Parliament of Tanzania

Spika Ndugai afungua Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam

Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai amefungua mashindano ya Nane ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huku akisisitiza michezo hiyo kudumisha umoja na ushirikiano katika Jumuiya hiyo.

Akizungumza katika ufunguzi wa michezo hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Sabasaba Jijini Dar es Salaaam alisema mbali na michezo kuimarisha afya lakini pia inadumisha umoja baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tutumie michezo hii kudumisha ushirikiano uliopo ndani ya Nchi za Afrika Mashariki ili uzidi kuwa na nguvu na Umoja huu uwe mfano kwa Nchi nyingine za Afrika,” alisema.

Alisema Tanzania ikiwa mwenyeji wa Mashindano hayo imejipanga kuhakikisha yanafanyika na kumalizika kwa usalama kwa kuwa hali ya Ulinzi na Usalama imeimarishwa.

Aidha, alisema Timu za Bunge za Tanzania zimejiandaa kisawasawa kuchukua ushindi katika michezo yote.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Seneti la Burundi, Mheshimiwa Reverien Ndikuriyo alishukuru kwa mapokezi mazuri kutoka Tanzania na kusisitiza pia kudumisha umoja katika michezo hiyo.

Awali akitoa maelezo ya mashindano hayo, Katibu wa Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai alisema michezo hiyo imeshirikisha Nchi nne za Uganda, Burundi, Kenya na Tanzania pamoja na Timu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Nchi za Rwanda na Sudan ya Kusini wameomba udhuru wa kutoshiriki mashindano haya kwa mwaka huu.

Naye Mwenyekiti wa Timu ya Bunge, Mheshimiwa William Ngeleja aliitaja michezo itakayochezwa katika mashindano hayo kuwa ni mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa pete, riadha, kuvuta kamba na gofu.

Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Kenya, Mheshimiwa Moses Cheboi, Kiongozi wa Upinzani kutoka Bunge la Uganda, mabalozi na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mara baada ya uzinduzi kulifanyika mchezo wa riadha na kuvuta kamba ambapo katika mchezo wa riadha Timu ya Wanawake ya Bunge la Tanzania iling’ara huku kwa wanaume Timu ya Kenya iliongoza.

Kwa upande wa Kuvuta Kamba Timu ya wanaume ya Tanzania iliibuka na ushindi huku wanawake ilishinda Timu ya Kenya.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's