| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 4 | 23 | 12 July 2011 | Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii | ||
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara, kwa kuandaa bajeti nzuri ya kisayansi ambayo imesheheni takwimu muhimu mbalimbali. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa angalizo kuhusu hali ya upungufu uliopo kwa muda mrefu katika hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati za Wilaya ya Kondoa hususani Jimbo la Kondoa Kaskazini. Kwanza, upungufu wa Madaktari na Wahudumu wengine wa afya kiasi kwamba inaathiri huduma za afya zinazotarajiwa kwa wananchi mfano, Vituo vya Afya na Zahanati nyingi hazina kabisa Madaktari, badala yake zinahudumiwa na Wauguzi. Pili, upungufu mkubwa wa dawa. Upo upungufu mkubwa sana wa dawa na vifaa muhimu katika hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati. Hali hiyo inaathiri mambo yafuatayo:- - Kushindwa kutimiza azma ya kutoa dawa na matibabu bure kwa wazee wasiojiweza, watoto chini ya miaka kumi na nane na wanawake wajawazito. - Kulazimisha wagonjwa kutafuta dawa nje ya hospitali za Serikali kwa gharama kubwa bila ya kuwepo na utaratibu wa kuwarejeshea gharama zao. Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara iandae mkakati wa dhati utakaowezesha upatikanaji wa Madaktari na vifaa/vitendea kazi kwa kiwango cha kukidhi mahitaji halisi. Pia kujenga mfumo mzuri wa kuiwezesha MSD kupata dawa, kuhifadhi na kuzisambaza katika kanda zilizopo kwa wakati na kwa gharama nafuu uli kukidhi mahitaji halisi katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati hususani katika Wilaya ya Kondoa na Jimbo la Kondoa Kaskazini. Mheshimiwa Naibu Spika, nawatakia kila la kheri katika majukumu yenu na ninaunga mkono hoja. |
|||||