Parliament of Tanzania

SPIKA AKUTANA NA CAG

Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zitafanya mafunzo ya kujenga uwezo kwa Wabunge juu ya matumzi bora zaidi ya fedha za serikali kwa taasisi zake na mashirika ya umma ili kuongeza ustawi kwa wananchi.

Katika kufanikisha hilo Spika wa Bunge la Kumi na Moja Mhe Job Ndugai amekutana mapema leo tarehe 21 Novemba, 2015 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Juma Assad ili kutafakari hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya uzinduzi wa Bunge ambayo ililisisitiza uwajibikaji,weledi na utawala bora na ujenzi wa uchumi imara na maendeleo endelevu ya rasilimali za nchi kwa maendeleo ya watu.

Mara baada ya mazungumzo na Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Juma Assad alisema ili kuhakikisha fedha za serikali zinakidhi malengo yake ni muhimu kuwapo kwa taasisi ya ukaguzi wa hesabu inayolenga kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha katika makusanyo na matumizi ya rasilimali za umma.

Pia alisema sheria ya bajeti ya mwaka 2014 ina mapungufu na hivyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho katika kudhibiti na kusimamia rasilimali.

Kwa upande wake Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai alisema moja ya mambo makubwa waliyozungumzia ni pamoja na kuzingatia matumizi bora ya fedha za serikali kwa taasisi ya Bunge, taasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na taasisi za serikali kwa ujumla wake.

“Tumezungumzia pia namna ambavyo Kamati za Bunge zinazoshugulikia masuala ya kifedha zinavyoweza kuundwa kwa namna bora zaidi pamoja na kutoa mafunzo kwa Wabunge juu ya matumizi bora ya fedha za serikali,” alisema Spika Ndugai.

Katika Hatua nyingine aliyekuwa Spika wa Bunge la Kumi Mhe. Anne Makinda amekabidhi ofisi kwa Spika wa Bunge la Kumi na Moja Mhe. Job Ndugai na kuahidi kumpa ushirikiano, halikadhalika Naibu Spika wa Bunge la Kumi Mhe. Job Ndugai amemkabidhi ofisi Naibu Spika mpya wa Mhe. Dkt Tulia Ackson Mwansasu.

Mhe Makinda pia alitumia fursa hiyo kuwaaga watumishi wa Ofisi ya Bunge na kuwashukuru kwa ushirikiano walimuonesha wakati wa Uongozi wake na kuwaasa kuendelea kudumisha nidhamu kazini.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's