You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Limbu, Dr. Festus Bulugu[CCM]

Magu Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
2 5 14 February 2011 Hoja ya Kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Kufungua Bunge Jipya, 2010
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya dakika kumi kulihutubia Bunge lako na Taifa kwa ujumla.

Napenda kuwashukuru sana wapigakura wa Jimbo la Magu kwa kunipa kura za ushindi, kuniamini na kuwa Mbunge kwa awamu ya tatu. Naahidi kwamba sitawaangusha na nitawatumikia kwa moyo wangu wote. Nitashirikiana nao katika kutatua changamoto na kero ambazo zinatukabili. Nawashukuruni sana Wanajimbo la Magu.

Mheshimiwa Spika, pili, napenda niipongeze sana Serikali kwa uamuzi iliyochukua kwa kuanzisha Mikoa miwili, Mkoa wa Geita na Mkoa wa Simiyu. Msongamano wa watu katika Mkoa wa Mwanza ulikuwa mkubwa sana, ulikuwa unaongoza baada ya Dar es Salaam. Msongamano wa watu katika Mkoa wa Mwanza ni wakazi 177 katika kila kilomita ya mraba ikifuatiwa na Kilimanjaro yenye watu 120, Mara yenye watu 90 na mwisho kabisa ni Lindi wenye watu 14 na Ruvuma na Rukwa zenye watu 21. Kwa hiyo, uamuzi wa Serikali kugawa Mkoa wa Mwanza, Geita ikawa Mkoa na Simiyu ikawa Mkoa, itafanya Serikali iongeze resources katika Mikoa hiyo na hatimaye tunaamini kwamba maendeleo yatakwenda haraka zaidi. Ninaamini kwamba kwa utaratibu wa Mkoa, Makuu ya Mkoa lazima yaunganishwe na Mikoa mingine kwa barabara ya lami, sasa kutoka Mwanza kwenda Bariadi barabara itakuwa ya lami ambapo naamini ndipo patakuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Spika, napenda nilete kilio cha wana Magu cha njaa. Hali ya hewa haikuwa nzuri, mwaka huu wakulima na wananchi walijitahidi sana, mvua ziliponyesha wakapanda lakini sasa mahindi yamekauka na mazao mengine yamekauka na hali ni mbaya. Kwa hiyo, naomba kwanza mgao wa chakula au tathmini ya chakula ifanywe haraka katika Jimbo la Magu na Wilaya ya Magu kwa ujumla ili wananchi waweze kupata msaada huo. Kuna Kata nyingi za Jimbo la Magu zimeathirika ikiwemo Kata ya Ng’aya, Shishani, Jinjimili, Sukuma, Magu Majini, Lubugu pamoja na Tarafa ya Sanyo, kwa ujumla sio nzuri.

