233,221, NPK 20:10:10 mifuko 57,600 na UREA mifuko 237,619. Madawa ya Confidor 70 WG (30gm) paketi 531,939, Yamaotea lita 108,182, Actara 25 WG ( 4gm) paketi 84,884, Bill dock kilo 2,691, Decis vidonge 873,413, vifungashio aina ya New hessian cloth marobota 6,222, Jute twine marobota 3,865 na Cotton twine 1.5 kilo spool.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Vyama Vikuu 41 na Chama Kilele vinavyojishughulisha na mazao ya kahawa, korosho, tumbaku, pamba na mazao mchanganyiko viliweza kupata mikopo kutoka NMB na CRDB plc. Mikopo ilitolewa kwa zao la kahawa Shilingi bilioni 18.6; korosho Shilingi bilioni 16.6; pamba Shilingi bilioni 6.6; tumbaku Shilingi bilioni 123.6 na mazao mchanganyiko Shilingi milioni 500. Vyama hivyo vilitoa huduma kwa wanachama na wasio wanachama ambapo kwa kipindi hicho viliweza kutoa huduma kwa wakulima zaidi ya milioni sita (milioni 6).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarisha uendeshaji wa SACCOS na Benki za Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilitoa mafunzo kwa Maafisa Ushirika 42 wa Mikoa ya Iringa, Mbeya, Lindi, Mtwara, Rukwa na Ruvuma kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kusimamia na kukagua SACCOS ili ziweze kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na viwango vinavyotakiwa. Aidha, Wizara ilichambua na kuidhinisha Mipango ya muda wa mwaka mmoja ya Vyama Vikuu vya Ushirika 23, benki za ushirika mbili na SACCOS 10 zenye mahitaji ya mikopo zaidi ya Shilingi milioni 500 na kuvipatia hati ya ukomo wa madeni (maximum liability certificates).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ilifanya ukaguzi maalum wa SCCULT, WETCU, MBIFACU, SONAMCU, TAMCU, ICU, NCU, KNCU, MBOCU, RUCU, MICU, KYECU, RIVACU, G32, RUARUKE, MCU, VUPO (chini ya Ufilisi) na Vyama 119 vya Ushirika vya Msingi ambavyo wanachama wa vyama hivyo waliwasilisha maombi kwa lengo la kubaini hali ya uendeshaji wa vyama husika. Matokeo yalionyesha kuwepo dosari mbalimbali kwa baadhi ya vyama ikiwa ni pamoja na uandishi mbovu wa vitabu, kutotunza vizuri daftari la wanachama na daftari la mali za chama, ucheleweshaji wa marejesho ya mikopo, matumizi makubwa kuliko mapato, ubadhirifu wa fedha za vyama na kutozingatiwa kwa utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya sheria. Wizara imetoa maelekezo kwa wanachama kuwawajibisha viongozi wa Bodi na Watendaji kupitia Mikutano Mikuu na kuchukua hatua za kisheria pale inapostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarisha taasisi za ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea kuimarisha taasisi za ushirika kwa kufanya maboresho ya uongozi, usimamizi na utendaji. Maboresho hayo yalifanywa katika Shirikisho la Vyama vya Ushirika pamoja na SCCULT ili kuwezesha vyama hivyo kutoa huduma zinazotarajiwa na wanachama. Aidha, Wizara iliendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika na Stadi za Biashara (Moshi University College of Cooperative and Business Studies - MUCCoBS) katika kufanya utafiti wa maendeleo ya ushirika na kutoa mafunzo kwa watumishi wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika, viongozi pamoja na watendaji wa Vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliendelea kulipatia ruzuku Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ili kuimarisha shughuli za ukaguzi wa vyama. Kwa mwaka 2010/2011, Shirika lilifanya ukaguzi katika Vyama 1,419. Vyama vilivyokaguliwa ni pamoja na AMCOS 644; SACCOS
711 na Vyama 64 vya aina nyingine. Aidha, Wizara ilitoa mafunzo kwa watumishi 30, kati yao watumishi 10 waliendelea kupata mafunzo ya uzamili, saba mafunzo ya stashahada, mmoja mafunzo ya cheti na 12 walipata mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi. Vilevile, Idara ilipatiwa vitendea kazi mbalimbali yakiwemo magari mawili ili kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea na mchakato wa uanzishaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais kwa lengo la kuleta msukumo mkubwa katika uhamasishaji, uanzishaji, uendelezaji, uimarishaji na usimamizi wa ushirika nchini. Baadhi ya majukumu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika yameanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uendelezaji wa maendeleo ya ushirika hususan katika ushirika wa masoko (Cooperative Marketing), Ushirika wa fedha (Cooperative Microfinance), Benki za Ushirika (Cooperative Banks) na usimamizi wa biashara ya vyama vya ushirika ili viweze kununua na kuuza mazao pamoja na kuwafikishia pembejeo wakulima. Aidha, mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika yameandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa mwaka 2011/2012, malengo ya Wizara, mpango na bajeti ya mwaka 2011/2012 umelenga katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia
2011/2012 hadi 2015/2016 wenye lengo la kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo (Tanzania Development Vision - TDV 2025). Aidha, mpango na bajeti utaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia; MKUKUTA II; Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka

2010; Azma ya Kilimo Kwanza; na Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia itatekeleza Programu Kabambe ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP) kupitia Mpango wa Uwekezaji ulioandaliwa na wadau (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan - TAFSIP); Mpango wa Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT); na Miradi ya Feed the Future na Bread Basket. Mipango hiyo inayolenga katika kuongeza tija na uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha mkulima itatekelezwa chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza mipango hiyo, Wizara inalenga kukabiliana na vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa Sekta ya Kilimo kama vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Baadhi ya vikwazo hivyo ni pamoja na kilimo cha kutegemea mvua pekee; uwekezaji mdogo; upatikanaji mdogo wa mikopo; tija ndogo; masoko duni; mabadiliko ya tabianchi (ukame na mafuriko); na uthamanishaji mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa vikwazo hivyo, Wizara itatekeleza maeneo ya kipaumbele yafuatayo: kupanua eneo la umwagiliaji; kuhimiza na kuongeza matumizi ya pembejeo na zana bora za kilimo; kuimarisha huduma za kitaalam (utafiti, ugani na mafunzo); kuhimiza matumizi bora ya ardhi ya kilimo; kuimarisha ushirika nchini; kuhimiza kilimo cha kibiashara na uongezaji thamani ya mazao; na kuendeleza rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo yatatekelezwa kupitia ASDP ambayo hutekelezwa katika ngazi ya Taifa na Wizara za Sekta ya Kilimo na katika ngazi ya Halmashauri kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs). Utekelezaji wa DADPs unaimarisha sera ya ugatuaji wa madaraka kwenda ngazi ya Halmashauri (Decentralization by Devolution – D-by-D) hivyo kuwawezesha wakulima kuibua, kupanga, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo yao katika kilimo na ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itasimamia na kuratibu utekelezaji wa ASDP katika ngazi ya Kitaifa na ngazi ya Halmashauri. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo, Wabia wa Maendeleo pamoja na wadau wengine itafanya tathmini ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ASDP. Matokeo ya tathmini hiyo yatatumika katika kuandaa awamu ya pili ya ASDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu 43, Kilimo cha Umwagiliaji, maji ndiyo pembejeo ya umuhimu wa kwanza katika kilimo. Kulingana na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, lengo ni kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta
1,000,000 ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada ifikapo mwaka 2015. Eneo la umwagiliaji lililoendelezwa hadi sasa ni hekta 345,690. Kutokana na ufinyu wa rasilimali tulizonazo itachukua muda mrefu kufikia lengo la hekta 1,000,000 kwa utaratibu ambao umekuwa ukitumika wa kutegemea miundombinu mikubwa peke yake ambayo ina gharama kubwa. Hivyo, msukumo mkubwa utawekwa katika kutumia teknolojia mbalimbali zikiwemo zenye ufanisi, gharama nafuu na kuhusisha sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la kuunda Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itakayosimamia kwa ukamilifu shughuli za umwagiliaji kwa kuandaa mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume hiyo. Aidha, kufuatia kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Umwagiliaji, Wizara itaitafsiri Sera hiyo kwa lugha ya kiswahili na lugha nyepesi kwa ajili ya kuifikisha kwa umma; kukamilisha uandaaji wa Mkakati wa Umwagiliaji; na kuandaa mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Umwagiliaji. Jumla ya Shilingi milioni 51.88 zimetengwa kwa utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, utekelezaji wa maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji utazingatia Sera ya Taifa ya Umwagiliaji (2010) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (2002). Katika utekelezaji huo, maeneo yanayolengwa ni: uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji; matumizi bora ya teknolojia za umwagiliaji zenye ufanisi na tija; kutoa huduma za kitaalam kwa Halmashauri; kuandaa Mkakati na Sheria ya Umwagiliaji; na kukamilisha uanzishaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Jumla ya Shilingi milioni 409.85 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji, Wizara itaendeleza miradi ya umwagiliaji yenye jumla ya hekta 40,000 na hivyo kufanya eneo la umwagiliaji kuongezeka kutoka hekta 345,690 mwaka 2010/2011 hadi hekta 385,690 mwaka 2011/2012. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 24, mabwawa nane na mashamba mawili ya Wakala wa Mbegu za Kilimo ya Kilangali na Msimba (Kilosa) kwa kutumia fedha za Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji ngazi ya Taifa (National Irrigation Development Fund – NIDF) ambapo Shilingi bilioni 10.60 zimetengwa katika kutekeleza kazi hizo. Aidha, skimu 136 zitaendelezwa kwa kutumia fedha za DADPs na Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji ngazi ya Wilaya (District Irrigation Development Fund – DIDF) ambapo Shilingi bilioni 32.89 zitatumika. Aidha, mitambo mikubwa 13 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji iliyopo katika kanda za umwagiliaji itakarabatiwa kwa lengo la kuzipa kanda hizo uwezo zaidi wa kuongeza eneo la umwagiliaji. Jumla ya Shilingi milioni 140.62 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya umwagiliaji 95 yenye jumla ya hekta 70,500. Miradi hiyo itatoka katika kanda zote saba za umwagiliaji kama ifuatavyo: Morogoro (27); Tabora (9); Mwanza (8); Kilimanjaro (5); Mbeya (13); Mtwara (15); na Kanda ya Kati (18). Miradi ambayo tayari imefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu na kuwa kwenye hatua mbalimbali ni 122 yenye eneo la hekta 81,182. Miradi hiyo ikijumuishwa na ile itakayofanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2011/2012 itafanya jumla ya miradi iliyofanyiwa upembuzi yakinifu kufikia 217 na hivyo kufanya eneo lote lililofanyiwa upembuzi yakinifu kufikia hekta 151,682. Jumla ya Shilingi bilioni 1.036 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuongeza eneo la umwagiliaji Wizara pia itaweka msukumo zaidi katika kutumia teknolojia za umwagiliaji zenye uwezo na ufanisi mkubwa katika matumizi ya maji. Teknolojia hizo ni pamoja na utumiaji wa mabomba kwa ajili ya kupitisha maji kutoka kwenye vyanzo; matumizi ya maji chini ya ardhi; matumizi ya pampu zinazotumia umeme na nishati mbadala ya jua na upepo; na umwagiliaji kwa njia ya matone na unyunyiziaji ambao utawezesha kwa kiasi kikubwa kuzalisha mazao yenye thamani kubwa (mbogamboga, zabibu, viungo, maua n.k.).

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya teknolojia hizo ni pamoja na kutumia maji kwa ufanisi zaidi; kuongeza tija na uzalishaji; kuongeza misimu ya kilimo kwa mwaka; na kuweza kulima mazao ya aina nyingi kwa mzunguko kwa mwaka (crop rotation). Utaratibu huo unawahakikishia wakulima usalama wa chakula na kuongeza pato la kaya. Mfano wa miradi ya aina hiyo ni pamoja na Misufini/Kochakindo hekta 50, Kyomu hekta 50 na Miwaleni hekta 100 (Moshi Vijijini); Kirya hekta 640 (Mwanga); Kisasida hekta
150 (Singida Manispaa); Chinangali hekta 200 (Chamwino); Mgama hekta 300, Wangama hekta 150, Tanangozi hekta 50 na Igingilanyi hekta 10 (Iringa Vijijini); Msoga hekta 200 (Bagamoyo); Nyatwali-Green Triangle Group hekta 5 (Bunda); Shirati-Bubombi Group hekta 5 (Rorya) na Gollan-Shuta-Shuta hekta 30 (Jiji la Tanga). Aidha, Wizara itatuma timu ya wataalam kwenda India kujifunza namna nchi hiyo ilivyoweza kuendeleza kilimo kwa kutumia teknolojia rahisi za umwagiliaji ikiwemo umwagiliaji kwa kutumia njia ya matone na matumizi ya nishati ya jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Taifa wa Umwagiliaji, Wizara yangu itafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kuuboresha kulingana na hali halisi na malengo ya Taifa ambayo ni pamoja na kupanua eneo la umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000 na kujitosheleza kwa chakula (mpunga na mahindi) kwa kiwango cha asilimia 120 ifikapo mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara itafanya utafiti katika masuala ya teknolojia mbalimbali za umwagiliaji zenye kuongeza na kuboresha uzalishaji na tija kwa mazao kutokana na matumizi ya maji ya umwagiliaji kwa ufanisi. Lengo ni kuhakikisha kuwepo kwa ufanisi na tija katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na hatua hizi, Wizara itaanzisha Kituo cha Utafiti na Mafunzo mkoani Morogoro kwa ajili ya utafiti wa teknolojia za umwagiliaji. Lengo ni kuongeza uzalishaji na tija na matumizi ya maji ya umwagiliaji kwa ufanisi. Vilevile, Wizara itawezesha kufanyika tathmini ya mazingira (Environmental and Social Impact Assessment-ESIA) katika miradi 13 ya umwagiliaji katika kanda zote saba za umwagiliaji. Jumla ya shilingi milioni 400.58 zimetengwa kutekeleza kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza tija katika skimu za umwagiliaji, Wizara imedhamiria kuongeza tija katika uzalishaji wa mpunga kwa kiwango cha kati ya asilimia 75-100 kwa kuanza na skimu 27 za umwagiliaji katika awamu ya kwanza zenye jumla ya hekta 10,159. Skimu hizo zitakarabatiwa na ujenzi wake kukamilishwa kwa kutumia fedha za DIDF ambazo zimetengwa moja kwa moja katika bajeti za

Halmashauri na fedha za NIDF. Wakulima katika skimu hizo watawezeshwa kupitia ruzuku ya pembejeo na DADPs kupata mbolea, mbegu bora, huduma za ugani, zana za kilimo na elimu ya matumizi bora ya ardhi na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza thamani ya zao la mpunga, Wizara kwa msaada wa Serikali ya Japan, (Japan Policy and Human Resource Development – PHRD Grant P125484) itaongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga kwa kuwezesha wakulima katika skimu za umwagiliaji 20 zenye hekta 15,431 kuanza kulima zao hilo kibiashara. Wakulima wapatao 33,108 wa skimu hizo watawezeshwa kuongeza thamani ya zao la mpunga kwa kutumia mashine bora za kuvuna, kukoboa, kuchambua mawe na kupanga mchele kulingana na madaraja mbalimbali. Kiasi cha shilingi bilioni 10.945 zitatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya umwagiliaji kwa wataalam na wakulima, katika mwaka
2011/2012, Wizara itawezesha mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 20 na mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 45 katika fani mbalimbali za umwagiliaji. Aidha, wakulima wa umwagiliaji 105 watapatiwa mafunzo kwa lengo la kuwawezesha kuzitambua na kuzitumia teknolojia mbalimbali zenye kutumia maji ya umwagiliaji kwa ufanisi na uzalishaji wa mazao wenye tija. Ili kufikia lengo hilo, Wizara itawawezesha Wahandisi wa umwagiliaji na Mafundi Sadifu (Irrigation Technicians) wa umwagiliaji kupata mafunzo katika Chuo cha Maendeleo na Usimamizi wa Maji (Water Development and Management Institute – WDMI), Chuo cha Ufundi cha Arusha (Arusha Technical College - ATC), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na MATI Igurusi – Mbeya. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa watumishi wa fani hiyo kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na matumizi bora ya maji ya umwagiliaji. Jumla ya shilingi milioni 613.25 zimetengwa kwa utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupunguza tatizo la upungufu wa wataalam wa umwagiliaji, Wizara inatarajia kupata wataalam 18 kutoka Vietnam kupitia mpango wa South South Cooperation. Kati ya wataalam hao, Wahandisi wa Umwagiliaji watakuwa sita na Mafundi Sadifu 12. Hatua hiyo ni ya muda mfupi wakati Wizara inaendelea kujenga uwezo. Jumla ya Shilingi milioni 61.47 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, Wizara itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Ushirikiano wa Kitaalam kati ya Tanzania na Japan (Tanzania Japan Technical Cooperation Project-TCP). Katika awamu hii, utekelezaji utahusisha kufundisha wataalam wa umwagiliaji na wakulima namna ya kutumia miongozo ya umwagiliaji iliyoandaliwa katika awamu ya kwanza. Mafunzo hayo yatatolewa katika skimu saba za umwagiliaji za mfano zilizochaguliwa kutoka katika kila kanda ya umwagiliaji. Skimu hizo ni Mvumi (Kilosa); Kivulini (Mwanga); Bahi-Sokoni (Bahi); Inala (Tabora Manispaa); Mahiga (Kwimba); Mshewe (Mbeya); na Narunyu (Lindi Vijijini). Wataalam wa kanda za umwagiliaji na Halmashauri husika pamoja na wakulima 13,468 watanufaika na mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo na zana za kilimo, katika kuharakisha mapinduzi ya kijani, matumizi ya pembejeo na zana bora za kilimo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na tija. Hata hivyo, matumizi ya pembejeo na zana za kilimo ni madogo hapa nchini kutokana na sababu mbalimbali hususan gharama kubwa ya pembejeo na zana na hivyo kufanya mkulima mdogo kushindwa kumudu gharama hizo. Kutokana na hali hiyo Serikali ilianzisha utaratibu wa kutoa ruzuku mwaka 2003/2004 ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo na zana kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Ruzuku. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kugharamia ruzuku ya mbolea, mbegu bora, miche bora ya kahawa na chai pamoja na madawa ya pamba na korosho. Idadi ya wakulima watakaonufaika na mpango wa ruzuku kwa mazao ya chakula kwa utaratibu wa vocha ni 1,800,000. Aidha, jumla ya mbolea itakayotolewa kwa utaratibu wa ruzuku ni tani 180,000 na mbegu bora kwa mazao ya mpunga na mahindi ni tani 18,157. Idadi ya wakulima wanufaika kwa mazao ya chakula itapungua ikilinganishwa na idadi ya wakulima 2,000,000 wa mwaka
2010/2011 kutokana na ufinyu wa bajeti. Aidha, wakulima 737,000 walioanza kupata ruzuku tangu mwaka
2008/2009 kwa utaratibu wa vocha wametimiza miaka mitatu ya kupata ruzuku na hivyo, tunaamini kuwa wakulima hao wana uwezo wa kununua pembejeo bila kutegemea tena ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia itaendelea kutoa ruzuku kwa mbegu bora za mtama tani 356, ambapo wakulima wapatao 127,300 kutoka Mikoa yenye ukame ya Dodoma, Shinyanga, Singida, Tabora, Mwanza na Mara watanufaika. Aidha, mikoa ya Shinyanga na Singida itapata mbegu za alizeti tani 50 kwa utaratibu wa ruzuku. Wizara pia itatoa ruzuku kwenye miche ya chai na kahawa. Jumla ya miche

milioni 10 ya kahawa na milioni 10 ya chai itazalishwa na kusambazwa. Aidha, ruzuku itatolewa kwa ajili ya tani 19,475 za mbegu za pamba na acrepack 3,324,200 za madawa ya pamba. Ruzuku pia itatolewa kwa madawa ya korosho tani 64,000. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa mpango wa ruzuku ni Shilingi bilioni
136.67.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa Mbegu Bora. Kwa ujumla mahitaji ya mbegu bora nchini ni makubwa. Mahitaji ya mbegu bora za nafaka, mikunde na mbegu za mafuta iwapo kila mkulima atatumia mbegu bora (potential demand) ni tani 120,000 kwa mwaka. Aidha, mahitaji halisi (actual demand) ya mbegu yanakadiriwa kuwa tani 60,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mbegu bora nchini kwa sasa ni tani 13,828 tu, hivyo Wizara itatekeleza mpango wa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini kwa lengo la kufikia angalau tani 60,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Maeneo ya utekelezaji yatakayozingatiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa ASA wa kuzalisha mbegu kwa wingi kwa kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali ikiwa ni pamoja na kupanua eneo linalolimwa na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili kuwezesha uzalishaji wa mbegu kufanyika mpaka mara tatu kwa mwaka; kuiwezesha ASA kuingia mikataba na makampuni ya mbegu ya Tanzania ili kuzalisha mbegu za msingi; kuhamasisha na kuyawezesha makampuni binafsi ya Tanzania kuanzisha mashamba ya mbegu au kuingia ubia na Serikali; na kuruhusu Sekta binafsi (Makampuni Binafsi) kuzalisha mbegu za msingi kwa kutumia mbegu mama zinazozalishwa na Vituo vya Utafiti vya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo itaongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 1,881 msimu wa 2010/2011 hadi tani 4,000. Pia, kwa kupitia utaratibu wa makubaliano yaliyopo kati ya ASA na Jeshi la Magereza/Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jumla ya tani 3,000 za mbegu bora zitazalishwa. Sekta binafsi inatarajiwa kuzalisha tani 15,000. Hivyo, uzalishaji wa mbegu bora nchini unatarajiwa kufikia tani 22,000. Miche ya matunda 200,000 na vipando vya mihogo
25,000,000 vitazalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa mashamba matatu ya mbegu ya Arusha (hekta 50), Msimba (hekta 100) na Kilangali (hekta 200) utaendelea ambapo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji utafanyika ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mbegu katika msimu wa uzalishaji. Jumla ya Shilingi bilioni 7.28 zimetengwa kwa kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (Tanzania Official Seed Certification Institute- TOSCI) itakagua jumla ya hekta 6,000 za mashamba ya mbegu za mazao mbalimbali ya makampuni binafsi, ASA na wakulima wanaozalisha Mbegu za Daraja la Kuazimiwa (QDS). Aidha, kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na kupima ubora wa mbegu zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa nchini kiasi cha takriban tani 18,000; kuthibitisha uhalisia wa aina 30 za mbegu mpya; na kukamilisha maandalizi ya taratibu za kujiunga na mashirika ya Organisation for Economic Cooperation and Development (OECD), International Seed Testing Agency (ISTA) na The International Union for the Protection of New Varieties of Plants - UPOV ili mbegu zinazozalishwa nchini ziweze kufikia viwango vya ubora vinavyokubalika Kimataifa. Katika kufanikisha hilo, Wizara itaijengea uwezo TOSCI kwa kununua vifaa vya maabara, madawa na jenereta ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake wa ukaguzi wa ubora wa mbegu zilizoko sokoni katika Halmashauri za Wilaya 40 ili kukabiliana na tatizo la mbegu zisizo na ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zana za kilimo. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora na mashine za usindikaji mazao ya kilimo kibiashara. Aidha, kwa kushirikiana na Center for Agricultural Mechanization and Rural Technology (CAMARTEC), Tanzania Automotive Technology Center (TATC) na Mzinga Corporation itaendeleza teknolojia zilizobuniwa kwenye Taasisi za utafiti katika Halmashauri 10. Halmashauri hizo ni Korogwe, Muheza, Handeni, Morogoro Vijijini, Kilosa, Newala, Tandahimba, Masasi, Nanyumbu na Lindi Vijijini. Mashine sita za kuchuna katani (decorticator) na mashine 30 za kubangua korosho zitanunuliwa na mafunzo juu ya uendeshaji wa mashine hizo yatatolewa katika Halmashauri husika; kazi hiyo imetengewa Shilingi milioni 36.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, CAMARTEC, SUA, TATC, MZINGA, Shirika la Viwanda Vidogo na Tume ya Sayansi na Teknolojia kuandaa taratibu za usimamizi wa ubora wa mashine za kilimo zinazoingizwa nchini. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya za Mtwara Vijijini, Kibaha, Mbarali na Singida itaanzisha na kuendeleza viwanda vinne vidogo vyenye uwezo wa kusindika tani 10 za muhogo kwa siku. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni

119. Vilevile, Wizara itahamasisha matumizi ya zana zinazoendeshwa na matrekta madogo ya mkono kwa kutoa mafunzo kwa wakulima katika skimu 40 za umwagiliaji. Mafunzo hayo yatahusu matumizi ya mashine za kukata mpunga; kupura mpunga na za kunyunyizia dawa. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 81.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara, itaendeleza na kutoa msukumo wa matumizi ya zana za kilimo hifadhi zinazokokotwa na trekta dogo la mkono (kipandio na tindo) kwenye Halmashauri 10 na kuhamasisha utengenezaji wa zana hizo hapa nchini. Halmashauri zitakazohusika ni Karatu, Arusha, Meru, Babati, Hanang, Handeni, Kiteto, Kongwa, Kilosa na Mvomero. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 105. Aidha, Wizara itatathmini mahitaji ya nguvu za mashine za kilimo kwenye kanda nne za kilimo za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na Kanda ya Magharibi ikijumuisha kukusanya takwimu, kuzihakiki na kuzihifadhi. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 37.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itatoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wataalam 15 wa zana kuhusu mashine za kilimo, usindikaji mazao ya kilimo na nishati jadidifu (renewable energy). Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 106.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Pembejeo. Katika mwaka 2011/2012, Mfuko wa Pembejeo utatoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 6.7 ikiwemo mikopo ya matrekta mapya makubwa 119 yenye thamani ya Shilingi bilion 4.76; matrekta madogo ya mkono (power tiller) yenye thamani ya Shilingi milioni 900; pembejeo za kilimo na mifugo (mbolea, mbegu, vifungashi, sumu na madawa ya mimea na mifugo) kwa wasambazaji 65 yenye thamani ya Shilingi milioni 744.74; vifaa vya umwagiliaji vyenye thamani ya Shilingi milioni 160; na vifaa vya usindikaji vyenye thamani ya Shilingi milioni 180.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Huduma za Kitaalam. Utafiti wa Kilimo. Katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kupitia vituo vyake vya utafiti itaendelea kutafiti aina za mbegu mpya za mazao zenye sifa za kuzaa sana, kukomaa mapema, kustahimili ukame, zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na visumbufu vya mimea na zinazokidhi viwango vya ubora na matakwa ya wadau na soko. Lengo ni kupata mbegu bora ambazo mkulima akizitumia atavuna mazao mengi hivyo kujitosheleza kwa chakula na kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara inatarajia kutoa angalau aina tano za mbegu bora za mazao mbalimbali ya nafaka, jamii ya mikunde, mbogamboga na matunda. Vilevile, Wizara itaendelea kutafiti mbinu bora za kilimo cha uzalishaji wa mazao mbalimbali katika maeneo husika kufuatana na ikolojia yanapolimwa katika kanda zote saba ili kuweza kupata angalau teknolojia bora tano za agronomia. Wizara inategemea kupata angalau teknolojia aina tatu za kudhibiti visumbufu vya mimea pamoja na madawa ya asilia na ya viwandani. Katika kutekeleza hayo mbinu za ushirikishwaji wa wadau zitatumika ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti kwa kutumia mashamba ya wakulima (on-farm research); shilingi milioni 902.76 zitatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzalisha Mbegu Mama (Breeder’s Seeds). Wizara itaendelea kuhifadhi na kuzalisha mbegu mama tani 30 za mazao ya jamii za nafaka, mikunde, mbegu za mafuta na vipingili
1,000,000 vya mazao ya mizizi. Mbegu mama ni chanzo cha mbegu bora ambazo zikizalishwa katika daraja la mbegu za msingi, zitawezesha kuzalisha mbegu zilizothibitishwa na kuweza kumpatia mkulima mbegu bora. Jumla ya Shilingi milioni 152.38 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa udongo na rutuba ya ardhi. Katika mwaka 2011/2012, Wizara, kupitia vituo vya utafiti vya Mlingano, Uyole, Selian na Ukiriguru itahakiki na kupendekeza teknolojia angalau tano za urutubishaji husishi wa udongo (Integrated Soil Fertility Management options) kulingana na ikolojia za kilimo zilizoko katika Wilaya 53 ambazo zinapata ruzuku ya pembejeo. Lengo ni kuwezesha wakulima kutumia aina na viwango sahihi vya mbolea kulingana na aina ya udongo katika maeneo yao. Aidha, Wizara itaendelea kutathmini hali ya udongo wa maeneo mbalimbali na kutoa ushauri wa matumizi sahihi ikiwa ni pamoja na kuhakiki na kutoa mapendekezo kuhusu viwango vya matumizi ya mbolea. Jumla ya Shilingi milioni 486.13 zitatumika kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa uratibu wa utafiti nchini. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendeleza mchakato wa uanzishwaji wa Taasisi inayojitegemea ya Utafiti wa Kilimo ili kuboresha utafiti na kuhakikisha kuwa teknolojia zinamfikia mkulima. Jumla ya Shilingi milioni 91.70 zimetengwa ili kutekeleza mchakato huo.Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mifumo ya kilimo na Sayansi ya Jamii. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kufanya uchambuzi wa gharama na mapato (farm budgets) inayopatikana katika kilimo kwenye ngazi ya wakulima vijijini ili kuwaonesha wakulima faida ya matumizi bora ya teknolojia kwa lengo la kuwawezesha kuchagua aina ya teknolojia zinazowafaa. Ili kujua kiwango na mafanikio yanayopatikana katika teknolojia zilizopelekwa kwa wakulima, Wizara itafanya tathmini za mafanikio ya upokeaji wa teknolojia. Shilingi milioni 367.00 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha Vituo na Kuimarisha Uwezo wa Watafiti. Katika mwaka
2011/2012, Wizara kupitia ASDP na Programu ya Kilimo ya Kuendeleza Tija na Uzalishaji katika Afrika ya Mashariki (Eastern Africa Agricultural Productivity Programme – EAAPP), itaendelea kukarabati baadhi ya nyumba za kuishi wafanyakazi wa vituo vya Selian kwa kujenga nyumba mpya moja, kufanya ukarabati wa nyumba moja kituo cha Ilonga na kujenga miundombinu ya vituo vya KATRIN pamoja na Ukiriguru ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi watafiti. Katika kuhakikisha teknolojia zinapatikana haraka kwa muda mfupi, vituo vya KATRIN, Ukiriguru na Dakawa vitajengewa mifumo ya umwagiliaji katika mashamba ya majaribio. Vilevile, Wizara itaendelea kupunguza matatizo ya vitendea kazi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari matano, pikipiki 15 na ukarabati wa nyumba mbili. Aidha, watafiti 11 wakiwemo tisa wa shahada za uzamili na wawili wenye shahada ya uzamivu watahitimu masomo yao. Pamoja na hao, jumla ya watafiti 60 watajengewa uwezo katika mafunzo ya muda mrefu. Kati ya hao watafiti 46 watapata ufadhili kutoka fedha zilizotengwa na Serikali kupitia COSTECH. Vilevile, watafiti na watumishi wengine wapatao 100 watapatiwa mafunzo mbalimbali kulingana na fani zao. Jumla ya Shilingi bilioni 2.54 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kufanya marekebisho ya kanuni za kusimamia matumizi salama ya bayoteknolojia (biotechnology) ili kuweka mazingira mazuri ya kuhawilisha na kuendeleza utafiti na matumizi ya taaluma ya uhandisi jeni (Genetic Engineering) katika Sekta ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za Ugani. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itashirikiana na TAMISEMI kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima kwa kuboresha uenezaji wa teknolojia kwa kutumia mbinu shirikishi jamii katika kilimo. Mbinu shirikishi katika kilimo zitaongeza matumizi ya Shamba Darasa kutoka mashamba 6,393 yenye wakulima 157,782 mwaka 2010/2011 hadi 9,500 yenye wakulima
237,500 katika Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara kupitia Programu ya Kilimo ya Kuendeleza Tija na Uzalishaji katika Afrika ya Mashariki itatoa mafunzo kwa wakulima 280 na wataalam wa ugani 150 katika maeneo yanayozalisha mpunga, muhogo na ngano; na pia itahamasisha uanzishaji na uendelezaji wa vikundi vya usindikaji 10 katika mazao hayo katika mikoa ya Kanda ya Kusini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini. Aidha, Wizara itaboresha uandaaji na uenezaji wa teknolojia sahihi katika kilimo hususan kwa mazao ya mpunga, muhogo na ngano kwa kutumia vipindi 36 vya redio na vipindi vinane vya TV.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itaboresha Kitengo cha Ukulima wa Kisasa ili kiweze kutoa elimu bora kwa wadau kwa njia ya redio, TV na machapisho na kusambaza teknolojia 20 za mazao mbalimbali hususan mpunga, mahindi, mtama, muhogo, mbegu za mafuta, mbogamboga na matunda katika Vituo vya Taaluma vya Kata 127 na Ofisi Kiungo za Mawasiliano za Kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kutumia mkulima kiongozi kuwafundisha wakulima wenzake (Farmer-to-Farmer Extension) utaimarishwa kwa kutoa mafunzo kwa wakulima ili waweze kusimamia uzalishaji wa mpunga katika skimu 27 za umwagiliaji katika mikoa 17 na wakulima wa mazao ya mahindi, muhogo, matunda, mbogamboga na mazao ya mbegu za mafuta. Vilevile, elimu kwa wakulima itatolewa kupitia vipindi vya redio, vijitabu, machapisho, vipeperushi, mabango na sinema vijijini kwa kuzingatia kanda za kilimo kwa kutumia Ofisi Kiungo za Mawasiliano za Kanda. Pia, Wizara itawezesha maonyesho ya teknolojia mbalimbali katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane na Siku ya Chakula Duniani na Miaka 50 ya Uhuru. kupitia mpango huo, kazi hizo zimetengewa kiasi cha Shilingi bilioni
1.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itadahili na kufundisha vijana 3,500 ngazi ya Stashahada na Astashahada kwa ajili ya kuongeza idadi ya Maafisa Ugani. Kazi hiyo itagharimu Shilingi bilioni 3.59. Aidha, Wizara itakarabati mabweni mawili ya Chuo cha Mbondo (Kigoma) ili kuweza kupokea wanafunzi 80 kuanzia Novemba - Desemba 2011. Kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 139.94. Vilevile, Wizara itanunua vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuboresha mazingira ya mafunzo kwenye chuo cha MATI Igurusi kwa kununua vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kufundishia somo la umwagiliaji na matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itawajengea uwezo wafanyakazi wa kilimo kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ambapo watumishi 150 watapata mafunzo katika fani mbalimbali. Kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 287. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI itatoa mafunzo ya kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima wa zao la mpunga katika skimu 12 za umwagiliaji. Lengo ni kuongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kufikia tani 5 kwa hekta; kazi hiyo imetengewa Shilingi milioni 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa visumbufu vya mimea na mazao. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea na udhibiti wa milipuko ya visumbufu mbalimbali ikiwemo ya nzige wekundu, kwelea kwelea, viwavijeshi na panya. Jumla ya Shilingi bilioni 2.99 zimetengwa kwa kazi hiyo. Vilevile, Wizara itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya ya Mimea kwa kutoa mafunzo kwa wakaguzi na kuajiri wakaguzi 52 wa mazao na madawa ya mimea ili wasimamie ipasavyo utekelezaji wa sheria hiyo kwa ufanisi zaidi. Aidha, Wizara itatoa huduma ya karantini ya mimea na mazao ili kuepukana na athari ya kuenea kwa visumbufu. Ili kukidhi viwango vya ubora unaotakiwa na masoko ya nje na kudhibiti uingizaji wa magonjwa ya mazao nchini, Wizara itaimarisha huduma ya ukaguzi wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendelezaji wa mazao ya kilimo. Uzalishaji wa Mazao Makuu ya Biashara. Wizara kupitia Bodi za Mazao Makuu ya Biashara itatekeleza mikakati inayolenga kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao. Juhudi maalum zitaelekezwa katika kuhakikisha wakulima wanapata bei ya haki kulingana na nguvu ya soko, na gharama za uzalishaji, hivyo Wizara itafanya tathmini ya makato yote yanayofanyika wakati wa kukokotoa bei za wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Bodi za Mazao zitaendelea kutoa huduma za elimu ya kilimo bora cha mazao hayo moja kwa moja kwa wakulima au kupitia kwa wataalam wa ugani katika Halmashauri zinazozalisha mazao hayo, kusimamia sheria na kanuni za uzalishaji na biashara ya mazao hayo na kuwapatia wakulima taarifa za bei dira za mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha mfumo wa masoko wa mazao, Wizara itashirikiana na Wizara za Kisekta, Wizara ya Fedha na wadau wengine kuandaa utaratibu utakaohakikisha kunakuwepo na mfumo rasmi wa masoko ya mazao ya wakulima kwa kutumia utaratibu wa Commodity Exchange Markets. Mfumo huo utaanza kutekelezwa katika mazao ambayo tayari yana mifumo ya ushirika na utaratibu wa kuuza mazao kupitia Stakabadhi za Maghala. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya Bodi za Mazao ili kutekeleza majukumu hayo ni Shilingi bilioni 8.19. Pamoja na hatua hizi Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanzisha kikosi kazi cha kuharakisha mchakato wa uanzishaji wa mfumo wa kuuza mazao kupitia Commodity Exchange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamba, matarajio ya uzalishaji wa pamba msimu wa 2011/2012 ni tani
250,000 za pamba mbegu kutoka katika hekta 469,345 zilizolimwa. Ongezeko la uzalishaji unaotarajiwa utachangiwa na bei waliolipwa wakulima msimu 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti. Tumbaku, katika mwaka 2011/2012, tani 93,000 za tumbaku zinatarajiwa kuzalishwa ikilinganishwa na tani 130,000 zilizozalishwa mwaka 2010/2011. Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa tumbaku nyingi katika masoko asilia ya tumbaku ya Tanzania hususan masoko ya Ulaya, Marekani na Japan ikilinganishwa na mahitaji. Kutokana na tatizo hilo la soko, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kutafuta masoko mengine duniani ili kupanua wigo wa soko la tumbaku ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pareto, lengo la uzalishaji wa pareto katika mwaka 2011/2012 ni tani
5,600. Lengo hilo linatarajiwa kufikiwa kutokana na upatikanaji wa miche bora, kuimarisha huduma za ugani, kuimarisha utafiti katika Kituo cha Uyole na kuongeza ubora wa maua. Aidha, wastani wa tani 4,000

za pareto zinatarajiwa kusindikwa na kutoa wastani wa kilo 160,000 za sumu ghafi zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 9.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chai, katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa chai unatarajiwa kufikia tani
35,000. Uzalishaji huo utachangiwa na ujenzi wa Kiwanda cha Kusindika majani mabichi ya chai katika Tarafa ya Lupembe unaofanywa na Kampuni ya Chai na Kahawa ya Mufindi (Mufindi Tea and Coffee Company Limited), kufufuliwa kwa mashamba ya Mlangali ambayo huchangia tani 300 za chai kwa mwaka na kuhamasisha matumizi ya pembejeo kwa wakulima wadogo wa chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari, katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa miwa unatarajiwa kufikia tani milioni 3.28 ikiwa ni sawa na tani 317,000 za sukari. Ongezeko hilo litafikiwa kutokana na uhamasishaji wa uzalishaji wa mashamba makubwa (block farming), kuimarisha utafiti wa mbegu mpya za miwa zilizoagizwa kutoka Afrika ya Kusini, Mauritius na Reunion chini ya usimamizi wa Kituo cha Utafiti wa Miwa (Sugar Research Institute-SRI) na kuhamasisha matumizi endelevu ya zao la miwa ili liweze kutumika katika kuzalisha nishati mbadala ya ethanol pamoja na umeme (co-generation).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa, katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa kahawa unatarajiwa kupungua kutoka tani 60,575 za mwaka 2010/2011 hadi tani 45,000. Upungufu huo unatokana na tabia ya zao la kahawa kupungua uzalishaji katika msimu unaofuatia msimu wa uzalishaji ulioongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkonge, katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa zao la mkonge unatarajiwa kuwa tani 35,000 sawa na msimu wa 2010/2011 kutokana na tatizo la umeme katika viwanda vya usokotaji wa mkonge. Aidha, uzalishaji wa mbegu za mkonge kwa kutumia teknolojia ya vikonyo (meristematic tissue culture) utaimarishwa; kuendeleza soko la mkonge na bidhaa zake ndani na nje ya nchi, kushirikiana na vituo vya utafiti na vyuo vikuu ili kuongeza teknolojia na utaalam katika hatua za uzalishaji (upandaji, palizi, uvunaji) na uzalishaji wa bidhaa za mkonge na kuendeleza kilimo cha mkataba kati ya wakulima wadogo na Kampuni ya Katani Ltd.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho, katika msimu wa 2011/2012, matarajio ni kuongeza uzalishaji kutoka tani 121,070 za msimu 2010/2011 hadi tani 127,000 za korosho ghafi. Lengo hilo linatarajiwa kufikiwa kutokana na kuongezeka kwa bei ya korosho msimu uliopita iliyosababishwa na matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Maghala na uhamasishaji wa matumizi ya korosho na mazao yake nchini na nje ya nchi. Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha ongezeko la uwezo wa ubanguaji korosho nchini hadi kufikia wastani wa asilimia 40 mpaka 45 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 30 hadi 40 kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendelezaji wa mazao ya bustani. Mazao ya bustani yana umuhimu mkubwa katika kuboresha lishe na katika kuongeza kipato kwa wakulima na kulipatia Taifa fedha za kigeni hasa kwa sababu mazao hayo yana thamani kubwa. Katika mwaka 2011/2012, Wizara kwa kushirikiana na wadau itaandaa Programu ya Kitaifa ya kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani na kusimamia utekelezaji wake. Aidha, Wizara itaimarisha bustani za Mpiji, Bugaga, Igurusi, Jaegetal, Kizugu na Songa ili kuhifadhi vinasaba vya mazao ya bustani kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa miche bora. Vilevile, Wizara itaendelea kuingiza nchini vinasaba bora zaidi vya mazao ya bustani kwa ajili ya kuboresha vinasaba vilivyopo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia itaendelea kuainisha na kuwasajili wazalishaji wa miche ya mazao ya bustani na kuwajengea uwezo kimafunzo ili wazalishe miche bora itakayoongeza uzalishaji na ubora wa mazao. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza mazao ya bustani katika nyanja mbalimbali zikiwemo: kuanzisha vituo vya ukusanyaji na uhifadhi wa mazao ya bustani; kuimarisha mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa taarifa za masoko na bei ya mazao ya bustani; kuimarisha uwezo wa Chuo cha HORTI - Tengeru ili kitoe mafunzo yanayolingana na mahitaji ya wadau kwa mazingira ya sasa; na kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kutangaza na kupanua wigo wa soko la bidhaa za Tanzania za mazao ya bustani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu za mafuta. Wizara inatambua umuhimu wa kuendeleza mazao ya mbegu za mafuta ili kuzalisha mafuta ya kula kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ndani na hivyo kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi na ikiwezekana kuuza ziada nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kusimamia utafiti na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta. Aidha, itaratibu na kuwaunganisha wadau wote wa sekta ndogo ya mazao ya mbegu za mafuta za ufuta, alizeti, karanga, kartamu (safflower), pamba, michikichi na soya pamoja na kusaidia katika kuanzisha umoja kati yao ili kuwa na uzalishaji endelevu na wa kibiashara kwa mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itafanya savei tatu za utabiri wa uzalishaji wa mazao ya chakula ili kubaini hali ya chakula nchini na hatua za kuchukuliwa. Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa usalama wa chakula itafanya tathmini za kina za hali ya chakula kwa lengo la kutambua kaya zenye upungufu wa chakula na kupendekeza hatua za kukabiliana na upungufu huo. Wizara itakusanya takwimu za hali ya mazao na mvua katika vituo 600 na kutoa ushauri na pia itaainisha na kusambaza teknolojia mbalimbali za kuhifadhi mazao ya chakula. Shilingi milioni 550 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya chakula. Katika mwaka 2011/2012, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula imepanga kununua tani 200,000 za nafaka kutoka Mikoa ya Rukwa, Iringa, Mbeya, Ruvuma na Kigoma na kuzihifadhi katika maghala yake ili kukabiliana na upungufu wa chakula utakaoweza kujitokeza. Jumla ya Shilingi bilioni 17.6 zimetengwa katika bajeti kwa ajili ya kazi hiyo. Aidha, fedha nyingine zinategemewa kutokana na mauzo ya mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi bora ya ardhi. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itatoa mafunzo ya kitaalam kwa maafisa 10 wa Kanda na 44 kutoka Halmashauri za Wilaya za Moshi Vijijini, Bahi, Kongwa, Kondoa, Chamwino, Kishapu, Meatu, Bariadi, Maswa, Igunga, Iramba na Singida Vijijini. Nyingine ni Kisarawe, Kilwa, Kilosa, Mvomero, Morogoro Vijijini, Handeni, Kilombero, Ngara, Karagwe na Misenyi. Mafunzo hayo yatahusu teknolojia za hifadhi ya udongo na maji mashambani na jinsi ya kuibua miradi ya matumizi bora ya ardhi ya kilimo katika Halmashauri hizo. Kazi hiyo imetengewa Shilingi milioni 114.28.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na FAO kutekeleza mradi wa Globally Important Agricultural Heritage Systems unaolenga kuainisha mifumo mbalimbali asilia ya kilimo na ufugaji endelevu katika Mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro na Ruvuma. Katika mwaka 2011/2012, shughuli za mradi huo zitatekelezwa katika Wilaya za Moshi Vijijini, Kata ya Uru, Kijiji cha Uru Shimbwe na Ngorongoro katika Kijiji cha Engarasero ambapo mafunzo yatatolewa kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia za kilimo mseto, matumizi endelevu ya ardhi ya kilimo na mbinu za kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto duniani. Jumla ya Shilingi milioni 28.51 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuchochea kasi ya uwekezaji katika kilimo cha kibiashara, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Sekretarieti za Mikoa na Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi itaendelea kutambua na kupima maeneo yanayofaa kwa kilimo cha kibiashara katika vijiji 10 vya mikoa ya Morogoro na Pwani vilivyoandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili hatimaye yajumuishwe kwenye benki ya ardhi (Land Bank). Aidha, mipaka ya maeneo ya kituo cha Mabogini (Moshi Vijijini), kituo cha majaribio Magugu (Babati), shamba la majaribio Ngaramtoni (Arusha Mjini), Shamba la mbegu Dabaga (Kilolo), shamba la Mpiji (Bagamoyo) na Taasisi ya Utafiti wa Madawa ya Visumbufu vya Tropiki (Tropical Pesticides Research Institute-TPRI) (Arusha), itahuishwa na kupimwa ili yapatiwe hati miliki ya ardhi ya Serikali. Fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 84.63.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya mazingira. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kuratibu, kudhibiti na kuhamasisha shughuli za hifadhi ya mazingira katika maendeleo ya kilimo. Wizara pia itatoa mafunzo kwa Halmashauri kuhusu masuala ya hifadhi ya mazingira katika kilimo kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Vilevile, Wizara itafanya tathmini ya athari za shughuli za kilimo kwenye mazingira katika skimu za umwagiliaji zilizopo katika Wilaya za Kwimba, Nzega, Mpwapwa, Mbarali, Kilolo, Mtwara Vijijini, Kilosa na Moshi Vijijini. Jumla ya Shilingi milioni 47.56 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya rasilimali watu. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itapandisha cheo watumishi 290 katika madaraja mbalimbali na kuajiri watumishi wapya 588 wa kada mbalimbali. Kati yao 142 ni Wahandisi wa Umwagiliaji, 52 ni Wakaguzi wa mazao, 60 ni Watafiti, 15 ni Wahandisi wa zana za kilimo na waliobaki 319 ni wa kada nyingine. Aidha, Wizara itashirikiana na TAMISEMI

kuajiri wagani 5,089 (wakiwemo 4,291 wa Astashahada na Stashahada; na 798 wa Shahada) na Maafisa
Ushirika 435 waliohitimu mwaka 2010 na 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kuwawezesha watumishi 17 wanaoishi hivi sasa na VVU na watakaojitokeza kupata lishe bora na matibabu. Kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 30. Aidha, Wizara itaendelea kusimamia Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS) katika vituo vyote vya Wizara. Kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 30. Vilevile, Wizara itaendelea kufanya ukaguzi wa watumishi (Human Resources Audit) ili kuiwezesha Wizara kusimamia vyema ankara ya mishahara na kupanga matumizi bora ya rasilimali watu; kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio ya Sekta ya Ushirika, sekta hiyo inaendelea kukabiliwa na vikwazo vingi ikiwa ni pamoja na idadi ndogo ya Maafisa Ushirika ikilinganishwa na idadi ya Vyama vya Ushirika. Kwa sasa Afisa Ushirika mmoja anasimamia vyama 17 ikilinganishwa na uwiano unaotakiwa wa Afisa Ushirika mmoja kusimamia vyama saba. Pia, baadhi ya viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika kukosa uaminifu na kutokuwajibika katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo; vyama vingi kukosa watendaji wenye sifa; na mitaji midogo katika kuendesha shughuli za vyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na vikwazo hivyo, katika mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kutekeleza Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika ikiwa ni pamoja na kutekeleza Sera, Sheria, Mikakati na usimamizi katika sekta ya Ushirika; kuimarisha na kuwezesha Asasi za Wananchi katika Ushirika; kuanzisha na kuijengea uwezo Tume ya Maendeleo ya Ushirika ikiwa ni pamoja na kuajiri maafisa ushirika 20 ili kutekeleza majukumu yake; kuimarisha Mfumo wa Ukusanyaji, Uhifadhi, Uchambuzi na Usambazaji wa takwimu na taarifa za Vyama vya Ushirika; kuimarisha utekelezaji endelevu wa Mkakati wa Taifa wa kupambana na rushwa; na kuboresha huduma na kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera, Sheria, Mikakati na Usimamizi katika Sekta ya Ushirika. Katika mwaka
2011/2012, Wizara itaendelea kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuhamasisha wananchi wengi kujiunga na Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali za uchumi; kuandikisha Vyama vya Ushirika imara kiuchumi na vyenye uwezo wa kujiendesha kibiashara; kuimarisha usimamizi na utawala wa fedha katika vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) na mabenki ya Ushirika; kusimamia na kuendeleza maadili, misingi ya ushirika, utawala bora; na kusimamia manufaa yatokanayo na ushirika kwa wanachama wake na jamii. Aidha, Wizara itachukua hatua zenye lengo la kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika. Jumla ya vyama 100 vitasajiliwa; mafunzo yatatolewa kwenye vyama vya ushirika 350; na ukaguzi utafanyika kwenye Vyama vya Ushirika 3,900 na Benki mbili za Ushirika. Vilevile, miongozo mitatu ya ukaguzi na 14 ya usimamizi wa vyama vya ushirika itakamilishwa na kusambazwa kwa wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya utekelezaji wa mpango huu ni kuwa na Vyama vya Ushirika imara kiuchumi vinavyojitegemea na vinavyoendeshwa kibiashara, kuweka nidhamu katika uendeshaji; kuimarisha uongozi; kuwepo kwa utawala bora; kudhibiti ubadhirifu ndani ya vyama kwa kuzingatia maadili ya uongozi; na kuwepo kwa taasisi imara za fedha za kiushirika. Aidha, kuunganisha au kufuta vyama dhaifu na kuondoa utitiri wa vyama vidogo vidogo katika kujenga vyama vikubwa vyenye nguvu na vitakavyokidhi mahitaji ya soko. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi bilioni 1.357.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga uwezo wa Asasi za Wananchi za Ushirika. Katika mwaka
2011/2012, Wizara itaendelea kuimarisha asasi za wananchi za ushirika kwa kuwezesha kuwepo kwa weledi, utaalam wa masoko na uongezaji wa thamani ya mazao katika Vyama vya Ushirika. Aidha, mafunzo yatatolewa kwa Vyama vya Ushirika vya mazao 400, SACCOS 300 na Benki za Ushirika mbili. Mafunzo hayo yatahusu uzalishaji na masoko na utawala wa fedha ikiwemo ujenzi wa mitaji ya vyama na mikopo. Pia, vijana wanaoshiriki katika kilimo watahamasishwa kuunda Vyama vya Ushirika vya uzalishaji na kusaidiwa kupata mitaji na masoko. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 349.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itakamilisha mapendekezo ya Muswada wa kutunga Sheria ya kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika na kuijengea uwezo Tume hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu na Taarifa za Vyama vya Ushirika. Katika mwaka 2011/2012, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi katika kuendeleza ushirika, Wizara itaendelea kuboresha utaratibu wa kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za ushirika kwa wadau. Mafunzo yatatolewa kwa Maafisa Ushirika 84 kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kigoma, Singida, Tabora na Dodoma. Mafunzo hayo yatahusu ukusanyaji wa takwimu, kuzitumia na kuzihifadhi. Aidha, kompyuta moja itatolewa kwa kila mkoa kwa ajili ya kuhifadhi takwimu zitakazokusanywa. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni
169.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa. Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Wanaushirika wa vyama 15 kuhusu mkakati wa kuzuia rushwa. Katika kutekeleza mkakati huo, vijarida na vipeperushi vinavyoonesha madhara ya rushwa vitachapishwa na kusambazwa kwa watumishi na Wanaushirika. Fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo ni Shilingi milioni 14.67.

Mheshimiwa Mwenyekiti, UKIMWI. Katika mwaka 2011/2012, Wizara itatoa elimu kwa watumishi 150 kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI na itawahamasisha kupima kwa hiari. Aidha, wale watakaojitokeza kuhitaji huduma za lishe na matibabu watasaidiwa; kazi hiyo itagharimu Shilingi milioni 33.45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani. Naomba nitumie nafasi hii kuzishukuru Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa ambayo yamesaidia sana Wizara katika juhudi za kuendeleza kilimo. Kwanza, napenda kuzishukuru nchi za Japan, Ireland, China, India, Israel, Indonesia, Korea ya Kusini, Marekani, Misri, Ubelgiji na Uholanzi. Nayashukuru pia Mashirika na Taasisi za Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD, DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, CFC, AVRDC, AGRA, WARDA, Rockfeller Foundation na Bill and Melinda Gates Foundation. Ushirikiano na misaada ya Nchi na Mashirika hayo bado tunauhitaji ili tuweze kuendeleza kilimo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za pekee, kwa wakulima wa nchi hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na mazingira magumu waliyonayo. Napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Mhandisi Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu; Katibu Mkuu Bwana Mohamed Said Muya; Naibu Katibu Mkuu Bibi Sophia Elias Kaduma; Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Mbogo Futakamba; Wakurugenzi wa Idara; Taasisi na Asasi zilizo chini ya Wizara; watumishi wote wa Wizara; na wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo kwa juhudi, ushirikiano na ushauri uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka
2010/2011 kama nilivyofafanua katika hotuba hii. Ni matarajio yangu kwamba Wizara itaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka 2011/2012. Mwisho, natoa shukrani kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha kuchapishwa kwa hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya fedha za mpango kwa Mwaka 2011/2012. Kwa kuzingatia maelezo niliyoyatoa, naomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe Shilingi 258,350,877,100 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Fungu 43. Kati ya fedha hizo, Shilingi 152,406,152,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 105,944,725,100 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Kati ya fedha za bajeti ya Maendeleo, Shilingi 14,260,042,000 ni fedha za ndani na Shilingi 91,684,683,100 ni fedha za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Wizara yangu kupitia Fungu 24 inaomba Shilingi
6,660,012,000 kwa ajili ya shughuli za kuendeleza ushirika nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.