Parliament of Tanzania

TAARIFA FUPI KUHUSU SHAURI LA KUVUNJA HAKI NA KINGA ZA BUNGE LINALOWAHUSU WAHARIRI NA WAANDISHI WA HABARI.

TAARIFA FUPI KUHUSU SHAURI LA KUVUNJA HAKI NA KINGA ZA BUNGE LINALOWAHUSU WAHARIRI NA WAANDISHI WA HABARI WA MAGAZETI YA MTANZANIA, MWANANCHI NA NIPASHE

________________


Waheshimiwa Wabunge, tarehe 8 Novemba, 2017, kwa mujibu wa Kanuni ya 4 (1) (a) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 nilielekeza pamoja na mambo mengine Kamati kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu yafuatayo: -

(a) Suala la Mhe. Zitto Kabwe (Mb) kusambaza nyaraka zinazohusu majadiliano aliyofanya na Kamati, maswali aliyoulizwa na majibu aliyotoa kutokana na kosa alilotuhumiwa nayo

(b) Suala la wahariri na waandishi wa habari wa magazeti kuchapisha na kusambaza mwenendo wa shauri lililokuwa likifanyiwa kazi na Kamati.

Waheshimiwa Wabunge, Kamati imekamilisha kusikiliza shauri linalowahusu Wahariri na Waandishi wa Habari na kunipa Taarifa kuhusu uchunguzi wake.

Waheshimiwa Wabunge, Katika Taarifa yake, Kamati imeeleza kuwa, chimbuko la suala hili inaanzia tarehe 21 Septemba, 2017 wakati Kamati ilipokuwa inasikiliza Shauri dhidi ya Mhe. Zitto Zuberi Kabwe (Mb) linalohusu kudharau Mamlaka ya Spika na Bunge, kutokana na kuandika kwenye mitandao ya kijamii, hususan ukurasa wake wa

Twitter wa Zitto Kabwe Ruyagwa@zittokabwe , maneno ya kumdharau Spika, Bunge na shughuli za Bunge. Siku hiyo, alitoa ushahidi wake na akaomba Kamati ipokee nyaraka aliyoleta ili ziwe sehemu ya ushahidi wake na Kamati ilimkubalia ombi lake.

Waheshimiwa Wabunge, siku iliyofuata, yaani tarehe 22 Septemba, 2017, magazeti ya Mtanzania, Mwananchi na Nipashe yalichapisha habari za mwenendo wa shauri na ushahidi uliotolewa na Mhe. Zitto Kabwe (Mb) mbele ya Kamati.

Waheshimiwa Wabunge, magazeti hayo yalichapisha habari zenye vichwa vya habari vifuatavyo:-

(a) Gazeti la Mtanzania, Toleo Na. 8676: “BUNGE LIMEKOSA MSHAWASHA”.

(b) Gazeti la Mwananchi, Toleo Na. 6265: “ZITTO ASHUSHA NYUNDO 10 KAMATI YA BUNGE”.

(c) Gazeti la Nipashe, Toleo Na. 0579345: “ZITTO AMWAGA MBOGA”.

Waheshimiwa Wabunge, tarehe 15 Novemba, 2017, Wahariri na Waandishi wa Habari wa magazeti hayo waliitwa mbele ya Kamati na kusomewa mashtaka ya kuandika na kuchapisha habari kuhusu mwenendo wa shughuli za Kamati (proceedings) kinyume na Kifungu cha 34(1) (f) na (g) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge,

Sura ya 296 [The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP.296 R.E. 2015]. Kwa mujibu wa Kanuni ya 117(10) na Kanuni ya 3 (2) ya Nyongeza ya Saba ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari, 2016, Kamati ya Maadili inafanya kazi zake kwa faragha. Hivyo, ni kosa kuingilia kazi zake.

Waheshimiwa Wabunge, Wahariri na Waandishi wa Habari waliohojiwa ni:-

(a) Ndg. Denis Msacky, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mtanzania.

(b) Ndg. Bakari Kimwanga, mwandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania.

(c) Ndg. Angetile Osiah, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.

(d) Ndg. Elias Msuya, mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi.

(e) Ndg. Edmond Msangi, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Nipashe.

(f) Ndg. Gwamaka Alipipi, mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe.

Waheshimiwa Wabunge, Wahariri na Waandishi hao wa magazeti tajwa, walikiri na kujutia makosa yao na kisha waliomba radhi kwa Mheshimiwa Spika na Bunge. Aidha waliahidi kutorudia kutenda kosa hilo.

Waheshimiwa Wabunge, Kamati ilijiridhisha kuwa Wahariri na Waandishi walitenda kosa la kuandika na kuchapisha mwenendo wa shauri lililokuwa mbele ya Kamati.

Waheshimiwa Wabunge, Kamati imependekeza adhabu kwa wahusika baada ya kuzingatia kuwa Wahariri na Waandishi hao:-

(a) waliitikia wito na kutoa ushirikiano kwa Kamati

(b) walikiri na kujutia makosa yao

(c) ni wakosaji wa mara ya kwanza

Waheshimiwa Wabunge, baada ya kuzingatia masuala yote hayo, Kamati imenishauri ifuatavyo:-

(a) Wahariri na waandishi wote waliohusika wapewe onyo kali (reprimand).

(b) Wachapishe habari za kuomba radhi Bunge katika kurasa za mbele za magazeti yao ndani ya siku tano kuanzia tarehe ya leo.

Waheshimiwa Wabunge, nimeupokea ushauri huu wa Kamati na adhabu zilizotolewa, nami kwa niaba yenu nakubaliana na Kamati. Hivyo basi, natoa onyo kali kwa wahusika wote, na naagiza wahariri wa magazeti hayo wachapishe habari za kuomba radhi Bunge katika kurasa za mbele za magazeti yao ndani ya siku tano kuanzia tarehe ya leo.

Job Y. Ndugai, MB.

SPIKA

17 Novemba, 2017

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's