Mheshimiwa Spika, ombi la pili naiomba Serikali kipindi hiki ambapo mvua zimeonesha dalili za kunyesha tupatiwe msaada wa mbegu za mtama ambazo zinastawi kwa muda mfupi. Halmashauri ya Wilaya imenunua na kusambaza tani saba mpaka sasa tunaomba Serikali iweze kutusaidia ili wananchi waweze kupata mbegu hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende kwenye mambo ya Kitaifa kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kulifungua Bunge lako Tukufu. Tunasheherekea miaka 50 ya uhuru mwaka huu. Miaka 25 ya kwanza ya uhuru nchi yetu, tulijaribu kujenga ujamaa, mwaka 1961 mpaka mwaka 1986. Kwa kweli mambo makubwa na mambo mengi yamefanyika. Miaka 25 iliyofuata tukawa na kitu soko huria na hatukutangaza moja kwa moja kwamba sasa hatujengi ujamaa lakini tukawa na soka huria lakini Ibara ya 3 na ya 9 ya Katiba inasema nchi yetu inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea. Kwa hiyo, tumeachana na ujamaa na kujetegemea kihalisia lakini bado kwenye Katiba yetu tunasema tunajenga siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Mheshimiwa Spika, sasa soko huria na ujamaa na kujitegemea sikuelewa sana kama hivi vitu vinaendana. Tulifanya liberalization kwa kizungu tukaruhusu kwamba sasa mishahara miwili ni ruksa, kufanya biashara ruksa, lakini Katiba yetu bado inasema tunafuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea sio mbaya lakini lilitakiwa liwepo tamko kama walivyofanya China, China walisema sasa tunaendelea kujenga ujamaa lakini tunasema tunakuwa na soko huria na mtu kuwa tajiri ni ruksa. Lakini sisi mpaka leo tunajificha, ukitaka kuonekana tajiri unajifichaficha wakati tumetangaza tunasoko huria. Nafikiri haya ni makosa ambayo yametufanya turudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa wazito kama nchi kufanya maamuzi. Kuna maamuzi yamechukuwa muda mrefu sana ambayo yametuvuta nyuma. Wenzetu kwa mfano mdogo, jirani zetu Kenya wamejenga Airport katikati ya Rombo na Mombasa ambayo inakuja kuua kabisa Kilimanjaro International Airport (KIA), wanajenga Bandari ya Lamu ambayo inakuja kuua kabisa Bandari ya Tanga, wamejenga bomba la mafuta kutoka Mombasa linakaribia Kampala, sisi tumepanga kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza liko kwenye makaratasi, tumekuwa wazito sana kufanya maamuzi ya msingi ambayo yangebadilisha maisha ya Watanzania. Tunahitaji tujifunze, katika miaka 25 inayokuja lazima na kwa sababu kuna fursa sasa kwamba tunaandika upya ama tunarekebisha au vyovyote utakavyosema Katiba yetu, naamini kwamba tutajipanga vizuri zaidi ili kwenda kwa speed zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye Idara ya Nishati na Madini. Kulingana na taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa ya mwaka 2009, ukurasa wa 205, inasema kwamba umeme unaopotea ni mwingi kuliko umeme unaotumika kwa ujumla kwenye viwanda na kwenye biashara mbalimbali. Mwaka 2009 umeme uliotumika viwandani ni Kilowatt/hour milioni 1500, viwanda vyote pamoja na biashara zote lakini umeme uliopotea ni kilowatt/hour milioni 1700. Sasa wakati tunafanya juhudi ya kupata umeme wa ziada lazima tujiulize tunafanya nini kupunguza huu upotevu wa umeme, vinginevyo tutaongeza umeme kwenye gridi, umeme mwingine utaendelea kupotea na hii itakuwa sio kitu kizuri.

Mheshimiwa Spika, kwenye mazingira, asimilia 97 ya wananchi hutumia kuni na mkaa. Bei ya umeme imepanda, bei ya gesi imepanda, sasa tunategemea nini? Wananchi hawa wataendelea kutumia mkaa na kuni, miti itaendelea kukatwa, mvua itaendelea kukosekana, jangwa litakuja, umeme wa maji utapungua, mgao utaendelea kuwepo na uchumi utaendelea kudorora. Naomba suala hili la bei ya umeme na gesi na matumizi ya kuni liangaliwe kwa makini, kama hakuna njia nyingine ya kufanya Watanzania wafanye nini sasa? Kama Watanzania asimilia 97 wanatumia kuni na umeme umepanda, lazima waendelee kukata kuni na hatuna juhudi za makusudi za kuhakikisha kwamba tunapanda miti kwa wingi ambayo ni ya mvua, tunasema kila mwaka tuna siku ya kupanda miti lakini baada ya hapo hakuna tunachofuatilia. Kasi ya kukata miti ni kubwa zaidi kuliko ya kupanda na kuongeza miti. Tunakata miti kama wendawazimu lakini hatupandi miti kama wendawazi. Naomba tujipange, tupande miti kama wendawazimu.

Mheshimiwa Spika, gesi ya magari, kuna wataalam wetu wamegundua kwamba unaweza ukabadilisha gari badala ya kutumia mafuta likatumia gesi. Wamefanya kazi nzuri na teknolojia hii inapunguza asilimia 50 ya matumizi ya mafuta ambayo sasa hivi tunatumia. Naomba pia tuingie huko.

Mheshimiwa Spika, madini tuliyoanza kuyachimba miaka ya karibuni, yametufanya tubweteke. Tumesahau sekta nyingine muhimu kama kilimo wakati tunajua kwamba madini yana mwisho. Tunayatumiaje kujenga economic base yetu hatimaye hata kama madini yatakuwa yameisha yaweze kutusaidia kwa miaka mingine ijayo?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja